101-Aayah Na Mafunzo: Msiyadadisi Mambo Ambayo Allaah Amenyamazia

Aayah Na Mafunzo

Al-Maaidah

Msiyadadisi Mambo Ambayo Allaah Amenyamazia

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَسْأَلُوا عَنْ أَشْيَاءَ إِن تُبْدَ لَكُمْ تَسُؤْكُمْ وَإِن تَسْأَلُوا عَنْهَا حِينَ يُنَزَّلُ الْقُرْآنُ تُبْدَ لَكُمْ عَفَا اللَّـهُ عَنْهَا ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ حَلِيمٌ ﴿١٠١﴾

101. Enyi walioamini! Msiulizie mambo ambayo mkifichuliwa yatakuchukizeni. Na mkiyaulizia pale inapoteremshwa Qur-aan mtafichuliwa. Allaah Ameyasamehe hayo. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mpole wa kuwavumilia waja.

قَدْ سَأَلَهَا قَوْمٌ مِّن قَبْلِكُمْ ثُمَّ أَصْبَحُوا بِهَا كَافِرِينَ ﴿١٠٢﴾

102. Walikwishayauliza hayo watu wa kabla yenu, kisha kutokana nayo, wakawa makafiri.

 

Mafunzo:

 

Abuu Tha’labah Al-Khushaniy (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah تعالى Amefaridhisha mambo ya Dini kwa hivyo msiyapuuze. Akaweka mipaka basi msiivuke, na Amekataza baadhi ya mambo kwa hivyo msiyafanye, na yale ambayo Amenyamazia ni kwa ajili ya rahmah Zake kwenu, si kwamba Ameyasahau kwa hivyo msiyadadisi.” [Ad-Daaraqutwniy na wengineo; Hadiyth Hasan].

 

 

Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremshwa kwa sababu ya wingi wa maswali waliyokuwa wakiuliza watu katika hali na wakati mbali mbali; ima kwa istihzaa au mitihani iliyowasibu au kwa talbiys (kufunika haki na kuipotosha). Mfano pale ilipoteremka Aayah ya kuwajibika Hajj: Na kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze Hajj katika Nyumba…” (3: 97) akashikilia mtu kuuliza kuhusu kuwajibika Hajj kama inawajibikia kila mwaka, jambo ambalo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) angejibu kuwa “Naam”, basi ingewajibikia kisha hapo ingekuwa ni amri na jambo gumu mno kulitekeleza. [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo].

 

Sababun-Nuzuwl: Pia, kama alivyohadithia Anas bin Maalik (رضي الله عنه) kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alitoa khutbah ambayo sijapatapo kuisikia kama hiyo kisha akasema: “Mngelikuwa mnayajua yale ninayoyajua, basi mngelicheka kidogo na mngelilia sana.” Waliposikia hivyo Swahaba wa Rasuli wa Allaah walijifunika nyuso zao wakalia mpaka sauti za vilio vyao vikasikika. Kisha mtu mmoja hapo akamuuliza: Nani baba yangu? Akamjibu: “Fulani.” Hapo ikateremka Aayah hii: “Enyi walioamini! Msiulizie mambo ambayo mkifichuliwa yatakuchukizeni…” (5:  101) [Al-Bukhaariy].  

 

Sababun-Nuzuwl: Pia Anas (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Siku moja walianza kumuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) maswali mengi mpaka akaghadhibika akapanda minbar akasema: “Hamtaniuliza lolote leo ila nitawajibu tu.” Nikatazama kuliani na kushotoni nikaona kila mtu amejifunika uso wake kwa nguo akilia. Hapo alikuweko mtu mmoja ambaye kila alipogombana na wenziwe aliitwa ‘mwana wa fulani asiyekuwa ni baba yake’. Akamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah, nani baba yangu? Akasema: “Hudhaafah.” Hapo ‘Umar akainuka akasema: Tumeridhika na Allaah kuwa ni Rabb, na Uislamu kuwa Dini, na Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa ni Rasuli. Tunajikinga kwa Allaah na fitnah! Hapo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Sijapatapo kuona khayr au shari kama siku ya leo, kwani imedhihirishwa mbele yangu Jannah na moto hadi kwamba nimeviona viwili hivi nyuma ya ukuta.”  Qataadah alipokuwa akihadithia Hadiyth hii alikuwa akitaja Aayah hii: “Enyi walioamini! Msiulizie mambo ambayo mkifichuliwa yatakuchukizeni…” (5: 101) [Al-Bukhaariy].

 

 

 

 

Share