Allaah Yuko Wapi?

 

Allaah Yuko Wapi?

 

Imetarjumiwa na Naaswir Haamid

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Allaah Ni Nani?

 

Allaah ni jina sahihi linalotumika kwa muabudiwa wa haki ambaye Yuko Mwenyewe kwa dhati Yake Mwenye Majina bora Matukufu na Sifa zisizo na shaka. Allaah ni Mmoja na Hana mfano Wake. Hana mtoto, mshirika wala mfano Wake. Yeye Ndiye Muumbaji pekee na Msimamizi wa ulimwengu. Kila kiumbe kinashuhudia Upweke Wake, Ukuu na Rubuubiyyah, na Utukufu na Majina ya kipekee.

 

 

Uwepo Wake haufanani na uwepo wa kawaida. Hayuko ndani ya kitu chochote, wala hakiingii kitu chochote Kwake.

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾

 Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Ash-Shuwraa: 11]

 

 

Yeye ni Mmoja, Pekee, Asiyegawanyika. Yeye ni Rabb (Baadhi hufasiri neno ‘Rabb’ kwa ‘Mlezi’, maana ya ‘Rabb’ iko mbali kimaana zaidi ya kubinywa katika neno moja kama ‘Mlezi’). Rabb, ina maana, miongoni mwa maana nyengine, Muumbaji, Mpaji, Mtoaji, Mwenye kuruzuku, Mwendeshaji mambo, Mlezi, Mfalme na ni Mmoja ambaye ndani ya mikono Yake kila jambo linafanyika, ambaye anafanikisha mambo yote, Allaah ni Mwenye Nguvu na Mwenye ujuzi.

 

 

‘Ilm Yake inaelewa kwa ukamilifu vitu vyote, vya siri na dhahiri. Ni Mkubwa kuliko ujuzi waliokuwa nao viumbe Vyake. Anajua kila kitu, Anafahamu kila kinachofanyika ndani ya ardhi na mbinguni. Allaah, Mtukufu, ni Rabb wa kila kitu na Anafanikisha mambo yote bila ya kulinganisha au kujifunza. Rahmah Zake zipo katika kila kitu. Yuko mbali na udhalimu au uadui. Ana hikmah katika matendo Yake yote, namna ambavyo Ana hikmah pia kwenye amri zake Zote. Uadilifu wake una hakikisha utulivu ndani ya ulimwengu, ambapo hakuna chochote kilicho nje ya ulinganizi.

 

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ ﴿١٦﴾

{Na kwa yakini Tumemuumba insani na Tunajua yale yanayowaza nafsi yake, na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo}. [Qaaf: 16]

 

 

Anaitika pale Muumini Anapomuomba pindi anapokuwa na haja au mkanganyo. Allaah Amekiteremsha Kitabu chake cha mwisho, Qur-aan, kwa Rasuli Wake wa mwisho, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa na jukumu la kufikisha Risala ya Uislamu kwa wana Aadam. Yeye ni Allaah Mtukufu. Sifa zote ni za Kwake.

 

 

Allaah Yuko Wapi?

 

Allaah, Aliyetakasika, Amejitambulisha Mwenyewe ndani ya Kitabu Chake, na kwa ulimi wa Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ni Mtukufu, Mkuu na Mwenye kujivuna. Qur-aan imesheheni ushahidi unaoendana na Kibriyaa cha Allaah.

 

 

Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah wanaamini katika kuthibitisha Sifa za Allaah bila ya kuharibu maana zake, na kwamba Allaah Yuko juu ya Mbingu Zake saba, juu ya ‘Arsh, na Ametenganishwa na viumbe Vyake, na viumbe Vyake vimetenganishwa Naye.

 

 

Makala hii itawasilisha ushahidi wa kimaandiko wa Allaah Mtukufu, ambao ni sehemu isiyotenganika na uelewa asili wa kumtambua Allaah ambao Allaah Amemuumba insaan. Ingawa ‘Aqiydah ya Utukufu wa Allaah ni sehemu ya ufahamu wa ndani wa mwana Aadam na ambao hauwezi kuhusishwa na nadharia tete ya mjadala wa kifalsafa, kuna baadhi ya makundi potofu yanayofuata matamanio yao na kuukana huu ukweli angavu na ushahidi unaojitosheleza. Kwa sababu hiyo, wamepindisha ushahidi wa Kitabu na kuziharibu maana, na kuyabadili maandiko ili kuendana na mjadala wao potofu.

 

 

Kwa hakika, sifa zote tukufu zinanasibishwa kwenye aina za sifa za Rabb Mtukufu. Hivyo, kuzikubali au kuzikataa ni lazima ziendane na kuukubali au kuukataa Utukufu wa Allaah. Yeyote anayeamini kwamba Allaah Yuko juu ‘Arsh Yake na Amejitenganisha na viumbe Vyake, halikadhalika ni budi awe anaamini sifa nyinginezo za Allaah, na anaamini kwamba mbingu na ardhi vinanyenyekea Kwake, na kwamba Yeye ni Rabb Mkuu wa ulimwengu. Allaah Anafanya vyovyote Anavyopenda na Anahukumu kwa mujibu wa matakwa Yake. Sifa zote zinastahiki Kwake.

 

 

Kukana sifa tukufu za Rabb Mtukufu ni miongoni mwa mafundisho ya kizushi ya Jahmiyyah (Wafuasi wa Jahm bin Safwaan; amefariki 128-745), mzushi mkubwa. Miongoni mwa mambo mengine, wanakana kwamba Allaah, Mtukufu, Yuko juu ya ‘Arsh yake na wanadai kwamba Yuko kila sehemu, na matawi yake Jahmiyyah wa leo (wanaendeleza uzushi huu) ili kuzichanganya akili za Waislamu. Kukana sifa hii tukufu pia kunapelekea kwa haja yake kukaidi sifa ya istiwaa ya Allaah kuwa yuko juu ya ‘Arsh Yake. Hakuna shaka yoyote kwamba kukana sifa za Allaah kunagongana na Aayah zilizo wazi za Qur-aan ambazo zinathibitisha sifa muhimu za kipekee na majina mazuri ya Allaah. Sifa hizi ni lazima ziwe sawa na Allaah.

 

 

Sifa tukufu muhimu za Allaah ni sehemu kuu ya uwepo Wake Allaah na hazihitajiki kuongezewa chengine chochote juu yake. Zinakubaliwa kilugha na Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah bila ya kuuliza ‘vipi’ kwa sifa hizi. Kuzikataa ni uwazi wa kutoamini na bila ya shaka yoyote ni uzushi. Ni kwa sababu hizi, makala hii imetayarishwa kueleza misingi ya Utukufu wa Allaah, au suala, ‘Allaah Yuko Wapi?’ kwa kutumia ushahidi wa maandiko kutoka kwenye Qur-aan na Ahaadiyth sahihi za Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), halikadhalika na mwenendo wa Waislamu wa mwanzo, na watangu wema waliopita.

 

 

Ushahidi Wa Qur-aan:

 

Allaah, Mtukufu, Amewaamuru Waumini pale wanapokuwa na migogoro kufanya rejeo ya Kitabu Chake na Sunnah ya Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾

{Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi}. [An-Nisaa: 59]

 

Hivyo, maneno ya Allaah, Mtukufu, pamoja na maneno ya Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni lazima yafanyiwe kazi kwa kiwango cha juu na pia kwenye kufikia maamuzi muafaka. Hakuna hukumu au maamuzi yao yatakayokuwa juu iwapo kwenye masuala yanayohusiana na sifa tukufu, au suala jengine lolote la Kidini.

