161-Aayah Na Mafunzo: Tahadharisho La Kufanya Khiyana

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Tahadharisho La Kufanya Khiyana

 

 

 

 وَمَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَغُلَّ ۚ وَمَن يَغْلُلْ يَأْتِ بِمَا غَلَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿١٦١﴾

161. Na haikuwa (ni tabia) kwa Nabiy yeyote kukhini (ngawira). Na yeyote atakayekhini atakuja na kile alichokikhini Siku ya Qiyaamah. Kisha italipwa kamilifu kila nafsi yale iliyoyachuma nao hawatodhulumiwa.

 

 

Mafunzo:

 

 

Sababun-Nuzuwl: Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alituma jeshi, likarejeshewa bendera yake (yaani halikukubaliwa jeshi hilo ‘amali yake hiyo). Kisha akalituma tena likarejeshewa halikukubaliwa ‘amali yake kwa sababu ya khiyaana iliyofanyika ya dhahabu iliyokuwa kubwa mfano wa kichwa cha mbuzi. Ndipo ikateremka: Na haikuwa (ni tabia) kwa Nabiy yeyote kukhini…” [Mu’jamu Atw-Twabaraaniy].

Pia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba: Aayah hii: Na haikuwa (ni tabia) kwa Nabiy yeyote kukhini…” imeteremshwa kuhusiana na mahameli jekundu lilopotea siku ya Badr, kisha baadhi ya watu wakasema ameichukua Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), Wakazidi kuendelea kusema basi Allaah Akateremsha: Na haikuwa (ni tabia) kwa Nabiy yeyote kukhini (ngawira). “Na yeyote atakayekhini atakuja na kile alichokikhini Siku ya Qiyaamah…” (3: 161) [Ameipokea Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy na akasema Hasan Ghariyb].

 

Na Abuu Maalik Al-Ashja’iy amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ghuluwl (khiyaana ya wizi) kubwa mbele ya Allaah ni kipande cha ardhi ambacho utakuta watu wawili majirani katika ardhi au katika nyumba kisha mmoja wapo akakata kipande cha ardhi ya mwenziwe (bila haki), basi akifanya hivyo, atafungwa nacho kutoka ardhi saba mpaka Siku ya Qiyaamah.” [Ahmad].

 

Pia, Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Alisimama mbele yetu Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akataja suala la kuiba ngawira, akalishadidia na kulitilia umuhimu jambo hilo, akasema: “Nisije kumkuta mmoja wenu siku ya Qiyaamah juu ya shingo yake kuna mbuzi anatoa sauti, juu yake kuna farasi anatoa sauti aseme: Ee Rasuli wa Allaah! Niokoe! Nitamwambia: Similiki kwako kitu chochote, hakika nilikubalighishia. Na juu ya shingo yake kuna ngamia anatoa sauti aseme: Ee Rasuli wa Allaah! Niokoe! Nitamwambia: Similiki kwako kitu chochote hakika nilikubalighishia. Na juu ya shingo yake kuna nguo zilizo chanikachanika zinapepea kisha aseme: Ee Rasuli wa Allaah! Niokoe! Nitamwambia: Similiki kwako kitu chochote hakika nilikubalighishia.[Al-Bukhaariy (2891)].

 

‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Siku ya vita vya Khaybar, Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) walimwendea na kusema: Fulani na fulani wamekufa shahidi, fulani na fulani wamekufa shahidi. Walipomtaja mmojawapo kuwa kafariki shahidi, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Hapana! Nimemuona motoni kwa sababu ya kanzu aliyoiiba (katika ngawira).” [Ahmad na Muslim kwa riwaayah nyingine].

Share