12-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Wa Swalaatul-Jumu'ah (Swalaah Ya Ijumaa)

 

بُلُوغُ الْمَرام

 

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلصَّلَاةِ

 

Kitabu Cha Swalaah

 

بَابُ صَلَاةُ اَلْجُمُعَةِ

 

12-Mlango Wa Swalaatul-Jumu'ah [1]

 

 

 

 

354.

عَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عُمَرَ، وَأَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمْ، {أَنَّهُمَا سَمِعَا رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  يَقُولُ عَلَى أَعْوَادِ مِنْبَرِهِ "لَيَنْتَهِيَنَّ أَقْوَامٌ عَنْ وَدْعِهِمُ اَلْجُمُعَاتِ، أَوْ لَيَخْتِمَنَّ اَللَّهُ عَلَى قُلُوبِهِمْ، ثُمَّ لَيَكُونُنَّ مِنَ اَلْغَافِلِينَ}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar na Abuu Hurayrah (رضيَ اللهُ عَنْهُمْ) wamesema: “Walimsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akisema huku akiwa juu ya Minbar: “Watu lazima waache kupuuza Swalaah za Ijumaa, vinginevyo Allaah Atapiga muhuri nyoyo zao, na kisha watakuwa miongoni mwa walioghafilika.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

355.

 وَعَنْ سَلَمَةَ بْنِ اَلْأَكْوَعِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ: {كُنَّا نُصَلِّي مَعَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  اَلْجُمُعَةَ، ثُمَّ نَنْصَرِفُ وَلَيْسَ لِلْحِيطَانِ ظِلٌّ نَسْتَظِلُّ بِهِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِلْبُخَارِيّ

وَفِي لَفْظٍ لِمُسْلِمٍ: {كُنَّا نَجْمَعُ مَعَهُ إِذَا زَالَتِ اَلشَّمْسُ، ثُمَّ نَرْجِعُ، نَتَتَبَّعُ اَلْفَيْءَ }

Kutoka kwa Salamah[2] bin Al-Akwa’ (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Tulikuwa tukiswali Swalaah ya Ijumaa pamoja na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kisha tunaondoka wakati kuta hazijawa na kivuli[3] tunachojihifadhi[4].” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Al-Bukhaariy]

 

Na katika Riwaayah ya Muslim: “Tulikuwa tukikusanyika pamoja naye jua linapoondoka halafu tunarejea tunatafuta vivuli.”

 

 

 

356.

وَعَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {مَا كُنَّا نَقِيلُ وَلَا نَتَغَدَّى إِلَّا بَعْدَ اَلْجُمُعَةِ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ

وَفِي رِوَايَةٍ: {فِي عَهْدِ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم}

Kutoka kwa Sahl bin Sa’d[5] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Tulikuwa hatulali mchana wala hatuli chakula cha mchana isipokuwa baada ya kuswali Ijumaa.”[6] [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]

 

Katika Riwaayah nyingine: “…zama za uhai wa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).”

 

 

 

357.

وَعَنْ جَابِرٍ {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم  كَانَ يَخْطُبُ قَائِمًا، فَجَاءَتْ عِيرٌ مِنَ اَلشَّامِ، فَانْفَتَلَ اَلنَّاسُ إِلَيْهَا، حَتَّى لَمْ يَبْقَ إِلَّا اثْنَا عَشَرَ رَجُلًا}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesimulia kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa anatoa khutuba kwa kusimama siku ya Ijumaa. Ukaja msafara kutoka Sham (Syria, Palestina, Lebanon na Jordan). Watu wakaukimbilia hadi hakuna aliyebakia na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) isipokuwa watu kumi na wawili.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

358.

وَعَنِ ابْنِ عُمَرَ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   مَنْ أَدْرَكَ رَكْعَةً مِنْ صَلَاةِ اَلْجُمُعَةِ وَغَيْرِهَا فَلْيُضِفْ إِلَيْهَا أُخْرَى، وَقَدْ تَمَّتْ صَلَاتُهُ}  رَوَاهُ النَّسَائِيُّ، وَابْنُ مَاجَهْ، وَاَلدَّارَقُطْنِيُّ، وَاللَّفْظُ لَهُ، وَإِسْنَادُهُ صَحِيحٌ، لَكِنْ قَوَّى أَبُو حَاتِمٍ إِرْسَالَهُ

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Endapo mtu yeyote kawahi Rakaa ya Swalaah ya Ijumaa au Swalaah yoyote nyingine[7], basi aongeze kuswali Rakaa ingine ndipo Swalaah yake itakamilika.[8][Imetolewa na An-Nasaaiy, Ibn Maajah na Ad-Daaraqutwniy na tamshi hili ni lake. Isnaad yake ni sahihi; lakini Al-Haatim aliipa nguvu kama Mursal]

 

 

 

359.

