090-Aayah Na Mafunzo: Wamelaaniwa Watu Kumi Wanaouhusika Na Pombe

Aayah Na Mafunzo

Al-Maaidah

Wamelaaniwa Watu Kumi Wanaouhusika Na Pombe

Na Sababu Ya Kuteremshwa Aayah

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾

90. Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; ni najisi na chukizo kutokana na kitendo cha shaytwaan; basi jiepusheni navyo, mpate kufaulu.

 

Mafunzo:

 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amelaani aina ya watu kumi wanaohusika na pombe amesema: “Mwenye kugema pombe, mwenye kutaka afanyiwe, mwenye kunywa, na mwenye kubeba, mwenye kubebewa, mwenye kunywesha, mwenye kuuza, mwenye kula thamani yake, mwenye kununua, na mwenye kununuliwa.” [At-Tirmidhiy na Ibn Maajah].

 

Sababun-Nuzuwl: Aayah hii na inayofuatia (5: 90-91-) zimeteremshwa kuwa ni haramisho la mwisho kunywa pombe. Rejea tanbihiaat za (2: 219), (4: 43) ambako kuna maelezo bayana ya Sababun-Nuzuwl ya Aayah hizi. Baada ya kuteremshwa Aayah hizi, hapo hapo Swahaba wakaacha moja kwa moja kulewa ikawa ndio kikomo cha kunywa pombe.

 

Sababun-Nuzuwl:

Pia, Imeteremshwa kuhusu makabila mawili katika Answaar walipokunywa pombe mpaka wakalewa mno kisha wakagombana na kuchafuana baadhi yao kwa baadhi mpaka athari zikawa zinaonekana katika nyuso zao. Kisha pale ulevi ulipowaondokea na akili zao zikawarejea, viliingia vinyongo katika nyoyo zao, hapo zikateremka Aayah hizi zinazoharamisha pombe moja kwa moja: Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; ni najisi na chukizo kutokana na kitendo cha shaytwaan; basi jiepusheni navyo, mpate kufaulu. Hakika shaytwaan anataka kukutilieni baina yenu uadui na bughudha katika pombe na kamari na akuzuieni kumdhukuru Allaah na Swalaah; basi je mtakoma?” (5: 90 - 91). [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) – amepokea Ibn Jariyr].

 

Share