11-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Wa Swalaah Ya Msafiri Na Mgonjwa

 

بُلُوغُ الْمَرام

 

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلصَّلَاةِ

 

Kitabu Cha Swalaah

 

بَابُ صَلَاةِ اَلْمُسَافِرِ وَالْمَرِيضِ

 

11-Mlango Wa Swalaah Ya Msafiri Na Mgonjwa

 

 

 

 

 

341.

عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {أَوَّلُ مَا فُرِضَتْ اَلصَّلَاةُ رَكْعَتَيْنِ ،  فَأُقِرَّتْ صَلَاةُ اَلسَّفَرِ وَأُتِمَّتْ صَلَاةُ اَلْحَضَرِ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْه

وَلِلْبُخَارِيِّ: {ثُمَّ هَاجَرَ،  فَفُرِضَتْ أَرْبَعًا،  وَأُقِرَّتْ صَلَاةُ اَلسَّفَرِ عَلَى اَلْأَوَّلِ} 

زَادَ أَحْمَدُ: {إِلَّا اَلْمَغْرِبَ فَإِنَّهَا وِتْرُ اَلنَّهَارِ،  وَإِلَّا اَلصُّبْحَ،  فَإِنَّهَا تَطُولُ فِيهَا اَلْقِرَاءَةُ } 

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Mwanzo kufaradhishwa Swalaah ni Rakaa mbili[1], baadaye zikabakishwa (Hizo Rakaa mbili) kuwa Swalaah ya safari. Na Swalaah ya mkazi ikatimizwa (kwa kuongezwa Rakaa mbili nyingine).” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na katika mapokezi ya Al-Bukhaariy: “Kisha (Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akahajiri kwa hiyo Rakaa zikafaradhishwa nne, na Swalaah ya safari ikaachwa juu ya hali yake ya mwanzo.”

 

Na Ahmad aliongezea: “Isipokuwa Swalaah ya Magharibi kwani hiyo ni (Swalaah ya) Witr ya mchana, na isipokuwa Swalaah ya Alfajiri kwani hurefushwa ndani yake kisomo.”

 

 

 

 

342.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا، {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم  كَانَ يَقْصُرُ فِي اَلسَّفَرِ وَيُتِمُّ،  وَيَصُومُ وَيُفْطِرُ.}  رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ،  وَرُوَاتُهُ ثِقَاتٌ. إِلَّا أَنَّهُ مَعْلُول

وَالْمَحْفُوظُ عَنْ عَائِشَةَ مِنْ فِعْلِهَا،  وَقَالَتْ: {إِنَّهُ لَا يَشُقُّ عَلَيَّ}  أَخْرَجَهُ اَلْبَيْهَقِيّ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akifupisha Swalaah safarini, na pia alikuwa akitimiza (Rakaa)[2], na alikua akifunga Swawm na akifuturu.” [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniyy, na wapokezi wake ni waaminifu, isipokuwa ni Hadiyth yenye ila]

 

Na imehifadhiwa kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) na ndivyo alivyokuwa anafanya na amesema (‘Aaishah): “Hakika (kufanya) hivyo si mashaka kwangu.” [Imetolewa na Al-Bayhqayy[3]]

 

 

 

343.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { إِنَّ اَللَّهَ يُحِبُّ أَنْ تُؤْتَى رُخَصُهُ كَمَا يَكْرَهُ أَنْ تُؤْتَى مَعْصِيَتُهُ}  رَوَاهُ أَحْمَدُ،  وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ،  وَابْنُ حِبَّانَ .

وَفِي رِوَايَةٍ: {كَمَا يُحِبُّ أَنْ تُؤْتَى عَزَائِمُهُ}

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakika Allaah Anapenda rukhusa Zake zitumiwe, kama Anavyochukia kufanywa maasi Yake[4].” [Imetolewa na Ahmad, na akaisahihisha Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan]

Katika mapokezi mengine: “Kama Anavyopenda utekelezwe wajibu Wake.”

 

 

 

344.

وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  إِذَا خَرَجَ مَسِيرَةَ ثَلَاثَةِ أَمْيَالٍ أَوْ فَرَاسِخَ،  صَلَّى رَكْعَتَيْنِ}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Pindi Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipokuwa akisafiri safari ya maili tatu[5] au faraasikh[6] tatu, anaswali Rakaa mbili.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

345.