وَعَنْ جَابِرِ بْنِ سَمُرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ ، {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم  كَانَ يَخْطُبُ قَائِمًا، ثُمَّ يَجْلِسُ، ثُمَّ يَقُومُ فَيَخْطُبُ قَائِمًا، فَمَنْ أَنْبَأَكَ  أَنَّهُ كَانَ يَخْطُبُ جَالِسًا، فَقَدْ كَذَبَ}  أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Jaabir bin Samurah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akitoa Khutbah akiwa amesimama[9], kisha anaketi, halafu anasimama tena. Na yeyote anayekuarifu kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akitoa khutbah huku amekaa chini, amedanganya.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

360.

وَعَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اَللَّهِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  إِذَا خَطَبَ، احْمَرَّتْ عَيْنَاهُ، وَعَلَا صَوْتُهُ، وَاشْتَدَّ غَضَبُهُ، حَتَّى كَأَنَّهُ مُنْذِرُ جَيْشٍ يَقُولُ: صَبَّحَكُمْ وَمَسَّاكُمْ، وَيَقُولُ: "أَمَّا بَعْدُ، فَإِنَّ خَيْرَ اَلْحَدِيثِ كِتَابُ اَللَّهِ، وَخَيْرَ اَلْهَدْيِ هَدْيُ  مُحَمَّدٍ، وَشَرَّ اَلْأُمُورِ مُحْدَثَاتُهَا، وَكُلَّ بِدْعَةٍ ضَلَالَةٌ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

وَفِي رِوَايَةٍ لَهُ كَانَتْ خُطْبَةُ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم  يَوْمَ اَلْجُمُعَةِ: {يَحْمَدُ اَللَّهَ وَيُثْنِي عَلَيْهِ، ثُمَّ يَقُولُ عَلَى إِثْرِ ذَلِكَ، وَقَدْ عَلَا صَوْتُهُ}

وَفِي رِوَايَةٍ لَهُ: {مَنْ يَهْدِهِ اَللَّهُ فَلَا مُضِلَّ لَهُ، وَمَنْ يُضْلِلْ فَلَا هَادِيَ لَهُ }

وَلِلنَّسَائِيِّ: {وَكُلَّ ضَلَالَةٍ فِي اَلنَّارِ }

Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdullaah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipokuwa akitoa khutbah, macho yake huwa mekundu, na sauti yake hupanda[10], na ghadhabu yake huwa kali, kama vile mtu anayelionya jeshi akiwaambia: “(Adui) atakushambulieni asubuhi na jioni.” Na anasema: Ammaa Ba’du[11], Hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah, na uongozi bora kabisa ni wa Muhammad, na mambo maovu ni ya uzushi (Bid’ah) na kila Bid’ah ni upotevu.[12][Imetolewa na Muslim]

 

Na katika Riwaayah yake nyingine: “Khutbah ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) siku ya Ijumaa ilikuwa hivi: Anamhimidi Allaah na anamsifu. Kisha anakhutubiu baada ya hayo na sauti yake inapanda.”

 

Na katika Riwaayah yake (Muslim) nyingine: “Na ambaye Allaah Amemhidi, basi hapana wa kumpotoa.” [Az-Zumar: 37], “Ambao Allaah Amewapotoa, basi hakuna wa kuwahidi” [Al-A’raaf: 186] na Ambaye Allaah Anampotosha hakuna yeyote anayeweza kumhidi.”

 

Na tamshi la An-Nasaaiy: “…na kila upotovu ni Motoni.”

 

 

 

361.

وَعَنْ عَمَّارِ بْنِ يَاسِرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  يَقُولُ: {إِنَّ طُولَ صَلَاةِ اَلرَّجُلِ، وَقِصَرَ خُطْبَتِهِ مَئِنَّةٌ مِنْ فِقْهِهِ}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa ‘Ammaar bin Yaasir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) anasema: “Urefu wa Swalaah ya mtu, na ufupi wa khutbah yake ni alama ya Fiqhi yake (uelewa)[13] katika Dini.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

362.

وَعَنْ أُمِّ هِشَامٍ بِنْتِ حَارِثَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {مَا أَخَذْتُ: "ق وَالْقُرْآنِ اَلْمَجِيدِ"، إِلَّا عَنْ لِسَانِ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  يَقْرَؤُهَا كُلَّ جُمُعَةٍ عَلَى اَلْمِنْبَرِ إِذَا خَطَبَ اَلنَّاسَ}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ .

Kutoka kwa Umm Hishaam[14] bint Haarithah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Sikuihifadhi Suwrah Qaaf[15] isipokuwa kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliyekuwa akiisoma kila siku ya Ijumaa juu ya Minbar[16] anapowakhutubia watu.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

363.

وَعَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { مَنْ تَكَلَّمَ يَوْمَ اَلْجُمُعَةِ وَالْإِمَامُ يَخْطُبُ فَهُوَ كَمَثَلِ اَلْحِمَارِ يَحْمِلُ أَسْفَارًا، وَاَلَّذِي يَقُولُ لَهُ: أَنْصِتْ، لَيْسَتْ لَهُ جُمُعَةٌ}  رَوَاهُ أَحْمَدُ، بِإِسْنَادٍ لَا بَأْسَ بِهِ

 وَهُوَ يُفَسِّرُ حَدِيثَ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  فِي "اَلصَّحِيحَيْنِ" مَرْفُوعًا: {إِذَا قُلْتَ لِصَاحِبِكَ: أَنْصِتْ يَوْمَ اَلْجُمُعَةِ وَالْإِمَامِ يَخْطُبُ، فَقَدْ لَغَوْتَ} 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kuzungumza siku ya Ijumaa wakati Imaam anakhutubia yeye ni kama punda aliyebeba vitabu[17], na anayemuambia: “Nyamaza!” basi hana Ijumaa.[18] [Imetolewa na Ahmad, kwa Isnaad isiyo na ubaya wowote]

 

Hadiyth hii inafanana na Hadiyth Marfuw’ ya Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) iliyopokewa katika Swahiyh mbili: “Utakapomuambia mwenzako: “Nyamaza!” wakati Imaam anakhutubia, basi umefanya upuuzi.”

 

 

 

364.

 وَعَنْ جَابِرٍ قَالَ: {دَخَلَ رَجُلٌ يَوْمَ اَلْجُمُعَةِ، وَالنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  يَخْطُبُ. فَقَالَ: "صَلَّيْتَ ؟" قَالَ: لَا. قَالَ: "قُمْ فَصَلِّ رَكْعَتَيْنِ"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Mtu mmoja aliingia Msikitini siku ya Ijumaa wakati Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akikhutubia. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Umeswali?” Akajibu: “Hapana.” Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Simama uswali Rakaa mbili.”[19] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

365.

 وَعَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ; {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم كَانَ يَقْرَأُ فِي صَلَاةِ الْجُمُعَةِ سُورَةَ الْجُمُعَةِ، وَالْمُنَافِقِينَ} رَوَاهُ مُسْلِم

وَلَهُ: عَنِ اَلنُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ: {كَانَ يَقْرَأُ فِي اَلْعِيدَيْنِ وَفِي الْجُمُعَةِ: بِـ "سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ اَلْأَعْلَى"، وَ: "هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ اَلْغَاشِيَةِ" }

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa anasoma katika Swalaah ya Ijumaa Suwrah Al-Jumu’ah na Al-Munaafiquwn.

Suwrah Al-Jumua’ah[20] na Al-Munaafiquwn[21].” [Imetolewa na Muslim]

Naye (Muslim) amenukuu Hadiyth ya Nu’maan bin Bashiyr[22] amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa anasoma katika Swalaah ya ‘Iyd mbili na Swalaah ya Ijumaa[23]

 

 

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى[24]  

na

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْغَاشِيَةِ[25]

 

 

 

 

 

 

366.

وَعَنْ زَيْدِ بْنِ أَرْقَمَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ: {صَلَّى النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  اَلْعِيدَ، ثُمَّ رَخَّصَ فِي الْجُمُعَةِ، فَقَالَ: "مَنْ شَاءَ أَنْ يُصَلِّيَ فَلْيُصَلِّ"}  رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ إِلَّا اَلتِّرْمِذِيَّ، وَصَحَّحَهُ ابْنُ خُزَيْمَة

Kutoka kwa Zayd bin Arqam (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliswali ‘Iyd (Siku ya Ijumaa), na akaruhusu iswaliwe Swalaah ya Ijumaa akasema: Anaetaka kuiswali aswali.”[26] [Imetolewa na Al-Khamsah (An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) isipokuwa At-Tirmidhiy. Na akaisahihisha Ibn Khuzaymah]

 

 

 

367.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { إِذَا صَلَّى أَحَدُكُمُ الْجُمُعَةَ فَلْيُصَلِّ بَعْدَهَا أَرْبَعًا}  رَوَاهُ مُسْلِم

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Yeyote kati yenu ataswali Swalaah ya Jumua’ah basi na aswali Rakaa nne baadaye.”[27] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

368.

