DNA Katika Uislaam Nini Hukmu Yake?

DNA Katika Uislaam Nini Hukmu Yake?

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

 

Asalam Aleikum,

Ningependa kujua kama ushahidi uliopatikana katika njia ya DNA unakubalika katika mahakama ya Kiislamu? Kama unakubalika ni kwa nini? Kwa vile sheria nyingi za Kiislam zinahitaji shahidi wa macho.

 

 

Na kama haukubaliki, hii haina maana kwamba mwizi ambaye ameacha fingerprints (alam za vidole) hawezi kuadhibiwa kwenye mahakama ya Kiislamu kwa vile hakuna shahidi wa macho aliyemuona? Nimependa makala zenu ninaishi Uingereza ningependa kujibiwa In shaa Allaah.  Wenu mpenda kujua

 

 

JIBU: 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Ni hakika isiyopingika kuwa Uislamu unakwenda sambamba na tafiti pamoja na nadharia sahihi za kisayansi.

 

 

Nadharia yoyote ambayo imefanyiwa uchunguzi wa kina haupingani na Aayah au Hadiyth Swahiyh. Ni nadharia kama za kina Charles Robert Darwin ambazo hazijafanyiwa utafiti ndio zinagongana na Qur-aan na Hadiyth. Hii ni kuwa nadharia hiyo imeletwa kwetu kwa malengo fulani. Ndio wanasayanyi wengi sasa wanasema nadharia hiyo ya "Ukuuzi wa mwana -Aadam" haina uthibitisho wala uhakika wowote.

 

 

Ni hakika pia katika nadharia za kisayansi kuwa lililo sahihi leo linaweza kuwa uongo kesho. Kwa hiyo, hizi nadharia huwa mara nyingi zinabadilika badilika. Nadharia zikingona na Qur-aan au Hadiyth Swahiy ni kuwa ima hatujaifahamu Aayah au Hadiyth hiyo au utafiti wa kisayansi haujafika katika uvumbuzi wa jambo hilo.

 

 

Jambo la sisi kujiuliza ni kuwa je, ushahidi wa DNA hauna shaka na ni thabiti au ni kinyume na hivyo?

 

 

Jawabu ni kuwa kuna tofauti kuhusu mas-ala haya miongoni mwa wajuzi wa kisayansi pamoja na ule uhakika kuwa matokeo mara nyingi yanabadilishwa kwa sababu moja au nyingine. Mara ngapi watu ambao wana ukimwi kwa sababu ya kuhonga au ujamaa wanaambiwa kuwa hawana chochote. DNA nayo ni hivyo hivyo kwani ulaghai na hongo unabatilisha mengi na kuwadhulumu wengine. 

 

 

Ikiwa tutazungumzia dola ambayo ni ya Kiislamu hata jambo la kwenda katika maabara ni la kupoteza wakati, kwani watu watakuwa ni wenye Iymaan ya hali ya juu.

 

 

kwa jinsi hiyo watakuwa wanajileta wenyewe ili watakaswe hata bila mashahidi, kwani Muumini anafadhilisha apigwe hapa duniani kuliko kupata adhabu kesho Aakhirah. Mfano ni kijana Maa'iz bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye alijipeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akarujumiwa [imepokewa na Abu Daawuud].

 

 

Na pia kesi ya mwanamke Ghamidiyyah ambaye naye alijipeleka mwenyewe ili atakaswe na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  

 

 

Hivyo suala la ushahidi wa macho ni muhimu sana na huwa halina utata aina yoyote. Uthibitisho unaowezekana hasa wa zinaa, ni kwamba ushahidi madhubuti uhakikishwe dhidi ya mhalifu. Vipengele muhimu vya Shariy’ah kuhusu hili ni:

 

 

1-Qur-aan wazi wazi inaamuru kwamba kuwe na angalau mashahidi wane walioshuhudia kwa macho yao ili kuthibitisha kosa hilo. Hayo yamekaririwa katika Suwratun Nuwr Aayah ya 4 na 13. Jaji hana mamlaka ya kuhumu kesi ya zinaa kwa msingi wa kulijua kwake tukio lenyewe hata kama ameona kwa macho yake huyo mwanamke na mwanamume wakitenda kitendo chenyewe.

    

                                                                                                                             

2-Mashahidi wawe ni wenye kuaminika kufuatana na sharia ya Kiislamu ya ushuhuda, ambayo inahitajia kwamba mashahidi wasiwe ni waongo katika ushuhuda wa tukio lolote lililopita, ithibitishwe kuwa hawajawahi kufanya uhalifu na kusiwe na uthibitisho kuwa wana chuki dhidi ya washitakiwa, na kadhalika. Ikiwa ushuhuda si wakuaminika basi hakuna adhabu kwa washitakiwa.

