121-ِِِAayah Na Mafunzo: Maana Ya Kuisoma Qur-aan Ipasavyo Kusomwa

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

Maana Ya Kuisoma Qur-aan Ipasavyo Kusomwa

 

 

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلَاوَتِهِ أُولَـٰئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ ۗ وَمَن يَكْفُرْ بِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿١٢١﴾

121. Wale Tuliowapa Kitabu wanakisoma kwa haki ipasavyo ya kusomwa kwake; hao ndio wanaokiamini, na atakayekikanusha basi hao ndio waliokhasirika.

 

 

Mafunzo:

 

 

Maana ya “kuisoma haki ipasavyo kusomwa”: ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) amesema: “Anapopita mtu panapotajwa Jannah, anamuomba Allaah Jannah, na anapopita panapotajwa moto anajikinga nao kwa Allaah.” 

 

Na Hudhayfah bin Al-Yamaan amehadithia kuhusu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba alipokuwa akiswali, pale anapopita Aayah ya rahmah aliomba rahmah, anapopita Aayah ya adhabu anajikinga nayo, anapopita Aayah ya kumsabihi Allaah anamsabihi (kumtukza) [Swahiyh Ibn Maajah (1119)]

 

Ibn Mas‘uwd (رضي الله عنه) amesema maana yake ni: “Anahalalisha Aliyohalalisha Allaah, na Anaharamisha Aliyoyaharamisha Allaah na anasoma kama Alivyoteremsha Allaah wala hapotoshi maneno sehemu zake wala hafanyii taawiyl lolote humo isiyokuwa taawiyl yake.” (Taawiyl: kukwepesha maana yake ya kihakika kwa kuipa maana ndogo au tofauti, ishara ambayo ni tofauti na maana ya juu; ni kukanusha maana).

 

Na Al-Hasan Al-Baswriy amesema: “Wanaifanyia kazi shariy’ah (hukmu) zake na wanaamini mutashaabih zake (mutashaabih: zilizofanana) na wanapeleka yanayowatatiza kufahamu kwa ‘Ulamaa wake.”

 
Pia, baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kuwa: Ni kuisoma kwa hukmu zake za tajwiyd, kufahamu maana yake, kuifanyia kazi maamrisho yake, kujiepusha makatazo yake, kujifundisha na kuifundisha. Hali kadhaalika kusabbih kila panapotajwa Tasbiyh, kumtukuza Allaah (عزّ وجلّ), kuomba Rahmah, kuomba maghfirah, kuomba kuingizwa Jannah (Peponi) na kuomba kinga ya Moto kila panapotajwa hayo.

 

 

 

Share