028-Aayah Na Mafunzo: Kumkufuru Allaah Ilhali Kuna Kufufuliwa Kuhesabiwa Na Kulipwa

Aayah Na Mafunzo

 

Al-Baqarah

 

Kumkufuru Allaah Ilhali Kuna Kufufuliwa Kuhesabiwa Na Kulipwa

 

 

كَيْفَ تَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَكُنتُمْ أَمْوَاتًا فَأَحْيَاكُمْ ۖ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٢٨﴾

28. Vipi mnamkufuru Allaah na hali mlikuwa wafu Akakuhuisheni, kisha Atakufisheni, kisha Atakuhuisheni, kisha Kwake mtarejeshwa?

 

Mafunzo:

 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba:

وَكُنتُمْ أَمْوَاتًا

“mlikuwa wafu” Kwa maana mlikuwa mchanga kabla ya kukuumbeni.  Basi hivi ni umauti.

فَأَحْيَاكُمْ

“Akakuhuisheni” Kwa maana; Akakuumbeni (mkazaliwa) basi huu ni uhai.

ثُمَّ يُمِيتُكُمْ

“kisha Akakufisheni” Kwa maana mtarudi makaburini, basi huu ni umauti mwengine.

ثُمَّ يُحْيِيكُمْ

“kisha Atakuhuisheni” Kisha Atakufufueni Siku ya Qiyaamah; kwa maani huu ni uhai mwengine. Basi hivyo ni kufa (umauti) mara mbili na uhai mara mbili kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

قَالُوا رَبَّنَا أَمَتَّنَا اثْنَتَيْنِ وَأَحْيَيْتَنَا اثْنَتَيْنِ

Watasema: “Rabb wetu! Umetufisha mara mbili na Umetuhuisha mara mbili [Ghaafir: 11] [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Imaam As-Sa’dy (Rahimahu Allaah) amesema: “Hili ni swali la kustaajabisha na onyo kali kwamba: Vipi iwe kwenu mnakufuru Allaah Ambaye Amekuumbeni na hali hamkuwa chochote hapo mwanzo, kisha Akakuneemesheni kila aina za neema, kisha Atakufisheni utakapofika wakati wenu ulioandikwa mfe, kisha Atakulipeni makaburini kisha Atakuhuisheni baada ya kufufuliwa na kukusanywa, kisha Kwake mtarudishwa Atakulipeni jazaa kamilifu. Basi madamu mko katika mageuzo Yake  na mabadiliko Yake, na chini ya amri Zake za kidini, na kisha baada ya  hapo kuna malipo; je, hivi inapasa kwenu mumkufuru? Na je, hii nini kama si ujahili mkuu kabisa na ujinga wa hali ya juu. Bali inayokupaseni ni kumcha Yeye na kumshukuru, na kumwamini na kuogopa adhabu Yake na kutaraji thawabu Zake.”

 

 

Share