وَعَنْهُ قَالَ: {خَرَجْنَا مَعَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  مِنْ اَلْمَدِينَةِ إِلَى مَكَّةَ، فَكَانَ يُصَلِّي رَكْعَتَيْنِ رَكْعَتَيْنِ حَتَّى رَجَعْنَا إِلَى اَلْمَدِينَةِ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ،  وَاللَّفْظُ لِلْبُخَارِيِّ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) tena amesema: “Tulitoka pamoja na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) toka Madiynah kwenda Makkah, akawa anaswali Rakaa mbili mbili mpaka tuliporejea Madiynah.” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Al-Bukhaariy]

 

 

 

346.

 وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {أَقَامَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم تِسْعَةَ عَشَرَ يَقْصُرُ} وَفِي لَفْظٍ: {بِمَكَّةَ تِسْعَةَ عَشَرَ يَوْمًا} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيّ

وَفِي رِوَايَةٍ لِأَبِي دَاوُدَ: {سَبْعَ عَشْرَةَ}

وَفِي أُخْرَى: {خَمْسَ عَشْرَةَ}

وَلَهُ عَنْ عِمْرَانَ بْنِ حُصَيْنٍ: {ثَمَانِيَ عَشْرَةَ}

وَلَهُ عَنْ جَابِرٍ: {أَقَامَ بِتَبُوكَ عِشْرِينَ يَوْمًا يَقْصُرُ اَلصَّلَاةَ}  وَرُوَاتُهُ ثِقَاتٌ،  إِلَّا أَنَّهُ اُخْتُلِفَ فِي وَصْلِه

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikaa siku kumi na tisa (safarini ambapo alikuwa) akifupisha (Swalaah zake).” Katika tamshi lingine: “Alikaa siku kumi na tisa Makkah.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

Na katika Riwaayah ya Abuu Daawuwd: “…Siku kumi na saba...[7]

 

Na katika mapokezi mengine tena: “…Siku kumi na tano…”

 

Yeye (Abuu Daawuwd) tena amepokea kutokana na masimulizi ya ‘Imraan bin Huswayn (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ): “…Siku kumi na nane…”

 

(Abuu Daawuwd) tena amepokea Hadiyth ya Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ): “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikaa Tabuwk siku ishirini, akifupisha Swalaah.” [Wapokezi wake wanategemewa, isipokuwa wamekhitilafiana kuhusu muunganiko wake]

 

 

 

347.

وَعَنْ أَنَسٍ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  إِذَا اِرْتَحَلَ قَبْلَ أَنْ تَزِيغَ اَلشَّمْسُ أَخَّرَ اَلظُّهْرَ إِلَى وَقْتِ اَلْعَصْرِ،  ثُمَّ نَزَلَ فَجَمَعَ بَيْنَهُمَا،  فَإِنْ زَاغَتْ اَلشَّمْسُ قَبْلَ أَنْ يَرْتَحِلَ صَلَّى اَلظُّهْرَ،  ثُمَّ رَكِبَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

وَفِي رِوَايَةِ اَلْحَاكِمِ فِي "اَلْأَرْبَعِينَ" بِإِسْنَادِ اَلصَّحِيحِ: {صَلَّى اَلظُّهْرَ وَالْعَصْرَ،  ثُمَّ رَكِبَ}.

وَلِأَبِي نُعَيْمٍ فِي "مُسْتَخْرَجِ مُسْلِمٍ": {كَانَ إِذَا كَانَ فِي سَفَرٍ،  فَزَالَتْ اَلشَّمْسُ صَلَّى اَلظُّهْرَ وَالْعَصْرَ جَمِيعًا،  ثُمَّ اِرْتَحَلَ}  

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipokuwa safarini na akaendelea safari kabla jua halijapinduka, aliakhirisha Swalaah ya Adhuhuri hadi wakati wa Alasiri. Kisha alishuka na akaziunganisha Swalaah zote mbili. Jua likipinduka kabla hajaondoka anaswali Adhuhuri kisha anapanda mnyama wake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Katika mapokezi ya Al-Haakim iliyonukuliwa katika Al-Arba’iyn kwa Isnaad Swahiyh: “Aliswali Adhuhuri na Alasiri kisha akapanda mnyama wake na akaendelea na safari yake.”

 

Na Abuu Nu’aym (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alisimulia katika matoleo ya Muslim: “Akiwa safarini, kama jua limevuka, alikuwa akiswali Dhuhuri na Alasiri pamoja, kisha aliendelea na safari yake.”

 

 

 

348.