 

Kwa kutilia kwao mkazo wa mantiki za kuthibitisha usahihi wa Diyn, watu wenye muono wa uwiano, watu wa kileo, na Jahmiyyah, wanadai (wanakubali) kutumika hoja dhidi ya Aayah tukufu. Hali ya kuwa Utukufu wa Allaah ambao umewekwa wazi ndani ya Qur-aan na Sunnah, upo mbali na kulinganishwa kwa mantiki.

 

Waumini wa kweli, tofauti na watu wenye muono wa uwiano, wanaamini kwamba ‘Arsh ya Allaah ipo juu ya mbingu saba. Pia wanaamini kwamba kwa kuwa Yeye ndiye muumbaji wa mbingu saba na ardhi na kilicho baina yake, Allaah, Mtukufu, Anayo ‘Arsh Yake Adhimu. Allaah Anasema:

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى ﴿١﴾

{Sabihi Jina la Rabb wako Mwenye ‘Uluwa Ametukuka kabisa kuliko vyote}. [Al-A’laa: 1]

 

Maneno “Mwenye ‘Uluwa”, kilugha, ni yenye kuonesha ubora kwamba Allaah Yuko juu kuliko kila kitu chochote na Yuko juu ya vitu vyote kwa kuanzisha, kinguvu na Asiyeshindwa. Kwa kuchangia katika hili, Ibn Al-Qayyim (Rahimahu Allaahu) amesema:

 

“Waislamu wote wa hapo zamani na wa sasa, pale wanapomuomba Allaah au kutaka msaada Wake, mara zote wananyoosha mikono kwa kuelekeza mbinguni vidole vyao vya mikono. Hawaelekezi mikono yao ilhali vidole vyao vikielekea ardhini, wala hawavielekezi kuliani au kushotoni, wala kuelekea mwelekeo mwengine wowote. Wananyoosha mikono yao juu, wakijua kwamba Allaah yuko juu yao. Waislamu pia wanasema wakiwa wanasujudu:

 

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى ﴿١﴾

{Sabihi Jina la Rabb wako Mwenye ‘Uluwa Ametukuka kabisa kuliko vyote}.” [Al-A’laa: 1]

 

Kama Allaah Yuko kila sehemu, kama wanavyodai makundi potofu, ni kwanini basi Aayah hiyo hapo juu haisomeki: “Mtaje Mola wako (akikuzunguka), (akiwa chini yako), au (kila sehemu)?” Allaah Anasema:

يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ ﴿٥٠﴾

{Wanamkhofu Rabb wao Aliye juu yao, na wanafanya yale wanayoamrishwa}. [An-Nahl: 50]

 

Aayah hii inawarudia Malaika ambao wapo juu yetu, na juu yao Yuko Rabb wetu, Aliyetukuka, Mwenye ‘Uluwa. Itokee mtu yeyote amechanganyikiwa, Allaah Anathibitisha ndani ya Aayah kwamba Yuko juu ya Malaika ambao ni wakaazi wa mbinguni:

مَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لِتَشْقَىٰ ﴿٢﴾

{Hatukukuteremshia Qur-aan ili upate mashaka}. [Twaahaa: 2]

 

Na:

 

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ  

Hakika Rabb wenu ni Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akawa juu (Istawaa)[1] ya ‘Arsh  [Al-A’raaf: 54]

 

Allaah pia Anasema:

 

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ﴿١٦﴾

Je, mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika?

 

 

أَمْ أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ كَيْفَ نَذِيرِ﴿١٧﴾

Au mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokutumieni tufani ya mawe basi mtajua vipi maonyo Yangu. [Al-Mulk: 16-17]

 

Wafasiri na washereheshaji maarufu wanakubaliana kwamba Yule Ambaye Yuko juu ya mbingu si mwengine ila ni Allaah Ambaye Amepanda juu ya ‘Arsh Yake na Yuko juu katika namna ambayo inalingana na Yeye Mwenye ‘Uluwa.

 

Wale wanaoamini kwamba Allaah Yuko kila sehemu wanaegemeza hoja zao kwenye Aayah mfano wa:

 

“Na Yeye ni Ilaah Yuko ndani ya Mbingu na Yeye ni Ilaah kwenye Ardhi!”

 

 

Neno ‘Ilaah’ ni la kiasili lenye maana, ‘mwenye kuabudiwa’, hivyo maana ya Aayah hiyo juu ni: “Yeye Ndiye muabudiwa wa haki mbinguni na ardhini”.

 

Itakuwa huko ni kujirejea iwapo Aayah zitakuwa zinazungumzia uwepo wa Allaah mbinguni na ardhini, kwani neno ‘Ilaah ni kivumishi cha Allaah, ilhali viwakilishi vyake ni ‘Yeye’ ndani ya Aayah vinatumika kwa nafasi ya neno ‘Allaah’. Hivyo, pale jina la ‘Allaah’ linapochukua nafasi ya kiwakilishi ‘Yeye’, tunapata maana sahihi ya Aayah:

 

وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَـٰهٌ وَفِي الْأَرْضِ إِلَـٰهٌ ﴿٨٤﴾

{Na ni Yeye Allaah Ndiye Mwabudiwa mbinguni na ardhini pia}. [Az-Zukhruf: 84]

 

Lakini kwa mujibu wa makundi potofu wanaofahamu neno ‘Ilaah’ kama ni ‘Allaah’, tunapata urejeaji wa maana, ‘Na Allaah ni Allaah mbinguni na Allaah Yuko ardhini’, sentensi yenye makosa ya kisarufi, kilugha na kimantiki. Qataadah, mfasiri maarufu, anafasiri Aayah hii kama ni:  “Yeye Ndiye Mwabudiwa mbinguni na ardhini”.

 

 

Imaam al-Aajurriy amesema: “Al-Ilaah, ni kuabudiwa. Yeye Anaabudiwa mbinguni na Anaabudiwa ardhini.”

 

 

Uwepo Wa Kila Pahala Wa Ujuzi Uliotukuka:

 

وَهُوَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ ۖ يَعْلَمُ سِرَّكُمْ وَجَهْرَكُمْ وَيَعْلَمُ مَا تَكْسِبُونَ ﴿٣﴾

{Na Yeye ni Allaah mbinguni na ardhini; Anajua ya siri yenu na ya dhahiri yenu; na Anajua yale mnayoyachuma}. [Al-A’naam: 3]

 

 

Wale wanaokana kwamba Allaah Yuko juu ya ‘Arsh Yake, kwa kujichanganya kwao, wanajadili kwamba Aayah hii inakubaliana na hoja zao. Hoja zao zinapingwa kwa kuelewa kwamba Aayah hii inarejea katika ujuzi wa Allaah, kwa mujibu wa wafasiri maarufu, si kwa uwepo Wake. Wanaendelea kudai kwamba Aayah hii inamaanisha kwamba ujuzi wa Allaah unazunguka vitu vyote mbinguni na ardhini. Rejeo ya ujuzi uliotukuka unarudiwa wazi ndani ya sentensi, ‘Anajua’ mara mbili ndani ya Aayah hii, ni kusema kwamba: “Allaah, Mtukufu, Anajua yaliyojificha na yaliyo wazi, na Anajua yale mliyoyachuma”.

