223-Aayah Na Mafunzo: (1) Haramisho La Kumuingilia Mwanamke Kwa Nyuma (2) Duaa Ya Kujimai

 

 

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

 

(1) Haramisho La Kumuingilia Mwanamke Kwa Nyuma (2) Duaa Ya Kujimai

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ ۖ وَقَدِّمُوا لِأَنفُسِكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّكُم مُّلَاقُوهُ ۗ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٢٢٣﴾

223. Wake zenu ni konde kwenu. Basi ziendeeni konde zenu (panapotoka kizazi) vyovyote mpendavyo. Na kadimisheni (mema) kwa ajili ya nafsi zenu. Na mcheni Allaah na jueni kwamba hakika nyinyi ni wenye kukutana Naye. Na wabashirie Waumini.

 

Mafunzo:

 

Haramisho la kumuingilia mwanamke kupitia dubur (uchi wa nyuma) yameharamishwa katika Hadiyth zifuatazo:

 

“Allaah Hatomtazama mwanamume mwenye kumuingilia mkewe kwa nyuma.” [An-Nasaaiy na Ibn Hibbaan kwa Isnaad nzuri].

 

"Amelaaniwa mwenye kumuingilia mwanamke kwa nyuma." [Ahmad, Abuu Daawuwd na Ibn 'Adiy]

 

"Mwenye kumuingia mwenye hedhi au mwanamke kwa nyuma au kumwendea mchawi na kumuamini kwa anayosema basi amekufuru kwa aliyoteremshiwa Muhammad." [Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah, na Isnadi yake ni Sahihi].

 

Faida: Kuhusu kauli ya Allaah “Na kadimisheni (mema) kwa ajili ya nafsi zenu.“ Yaani, jikurubisheni kwa Allaah kwa ‘amali njema na kumuingilia mke kwa kutaja Jina la Allaah kwa kusema, BismiLLaah – kabla ya kuanza jimai na kutaraji kupata kizazi chema; Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Iwapo mmoja wenu atamuingilia mke wake kisha akasema:

بِسْمِ الله اللّهُـمَّ جَنِّبْنا الشَّيْـطانَ، وَجَنِّبِ الشَّـيْطانَ ما رَزَقْـتَنا

BismiLLaah, Allaahumma Jannibnash-shaytwaan wa Jannibish-shaytwaan maa Razaqtanaa’  (Kwa Jina la Allaah, Ee Allaah! Tulinde na shaytwaan pia kilinde Ulichoturuzuku kutokana na shaytwaan) basi iwapo watakuwa wameandikiwa kupata mtoto, shaytwaan hatoweza kumdhuru)) [Al-Bukhaariy kama ilivyo katika Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

 

Share