وَعَنْ مُعَاذٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ: {خَرَجْنَا مَعَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  فِي غَزْوَةِ تَبُوكَ، فَكَانَ يُصَلِّي اَلظُّهْرَ وَالْعَصْرَ جَمِيعًا،  وَالْمَغْرِبَ وَالْعِشَاءَ جَمِيعًا}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Mu’aadh (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Tuliondoka pamoja na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) katika vita vya Tabuwk akawa anaswali Adhuhuri na Alasiri pamoja[8], na Swalaah ya Magharibi na ‘Ishaa pamoja.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

349.

وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  : { لَا تَقْصُرُوا اَلصَّلَاةَ فِي أَقَلَّ مِنْ أَرْبَعَةِ بُرُدٍ; مِنْ مَكَّةَ إِلَى عُسْفَانَ}  رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ  وَالصَّحِيحُ أَنَّهُ مَوْقُوفٌ، كَذَا أَخْرَجَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ

Kutoka kwa Ibn ‘Abaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema:  Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Msifupishe Swalaah katika umbali usiozidi burud nne;[9] kutoka Makkah mpaka ‘Usfaan.” [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniyy kwa Isnaad dhaifu, lililo sahihi ni kuwa hiyo ni Mawquwf, kadhalika ameipokea Ibn Khuzaymah]

 

 

 

350.

وَعَنْ جَابِرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {خَيْرُ أُمَّتِي اَلَّذِينَ إِذَا أَسَاءُوا اِسْتَغْفَرُوا،  وَإِذَا سَافَرُوا قَصَرُوا وَأَفْطَرُوا}  أَخْرَجَهُ اَلطَّبَرَانِيُّ فِي "اَلْأَوْسَطِ" بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ.

وَهُوَ فِي مُرْسَلِ سَعِيدِ بْنِ اَلْمُسَيَّبِ عِنْدَ اَلْبَيْهَقِيِّ مُخْتَصَر

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Walio bora katika Ummah wangu ni wale ambao wakitenda dhambi huomba maghfirah kwa Allaah, na wakiwa safarini, wanafupisha Swalaah na kuacha kufunga Swawm.” [Imetolewa na Atw-Twabaraaniyy ameiandika katika Al-Aswatw kwa Isnaad dhaifu]

 

Al-Bayhaqiyy ameipokea kwa ufupi kuwa ni Mursal kutoka kwa Sa’iyd bin Al-Musayyib.

 

 

 

351.

 وَعَنْ عِمْرَانَ بْنِ حُصَيْنٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {كَانَتْ بِي بَوَاسِيرُ،  فَسَأَلْتُ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم عَنْ اَلصَّلَاةِ؟ فَقَالَ: "صَلِّ قَائِمًا،  فَإِنْ لَمْ تَسْتَطِعْ فَقَاعِدًا،  فَإِنْ لَمْ تَسْتَطِعْ فَعَلَى جَنْبٍ"} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ.

Kutoka kwa ‘Imraan bin Huswayn (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Nilikuwa na maradhi ya bawasiri, nikamuuliza Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) juu ya Swalaah. Akasema: “Swali kwa kusimama, na ukiwa huwezi hivyo swali kwa kukaa, na ukiwa huwezi hivyo, swali kwa kulalia ubavu.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

 

 

352.

 وَعَنْ جَابِرٍ قَالَ: {عَادَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم مَرِيضًا،  فَرَآهُ يُصَلِّي عَلَى وِسَادَةٍ،  فَرَمَى بِهَا،  وَقَالَ: "صَلِّ عَلَى اَلْأَرْضِ إِنْ اِسْتَطَعْتَ،  وَإِلَّا فَأَوْمِ إِيمَاءً،  وَاجْعَلْ سُجُودَكَ أَخْفَضَ مِنْ رُكُوعِكَ"} رَوَاهُ اَلْبَيْهَقِيُّ. وَصَحَّحَ أَبُو حَاتِمٍ وَقْفَهُ.

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alizuru mgonjwa, akamkuta anaswali juu ya mto (tandiko). Akalitupa na akamuambia: “Swalia juu ya ardhi ukiweza, laa sivyo swali kwa ishara[10], na zifanye Sijdah zako kuwa chini zaidi kuliko rukuu zako.” [Imetolewa na Al-Bayhaqiyy, na Abuu Haatim akaipa daraja Mawquwf]

 

 

 

353.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {رَأَيْتُ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم  يُصَلِّي مُتَرَبِّعًا}  رَوَاهُ النَّسَائِيُّ. وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Nilimuona Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) anaswali huku ameketi chini kwa kuikunja miguu yake.[11] [Imetolewa na An-Nasaaiy na akaisahihisha Al-Haakim]

 

 

 

 


[1] Hii inajulisha kwamba hapo mwanzoni, Swalaah ya fardhi ilikuwa inaswaliwa kwa Rakaa mbili tu (kama Swalaah ya safari). Baadaye urefu wa Swalaah za wakazi wa kudumu uliongezwa na urefu wa Swalaah ya safari ukabakia Rakaa mbili,   Haijathibitishwa na mlolongo wa wapokezi kwamba Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliswali Swalaah kamili wakati wa safari.