 

 

Iwapo Aayah ingelimalizika kwa neno, ‘ardhi’, mtu angezichukulia maanani hoja zao tata, lakini Allaah, Mtukufu, Ameweka wazi mara zaidi ya moja kwamba ni ujuzi Wake, si uwepo Wake kwamba unajumuisha vitu vyote. Hoja nyingine tata inawasilishwa na wale wanaokana ukweli wa kwamba Allaah, Mtukufu, Yuko juu ya ‘Arsh Yake, kwa kudai kwamba Aayah ifuatayo inakubaliana na hoja zao.

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَىٰ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا ۖ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿٧﴾

{Je, huoni kwamba Allaah Anajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo ardhini? Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao (kwa ujuzi Wake), na wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao (kwa ujuzi Wake), na wala chini kuliko ya hivyo, na wala wengi zaidi isipokuwa Yeye Yu pamoja nao (kwa ujuzi Wake) popote watakapokuwa; kisha Siku ya Qiyaamah Atawajulisha yale waliyoyatenda. Hakika Allaah kwa kila kitu ni ‘Aliym}. [Al-Mujaadalah: 7]

 

 

Wanadai, kwa kutumia Aayah hiyo hapo juu, kwamba inamaanisha Allaah Yuko kihalisia sehemu zote. Hoja hii inakataliwa na mfasiri mbobezi, Ibn Kathiyr anayesema:

“Hii ina maana kwamba Allaah Anatambua vyema kwa yale wanayozungumza, na mazungumzo yao ya siri na fikra zao.”

 

 

Al-Qurtubiy ametoa maoni juu ya Aayah hii kwa kusema:

“Yeye Anatambua na anasikia minong’ono yao ya siri. Hii (inaonesha kuwa) ushahidi unatolewa juu ya ukweli kwamba ufunguzi na umalizikaji wa maneno ya Aayah hii unathibitisha ujuzi wa Allaah”.

 

 

Al-Qaasimiy anasema:

“Wanachuoni miongoni mwa Maswaahabah wa Rasuli, walioifikisha maana ya Qur-aan kwa wanaowafuata, wamekubali maana ya Aayah hii kwamba Allaah Yuko juu ya ‘Arsh Yake, lakini ujuzi Wake upo kila sehemu”.

 

 

Uchambuzi wa wataalamu wa lugha kwa Aayah hii unathibitisha nukta zifuatazo:

 

1. Maneno yaliyoanziwa katika Aayah hiyo juu yanazungumzia ujuzi wa Allaah, si mahali Pake.

 

 

2. Mnong’ono wa siri, au mazungumzo ya siri, ndio mada kuu ya Aayah hii. Allaah Anasema:

 

مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ ﴿٧﴾

{Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao (kwa ujuzi Wake)}. [Al-Mujaadilah: 7]

 

Wala Hasemi, “Hawawepo watatu, isipokuwa Yeye ni wa nne’. Hivyo maana inaonekana wazi kwamba ni ujuzi wa Allaah umewazunguka viumbe Vyake vyote.

 

 

3. Allaah Anathibitisha kwamba Atawaeleza mazungumzo yao ya siri siku ya Ufufuo.

 

 

4. Aayah inamalizika (hapo), hivyo, kuthibitisha ujuzi wa Allaah.

 

 

5. Aayah inaanza katika Suwratul-Mujaadilah (Suwrah ya 58), ambayo Aayah inayojadiliwa ni sehemu yake, kwa Aayah ifuatayo:

 

قَدْ سَمِعَ اللَّـهُ قَوْلَ الَّتِي تُجَادِلُكَ فِي زَوْجِهَا وَتَشْتَكِي إِلَى اللَّـهِ وَاللَّـهُ يَسْمَعُ تَحَاوُرَكُمَا ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ﴿١﴾

{Allaah Amekwishasikia kauli ya yule mwanamke anayejadiliana nawe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu mumewe, na anamshitakia Allaah; na Allaah Anayasikia majibizano yenu. Hakika Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote}. [Al-Mujaadilah: 1]

 

Allaah, Mtukufu, Anaeleza kwamba Amesikia kwamba mwanamke amelalamika kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na bila ya shaka yoyote Amesikia huyo mwanamke akijibishana na mumewe, lakini Hakueleza ndani ya Aayah kwamba Alikuwa ni wa tatu wao.

 

Katika Aayah inayofuatia, Allaah Anasisitiza kwamba Yuko na ufahamu kamili wa matendo ya waja Wake. Iwapo mtu angeliamini kwamba Allaah yuko kila sehemu kiuhalisia, basi halikadhalika itakuwa na maana kwamba Anaishi kwenye sehemu chafu. Ni mtu asiye na akili pekee ndie atadiriki kutoa sifa kama hiyo kwa Allaah. Allaah Yuko mbali kwa yale wanayomzulia.

 

Pia itakuwa na maana kwamba Allaah Anajichanganya pamoja na viumbe Vyake mbinguni na ardhi. Iymaan ambayo imepelekea kwenye Upanesia (Wahdatul-Wujuwd), na kukuza hadithi za mwabudiwa aliye na mwili. Allaah Yuko mbali kwa yale wanayomzulia. Upanesia (Wahdatul-Wujuwd) ni iymaan kwamba Allaah na ulimwengu ni kitu kimoja, kinyume na iymaan kuu ya Upekee (Ahad) ya Allaah na Utakatifu Wake wa kujitenga na viumbe Vyake, kama ilivyosisitizwa na Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah.

 

 

Hakuna budi kuwekwa wazi ndani ya vichwa vya Waumini sahihi kwamba hakuna chochote kinachomzunguka Allaah, Mwenye ‘Uluwa, wala hakuna sehemu ambayo Yeye yumo. Vitu na sehemu ni viumbe, na Allaah Yuko juu ya viumbe Vyake. Viumbe vyote vinamhitajia Yeye, hali ya kuwa Yeye Amejitenganisha na viumbe Vyake, na Anasimama Akiwa Hana haja ya kiumbe chochote.

 

 

6-(Wanaodai Allaah Yuko kila mahali, wanadai) mbingu ni Qiblah cha Du’aa anazoomba Muislamu kwa Allaah, viganja vikiwa vimeelekezwa juu wakiamini Allaah Yuko mbinguni. Wanapokabiliwa kujibu uhakika huo (wa madai hayo), wale wanaokana Utukufu wa Allaah wanadai kwamba Waislamu wanaomba kwa njia hii kwa sababu tu mbingu ni Qiblah cha du’aa au maombi.

 

 

7. Madai yaliyopo hapo juu, kwa kuanzia, hayana ushahidi ndani ya Qur-aan au Sunnah, na hayawezi kuhusishwa kwa Swahaba yeyote wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala kwa Taabi’iyn. Hakujatajwa tamko hili ndani ya Kitabu cha Allaah au Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Suala la Qiblah ni moyo wa Diyn ya Uislamu, kwa hivyo kila Muislamu ni lazima alitambue na haswa Wanachuoni wa Ummah wa Kiislamu ni lazima wangekuwa wanafahamu hilo.

