Kumpa Zawadi Asiye Mahram Wako Inafaa?

SWALI:  

Asalaam Alaykum, miongoni mwa mambo yanayoongeza udugu wa kiislam ni waislam kupeana zawadi mbali mbali. Je zawadi inaruhusiwa kumpatia mtu ambaye si maharim wako? 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kupeana zawadi ni katika maagizo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa:

Peaneni zawadi mtapendana.

Lakini swali laja hapa, je, ni watu gani wapeane zawadi? Kupeana zawadi inalazimisha watu wawe karibu kimahusiano ya kisheria, na Uislamu umeweka vikwazo katika tangamano baina ya mwanaume na mwanamke. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Hakai mwanamme na mwanamke faragha isipokuwa watatu wao anakuwa shetani. Na shetani anatembea katika mwili wa mwanaadamu kama damu inavyopita katika mishipa” (Al-Bukhaariy).

Ukaribu huo wa kuanza kupeana vijizawadi kunamkaribisha Muislamu na zinaa, kwa mfano ya macho kwa kuangalia, ya mdomo kwa kuzungumza, ya miguu kwa kutembea, ya mikono kwa kushika.

Allaah Aliyetukuka Ametuusia pale Aliposeama:

Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (17: 32).

Allaah Aliyetukuka Hakutuambia tusizini bali hata tusiikaribie. Ndio mshairi wa hivi karibuni alisema: “Kutazama, kisha kutabasamu, baadaye salamu, kisha miadi, kisha makutano na mwisho kabisa uharara wa kitandani”. Tusithubutu tukaenda kufikia hatua hizo kabisa.

Ikiwa umempenda na unaona anakufaa kama mume au mke, Uislamu umeweka njia zake. Tazama jinsi gani Khadiyjah binti Khuwaylid (Radhiya Allaahu 'anha) hata kabla ya kusilimu alivyotuma watu kumposa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na ikiwa ni mume anamtaka mwanamke basi njia ni sahali kabisa. Tusiache mambo yatuzunguke kisha tukajuta baadaye. Kupeana zawadi kunakubalika kwa watu wa jinsiya moja – mwanamke kwa mwanamke na mwanaume kwa mwanaume na huko kupeana zawadi ni ishara kupendana na kupendana kunaashiria Imani.

Lakini kwa nyinyi ambao hamna uhusiano wa kidamu haifai kabisa na jiepushe kabisa na mahusiano ya aina yoyote na asiye maharimu wako, na kama kuna zawadi ulishaipokea kutoka kwa asiye maharimu wako, basi unatakiwa uirejeshe haraka ili uwe katika kuepukana na aina yoyote ya madhambi na mambo yenye utata na ili dini yako iwe salama.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share