159-Aayah Na Mafunzo: Unyenyekevu Wa Nabiy Kutaka Ushauri Kwa Maswahaba

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Unyenyekevu Wa Nabiy Kutaka Ushauri Kwa Maswahaba

 

 

فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ ۖ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ ۖ فَإِذَا عَزَمْتَ فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚإِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَوكِّلِينَ ﴿١٥٩﴾

159. Basi ni kwa rahmah kutoka kwa Allaah umekuwa mpole kwao (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na lau ungelikuwa mjeuri mwenye moyo mgumu wangelitawanyika mbali nawe. Basi wasamehe na waombee maghfirah na washauri katika mambo. Na unapoazimia basi tawakali kwa Allaah. Hakika Allaah Anapenda wanaotawakali

 

Mafunzo:

 

Fadhila na upole wa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) umetajwa mare tele katika Qur-aan na Sunnah, na rejea Aayah (9: 128).

 

Amri na pendekezo la kutafuta ushauri: Allaah  (سبحانه وتعالى) Amemuamrisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) atake ushauri kwa Maswahaba zake, naye (صلى الله عليه وآله وسلم) akawataka wamshauri katika hali kadhaa ili awatulize nyoyo zao. Na hili ni funzo kwamba ushauri ni jambo muhimu na pia mkubwa au mwenye cheo anaweza kutafuta ushauri kwa wadogo wake au walio duni yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwataka ushauri Maswahaba zake katika mambo mbali mbali, mfano; aliwataka ushauri katika vita vya Badr kama kuteka msafara wa Abuu Sufyaan au kupigana vita wakamshauri kupigana vita. Pia aliwataka pia ushauri katika vita vya Uhud alipowauliza kama wanaona bora kuweka boma Madiynah au waende kupigana vita, basi wengi wao wakashauri kwenda vitani. Pia alichukua ushauri wao katika vita vya Khandaq kuhusu kufanya sulhu na makabila ya Al-Ahzaab (makundi ya washirikina wa Makkah), ili badala yake wawape thuluthi moja ya mazao ya Madiynah, lakini Sa’d bin ‘Ubaadah na Sa’d bin Mu’aadh (رضي الله عنهما) wakakataa bali wakakhitari na wakashauri vita. Pia aliwataka ushauri kama wawahujumu washirikina siku ya Hudaybiyyah, lakini Abuu Bakr alikataa akasema: “Hatukuja kupigana bali tumekuja kutekeleza ‘Umrah.” Akawataka ushauri katika tukio la Ifk (kusingiziwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها)) Na katika hali nyinginezo mbalimbali alikuwa akiwataka ushauri Maswahaba zake (رضي الله عنهم).

 

 

 

Share