 

 

8. Ni ukweli uliokubaliwa kwamba Ka’bah ni Qiblah rasmi ya kuswalia na du’aa au maombi. Kudai mbingu au sehemu nyingine yoyote kuwa ni Qiblah cha du’aa ni bid’ah (uzushi) mbaya kabisa na kwenda kinyume kabisa ya Qur-aan, Sunnah, na makubaliano ya Ummah, kwa sababu Waislamu wote wana Qiblah kimoja, Ka’bah.

 

 

9. Qiblah ndio kielekeo ambacho Waislamu wanaelekea au kuelekeza nyuso zao pale wanaposwali, na kueleza uso kwa kitu ni kukiangalia upande wake. Kama mbingu zingekuwa ni qiblah, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angeliamuru Maswahaba zake, ambao Allaah Ameridhika nao, kuelekeza nyuso mbinguni pale wanaposwali. Kinyume chake, Waislamu wanakatazwa kuelekeza macho yao juu wanaposwali, lakini wanalazimika kuwa makini na sehemu ambayo nyuso zao zitatulia wakati wa kusujudu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza: “Wale wanaoelekeza macho yao juu wakati wanaposwali waache kufanya hivyo, vinginevyo watakuja kuwa vipofu”. [Imaam Al-Bukhaariy, Imaam Muslim na wengineo].

 

Aayah za Qur-aan haziruhusu nafasi yoyote kwa maoni kama hayo. Allaah, Mtukufu, Ameamuru makhsusi kwa Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Ummah wake kuelekeza nyuso kuelekea Ka’bah pale wanaposwali, Akisema:

 

وَمِنْ حَيْثُ خَرَجْتَ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ ﴿١٥٠﴾

{Na popote utokako (ili kuswali) basi elekeza uso wako upande wa Al-Masjidil-Haraam}. [Al-Baqarah: 150].

 

Kisha Allaah Anawataka Waislamu:

 

وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّوا وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ ﴿١٥٠﴾

{Na popote mtakapokuwa basi elekezeni nyuso zenu upande wake}. [Al-Baqarah: 150].

 

Utukufu wa Allaah pia unathibitishwa kwa Aayah ifuatayo:

تَعْرُجُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ ﴿٤﴾

{Malaika na Ar-Ruwh (roho za viumbe au Jibriyl) wanapanda Kwake}. [Al-Ma’aarij: 4]

 

Aayah hii ina maneno yaliyo wazi ya Allaah, neno lake “kupanda” ni kitendo kinachotumika kuonesha kwamba Allaah Yuko juu na kutenganishwa na viumbe Vyake. Upandishwaji wa matendo juu pia unathibitishwa kwa maneno ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akieleza muda bora ambao ni muda mchache kabla ya adhuhuri (zawaal). Amesema:

 

“Huu ni muda ambao milango ya mbingu inafunguliwa, nataraji kwamba matendo yangu mema yatapandishwa kwa Allaah.”

 

Kitendo ‘kupanda’ katika maandiko kinaonesha kwamba matendo mema yanapandishwa juu kumfikia Allaah, Mtukufu. Na Allaah Anasema:

 

تَعْرُجُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ خَمْسِينَ أَلْفَ سَنَةٍ ﴿٤﴾

{Malaika na Ar-Ruwh (roho za viumbe au Jibriyl) wanapanda Kwake katika siku kadiri yake ni miaka khamsini elfu}. [Al-Ma’aarij: 4].

 

 

Utukufu wa Muumbaji umeoneshwa wazi kwa muda mrefu unaotenganisha Malaika wanaoishi mbinguni na Rabb wao juu yao. Na Allaah Anasema:

يُدَبِّرُ الْأَمْرَ مِنَ السَّمَاءِ إِلَى الْأَرْضِ ﴿٥﴾

{Anadabiri mambo kutoka mbinguni mpaka ardhini}. [As-Sajdah: 5]

 

 

Ieleweke ndani ya vichwa kwamba Aayah hii imetanguliwa na maneno ya Allaah: “Yuko juu ya ‘Arsh”. Na Allaah pia Anasema:

 

يَا عِيسَىٰ إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ ﴿٥٥﴾

{Ee ‘Iysaa, hakika Mimi ni Mwenye kukuchukua usingizini na Mwenye kukupandisha Kwangu}. [Aal-‘Imraan: 55].

 

 

Kwa vile Allaah Anamwambia ‘Iysaa (‘Alayhis-Salaam) kwa kusema: “Nitakupandisha Kwangu”, je watajibu nini wale wanaoamini kwamba Allaah Yuko kila sehemu pale wanapoulizwa: “‘Iysaa (‘Alayhis-Salaam) yuko wapi hivi sasa?” Aidha watasema kuwa ‘Iysaa (‘Alayhis-Salaam) yuko kila sehemu, au yuko mbinguni. Iwapo wanadai kwamba ‘Iysaa (‘Alayhis-Salaam) yuko kila sehemu, matokeo yake ni kwamba watakufuru kwa kumlinganisha ‘Iysaa (‘Alayhis-Salaam) na Allaah kwa mujibu wa dai lao kwamba Allaah yuko kila sehemu. Dai linalofanana na itikadi za Kikristo za kuwa muabudiwa ana mwili. Lakini iwapo watasema: “‘Iysaa (‘Alayhis-Salaam) yuko mbinguni,” watakuwa wamekubali kwamba hakika Allaah Alimpandisha ‘Iysaa (‘Alayhis-Salaam) juu mbinguni, na kwamba Allaah Yupo juu ya mbingu. Allaah Anasema:

 

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ﴿٥٤﴾

{Hakika Rabb wenu ni Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akawa juu (Istawaa) ya ‘Arsh  }. [Al-A’raaf: 54]

 

‘Istawaa’ inatokana na kitenzi cha sawiya na mizizi yake inayoifanya istiwaa kuwa na maana ya ‘Arsh. Ashaa’irah, Mu’tazilah na Jahmiyyah, na wale wenye itikadi kama ya Jahmiyyah (kama Maibadhi na Mashia), wanaamini sifa ya Istiwaa kuwa ni ya kialama tu, hali ya kuwa Ahlus-Sunnah wanaikubali na sifa nyinginezo za Allaah kilugha bila ya kuongeza vitu.

 

 

Hii ni moja ya Aayah saba za Qur-aan ambayo Allaah, Mwenye ‘Uluwa, Anaelezea istiwaa’ Yake juu ya ‘Arsh Yake.

 

 

Ahlus-Sunnah wana uhakika kwamba ‘Arsh tukufu ya Allaah ipo juu ya mbingu saba. Pia wanaamini kwamba Allaah, kwa kuwa Ameumba ardhi na Amepangia mahitaji yake yote, Amepanda juu ya ‘Arsh Yake tukufu. Ni wale tu wanaoamini vinginevyo wanashikilia Aayah hizi kuwa zina maana zilizojificha. Wanasema kuwa Allaah “yupo kila sehemu”, wakikana kwamba Allaah Yupo juu ya ‘Arsh. Allaah Mtukufu, na Yupo mbali kwa yale wanayoyanasibu. Kwa kunukuu Aayah zote au baadhi tu ya zile zinazoonesha Sifa tukufu za Allaah hazitosaidia kitu zaidi ya kukuza ukubwa wa suala hili. Kuna kiasi ya Aayah 215 ndani ya Qur-aan zenye kitendo ‘kuteremshwa chini’ kwa rejeo ya aidha Qur-aan, Vitabu vilivyopita au Malaika.

