Kutumia Neno La Sayyid Kumwita Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Au Swahaba

 

 

 

SWALI:

Assalam aleikum warahmatullah, wabaad. swali langu ni kuhusu kulitumia hili neno SAYYID wakati tunapomuita Mtume s.a.w au maswahaba zake r.a.a je inafaa?

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani sana kwa muulizaji lake hili kuhusu haya mas-ala ya kumuita Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Swahaba au mtu mwingine yeyote kwa jina la SAYYID.

 

Kabla ya kuja kuhitimisha kauli yetu inafaa sisi tufahamu maana ya neno hilo. Neno hilo lina maana ya Mtukufu au Bwana katika lugha. Hata katika matumizi inatumika Sayyid al-Bayt (yaani bwana au mkubwa wa nyumba).

 

Hakika Allaah Aliyetukuka Amelitumia neno hili kwa Nabii Wake Yahyaa (‘Alayhis Salaam), pale Aliposema: “Alipokuwa kasimama chumbani akiswali, Malaika kamnadia: Hakika Allaah Anakubashiria Yahyaa, atayekuwa mwenye kusadikisha neno litokalo kwa Allaah, na ni Sayyid (bwana) na mtawa na Nabii kwa watu wema” ().

 

Pia kuhusu waziri wa Misri, “Na wote wawili wakakimbilia mlangoni, na mwanamke akairarua kanzu yake Yuusuf kwa nyuma. Na wakamkuta Sayyid (bwana) wake mlangoni. Mwanamke akasema: Hapana malipo ya mwenye kutaka kumfanyia maovu mkeo isipokuwa kufungwa au kupewa adhabu iumizayo” ().

Na katika Hadiyth neno hili limetumika mara nyingi sana kwa mfano,

ألا كلكم راع وكلكم مسؤول عن رعيته ، فالإمام الذي على الناس راع وهو مسؤول عن رعيته ، والرجل راع على أهل بيته وهو مسؤول عن رعيته ، والمرأة راعية على أهل بيت زوجها وولده وهي مسؤولة عنهم ، وعبد الرجل راع على مال سيده وهو مسؤول عنه ، ألا فكلكم راع وكلكم مسؤول عن رعيته

Hii Hadiyth inaonyesha kila mmoja wetu ana mas-uliya (majukumu) yake na ataulizwa kuhusu alichokichunga. Ibara tuliyoipiga msitari ina maana: “Na mtumwa wa mtu ni mchunga wa mali ya bwanake, naye ana jukumu kwayo” (al-Bukhaariy).

 

Hadiyth nyingine inasema: “Alikuja mtu anayeitwa Thumaamah bin Athal naye alikuwa ni Sayyid wa watu wa Yamaamah” (al-Bukhaariy).

 

Na nyingine: “Akasimama Sa‘d bin ‘Ubadah, naye alikuwa Sayyid (Chifu) wa Khazraj” (al-Bukhaariy).

 

Hadiyth kuhusu neno hili ni nyingi sana lakini kufupisha katika Hadiyth iliyo sahihi, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Mimi ni Sayyid (bwana na mtukufu) katika watoto wa Aadam Siku ya Qiyaama” (Muslim).

 

Pia, “Mimi Sayyid wa watu Siku ya Qiyaama, na mnajua ni nini hiyo” (al-Bukhaariy).

 

Pia, “Alikuja Hasan kwake, naye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, ‘Mtoto wangu huyu ni Sayyid, huenda Allaah kwake akasuluhisha baina makundi mawili ya Waislamu” (al-Bukhaariy). Na ndivyo ilivyokuwa, maana Hasan aliweka suluhu na Mu’aawiyah na hivyo kuokoa umwagikaji mkubwa wa damu ambao ungesababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

 

Na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) wakati wa ukhalifa wake alisema: “Abu Bakar ni Sayyid wetu na alimuacha huru Sayyid wetu (yaani Bilaal bin Rabaah)”. (al-Bukhaariy kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillahi [Radhiya Allaahu ‘anhuma]).

 

Hivyo, kumuita Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Swahaba kwa jina hili kama cheo chake cha daraja halina neno katika sharia, ila haifai kumuita hivyo ndani ya Swalah kwenye Tashahhud au kwenye Adhaan au Iqaamah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share