Ribaa Inayotokana Na Kuwekeza Katika Saccos

SWALI:

Assalaam Allaykum

Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia pumzi hadi dakika hii. Pia na muomba Allaah awajalie yaliyo mema kwa yale mnayoyanya kwa kutuelimisha; awafanya muwe waislamu mpaka pale atakapowahitaji.

Ninapenda kuuliza ya kuwa kwa sasa kumezuka mpango kuanzisha saccos yaani watu watu wanaunda kikundi chao na wanaweka pesa na baadaye mwanachama anakopa na anaporejesha anatakiwa arejeshe na ribaa.Ile ribaa inakuwa ndiyo gharama ya kuendeshea chama/kikundi na mwisho mwaka wanaangalia kiasi cha matumizi na kiasi cha ribaa kilichobakia wanagawana kutokana na hisa ya mwanachama Sasa kwa kuwa kila mwanachama anafaidika na hiyo ribaa je itakuwa ni halali kujiunga na vikundi kama hivi? Naomba majibu ili nielimike kwa hilo

Mwanyezi Mungu tunakuomba utunusuru na ghadhabu yako, utujaliye yaliyo mema

Ni ndugu yenu katika Uislamu


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru ndugu yetu katika Iymaan kwa suala lako hilo. Mas-alah haya ya ribaa yamekuwa yakijitokeza kila wakati kwa watu kutaka kufahamu kuhusu suala hilo. Mara nyingi watu huwa hawaridhiki na majibu wanayopatiwa kwani wanadhania huenda siku moja wakapata mengine yanayoendana sambamba na maslahi yao.

 

Hakika ni kuwa Allaah Aliyetukuka Ametangaza vita na yeyote anayechukua ribaa pale Aliposema: “Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na acheni ribaa zilizobakia, ikiwa nyinyi ni Waumini. Basi mkitofanya jitangazieni vita na Allaah na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe” [2: 278-279].

 

Baadhi ya wajinga wanakuwa ni wenye kulinganisha baina ya ribaa na faida ya biashara kwa hivyo zote mbili hazina matatizo na ni halali. Allaah Aliyetukuka Anawajibu: “Biashara ni kama ribaa. Lakini Allaah Ameihalalisha biashara na Ameiharimisha ribaa” [2: 275].

 

Ni hakika kuwa pesa za sadaka huvia na za riba hunywea na kuleta hasara kwa mwenye kukengeuka na amri ya Allaah. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Allaah huiondolea baraka ribaa, na huzibariki sadaka. Na Allaah hampendi kila mwenye kukanya na afanyae dhambi” [2: 276].

 

Kuchukua mikopo ya riba ikiwa ni kutoka kwa mtu binafsi, shirika, saccos, banki na kadhalika zote ni haramu. Kila mmoja atazame hasara inayopatikana hapa duniani kwa watu hao ambao wanakiuka amri za Allaah na kesho Akhera watakuwa na adhabu kali zaidi. Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia: “Dirhamu (pesa za fedha) moja ya ribaa ambayo mtu anaila kwa kujua ni mbaya zaidi kuliko kuzini mara thelathini na sita [36]” [Ahmad].

 

Ni nasiha zetu kwa ndugu zetu katika Iymaan wakiepushe kabisa na muamala wowote ambao ni wa ribaa. Tukifanya hivyo bila shaka Allaah Aliyetukuka Atatutolea njia katika mambo yetu. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na anayemcha Allaah Humtengezea njia ya kutokea. Na humruzuku kwa njiya asiyotazamia. Na anayemtegemea Allaah Yeye humtosha” [65: 2-3].

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share