 

 

Ushahidi Kutokana Sunnah Za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):   

 

Kuna maandiko mengi na pia ushahidi mwingi wa Utukufu wa Allaah kutoka kwa Sunnah sahihi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), simulizi za Maswahaba wa Rasuli (Radhwiya Allaahu ‘Anhum), kazi za Maimamu Wanne na watangu Wachaji Allaah waliopita. Allaah, (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Anamsifu Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuthibitisha ukweli wake na uhalisia wake kwa kusema:

 

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾

Na wala hatamki kwa hawaa.

 

 إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ﴿٤﴾

Hayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa.

 

 عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ ﴿٥﴾

 Amemfunza (Jibriyl) mwenye nguvu shadidi. [An-Najm: 3-5]

 

  

 

 

Na Allaah Anasema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ﴿٧﴾

{Na lolote analokupeni Rasuli (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم )basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni}. [Al-Hashr: 7]

 

 

1. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Nimepewa Qur-aan na mfano wa hiyo”. [Abuu Daawuwd]

 

 

2. Sunnah iliyotakasika ni ile ambayo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemaanisha kusema: “na mfano wa hiyo”. Sunnah ni chanzo cha pili cha Shariy’ah. Ahaadiyth nyingi zinazungumzia Sifa za Allaah Mtukufu. Zifuatazo ni baadhi ya Hadiyth sahihi zilizochaguliwa ambazo Wanachuoni wote wa Hadiyth wa zama zote wamekubaliana na usahihi wake.

 

 

3. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) amesimulia safari yake muhimu kutoka Makkah hadi Quds na kutoka hapo hadi juu mbinguni kama ifuatavyo: Jibriyl alinichukua hadi mbingu ya chini kabisa na kuwaomba walinzi wake kufungua mlango. Aliulizwa, “Huyu ni nani?” Alijibu: “Jibriyl”. Waliuliza “Upo na nani?” Akajibu “Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).” Wakauliza. “Je amepata mwaliko?” Jibriyl akajibu “Ndio”. Kisha akakaribishwa kwa tamko la “Anakaribishwa sana.” Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaendelea na safari, ulipofunguliwa mlango, nikaingia na hapo nikakutana na Aadam. Jibriyl akaniambia, “Huyu ni baba yako, msalimie.” Aadam akanisalimia, kwa kusema: “Karibu, mwana Mchaji Allaah na Rasuli Mchaji Allaah.” Kisha Jibriyl akapanda hadi mbingu ya pili na kuwaomba walinzi wake kufungua mlango. Masuala yaliyoulizwa kwenye mbingu ya chini yalirudiwa kabla ya mlango kufunguliwa. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alieleza alichokiona katika kila mbingu, hadi mwisho akachukuliwa hadi mbingu ya saba ambapo Swalaah za fardhi zikalikabidhiwa kwake. [Imaam Al-Bukhaariy, Imaam Muslim na wengineo]

 

 

Hadiyth hii ni Mutaawatir, sahihi (na hili ni kundi lenye Ahaadiyth sahihi zaidi) inazungumzia wazi na kwa maneno yasiyotatiza na ya moja kwa moja yasiyo na utata au tafsiri mbaya. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichukuliwa juu kwa Rabb wake kutoka mbingu moja baada ya nyengine.  Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah wanaamini kwamba Mi’raaj haikuwa ni hali ya udanganyifu au hisia, bali ni safari ya kweli na hakika kabisa. Iwapo Allaah Yupo kila sehemu, ni kwanini Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichukuliwa njiani kote hadi mbingu ya saba? Bila ya shaka Allaah Angelimkabidhi Swalaah ardhini kuliko mbingu ya saba.

 

 

 4. ‘Abdullaah bin ‘Amr amesimulia kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Kuwa na huruma kwa waliopo ardhini, ili Yule Aliyeko juu ya mbingu Apate kuwa na Rahmah kwako”. [Imaam Al-Bukhaariy, Imaam Muslim na wengineo]

 

Abu Hurayrah amesimulia kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kawaida ya Malaika wa kutoa roho huwa wanamfikia mtu anayefariki. Iwapo ni Mchaji Allaah, wataiambia roho yake, “Ee roho njema! Toka nje ya mwili mzuri, na furahia kwa kupata rahmah na ulinzi kutoka kwa Rabb Ambaye Ameridhika nawe.” Malaika wataendelea kuisisitiza kwa maneno haya hadi roho inapotoka nje ya mwili. Kisha itachukuliwa juu hadi mbinguni ambapo ruhusa ya kufungua milango ya mbingu itaombwa. Walinzi watauliza, “Ni nani huyu?” Malaika watajibu. “Fulani mwana wa fulani” Walinzi watasema: “Unakaribishwa sana ee roho njema.”  Roho hiyo itasifiwa kwa maneno hayo hadi mwishoni itakapochukuliwa juu ya mbingu ambako ni kwa Allaah.” [Imaam Ahmad, Al-Haakim na wengineo].

 

 

Ni ushahidi wa wazi kwamba Allaah, Mwenye ‘Uluwa, Yupo juu ya mbingu saba. Vinginevyo, ni kwanini roho na matendo mema yanapandishwa hadi mbinguni kumfikia Allaah?

 

 

5. Abuu Hurayrah amesimuliwa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Malaika wa kutoa roho alikuwa na kawaida ya kuwapitia watu ambao roho zao zitakusanywa. Alipomfikia Rasuli wa Allaah, Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) ili kuichukua roho yake, Muwsaa alimpiga ngumi katika macho yake. Malaika wa kifo alipanda juu kwa Rabb wake, Mtukufu, na kusema Kwake: “Rabb wangu! Umeniteremsha chini kwa Muwsaa ambaye amenipiga machoni mwangu. Kama si kwa kukutii Wewe, ningelimpa wakati mgumu.”  Malaika wa kifo aliteremka kwa Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) kutoka mbinguni ili kuichukua roho yake. Hakutokea mashariki, magharibi, kaskazini au kusini, wala hakutokea kutoka ardhini, kisha akapanda kwa Rabb Wake ambaye Yupo ya mbingu.

 

 

6. Abuu Hurayrah amesimuliwa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kuna daraja mia moja Jannah ambazo amezitayarisha Allaah kwa ajili ya Mujaahidiyn wanaopigana kwa ajili Yake. Baina ya sehemu moja na sehemu nyengine, ni masafa sawa ya baina ardhi na mbingu. Unapomuomba Allaah ('Azza wa Jalla) muombe Firdaws, kwa sababu ipo katikati ya Jannah na ni sehemu ya juu kabisa ambamo mito ya Jannah inapita, na juu yake kuna ‘Arsh ya Rabb Mtukufu”. [Imaam Al-Bukhaariy, Ahmad na wengineo]

 