وَعَنِ السَّائِبِ بْنِ يَزِيدَ، أَنَّ مُعَاوِيَةَ قَالَ لَهُ: {إِذَا صَلَّيْتَ الْجُمُعَةَ فَلَا تَصِلْهَا بِصَلَاةٍ، حَتَّى تُكَلَّمَ أَوْ تَخْرُجَ، فَإِنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  أَمَرَنَا بِذَلِكَ: أَنْ لَا نُوصِلَ صَلَاةً بِصَلَاةٍ حَتَّى نَتَكَلَّمَ أَوْ نَخْرُجَ}  رَوَاهُ مُسْلِم

Kutoka kwa As-Saaib bin Yaziyd[28] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Mu’aawiyah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alimuambia: “Unaposwali Ijumaa usiiunganishe na Swalaah nyingine hadi umeongea au umekwenda nje. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alituamrisha hivyo, kuwa tusiunganishe Swalaah moja na Swalaah nyingine, mpaka mtu tumeongea au tumetoka nje.”[29] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

369.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { مَنِ اغْتَسَلَ، ثُمَّ أَتَى الْجُمُعَةَ، فَصَلَّى مَا قُدِّرَ لَهُ، ثُمَّ أَنْصَتَ، حَتَّى يَفْرُغَ اَلْإِمَامُ مِنْ خُطْبَتِهِ، ثُمَّ يُصَلِّي مَعَهُ: غُفِرَ لَهُ مَا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجُمُعَةِ اَلْأُخْرَى، وَفَضْلُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ}  رَوَاهُ مُسْلِم

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kuoga, kisha akaja kuswali Ijumaa na akaswali alichopangiwa[30], halafu akanyamaza mpaka Imaam amemaliza khutbah, halafu akaswali pamoja naye, ataghufiriwa (madhambi) kati ya Ijumaa hiyo na inayofuatia na kwa siku tatu zaidi.”[31] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

370.

وَعَنْهُ; أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  ذَكَرَ يَوْمَ الْجُمُعَةِ فَقَالَ: {فِيهِ سَاعَةٌ لَا يُوَافِقُهَا عَبْدٌ مُسْلِمٌ وَهُوَ قَائِمٌ يُصَلِّي، يَسْأَلُ اَللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ شَيْئًا إِلَّا أَعْطَاهُ إِيَّاهُ، وَأَشَارَ بِيَدِهِ يُقَلِّلُهَا}  مُتَّفَقٌ عَلَيْه

وَفِي رِوَايَةٍ لِمُسْلِمٍ: {وَهِيَ سَاعَةٌ خَفِيفَةٌ}  

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema tena kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliitaja siku ya Ijumaa akasema: “Katika siku hii kuna muda ambapo hakuna mja Muislamu atakayesimama kuswali na anamuomba lolote isipokuwa Allaah (عَزَّ وَجَلَّ) Atampa hilo jambo”[32] Akaashiria kwa mkono wake kuwa muda huo ni mdogo sana.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

Na katika Riwaayah ya Muslim: “Na muda huo ni hafifu.”

 

 

 

371.

وَعَنْ أَبِي بُرْدَةَ عَنْ أَبِيهِ سَمِعْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  يَقُولُ: {هِيَ مَا بَيْنَ أَنْ يَجْلِسَ اَلْإِمَامُ إِلَى أَنْ تُقْضَى اَلصَّلَاةُ}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ،

 وَرَجَّحَ اَلدَّارَقُطْنِيُّ أَنَّهُ مِنْ قَوْلِ أَبِي بُرْدَةَ

وَفِي حَدِيثِ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ سَلَامٍ عِنْدَ ابْنِ مَاجَه

وَجَابِرِ عِنْدَ أَبِي دَاوُدَ، وَالنَّسَائِيِّ  : {أَنَّهَا مَا بَيْنَ صَلَاةِ اَلْعَصْرِ إِلَى غُرُوبِ اَلشَّمْسِ}

وَقَدْ اِخْتُلَفَ فِيهَا عَلَى أَكْثَرَ مِنْ أَرْبَعِينَ قَوْلًا، أَمْلَيْتُهَا فِي "شَرْحِ اَلْبُخَارِيِّ

Kutoka kwa Abuu Burdah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa baba yake amesema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akisema: “Muda huo ni baina ya Imaam anapokaa mpaka mwisho wa Swalaah.” [Imetolewa na Muslim]

 

Na Ad-Daaraqutwniyy ana kauli kama ya Abuu Burdah.

