Maana Ya Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

Maana Ya Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalaam Aleykum Warhmatullah Wabarakat, Sifa zote kwa ALLAH muenezi wa kila jambo hapa duniani na huko mbinguni. 

Sasa ndugu zangu katika imani mimi nimepata kusilimu na kusilimu kwangu kumenifanya taratibu taratibu naelewa zaidi na kupata nur ya Allah muweza yote.

Sasa Swali langu tena hili sio swali bali ni kama fursa kwangu ya kuzidi kuuelewa uislam kama kitajaliwa kupata majibu (In shaa Allah)

SWALI:- Je waislam tunamswalia nani??? yani swala zetu ni kwa ajili ya Allah au Mtume Wetu Mohammad Swallallahu Alaihi Wasalam?? maana uwa nasikia inasemwa tumswalie mtume sasa kwangu umekuwa mtihani kidogo wa kupambanua maana ya neno hilo. Mwenyezi Mungu atie wepesi najibiwe Inshallah.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kujua umesilimu hakika hiyo ni neema Aliyokujaalia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na ni dalili ya mapenzi Yake Kwako kukujaalia Uongofu wa haki. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aendelee kukuthibitisha katika Dini hii tukufu na upate mafanikio Aakhirah ambako ndiko mwenye maisha ya milele.

 

Ama kuhusu ilivyokusudiwa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haimaainishi kuwa tunamswalia yeye kama vile tunavyoswali kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwenye Swalaah zetu kwa kusimama na kurukuu na kusujudu na kuomba na kadhalika. Bali inapotajwa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inakusudiwa kumuombea du’aa za Rahmah na amani zimshukie .

 

Tambua ndugu yetu kwamba lugha ya Kiarabu ni pana mno, kwa mfano maana ya neno moja linaweza kuwa na maana nyingi kabisa. Ukitaka kujua maana ya neno la Kiarabu kwanza ujue maana yake ya kilugha, kisha ujue maana yake ki-Shariy’ah (katika Dini ya Kiislamu) ambao huwa inatofautiana na maana ya asili.  Na katika maana ya Swalaah kilugha inamaanisha ni du’aa. Ama katika Shariy’ah inaamanisha ni ‘ibaadah (kumwabudu Allaah) 

 

Chukulia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾

Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa.  [Al-Ahzaab 33: 56]

 

Ni kwamba: Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) maana yake ni kumsifia kwa Malaika, kumteremshia rahmah na baraka, fadhila n.k.

Ama Malaika Wake kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kumuombea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  du’aa Amghufurie na Amteremshie baraka.  

 

Na ndio sisi Waumini tumeamrishwa pia kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Aayah hiyo na maana yake ni hiyo ya kumuombea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) du’aa ya rahmah na amani.

 

Na alipoulizwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) jinsi gani kumswalia alijibu kuwa ni kumswalia kama vile tunavyomswalia ndani ya Swalaah katika kikao cha Tashahhud pale kwenye du’aa inayoitwa Swalaatu Ibraahimiyyah (Swalaah ya Ibrahiym) ambayo imekuja katika matamshi  mbali mbali yanayotofautiana kidogo; mojawapo ni kama ifuatavyo:

 

Allaahumma Swalli ‘alaa Muhammadin, wa ‘alaa aali Muhammadin, kamaa Swallayta ‘alaa  Ibraahiyma, wa ‘alaa  aali Ibraahiyma, Innaka Hamiydun Majiydun, Allaahumma Baarik ‘alaa Muhammadin  wa ‘alaa aali Muhammadin  kamaa Baarakta ‘alaa  Ibraahiyma wa ‘alaa  aali Ibraahiyma  Innaka Hamiydun Majiydun

 

Ee Allaah! Mswalie Muhammad, na ahli wa  Muhammad  kama Ulivyomswalia Ibraahiym na juu ya ahli zake Ibraahiym, hakika Wewe ni Mwenye kustahiki kuhimidiwa, Mwenye utukufu. Eee Allaah! Mbariki Muhammad na jamaa zake Muhammad kama Ulivyombariki  Ibraahiym na juu ya ahli zake Ibraahiym, hakika Wewe Ni Mwenye kustahiki kuhimidiwa, Mtukufu.

 

Tunatumai kuwa utafahamu swali lako na tunakunasihi sana ujifunze lugha ya Kiarabu  kwani ndio ufunguo wa elimu zote za Dini tukufu.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share