Kushika Msahafu Kusoma Suwrah Katika Swalah

 SWALI:

 

 Ni: ukiwa una taka kuswali na hujui sura fulani kwa moyo, je inafaa kueka msahafu mbele yako unaposwali ili uisome kwa kuangalia? Nitashkuru sana kwa jawabu yenu kwani huenda nikawa sipati kitu kwa kuswali makosa. Mungu atawabarik na kuwazidishia nyoyo za iman. (Amin)

Asalam aleykum.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mas-alah haya ni kuwa haifai kushika Msahafu na kusoma katika Swalah za faradhi. Hii ni kuwa yule anayefaa kuswalisha ni yule mwenye ilimu na kuielewa pamoja na kuisoma Qur-aan barabara.

 

Swalah ya faradhi inatakiwa iswaliwe katika jamaa'ah hivyo kunakuwa na Imaam mjuzi. Hata ikiwa unaswali peke yako Swalah ya faradhi unahitajika kusoma kile ulichohifadhi, hivyo tunatakiwa kujiwekea umuhimu kati yetu katika mas-alah ya kuhifadhi.

 

Katika Swalah ya Sunnah wamekhitilafiana Wanachuoni kufaa na kutofaa kwake. Wanaoona inafaa wametegemea kuswalisha mtumishi wa mama 'Aaishah aitwaye Dhakwaan aliyekuwa akiswalisha nyumbani kwa kushika Msahafu. 

 

Wanaopinga wanaona kuwa mtu asome alichohifadhi na kushika Msahafu katika Swalah kunaharibu Sunnah mbalimbali za Swalah kama kufunga mkono katika Swalah na vilevile kushughulishwa mtu kutazama Msahafu na pia kufungua kurasa zake na hata kutomwezesha mtu kutoweka mikono vizuri wakati wa kurukuu na kusujudu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share