 

 

3-Mashahidi watoe ushahidi kuwa wamewaona (mwanaume na mwanamke) katika kitendo chenyewe cha kujamiiana kabisa kama kamba ndani ya kisima.

     

       

4-Ushahidi wa mashahidi uafikiane kabisa kuhusu wakati, mahali na watu waliofanya kitendo hicho. Khitilafu yoyote kuhusu hayo itabatilisha ushahidi wao kama ilivyotokea wakati wa ukhalifa wa 'Umar bin al-Khatwtwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) pale Abu Bakrah, Naafi', Shibli na Ziyaad walipokuwa mashahidi ya kuwa wamemuona Mughiyrah bin Shu'bah akizini na Umm Jamiyl, lakini walipotafautiana ushahidi wao ukatupiliwa mbali.

 

 

Masharti haya yanadhihirisha kuwa Shariy’ah ya Kiislamu haidhamirii kuwaadhibu watu hivi hivi. Inatoa adhabu kali sana, pale tu ambapo juu ya hatua zote za marekebisho hazikufua dafu. Mimba ya mwanamke kulingana na Wanachuoni wengi si thibitisho la kumpelekea mwanamke kurujumiwa au kupigwa mijeledi.

 

 

Adhabu hiyo kali ni lazima zitegemezwe aidha juu ya ushahidi au kukiri kosa kwa mshitakiwa kama walivyokiri wale waliozini.

 

 

Moja kati ya kanuni za msingi za Shariy’ah ya Kiislamu ni kwamba faida ya shaka imwendee mshtakiwa. Hili linaungwa mkono na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Epukeni adhabu kila mnapokuta mpenyo wa kuiepuka" [Ibn Maajah].

 

 

Katika Hadiyth nyingine alisema: "Jaribuni kuepuka kuwaadhibu Waislamu kila inapowezekana, na kama kuna njia kwa mshtakiwa kuiepuka adhabu, mwachilieni. Kosa katika hukumu ya kumwachilia mshtakiwa ni bora kuliko kosa la kumwadhibu bila haki" [at-Tirmidhiy]

 

 

Kufuatana na kanuni hii, kuwepo kwa mimba si ushahidi thabiti wa zinaa, japokuwa una nguvu zaidi upande wa shaka. Kwani upo uwezekano kwa moja katika milioni kwa mbegu ya kiume ya mwanamume kuingia katika uzao wa mwanamke kwa njia moja au nyingine bila ya kujamiina, hivyo kumfanya mwanamke mja mzito.  

 

 

Ndio tunapata ya kwamba Maa'iz alipokuwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuhoji na kugeuza uso wake mara nne, kila kijana huyo alipotaka kutakaswa. Akawa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anamwambia labda umembusu tu, au umemkumbatia, au umemshika shika tu au labda ulimtazama kwa tamaa. Lakini kijana huyo alikariri kuwa amejamiiana kabisa. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwuliza kama dhakari yake iliingia kabisa katika utupu wa mwanamke kama vile mchi wa mashine katika bomba. Alipojibu kuwa ndio, hapo ndipo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru aadhibiwe.

 

 

Mwingine alipokuja Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza kama akili yake ni timamu, je amelewa? Na maswali mengine kama hayo.  

 

 

Kwa hiyo katika mas-ala nyeti kama haya kuchukua DNA pekee haitatosha. Ama kuhusu fingerprints, Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Anatuelezea:

 

بَلَىٰ قَادِرِينَ عَلَىٰ أَن نُّسَوِّيَ بَنَانَهُ﴿٤﴾

Ndio! Tuna uwezo wa  kusawazisha sawasawa ncha za vidole vyake .[Al-Qiyaamah: 4]

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hapa Anatuonyesha uwezo Wake mkubwa wa kuweza kurudisha alama zetu za vidole pindi Atakapotufufua.

 

Inajulikana kuwa alama hizi ndio zinazotumika katika kutambua uhalifu kwani kila mmoja ana alama za kipekee ambao hata ndugu yake au baba yake hana.

 

 

Uchunguzi katika uhalifu wowote unaweza kuangalia mas-ala ya DNA na alama ya vidole lakini haiwezi kuchukuliwa kuwa kufanana huko moja kwa moja aliyepatikana ni mhalifu. Mfano, kumetokea wizi kwenye nyumba moja na ikaonekana alama ya vidole sehemu ambayo inafanana na mtu. Mtu yule anaweza kujitetea kuwa mimi nilifika pale ili kusaidia na nikashika sehemu fulani ambazo ilibakisha alama hizo zangu. Huyu anaweza kuchukuliwa kuwa ni mshtakiwa ambaye anaweza kusaidia katika uchunguzi lakini si moja kwa moja ni mhalifu.

 

 

Nyenzo hizi za kisayansi zinaweza kutumika sehemu nyingine kama ushahidi lakini si wa moja kwa moja katika kuhukumu jambo lolote.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share