Majina Ya Watoto Na Maana Yake

Majina Ya Watoto Na Maana Yake

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam alaykum

Naomba maana ya majina yeyote tuwapao watoto wetu AU mnielekeze wapi naweza kupata labda katika kitabu cha fasiri ya majina mazuri tuliyohusiwa na MTUME  S.A.W

kwa mfano; Maryam  maana yake mtumishi wa Allaah Adia maana yake zawadi RAMADHANI, SHABANI, RAJABU NAFAHAMU MAANA JE LATIFAH, FATMAH, AMOUR, NILAYA  NA MENGINE MENGI

Waa hadha assalam alaykum w,w

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu majina.

 

 

Hakika ni kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia muongozo kuhusu kuwapatia watoto wetu majina.

 

 

Ametuusia sana majina tunaowapa watoto wetu yasiwe mabaya bali yawe ni yale mazuri.

 

 

Katika muongozo huo ametukataza kujiita majina kama

Aflah, Naajih (aliyefaulu),

Naafi (mwenye manufaa),

Yaasar (usahali)

[Muslim, Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy]

 

 

Vile vile amekataza jina la:

Maalikul Muluuk (mfalme wa wafalme) [Muslim].

Pia majina kama Al-‘Aasw (muasi),

‘Aziyz (mshindi), ‘Atla (ugumu),

Shaytwaan (shetani),

Al-Hakam (hakimu),

Ghuraab (kunguru),

Hubab (nyoka),

Harb (vita),

Al-Mudhtwaji‘ (aliyelala),

Bani zaaniyah (wana wa zina)

[Abuu Daawuwd.

 

 

Pia amekataza majina baridi kama vile:

Hayfaa (sifa ya mwanamke mwenye tumbo jembamba na kiuno kinene),

Ahlaam (ndoto),

Sausan (yungiyungi),

na kadhalika.

 

 

Pia wazazi wajiepushe na majina ya vitu au viumbe vinavyoabudiwa kinyume na Allaah kama vile:

‘Abdul-‘Uzza (mtumwa wa Uzza – mungu sanamu),

‘Abdul-Ka‘bah (mja wa Ka‘bah),

‘Abdun-Nabiy, ‘Abdur-Rasuul (mtumwa wa Nabii),

‘Abdul-Husayn (mja wa Husayn, kama wanavyojiita Mashia)

na kadhalika.

 

 

Ama kuhusu majina uliyoyataja hakuna jina la Adia bali inatakiwa iwe ni Hadiya (zawadi).

 

 

Bila shaka majina kama Ramadhwaan, Sha‘baan na Rajab yanatokana na miezi ya Kiislamu.

 

Ama jina Latwiyfah ni jina la kike lenye maana ya upole au ulaini, ‘Amuur ni kukaa au maskani na Faatwimah ni jina la bintiye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa ndiye kipenzi chake.

 

Ama Nilaya hatujui ni lugha gani.

 

Kadhaalika, katika Qur-aan utapata majina ya Manabii na watu wema ambayo unaweza kuwapatia watoto wako na pia majina ya Maswahaba na wema waliopita kama Maimaam, Maulamaa na wengineo.

 

 

Na jiepushe na majina ya watu waovu ambayo unatakiwa uepuke kuwapa majina hayo watoto wako. Ama katika vitabu vya Hadiyth kama vile Sahiih al-Bukhaariy, Muslim na wengineo utayapata hayo yakiwa yamejaa.

 

 

Pia vipo vitabu ambavyo vinauzwa katika maduka ambayo yametaja majina ya Kiislamu pamoja na maana yake.

 

 

Na kuna majina tunayoyatumia katika nchi zetu ambayo hayana maana nzuri na zaidi kusababisha watu kutaniwa nayo na kubezwa nayo ni bora kuyaepuka na hata inaruhusiwa kisharia kuyabadilisha kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyowabadilisha baadhi ya Maswahaba majina yao, kama kina Abu Hurayrah, Abu Bakr na wengineo ambao walikuwa na majina yasiyo mazuri kama ‘Abdu Shams (mja wa jua) n.k.

 

 

Hivyo tusiwaite watoto wetu majina kama:

Chausiku, Cheusi (kwa sababu mweusi sana),

Cheupe (kwa sababu kazaliwa mweupe sana),

Pondamali,

Kufakulala (kwa kuwa analala sana),

Mchambawima,

Kupekupe,

Langare, Kiguru, Kitenguru (kwa sababu kilema cha mguu),

Mzungu au Zungu (kwa sababu mweupe sana) n.k.

 

 

 

Majina yasiyo na maana na yasiyopendeza ni vizuri watu kuyaepuka in shaa Allaah.

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atutunuku watoto wa kike/kiume wenye Dini na maadili pamoja na watoto wema tutakaowapa majina mazuri.

 

www.alhidaaya.com

Share