 

Katika Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Salaam iliyopokewa na Ibn Maajah

Pia Hadiyth ya Jaabir iliyopokewa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy: “Muda huo ni baina ya Swalaah ya Alasiri na kukuchwa kwa jua (Magharibi).”

 

Kuna kauli zaidi ya arubaini kuhusu muda huo, na nimezinukuu katika “Sharh Al-Bukhaariy”

 

 

 

372.

وَعَنْ جَابِرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ: {مَضَتِ السُّنَّةُ أَنَّ فِي كُلِّ أَرْبَعِينَ فَصَاعِدًا جُمُعَةً} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ بِإِسْنَادٍ ضَعِيف

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Sunnah[33] imekuwa ni kuwa katika kila watu arubaini au zaidi ni Ijumaa.” [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniy kwa Isnaad dhaifu[34]]

 

 

 

373.

وَعَنْ سَمُرَةَ بنِ جُنْدُبٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم كَانَ يَسْتَغْفِرُ لِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ كُلَّ جُمُعَةٍ}  رَوَاهُ اَلْبَزَّارُ بِإِسْنَادٍ لَيِّن

Kutoka kwa Samurah bin Jundub (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiombea maghufirah Waumini wanaume na Waumini wanawake katika kila Ijumaa.” [Imetolewa na Al-Bazzaar kwa Isnaad laini]

 

 

 

374.

وَعَنْ جَابِرِ بْنِ سَمُرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم  كَانَ فِي اَلْخُطْبَةِ يَقْرَأُ آيَاتٍ مِنَ اَلْقُرْآنِ، وَيُذَكِّرُ اَلنَّاسَ}  رَوَاهُ أَبُو دَاوُد وَأَصْلُهُ فِي مُسْلِم

Kutoka kwa Jaabir bin Samurah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipokuwa anakhutubia alisoma Aayah kadhaa za Qur-aan, na anawakumbusha watu[35].” [Imetolewa na Abuu Daawuwd, na chanzo chake ni katika Swahiyh Muslim]

 

 

 

375.

وَعَنْ طَارِقِ بْنِ شِهَابٍ; أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  قَالَ: {الْجُمُعَةُ حَقٌّ وَاجِبٌ عَلَى كُلِّ مُسْلِمٍ فِي جَمَاعَةٍ إِلَّا أَرْبَعَةً: مَمْلُوكٌ، وَاِمْرَأَةٌ، وَصَبِيٌّ، وَمَرِيضٌ}  رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَقَالَ: لَمْ يَسْمَعْ طَارِقٌ مِنَ اَلنَّبِيِّ

وَأَخْرَجَهُ اَلْحَاكِمُ مِنْ رِوَايَةِ طَارِقٍ اَلْمَذْكُورِ عَنْ أَبِي مُوسَى 

Kutoka kwa Twaariq bin Shihaab[36] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Swalaah ya Ijumaa kwa jamaa ni waajibu kwa kila Muislamu isipokuwa wane: mtumwa, mwanamke, mtoto na mgonjwa.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na akasema: Twaariq hakusikia (haya) kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ)]

 

Al-Haakim ameyapokea haya kutoka kwa Twaariq aliyetajwa hapa, naye kutoka kwa Abuu Muwsaa.

 

 

 

376.

وَعَنِ ابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {لَيْسَ عَلَى مُسَافِرٍ جُمُعَةٌ}  رَوَاهُ اَلطَّبَرَانِيُّ بِإِسْنَادٍ ضَعِيف

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Swalaah ya Ijumaa si lazima kwa msafiri.”[37] [Imetolewa na Atw-Twabaraaniyy kwa Isnaad dhaifu]

 

 

 

377

وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  إِذَا اسْتَوَى عَلَى الْمِنْبَرِ اسْتَقْبَلْنَاهُ بِوُجُوهِنَا}  رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ

وَلَهُ شَاهِدٌ مِنْ حَدِيثِ الْبَرَاءِ عِنْدَ اِبْنِ خُزَيْمَة

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas-‘uwd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa sawasawa juu ya minbar, sisi tunamuelekea kwa nyuso zetu.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy kwa Isnaad dhaifu]

 

Nayo ina ushahidi wa Hadiyth ya Al-Baraa iliyopokelewa na Ibn Khuzaymah.

 

 

 

378.