7.Amesimulia Mu’awiyah As-Sahmiy (Radhwiya Allaahu 'anhu): Nilikuwa na kondoo ambao niliwaweka baina ya Uhud na Juwaniyyah, wakiwa na mtumwa wa kike ili kuwaangalia. Siku moja, nilienda nje kuwaangalia kondoo wangu na kugundua kwamba mbwa mwitu amemnyakua mmoja wao. Kwa vile mimi ni binaadam tu, (nilighadhibika) na kumpiga msichana kofi. Baadaye, nilienda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumsimulia tukio hilo, naye akanichukulia kuwa nimetenda kitendo kikubwa (kibaya). Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Je nimuachie huru (kama ni njia ya kujiokoa na dhambi yangu).  Akasema “Muite.” Nilipomuita, alimuuliza: “Allaah Yuko wapi?” Alisema: Juu ya mbingu.  Kisha akamuuliza: “Ni nani mimi?” Akasema: Rasuli wa Allaah.  Baada ya hapo, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliniamuru akiniambia: “Muache huru, Yeye ni Muumini.” [Imaam Muslim, Abuu Daawuwd, na wengineo]

 

 

Hadiyth hiyo hapo juu, kwa mujibu wa Shaykh Khaliyl Al-Harraas, ina ushahidi mzuri wa Utukufu wa Allaah. Hapa ni mtu aliyemkosea mtumwa wake wa kike kwa kumpiga, na alitaka kujiokoa dhambi yake kwa kumuachia huru kama ni njia ya kumlipa. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichagua suala moja makhsusi, “Allaah Yuko wapi?” Kisha mtumwa wa kike akampatia jibu sahihi, “Juu ya mbingu.” Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtangaza kuwa ni Muumin. Je, haisimami Hadiyth hiyo hapo juu ni ushahidi mzito kwamba Allaah Yuko mbinguni? Bila ya shaka yoyote, huyo mtumwa wa kike, mchungaji, alimfahamu Rabb wake kuliko hao wajinga wanaodai kwamba Allaah Yuko kila sehemu!

 

 

8. Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesimulia kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Rabb wetu, Mwenye ‘Uluwa, Mtukufu, Anashuka hadi mbingu ya chini kabisa kila usiku, mnamo thuluthi ya mwisho ya usiku, na kusema: “Yeyote anayeniomba, Nitamuitikia. Je, Kuna yeyote anayeomba chochote? Nitampatia? Je, kuna mtu yeyote anayeoomba maghfirah yangu, nitamsamehe?.” [Imaam Maalik, Imaam Al-Bukhaariy, Imaam Muslim na wengineo].

 

Maneno ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Rabb wetu, Mwenye ‘Uluwa, Mtukufu, Anashuka hadi mbingu ya chini.” ni dhahiri yanaonesha alama kuu ya Ukubwa au ‘Uluwa wa Allaah, Aliyetukuka. Ingekuwa Allaah Yuko kila sehemu, kusingekuwa na haja ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anayemfahamu Allaah zaidi, kusema, “Allaah Anashuka”, wala kusingekuwa na sababu ya kutofautisha sehemu moja ya usiku kwa nyingine. Kuna jibu moja tu kwa hili: Allaah, Mwenye ‘Uluwa, Mtukufu, Yuko juu ya mbingu saba, na juu ya ‘Arsh Yake tukufu.

 

 

9. Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesimulia kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Atashuka kwa watumwa Wake Siku ya Kufufuliwa”. [At-Tirmidhiy na wengineo] Ni Siku ambayo Allaah atakuja chini kutoa uamuzi wa hukumu Yake.

 

 

10. Katika Hadiyth nyingine, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Atawakusanya waja wake kutoka wa mwanzo hadi wa mwisho katika Siku maalum, ambapo kwa miaka arobaini macho yao yatabaki yakielekea juu mbinguni kusubiri hukumu sahihi. Allaah kisha Atashuka kupitia mawinguni kutoka kwenye ‘Arsh yake hadi Kursiy.”

 

 

 

Msimamo Wa Maswahabah (Radhwiya Allaahu ‘Anhum):

 

 

1. Zaynab (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), mke wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alikuwa akijinasibu kuwa na hadhi ya juu dhidi ya wakeze wengine kwa kuwaambia, “Ni wazee wenu tu ndio waliowaidhinisha kufunga ndoa pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ilhali ni Allaah Ndiye aliyeniidhinisha kwake kutoka mbingu ya saba huko juu”. [Al-Bukhaariy]

 

 

2. Katika simulizi nyingine, alisema kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Ni Rahmaan, Mwenye ‘Uluwa, Aliyeniozesha kwako kutoka juu ya ‘Arsh Yake.”

 

 

3. Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu), alimwambia ‘Aaishah, mke wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akikata roho: “Kati ya wakeze wote wewe ulikuwa kipenzi chake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na alikuwa akiishi kwenye utakaso mtupu. Allaah, Mtukufu Amekuteremshia heshima yako kutoka juu ya mbingu saba iliyoshushwa na Jibriyl. Hakuna Msikiti hata mmoja miongoni mwa Misikiti ya Allaah ambamo Aayah za heshima yako hazisomwi mchana na usiku”. (Aayah zake zipo katika Suwratun-Nuur, 11 hadi 20). Huyu ndiye ‘Aaishah, mke wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapa duniani na Aakhirah, Mama wa Waumini, ambaye yale makundi yasiyojielewa (Mashia) yamejaribu kumchafua, lakini Allaah, Mtukufu, Amempatia heshima yake na kuuvunja uongo wao dhidi yake.

 

 

4. Katika risaalah yake baada ya kifo cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr Asw-Swiddiyq amesema: “Yule aliyekuwa akimuabudu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), (na atambue kwamba) Muhammad amekufa, na yule anayemuabudu Allaah, (na atambue kwamba) Allaah Yuko juu ya mbingu Milele Anaishi, wala hafi.” [Imaam Al-Bukhaariy na wengineo]

 

 

5. Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipita kwa mchungaji (mtumwa) na kumuuliza, “Je, unaye kondoo mzuri kwa ajili ya kumchinja?” Mchunga kondoo akamjibu: “Mmiliki wake yupo hapa.” Ibn ‘Umar akamwambia: “Mwambie kwamba mbwa mwitu amemchukua.” Hapo, mchungaji akainua kichwa chake juu na kusema, “Basi Allaah Yuko wapi?” Ibn ‘Umar akajibu, “Naapa kwa Allaah. Ni mimi ndiye niliyewajibika kusema, “Allaah Yuko wapi.” Baadaye akamnunua kondoo na mchungaji na kumuachia huru mchungaji na kisha akampatia huyo kondoo. [Adh-Dhahabiy]

 

 

6. ‘Abdur Rahmaan Al-Mahdi (Rahimahu Allaah); Alikuwa ni Mwanachuoni mkubwa na tegemezi kuu kwa kuandika mwenendo wa Rasuli, na ni mfuasi wa Imaam Ash-Shaafi’iy (135-198H). Al-Mahdi amesema: “Hakuna ovu jengine miongoni mwa watu wa kufuata matamanio kuliko wafuasi wa Jahm. Iymaan zao zote potofu zimo ndani ya mada moja; ‘Hakuna aliyepo juu ya mbingu.’ Ninaamini kwamba, kwa Allaah, wasifungishwe ndoa, wala wasiwarithi Waislamu wala wasirithiwe na Waislamu.” Rai hii ya Ibn Mahdiy inatumika miongoni mwa waongofu waliopita.

 

7. Wahab bin Jariyr amesema: “Kuwa na hadhari kwa maoni ya wafuasi wa Jahm, kwani wanawalazimisha watu kwamba hakuna chochote juu ya mbingu. Matamko yao si chochote zaidi ya wahyi wa Ibliys, na si chochote zaidi ya ukafiri”.