[2] Mlolongo wa wapokezi kuhusu Hadiyth hii ni pamoja na ‘Alaa bin Zuhayr ambaye juu ya kujulikana kwake kuwa haifai, anajulikana kuwa si mkweli. Imaam Ibn Taymiyyah anasema kuwa anayosingiziwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ni ‘Uongo’. Katika Swahiyh mbili kupitia kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) hakuswali kamwe zaidi ya Rakaa mbili alipokuwa safarini.

[3] Hadiyth hii haiwezi kutumika kama ushahidi kwa sababu katika mlolongo wa wapokezi yupo ‘Alaa bin Zuhayr ambaye si wa kutegemewa. Pia inaipinga Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) na iliripotiwa na Al-Bukhaariy na Muslim kwamba, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kamwe hakuswali Rakaa zaidi ya mbili ya Swalaah za Rakaa nne.

[4] Hadiyth hii inadhihirisha kuwa, ni bora zaidi kuswali Swalaah ya Rakaa mbili, na kuswali kamili ni kukosa kutumiza Sunnah.

[5] Kuna mashaka katika Hadiyth hii kama ilitajwa maili tatu au farsakh tatu. Hadiyth ya awali haikutaja hili, lakini ni mashaka ya msimuliaji wa mlolongo wa wapokeaji kama Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alitumia maneno: “Maili tatu” au “farsakh tatu”. Ni lazima tujue hilo ili tuweze “kuswali Swalaah ya Rakaa mbili.” Hakuna umbali uliotajwa katika Hadiyth yoyote, kama ile ruhusa ya kuchukua wudhuu kwa Tayammum (kutwawadha kwa mchanga) wakati mtu yumo safarini, umbali wakati wa safari umeachwa wazi sana kiasi kwamba imeruhusiwa kuswali Rakaa mbili wakati wa safari yoyote ile. Inaelekea Hadiyth hii inaonyesha kuwa “Safari ya maili tatu” ni safari khasa, lakini kwa kuwa Shu’ba anaitilia shaka, Wanazuoni wengine wameamua kuwa umbali uwe farsakh tatu (yaani maili tisa). Wanazuoni wengine wamependekea maili 36, wengine maili 48, na wengine maili 52. Rejea ya kuhusu maili 48 ni imara zaidi, kwa kuwa Ahnaf na Wanazuoni wa Hadiyth wanapendekeza hiyo. Lakini hizi zote ni makisio ya kubahatisha tu, na hayajatolewa ushahidi wowote.

[6] Faraasikh (uwingi wa farsakh) ni kipimo cha Kiajemi cha umbali ambacho ni sawa na takribani maili tatu.

[8] Hadiyth hii inadhirisha kuwa inaruhusiwa kuunganisha Adhuhuri na Alasiri pamoja na Magharibi na ‘Ishaa wakati wa safari, bila kujali kuwa Swalaah hizo zinaswaliwa wakati mahususi wa Swalaah ya mwanzo au wakati wa Swalaah ya pili. Hali zote hizi mbili zinathibitishwa kwa mfano au desturi za Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Wafuasi wa Kihanafi hawaafiki desturi hii, ambayo inamaanisha kuwa wao hawaiafiki Hadiyth hii.

[9] Burud ni wingi wa barid, ambayo inamaanisha farsakh tatu, na farsakh moja ni sawa na maili tatu.

[10] Endapo mtu hawezi hata kutoa ishara, basi husamehewa kwa muda wajibu wa kuswali. Lakini mara atakavyopona na kurejesha afya na nguvu zake, lazima aziswali zote kama deni. Ikiwa mtu amezirai na amepotewa na fahamu kabisa, husamehewa Swalaah zake kadiri anavyokuwa hana fahamu.

[11] Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliketi chini vile kwa sababu maalumu. Hadiyth nyingine inasema kwamba, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliugua jipu pajani, na kadiri mtu anavyougua maradhi, anaweza kuswali kwa mkao wowote anaouweza bila kushurutishwa vyovyote. Hiyo ni zawadi kutoka kwa Allaah (عزّ وجلّ).   

Share