وَعَنِ اَلْحَكَمِ بْنِ حَزْنٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ: {شَهِدْنَا الْجُمُعَةَ مَعَ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم  فَقَامَ مُتَوَكِّئًا عَلَى عَصًا أَوْ قَوْسٍ}  رَوَاهُ أَبُو دَاوُد

Kutoka kwa Al-Hakam bin Hazn[38] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Tulihudhuria Swalaah ya Ijumaa pamoja na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), naye akasimama wima akiegemea fimbo au upinde.”[39] [Imetolewa na Abuu Daawuwd]

 

 

 

 

 


[1] Siku ya Ijumaa ilikuwa ikijulikana kama Al-‘Aruwbah zama za Jaahiliyyah (kipindi kabla ya Uislamu kuja). Uislamu ukaita Jumua’ah kwa kuwa Waislamu wa mji hukusanyika (Jamaa) ili kuswali na kumwabudu Allaah (عزّ وجلّ). Zaidi ya hizi, zipo sababu zingine pia.

[2] Salamah bin Al-Akwa’ ndiye Abuu Muslim, Salamah bin ‘Amr bin Al-Akwa’ Sinaan bin ‘Abdillaah Al-Aslamiy Al-Madaniy. Alikuwa mmoja wa Maswahaba mashujaa, na alikuwa akikimbia kwa kasi zaidi kuliko farasi kwa miguu yake. Alikuwa ni mtu mzuri, Mwenye taqwa, na mkarimu sana. Alifia Al-Madiynah mnamo mwaka wa 74 A.H.

[3] Hadiyth hii inasema wazi kwamba, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akimaliza Swalaah yake ya Ijumaa katika wakati ambao vivuli vya kuta vilikuwa havitoshi kuwafunika watu. Yaani Swalaah ya Ijumaa ni sharti iswaliwe mapema.

[4] Kwa mujibu wa Imaam Ahmad bin Hambal, inaruhusiwa kuanza kuswali Swalaah ya Ijumaa kabla ya Zawaal (jua halijageuka). Maimaamu waliobaki na Wanazuoni wengi wanasema kwamba Swalaah ya Ijumaa sharti ianze kuswaliwa mara baada ya zawaal. Siku hizi imekuwa desturi kuiahirisha Swalaah ya Ijumaa mbele zaidi, hata baada ya Adhuhuri yenyewe, ambaye ni kinyume na mwenendo wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).

[5] Sahl bin Sa’d ndiye Abdul-‘Abbaas Al-Khazraji As-Sa’d Al-Answaariy. Aliripoti Hadiyth mia moja, na alifariki mnamo mwaka 91 A.H. akiwa na umri wa takribani miaka mia moja. Inasemekana kuwa alikuwa Swahaba wa mwisho kufariki Al-Madiynah.

[6] Haimaanishi kuwa alikuwa akiswali Swalaah ya Ijumaa hata kabla ya wakati wa zawaal (kugeuka kwa jua). Swalaah ya Ijumaa huitangulia Swalaah ya Adhuhuri. Na kadri inavyohitaji kusomwa khutbah, ni waajibu kuswali haraka, ili Swalaah imalizike ndani ya wakati wa mwanzo wa Adhuhuri.

[7] Usimulizi ambao unanasibishwa na Abuu Hurayrah katika Swahiyh mbili, haikusudii Swalaah ya Ijumaa peke yake, bali umejumuisha Swalaah zote. Madhali mtu kawahi Rakaa kamili na Imaam, anapata thawabu za Swalaah ya jamaa. Hii inahusu Swalaah ya Ijumaa pia. Kisha mtu huyo asimame na kukamilisha sehemu ya Swalaah iliyobakia.

[8] Hadiyth hii inakanusha maoni ya wale wanaodai kuwa Swalaah ya Ijumaa haikubaliki hadi mtu awe kasikiliza sehemu ya khutbah.

[9] Hadiyth hii inadhihirisha kwamba Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiwakhutubia watu Msikitini huku amesimama wima. Pia inadhihirisha kwamba, katika Swalaah ya Ijumaa, kutoa khutbah kwa sehemu mbili kunafuata Sunnah, na kwamba ni Sunnah pia kuketi chini kwa muda mfupi katika sehemu mbili hizo za khutbah; na kuikhalifu Sunnah hii ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kunahesabika kuwa ni bid’ah (iuzushi).

[10] Hadiyth hii inatufunza kwamba, khutbah ni sharti itolewe kwa sauti kubwa, na itolewe kwa njia mbayo itatoa athari ya kutosha kwa wanaosikiliza.

[11] Hayo ni maneno ya ufunguzi wa khutbah ya Kiislamu inayomaanisha: “Baada ya huo utangulizi.”

[12] Kwa mujibu wa Shariy’ah, bid’ah ni tendo lolote ambalo halijatajwa au kuthibitishwa na Qur-aan wala Sunnah, wala haitokani na hizo. Maneno yale yasemayo “Kullu bid’ah (kila uzushi)” inaashiria kuwa bid’ah zote ni mbaya au hakuna uzushi (bid’ah) uliokuwa na uzuri wowote, kwa taarifa za kina, rejea kitabu cha Al-I’tiswaam cha Imaam Ash-Shaatwibiyy.

