Al-Lajnah Ad-Daaimah: Nadharia Batili Ya Kidarwini (Darwnism) Kuwa Mwana Aadam Katokana Na Nyani

Nadharia Batili Ya Kidarwini (Darwnism)

Kuwa Mwana Aadam Katokana Na Nyani

 

Al-Lajnah Ad-Daaimah

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Tumesoma kitu kuhusu nadharia ya Mageuzi na yote yanayohusiana na uumbaji wa mada hii ni sehemu ya mtaala wa elimu yetu. Namna ninavyoendelea kusoma somo hili, ndivyo ninavyozidi kushawishika kwamba Allaah Peke Yake Ndiye Aliyeumba ulimwengu huu na kila kilichomo ndani yake.

 

Hata hivyo, nimesikitishwa mno kukutana na kitabu kilichoandikwa na mwandishi Muislamu kuithibitisha nadharia ya Mageuzi na kuikubali kwa kuitumia Qur-aan! Zaidi ya hivyo, mmoja miongoni mwa walimu wangu Waislamu aliniuliza: “Kwa vile Uislamu unakataza mwanamme kumuoa dada yake; ni kwanini wakaoana ndugu wa kiume na wa kike miongoni mwa kizazi cha Aadam na Hawaa?”

 

 

JIBU:

 

Nadharia ya Mageuzi ambayo ni maarufu kwa jina la nadharia ya Darwin inakinzana na Qur-aan, Sunnah (simulizi yoyote inayosimuliwa kutoka kwa Rasuli), na Ijmaa’ (makubaliano ya Wanachuoni).

 

Kwa hivyo, kuna ushahidi mwingi kutoka Qur-aan na Sunnah sahihi zinazoeleza kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amemuumba Aadam kutokana na udongo kisha Akamuumba Hawaa kutokana na Aadam.

 

Kwa mnasaba wa kwamba Aadam (‘Alayhis-Salaam) amewaozesha watoto wake wa kiume kwa mabanaat zake, hili ni jambo ambalo ni amri ya Allaah ndiyo iliyomshurutisha yeye kufuata hivyo, ambayo hatuna haki ya kulijadili hilo.

 

Hata hivyo, kwa mujibu wa Shariy’ah (Sheria ya Kiislamu) ambayo imeshushwa kwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); Allaah Ameharamisha (Amekataza) kwa mwanamme kumuoa dada yake pamoja na matabaka mengine maarufu ya wanawake ambayo mwanamme haruhusiwi kuoa.

 

Kwa upande mwengine, kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amesema: “Kwa kila (ummah) katika nyinyi Tumeujaalia shariy’ah na manhaj.” [Al-Maaidah: 48], na wakati huo huo Ametaja Shariy’ah za Tawraat, Injiyl na Qur-aan, namna hivyo ndivyo inavyofanya kazi kwa Aadam (‘Alayhis-Salaam); ni kusema kwamba alikuwa na Shariy’ah yake makhsusi ya kuifuata.

 

Allaah Atujaalie mafanikio! Rahmah na amani ziwe juu ya Nabiy wetu Muhammad, watu wake na Maswahaba zake!

 

 

Kamati Ya Kudumu Ya Utafiti wa Kielimu Na Utoaji Fatwa

 

`Abdul-`Aziyz bin `Abdullaah bin Baaz – Mwenyekiti

`Abdur-Razzaaq `Afifiy – Naibu Mwenyekiti

`Abdullaah bin Qa`uwd – Mjumbe

`Abdullaah bin Ghudayyaan – Mjumbe

 

[Kamati Ya Kudumu Ya Fatwa, Fungu la 2, Sura Ya 1: ‘Aqiydah, Tawhid Ar-Rubuwbiyyah, Mageuzi, Nadharia ya Kidarwini, Suala La Kwanza Kwa Fatwa namba 2872]

 

 

Share