Ushauri Muhimu Kwa Mahujaji

 

Ushauri Muhimu Kwa Hujaji

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

((الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلاَ رَفَثَ وَلاَ فُسُوقَ وَلاَ جِدَالَ فِي الْحَجِّ وَمَا تَفْعَلُواْ مِنْ خَيْرٍ يَعْلَمْهُ اللّهُ وَتَزَوَّدُواْ فَإِنَّ خَيْرَ الزَّادِ التَّقْوَى وَاتَّقُونِ يَا أُوْلِي الأَلْبَاب))  

((Hijjah ni miezi maalum. Na anayekusudia kufanya Hijjah katika (miezi) hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika hiyo Hijjah. Na kheri yoyote mnayoifanya, Allaah Huijua.  Na chukueni masurufu (ya kutumia njiani, msiombe). Na hakika masurufu bora ni yale yanayomfanya mtu asiombe (kwa kuwa yanamtosha).  Na nicheni Mimi, enyi wenye akili.)) [Al Baqarah: 197]

 

Kumtambua Allaah

 

Njia bora ya kumridhisha Allaah ni kuwa na msimamo wa makini juu Yake, kumtambua pamoja na kumuogopa Yeye katika matendo na mazungumzo yako yote.

 

Kuwa na 'Aqiydah Sahihi

 

Kila Muislaam ni lazima aelewe ya kwamba ikiwa imani au 'Aqidah yake sio madhubuti, Hijjah au 'Ibaadah yake yoyote huwa haikubaliwi. Kwa hivyo daima jaribu kurekebisha imani yako kwa kuuliza Maulamaa ambao wataweza kukupa ushahidi kutoka kwenye Qur-aan na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Niyyah Iliyotakasika

 

Allaah Mtukufu Halikubali jambo lolote ambalo halikuelekezwa Kwake Yeye Pekee. Kwa hivyo, ni lazima uwe na moyo mkunjufu na niyyah iliyotakasika kwa ajili ya kutekeleza Hijjah.

 

Uhakika wa Vitendo vya 'Ibaadah

 

Tendo lolote halikubaliwi isipokuwa liwe limetendwa sawasawa, kama vile ambavyo limefanywa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ameonya:   

( من أحدث في أمرنا هذا ما ليس منه فهو رد) متفق عليه.

((Atakayezusha katika jambo yasiyokuwa (katika Dini) yetu basi litarudishwa)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Uvumilivu

 

Ugumu wa utekelezaji 'Ibaadah ya Hijjah unahitaji kila hujaji kuwa mvumilivu na kuwasamehe wenzake.

 

Kutubia

 

Fanya jitihada kwa kadiri ya uwezo wako ili Hijjah yako iwe ni toba ya madhambi yako yote.  Toba hii inahitaji kudumishwa ili usije ukarudia tena kutenda madhambi.

 

Huruma

 

Fanya jitihada ya kuwasaidia Waislamu, jiepushe na kuwasukuma au kuwaumiza wakati wa kutekeleza Hijjah, hususan wakati kufanya Twawaaf, Sa'y, kurembea vijiwe, ambapo huwa kuna misongamano mikubwa.

 

Usafi

 

Usafi ni alama ya kweli ya imani. Kwa hivyo, huna budi kuusafisha moyo wako, kiwiliwili chako, chakula chako, kinywaji chako na kila kitu.  Vile vile wahimize watu wengine kuyafanya matendo na pahala pa 'Ibaadah kuwa safi kwa kadiri ya uwezo wao.

 

Fedha

 

Usijali kuhusu ubadishaji wa fedha.  Unaweza kubadilisha kwa wepesi pahali popote katika miji ya Saudi Arabia.

 

Vikundi Vidogo Vidogo

 

Uchunguzi wa karibu unaonyesha kuwa watu wanaotembea kwenye makundi makubwa huwa ni rahisi mmoja kati yao au mwengine kupotea, na hii hupelekea kupoteza au kuchelewa kutenda baadhi ya matendo ya Hijjah ambapo Hujaji hutakiwa baadae afanye fidia aidha kwa kuchinja mnyama, kufunga au kufanya jambo jengine.

 

Fuatana na Watu Wazuri

 

Hakikisha unachagua watu wazuri wa kufuatana nao katika nyendo zako zote, hii ni kwa sababu wataweza kukusaidia kuepukana na mizozo na vile vile watakusaidia katika kuitekeleza Hijjah yako kwa uhakika

 

Jiepushe na Kupotea

 

Inashauriwa kupanga kwa vizuri na watu unaofuatana nao wapi na ni wakati gani mkutane na kitu gani cha kufanya pindi mmoja wenu akichelewa kufika au kupotea.  Hatua zifuatazo huenda zikasaidia:

 

- Panga kukutana pahala pa uwazi, penye alama enye rangi au alama za mji.

- Ainisha muda maalumu wa kukutana kwa wale watakaochelewa kutokana na sababu fulani, ukizingatia ya kwamba muda huo hautoathiri vitendo vya Hijjah vinavyofuata.

- Hakikisha kwamba kila mtu katika kikundi chenu ameelezewa na kufahamu sawasawa.

 

Chakula

 

Usichukue chakula kutoka nchi yako: karibia kila kitu kinapatikana huko.  Vile vile kumbuka kwamba pindi ukichukua chakula huenda ukanyang’anywa kwenye uwanja wa ndege.

Fuata maelekezo yafuatayo ili uwe na mpangilio mzuri ya kula.

- Jiepushe na kula chakula kingi, hii ni kwa sababu si katika kujijengea afya njema na pia haisaidii katika kutekeleza vitendo vya Hijjah.

- Vyakula bora vya kuliwa ni matunda, na vinywaji bora ni maji na juisi (juice).  Hivi vipo kila pahala na vinauzwa (bei) rahisi.

- Tia chakula kinachobakia (makombo) kwenye mfuko wa plastiki na kisha weka kwenye mapipa ya taka.

 

Matibabu

Chukua dawa zile ambazo tu ni muhimu kwa afya yako.  Dawa nyengine ambazo ni maarufu hupatikana katika maduka yoyote ya kuuzia madawa.  Unaweza kupata huduma ya kwanza (first aid) kwenye sehemu zote za 'Ibaadah.

 

Hifadhi

 

Jihadhari na sehemu zenye joto kali katika sehemu za 'Ibaadah. Jiepushe kupigwa na jua kwa muda mrefu.  Chukua mwamvuli na vinywaji vya kutosha.

 

Huduma kwa wasiojiweza

 

Huduma maalumu zinapatikana kwa waliodhaifu, wagonjwa, wasiojiweza, na wazee.  Viti na vitanda vya kubebea vinakodishwa kwa wale wanaohitajia.  Uliza wasimamizi wa huduma hizi ndani ya Msikiti.  Wakati mwengine huduma hii hupatikana bure, lakini kwa kawaida hupatikana kwa bei rahisi.  Faidika na huduma hizi pindi ukizihitajia.

 

 

Share