005-Swahiyh Twibbin-Nabawiy: Maradhi Ya Kiwiliwili Yanayoshambulia Mwili

Swahiyh Twibbin-Nabawiy

 

005-Maradhi Ya Kiwiliwili Yanayoshambulia Mwili

 

 

 

 

Ama maradhi ya viwiliwili Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

لَّيْسَ عَلَى الْأَعْمَىٰ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ  

Si vibaya kwa kipofu, na wala si vibaya kwa kilema, na wala si vibaya kwa mgonjwa,   [An-Nuwr: 61]

 

 

Na yametajwa maradhi ya mwili katika Hijjah, Swawm na udhu. Kwa siri kubwa ya ajabu, inayoweza kukubainishia utukufu wa Qur-aan vilivyo akatosheka na Qur-an tu. Nayo: Kwamba msingi ya tiba ya viwiliwili ni tatu:

 

 

1-Kuhifadhi siha

2-Kujilinda na madhara

3-Kutakasa na kuondosha maada mbovu na zenye madhara mwilini.

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema kuhusu misingi hii mitatu katika sehemu tatu tofauti:

 

  فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۚ  

Lakini atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini, basi (inapaswa kulipa) idadi sawa katika masiku mengineyo. [Al-Baqarah 2: 184].

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akahalalisha kufuturu kwa mgonjwa, kwa udhuru wa maradhi na kadhalika msafiri anayo ruhusa kula ili kuhifadhi afya yake na nguvu isije ikaondoshwa nguvu hiyo kwenye safari, kwa kukutana na mazonge ya harakati, ambazo hupelekea kuyayuka kwa chakula wakati hakuna chakula cha badala ya kinachoyeyushwa tumboni ikiwa yuko katika Swawm. Matokeo yake nguvu hutoweka, na kudhoofu, kwa ajili hiyo msafiri ni halali kwake kufuturu. Kwa kuhifadhi afya yake na nguvu yake na kuepuka kinachodhoofisha afya.

 

Na katika Hajj Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ بِهِ أَذًى مِّن رَّأْسِهِ فَفِدْيَةٌ مِّن صِيَامٍ أَوْ صَدَقَةٍ أَوْ نُسُكٍ ۚ

Na atakayekuwa miongoni mwenu mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake (ikambidi anyoe); basi atoe fidia kwa kufunga Swiyaam au kutoa swadaqah au kuchinja mnyama. [Al-Baqarah: 196]

 

Akamhalalishia mgonjwa na mwenye udhia kichwani, kama chawa, au muwasho au mengineyo, huyo anayo ruhusa ya kunyoa nywele zake katika Ihraam ili kuondosha maada za mvuke mbaya ambao umemletea udhia ule kichwani chini ya nywele, basi atakaponyoa nywele zake, hufunguka tundu za ngozi, mvuke ule hutoweka, uondoshaji huu wa udhia hupimiwa kwa hali zote zenye kuleta udhia kwa kufungika tundu za mwili.

 

 

Kuna vitu kumi ambavyo huleta udhia kwa kufungika na kuleta nguvu kinzani: Damu inapopanda, manii yakizidi, mkojo, haja kubwa, upepo, matapishi, chafya, usingizi, njaa, na kiu.

 

 

Kila moja katika hayo kumi huleta maradhi endapo litazuiliwa na kuleta ugonjwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akazindusha kwa kuondosha udhia mdogo ulio chini ya hayo yote, ambao ni mvuke uliopenya kichwani, kwa kuondosha udhia mgumu kuliko huo, kama ilivyo njia ya Qur-aan; Kuzindua jambo la juu kupitia la chini kwa daraja. Ama kuhami nafsi na madhara Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

  وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا  

Na mkiwa wagonjwa au safarini au mmoja wenu ametoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi mtayammam (ikusudieni) ardhi safi ya mchanga. [An-Nisaa: 43]

 

 

Akamhalalishia mgonjwa kutumia udongo badala ya maji kwa ghera ya maslahi yake, kwamba isiwe mwili wake umesibu kinachoweza kudhuru, hii pia ni tanbihi ya ghera dhidi ya kila chenye kumdhuru kwa ndani na nje ya mwili. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amewaelekeza waja Wake katika misingi ya tiba. Nasi tunataja mwongozo wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika hilo, na tunabainisha kuwa mwongozo wake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni mkamilifu mno.

 

Ama tiba ya nyoyo. Wamepewa Rusuli (‘Alayhim salaam) na hakuna njia ya kupata ila kutoka kwao[1], kwani uzima wa nyoyo, kutengenea kwa nyoyo ni pale nyoyo hizo zinapomjua Rabb wake, na Majina Yake na Sifa Zake, matendo Yake, na hukumu Zake na ziwe zinamridhisha katika kumpenda na kufanya yanayomridhisha. Na pia ziepuke makatazo na machukizo yake. Wala hapana siha kwa nyoyo bali hakuna maisha kamwe bila ya kufanya hivyo. Na hakuna namna ya kupata siha hiyo isipokuwa kupitia Rusuli (‘Alayhim salaam). Na ile dhana iliyopo kuwa yawezekana kupata siha ya nyoyo bila ya kuwafuata hao, basi wanaodhani hivyo wanakosea. Hayo ni maisha ya nafsi ya kihayawani yenye tabia ya kimatamanio, nguvu na afya ya nyoyo hizo ni mbali mbali na afya za kimwana Aadam kimoyo. Na mtu asiyetofautisha kati ya nyoyo hizi na zile, huyo ndie wa kusikitikia uhai wa moyo wake. Kwani huyo yumo miongoni mwa watu wafu, na kwa nuru yake kwani yumo kwenye mkondo wa bahari yenye giza.

 

 

 

 

 

 

[1] Kwa hakika kumwamini Allaah, Rusuli Wake, na ‘Aqiydah  iliyotua ni miongoni mwa tiba ya hali za wenye maradhi ya nyoyo, yaani maradhi ya nafsi.

Share