 

 

Msimamo Wa Maimamu Wakuu Wanne:

 

Imaam Abuu Haniyfah (Rahimahu Allaah); alikuwa ni mmoja miongoni mwa Maimaam wanne alikuwa ni Mwanachuoni maarufu aliyeishi mwaka 80 hadi 150H.

Abuw Mutwi’ Al-Balkhi amesimulia: “Nilimuuliza Imaam Abuu Haniyfah kuhusiana na mtu anayesema, “Sijui iwapo Rabb wangu Yuko, juu ya mbingu au ardhini?” Abuu Haniyfah, (Rahimahu Allaahu), amesema: “Mtu anayesema hivyo anakuwa ni kafiri kwa sababu Allaah, Mwenye ‘Uluwa Anasema: “Allaah Mtukufu Yuko juu ya ‘Arsh, na ‘Arsh ya Allaah ipo juu Mbinguni.” Nikamuuliza zaidi Abu Haniyfah, “Je, iwapo mtu huyo akakubali, Allaah Yuko juu ya ‘Arsh Yake, lakini akawa na mshangao, sijui iwapo Rabb wangu Yuko juu ya mbingu au ardhini?” Abuu Haniyfah akamjibu: “Iwapo anakataa kwamba ‘Arsh ipo juu mbinguni, huyo ni kafiri.” [Sharh Atw-Twahawiyyah, uk. 288].

 

Iwapo atakufuru (zaidi) kwa kusema kwamba haelewi wapi iko ‘Arsh ya Allaah, kwa usahihi basi mtu anayekana Utukufu wa Allaah kwa pamoja ni mbaya kuliko kafiri.

 

Imaam Maalik bin Anas (Rahimahu Allaah); ni mmoja miongoni mwa Maimaam wanne alikuwa ni Mwanachuoni maarufu aliyeishi mwaka 93 hadi 179H.

Abdullah bin Nafi’ amesimulia: Maalik bin Anas amesema: “Allaah Yuko juu mbinguni, lakini ujuzi Wake unajumuisha kila kitu. Hakuna chochote kinachompita Asikitambue kwa ujuzi wake.” [‘Abdullaah bin Ahmad, As-Sunnah, na wengineo]

 

 

Imaam Ash-Shaafi’iy (Rahimahu Allaah); ni ‘Abdullaah Muhammad bin Idriys Ash-Shaafi’iy, ni mmoja miongoni mwa Maimaam wanne alikuwa ni Mwanachuoni maarufu aliyeishi mwaka 150 hadi 204H.

Imaam Ash-Shaafi’iy (Rahimahu Allaah) amesema: “Itikadi ninayokubaliana nayo ni itikadi sawa na ile waliyoikubali ya Waislamu walionitangulia, kwa kuitaja, Kiapo cha Iymaan: “Hakuna muabudiwa anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, na kwamba Allaah Yuko juu ya ‘Arsh Yake, juu ya mbingu. Anashuka chini ya mbingu ya mwisho pale Anapotaka.”.[Al-Juyuwsh Al-Islaamiyyah, Ibn al-Qayyim, uk. 93]

 

Imaam Ibn Khuzaymah (Rahimahu Allaah), ambaye yeye mwenyewe ni Shaafi’iy, amesema: “Yeyote anayekataa kwamba Allaah Yuko juu ya ‘Arsh Yake, juu ya mbingu Zake saba, na kwamba Yuko mbali na viumbe Vyake, ni kafiri. Mtu kama huyo ni lazima aamuriwe kutubu na kuikana iymaan yake, vinginevyo ni lazima akatwe kichwa na atupwe kwenye takataka ili kwamba si watu Ahlul-Qiblah (Waislamu kwa ujumla wao) wala Ahlul-Dhimmah (Wakristo au Mayahudi ndani ya nchi ya Waislamu) watakaokirihishwa kwa harufu mbaya ya mzoga wake.”

 

 

Abuu Bakr Muhammad At-Tamiymiy (Rahimahu Allaah), Imaam wa Kishaafi’iy wa Naysabuur, amesema: “Siswali nyuma ya mtu anayekataa sifa za Allaah na hatambui kwamba Allaah Yuko juu ya ‘Arsh Yake.”

 

 

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah); ni Ahmad bin Muhammad bin Hanbal, Imaam mkuu, alipewa jina la Imaam wa Ahlus-Sunnah. Jina hili likaja kuwa ni jina linaloangaliwa sana ndani ya Uislamu kwa [kuweka kwake wazi] imaani zisizofaa. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaahu), alikuwa ni shujaa na muathirika wa maonevu yaliyofanywa kipindi cha utawala wa Kiongozi Al-Ma’muwn, ambaye aliamuru watu wake, chini ya maumivu ya adhabu zake kali, kutumia iymaan kwamba maneno ya Allaah ambayo Qur-aan imeandikiwa kwayo ni kiumbe (Qur-aan imeumbwa), hivyo kushabihiana na iymaan ya Wakristo. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah), aliyekana iymaan hii (kuwa Qur-aan ni kiumbe na si Maneno ya Allaah) alidhalilishwa, alifungwa na kuteswa.

 

 

Aliulizwa: “Je, Allaah Yuko juu ya ‘Arsh Yake, juu ya mbingu ya saba, akiwa mbali na viumbe Vyake, na kwa utambuzi Wake na uwezo Wake unajumuisha kila kitu kila mahala?” Alijibu: “Hakuna shaka yoyote, Yuko juu ya ‘Arsh Yake na hakuna chochote kinachokimbia nje ya utambuzi Wake.” [Al-Juyuwsh Al-Islaamiyyah, Ibn al-Qayyim, uk. 123]

 

Matamko yote hapo juu yanaonesha kwamba Ummah wote wa Waislamu, wa kale na sasa, wanaungana kuhusiana na iymaan ya Utukufu na ‘Uluwa wa Allaah, Aliyetukuka.

 

 

Mijadala Yenye Kutia Shaka:

 

Wafuasi wa baadhi ya makundi potofu wanahamasisha iymaan za uongo kwamba Allaah ni mwenye kuwepo kila sehemu Ambaye anaishi ndani ya viumbe Vyake. Zipo hoja za kimantiki nyingi zinazokana uovu wa Jahmiyyah na wale wanaojaribu kuhuisha iymaan zao hivi leo (Maibadhi na Mashia).

Kuthibitisha kwamba Allaah Yuko juu ya ‘Arsh Yake, na juu ya mbingu saba kwa namna ambayo inamstahikia Mwenye Utukufu, Imaam wa Ahlus-Sunnah, Ahmad bin Hanbal, (Rahimahu Allaahu), amezikana iymaan zao miaka zaidi ya alfu iliyopita, pale alipoandika: “Allaah Yuko wapi na Wapi Hayuko – Ufafanuzi wa Jahmiyyah wa kukana kwamba Allaah Yuko juu ya ‘Arsh.”

 

Tuliwauliza “Ni kwanini mnakataa kwamba Allaah Yuko juu ya ‘Arsh ilhali Amesema:

 

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾

Ar-Rahmaan; Yuko juu (Istawaa) ya ‘Arsh. [Twaahaa: 5]

 

tena:

اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ﴿٤﴾

 

Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake katika siku sita, kisha Akawa juu (Istawaa) ya ‘Arsh.    [As-Sajdah: 4]

 

 

Walijibu: “Yuko chini ya ardhi saba namna ambavyo Yuko juu ya ‘Arsh; Yuko mbinguni, juu ya ardhi na kila sehemu; hakuna sehemu ambayo Hayuko, wala Hayuko sehemu moja tofauti na nyingine.” Na wakanukuu Aayah: “Na Yeye ni Ilaah Mbinguni na Yeye ni Ilaah kwenye Ardhi!”