[13] Hii inadhihirisha kwamba, mtu sharti arefushe Swalaah yake na aifupishe khutbah. Baadhi ya Makhatibu   siku hizi hurefusha mno khutbah, kiasi kwamba huuingilia muda wa Swalaah, na kisha hujaribu kuimaliza Swalaah kwa haraka. Hii ni kinyume na mwenendo wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ)

[14] Umm Hishaam ndiye Umm Hishaam bint Haarithah bin Nu’umaan, dada (kwa upande wa Mama) wa ‘Umrah bint ‘Abdir-Rahmaan. Yeye ni Answaariyyah kutoka katika ukoo wa Najjaar. Inasemekana kuwa alishiriki katika Bay’atur-Ridhwaan.

[15] Qaaf (50)

[16] Hii ndiyo Shariy’ah kwetu kuwa, wakati tunawakhutubia watu kabla ya kuwaswalisha Swalaah.

[17] Mtu kama huyo anafanana na punda (mnyama wa kubeba mizigo), kwa vile hapati faida yoyote kwa kule kubeba vitabu vingi mgongoni kwake. Halikadhalika mtu huyo hapati faida yoyote kwa kuswali Swalaah ya Ijumaa.

[18] Zingatia kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) hakusema Swalaah ya mtu huyo haitakubaliwa, bali atanyimwa fadhila za Swalaah ya Ijumaa. Kwa hivyo Wanazuoni wamebainisha kutoka katika hilo kuwa mtu yeyote atakayeshiriki mazungumzo bila shaka atapata thawabu za Swalaah, lakini atanyimwa thawabu zinazonasibishwa na Swalaah ya Ijumaa.

[19] Usimulizi wa Al-Bukhaariy unao neno: “Khafiyfatayn (Khafifu mbili)” baada ya neno “Raka’tayn (Rakaa mbili)”, yaani inamaanisha kuwa yule mtu aliagizwa aswali Rakaa mbili lakini ziwe nyepesi ili ahifadhi muda mrefu zaidi wa kusikiliza khutbah.

[20] Al-Jumua’ah  (62)

[21] Al-Munaafiquwn (63)

[22] Nu’umaan bin Bashiyr ndiye Abuu ‘Abdullaah Al-Answaariyy Al-Madaniy, na alikuwa mtoto wa kwanza wa Kianswaar kuzaliwa baada ya Hijrah (kuhama) ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Alizaliwa mnamo mwezi wa kumi na tatu wa Hijrah. Alilowea Sham na baadaye akawa gavana wa Kufa na kisha Hims. Khaalid bin Khali Al-Kilaa’i alimuua yeye Abuu ‘Abdullaah Al-Answaariyy katika siku ya Rahit mnamo mwaka 64 A.H.

[23] Miongoni mwa Suwrah hizi alikuwa akisoma Suwrah tofauti nyakati mbalimbali.

[24] [Al-A’laa (87)]

 

[25] Al-Ghaashiyah (88)

[26] Hii inaleta ushahidi kwamba, iwapo siku kuu ya ‘Iyd inaangukia siku ya Ijumaa, siyo lazima kuswali Swalaah ya Ijumaa, lakini ni bora kuswali Ijumaa.

[27] Kuna tofauti ya maoni ya Rakaa ngapi ziswaliwe kama Sunnah baada ya Swalaah ya Ijumaa. Wengine wanatambua Rakaa mbili tu, wakati wengine hupendelea kuswali Rakaa nne. Imaam Shaafi’y na Imaam Ahmad na wengi wa Wanazuoni wameshikilia maoni hayo hayo ambayo ndiyo bora zaidi. Hadiyth ya Rakaa nne ni usemi wa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) mwenyewe, kwa hivyo watu wautekeleze.

[28] As-Saaib bin Yaziyd ndiye Abuu Yaziyd Al-Kindiy. Alizaliwa mnamo mwaka wa 2 A.H. na alihudhuria ile Hijjatul Wadaa’i pamoja na baba yake. Alikufa mnamo mwaka 80 A.H.

[29] Hadiyth hii inadhihirisha kwamba, endapo mtu ataiswali Swalaah fulani mahali fulani, basi asiswali Swalaah nyingine mahali palepale katika wakati uleule. Lazima uwepo umbali kati ya Swalaah hizo mbali ama kwa kubadilisha mahali au kwa njia ya Adhkaar (Kumdhukuru Allaah). Lengo la niyyah njema la kutenda hivi ni kwamba, rikodi ya matendo yake ipate kuonyeshe kuwa aliswali mahali pengi mbalimbali kadiri iwezekanavyo, au ionyeshe kuwa ameswali mara nyingi.

