186-Aayah Na Mafunzo: Madamu Utamuomba Allaah Pekee Atakauitikia
Aayah Na Mafunzo
Al-Baqarah
Madamu Utamuomba Allaah Pekee Atakauitikia
وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾
186. Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka.
Mafunzo:
Du’aa hupokelewa tu madamu Muislamu atamkabili Allaah (تعالى) bila ya kumshirikisha: Salmaan (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Rabb wenu (تبارك وتعالى) (Aliyebarikika na Aliyetukuka), Yuhai, Mkarimu, Anastahi kutoka kwa mja Wake anaponyanyua mikono yake kisha Airudishe sifuri.” [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah]
Pia; Abuu Sa’iyd (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna Muislamu atakayeomba du’aa ambayo haina dhambi wala kukata undugu wa uhusiano wa damu isipokuwa Allaah Atampa mojawapo ya matatu; ima Amharakishie du’aa yake, au Amuwekee akiba Aakhirah au ima Amuepushe nayo ovu kama hilo.” Wakasema: Basi tutazidisha (kuomba du’aa). Akasema: “Allaah Mwingi zaidi (wa kuongeza).” [Ahmad]
