Imaam Ibn Baaz: Maana ya Hadiyth "Allaah Amemuumba Aadam Kwa Sura Yake"

 

Maana ya Hadiyth: "Allaah Amemuumba Aadam Kwa Sura Yake"

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

Kuna Hadiyth imesimuliwa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayozuia kuiumbua sura, na kueleza kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amemuumba Aadam kwa Sura Yake. Je, kuhusu Hadiyth hii ni iymaan gani ipo sahihi?

 

 

JIBU:

 

Hadiyth hii imesimuliwa kwa uthibitisho kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambapo alisema:

“Yeyote anapompiga (mtu mwengine), basi na aepuke uso, kwani Allaah Amemuumba Aadam kwa Sura Yake.”

 

Katika simulizi nyingine:

 

“Katika Sura ya Ar-Rahmaan (Mwenye Kuneemesha).”

 

Hii haina maana ya Tashbiyh (kulinganisha) au Tamthiyl (kufananisha Sifa za Allaah kwa zile za viumbe Vyake).

 

Kwa mujibu wa maoni ya Wanachuoni, hii ina maana kwamba Allaah (Mtukufu) Amemuumba Aadam ni mwenye kusikia, kuona na kuzungumza kama Anavyopenda (Allaah).

 

Hizi pia ni Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), kwani Yeye mara zote ni Mwenye Kusikia, Mwenye Kuona, Kuzungumza na Ana Uso (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Hata hivyo, hii haina maana ya Tashbiyh au Tamthiyl, kwani Sura ya Allaah ni tofauti kabisa kabisa na sura ya kiumbe chochote. Isipokuwa, ina maana kwamba Yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) ni Msikivu, Mwonaji, Ana Uso na Msemaji Anapotaka. Vivyo hivyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amemuumba Aadam kwa sura hiyo hiyo; akiwa ni mwenye kusikia, macho, uso, mikono na miguu na mzungumzaji anapotaka kuzungumza.

 

Lakini bado usikivu wake si sawa na wa Allaah na hivyo hivyo kwa uoni na uzungumzaji wake.

 

Uso wake mwana Aadam haufanani kabisa kabisa na Uso wa Allaah kwani hakuna kinachofanana na Sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Badala yake ni kwamba zipo Sifa ambazo ni maalum kwake Yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) peke Yake.

 

Halikadhalika, waja wa Allaah wana sifa zinazowahusu wao peke yao. Sifa hizo zimo katika kutoweka, kasoro na udhaifu. Hata hivyo, Sifa za Allaah ni Kamilifu zisizo na kasoro yoyote, udhaifu wowote au kutoweka kwa namna yoyote.

 

Kwa maana hiyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١١﴾

 

{Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote}. [Ash-Shuwraa: 11]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

لَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ ﴿٤﴾

 

{Na wala haiwi Awe na yeyote anayefanana na kulingana Naye}. [Al-Ikhlaasw: 4]

 

Kwa maana hiyo, hairuhusiki kuupiga uso au kuumbua uso.

 

 

[Fataawaa Nuwr ‘Alaa Ad-Darb, Sura ya 1, Juzuu kuhusu ‘Aqiydah, Juzuu kuhusu Majina ya Allaah na Sifa Zake, Maana ya Hadiyth: “Allaah Amemuumba Aadam kwa Sura Yake.”]

 

 

 

Share