[30] Hakuna kikomo cha Swalaah za Sunnah (Nawaafil) mtu anazoweza kuziswali wakati akingojea Swalaah ya Ijumaa, na hakuna kikomo cha wakati. Lakini kama Hadiyth nyingine inavyosema kuwa hakukatazwi kuswali Swalaah za khiari siku ya Ijumaa hata iwe ni wakati wa zawaal.

[31] Ni ghuslu (Kuoga josho) mnamo siku ya Ijumaa ni tendo la Sunnah  kwa mujibu wa Wanazuoni wengi, ambayo ndiyo sahihi. Wengine wanaitambua kuwa ni waajib.

[32] Kuna wakati unaopatikana kila siku ya Ijumaa ambapo du’aa ya Muislamu hutakabaliwa bila shaka. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْه وَآلِهِ وَسَلَّمْ) hakuuutaja wakati huu maalumu. Wakati huo umefichwa kama ulivyofichwa Laylatul-Qadr   ili watu watumie muda mwingi zaidi kuutafuta, na kwa hivyo wapate thawabu nyingi zaidi. Kuna nukuu mbili juu ya wakati huu. Ya kwanza inasema wakati huo ni kati ya Alasiri na machweo ya jua. Ya pili inasema wakati huo umo ndani ya wakati Imaam anapowasomea watu khutbah yake. Waislamu wajitahidi kuutafuta  wakati huu nyakati zote za siku ya Ijumaa na khasa nyakati mbili hizo.

[33] Suala kuhusu watu wangapi wakusanyike pahala ili liswihi sharti la kuswali Swalaah ya Ijumaa nalo bado lina khitilafu miongoni mwa Wanazuoni. Tarakimu tofauti zimetolewa na watu mbalimbali watu watatu, wane, tisa, kumi na mbili, ishirini, arubaini, khamsini na sabiini. Ukweli ni kwamba hakuna tarakimu iliyotolewa na Hadiyth. Swalaah zote mbili, Swalaah ya Ijumaa hata kama kuna watu wawili tu wanaoziswali. Hadiyth hii inayotaja tarakimu ni dhaifu. Imeripotiwa katika Hadiyth kwamba, Swalaah ya kwanza kabisa ya Ijumaa katika Usilamu iliswaliwa katika kijiji cha Juwaathaa.

[34] Ameipokea ‘Abdul Aziyz bin ‘Abdir-Rahmaan ambaye Hadiyth zake zimeelezewa na Wanazuoni kuwa ni za “uongo”, za ‘kughush’ na yeye mwenyewe ahisabika kuwa “si wa kutegemewa.” Kwa hivyo sharti hilo kwa Swalaah ya Ijumaa siyo sahihi.  

[35] Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiwapa mawaidha watu juu ya misingi ya Uislamu, mambo ya msingi ya lazima ya Dini, na alikuwa akiwaonya watu wasighurike na anasa na starehe za dunia hii bali akiwavutia watu waelekee katika maisha ya Aakhirah.

[36] Twaariq bin Shihaab ni wa Ahmusi, Bajali, na wa Kufi, na aliishi muda mrefu katika zama za Jaahiliyyah na zama za Uislamu. Alimuona Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) lakini hakuwahi kusikia Hadiyth kutoka kwake. Alishiriki katika misafara ya kivita wakati wa Ukhalifa wa Abuu Bakr na ‘Umar. Alikufa mnamo mwaka 82 A.H.

[37] Hadiyth zote hizi zinaelezea kuwa, kuna aina sita za watu ambao kwao wao Swalaah ya Ijumaa siyo lazima. Hao ni watumwa, wanawake, watoto, wasafiri, wagonjwa na wanaohamahama, aina zingine mbili zaidi, yaani vipofu na walemavu wametajwa ndani ya Qur-aan. Hao wakiswali Swalaah ya Ijumaa basi hawatawajibika tena  Swalaah ya Adhuhuri.

[38] Al-Hakam bin Hazn ndiye Al-Hakam bin Hazn bin Abdil-Waahaab Al-Makhzuwm. Alisilimu katika mwaka ilipokombolewa Makkah. Na kwa hivyo akahudhuria Swalaah ya Ijumaa pamoja na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).

[39] Hii inathibitisha kwamba, Khatiyb anapotoa khutbah anaweza kuegemea kitu ili kuepusha uchovu kutokana na kisimamo cha muda mrefu.

 

 

 

Share