 

 

Iwapo utapenda kuthibitisha uongo wa Jahmiyyah wanaodai kwamba Allaah Yuko kila sehemu, si sehemu moja maalum, waulize, “Je, si kweli kwamba Allaah Alikuwepo wakati ambao kulikuwa hakuna kitu?” Jibu la Jahmiyyah linaweza kuwa: “Bila ya shaka yoyote, kulikuwa hakuna kitu chochote kabla ya Allaah.” Kisha waulize, “Je, Allaah Aliumba viumbe ndani Yake mwenyewe au nje Yake mwenyewe?” Jahmiyyah watalazimika kuchagua moja miongoni mwa majibu matatu yafuatayo:

 

 

1. Iwapo Jahmiyyah watadai kwamba Allaah Ameumba viumbe ndani yake mwenyewe, basi watakuwa wamefikia katika ukafiri moja kwa moja kwa kudai kwamba majini, Insaan na mashaytwaan wote wanaishi ndani ya Allaah.

 

 

2. Iwapo Jahmiyyah watadai kwamba Allaah Ameumba viumbe nje Yake mwenyewe lakini Akaishi ndani yake baadaye, pia halikadhalika watakuwa wamekufuru moja kwa moja kwa kudai kwamba Allaah Anaishi ndani ya viumbe Vyake.

 

 

3. Lakini iwapo Jahmiyyah watasema kwamba Allaah Ameumba viumbe nje Yake Mwenyewe na Hajapatapo kuishi ndani yao, kwa kupitia jibu lifuatalo, watakuwa wamejumuika na Ahlus-Sunnah, kwani kwa kutoa jibu hili watakuwa wamekana iymaan zao potofu wenyewe.

 

Allaah, Mtukufu, Amejitolea ufafanuzi Mwenyewe ndani ya Tawraat pia kwamba Yuko juu ya viumbe vyake. Ka’bul-Ahbaar amesema: “Allaah ('Azza wa Jalla)  Amesema ndani ya Tawraat, “Mimi, Allaah Niko juu ya waja Wangu, na ‘Arsh Yangu iko juu ya viumbe Vyangu, na Mimi Nipo juu ya ‘Arsh nikitimiza mambo ya waja Wangu. Hakuna chochote Kinachonificha Mimi si mbinguni wala ardhini”. [Adh-Dhahabiy na wengineo]

 

Mwisho, itakuwa ni vizuri kusema kwamba hata adui wa Allaah, Fir’awn, ambaye waziwazi amedai kuwa yeye ni muabudiwa wa watu wake, alikuwa akitambua wapi Allaah Yuko kuliko wafuasi wa leo wa Jahmiyyah (Maibadhi na Mashia). Allaah Anasema:

 

وَقَالَ فِرْعَوْنُ يَا هَامَانُ ابْنِ لِي صَرْحًا لَّعَلِّي أَبْلُغُ الْأَسْبَابَ ﴿٣٦﴾

أَسْبَابَ السَّمَاوَاتِ فَأَطَّلِعَ إِلَىٰ إِلَـٰهِ مُوسَىٰ وَإِنِّي لَأَظُنُّهُ كَاذِبًا ﴿٣٧﴾

{Na Fir’awn akasema: “Ee Haamaan nijengee mnara ili nifikie njia. “Njia za mbinguni ili nimchungulie Ilaah wa Muwsaa, kwani hakika mimi namdhania ni muongo}. [Ghaafir: 36-37]

 

 

Basi sasa angalia maneno ya Fir’awn aliyemtaka Haamaan amjengee mnara kwa ajili yake ili aweze kupanda na kupita njia yote hadi mbinguni kumuona Rabb wa Muwsaa (‘Alayhis-Salaam), kwani Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) alikwishamwambia kwamba Allaah Anayemlingania kumuabudia Yuko juu ya mbingu, na linganisha hili kwa hoja zisizo na mashiko za Jahmiyyah hivi leo. Muislamu anashangaa ni kwa namna gani walioamini kwamba Allaah yuko kila sehemu wanalikubali dai kama hilo wakielewa kwamba, Allaah Mwenye Nguvu, Ataikusanya ardhi ndani ya Mkono Wake na kuikunja mbingu ndani ya Mkono wa Kuliani, kama ilivyotolewa ushahidi kwa kupitia indhari kali ifuatayo:

 

وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٦٧﴾

{Na hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria; na hali ardhi yote itakamatwa Mkononi Mwake Siku ya Qiyaamah; na mbingu zitakunjwa Mkononi Mwake wa kulia. Subhaanahu wa Ta’aalaa! (Utakasifu ni wa Allaah na Ametukuka kwa ‘Uluwa) kutokana na yale yote wanayomshirikisha}. [Az-Zumar: 67]

 

Iwapo Aayah hiyo hapo juu ni pekee yenye ushahidi wa Utukufu wa Allaah, ingelikuwa zaidi ya kutosheleza. Hakika inawatosha kwa wale wanaomkhofu Allaah na kumpa Yeye heshima sahihi kwa namna inayomstahikia Yeye.

 

 

Hitimisho:

 

Vizazi vitatu vya mwanzo vya waja wema (Salafus-Swaalih) ambavyo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewathibitishia, na matendo yao mema yalizidi kuliko vizazi vinavyofuata, ni Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na vizazi viwili vilivyofuata. Wote waliamini tafsiri iliyo wazi ya Aayah ya Qur-aan pamoja na sifa za Kiutukufu bila ya kuziharibu maana kwa kuegemea falsafa za Kigiriki.

 

 

Muumini ni lazima aamini kwamba hakuna mfano wake kama Allaah, Mtukufu, kwa Uwepo Wake, sifa Zake wala matendo Yake. Ni lazima aamini kwamba Allaah Anasimama bila ya haja ya kiumbe Chake chochote. Hana ndani Yake kitu wala sehemu yoyote. Yupo juu ya ‘Arsh Yake, juu ya mbingu saba, na juu ya viumbe Vyake vyote kimsingi na kihalisia wala si kidhanifu.

 

 

Hakuna yeyote katika viumbe Vyake Vinavyomgusa. Kwa kutegemea hili, haiwezekani kusema kwamba Allaah Yuko kila sehemu, au Yuko Anaishi ndani ya viumbe Vyake, kwani Allaah Alikuweko kipindi ambacho kulikuwa hakuna kitu chochote. Yule anayejidai kwamba Allaah Hayuko nje ya ulimwengu, si tu kwamba anakana uwepo wa Allaah, lakini anamuabudu muabudiwa ambaye hayuko.

 

 

 Tunamuomba Allaah Atuhifadhi katika njia sahihi ya Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake na kutujumuisha pamoja nao Siku ambayo hakutokuwa na manufaa kutokana na utajiri au kizazi.

 

 

 

 

[1] Faida: Maana ya Istawaa: Yuko juu kabisa kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye Mwenyewe Allaah. Pia rejea tanbihi (2: 29).

 

Share