Umuhimu Wa Kukimisha Swaalah

 

Umuhimu Wa Kukimisha Swalaah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣﴾

Ambao huamini ya ghayb na husimamisha Swalaah na katika vile Tulivyowaruzuku hutoa. [Al-Baqarah: 3]

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ ﴿٥﴾

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara. [Al-Bayyinah: 5]

 

Maana ya kukimisha Swalaah:

 

Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: “Ni kuswali kwa kuzingatia nguzo na sharti zake.”  Adhw-Dhwahaak amesema kuwa Ibn ‘Abbaas alisema: “Iqamaat Asw-Swalaah maana yake ni kukamilisha rukuu, sujuwd, kusoma Qur-aan, khushuu (unyenyekevu), na kuhudhurisha moyo katika Swalaah.” Qataadah alisema: “Iqamaat Asw-Swalaah maana yake ni kuchunga wakati, wudhuu, rukuu na sujuwd za Swalaah.” Muqaatil bin Hayyaan alisema: “Iqaamat Asw-Swalaah ina maana: Kuchunga wakati, kujitwaharisha kwa ajili yake, kukamilisha rukuu, sujuwd na kusoma Qur-aan, tashahhud na kumwombea rahmah Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Hiyo ndiyo Iqaamat Asw-Swalaah.” [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

 

Swalaah ni nguzo ya pili katika Uislamu na nguzo hii  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametufanyia kuwa ni waajib ili iwe ni hakikisho kuwa tunabaki kwenye njia ya Uislamu ambayo inaongoza kwenye Rahmah Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na maghfirah na manufaa yetu ya duniani na Aakhirah.

 

 

Swalaah ni kiunganisho chetu kwa Rabb wetu ‘Azza wa Jalla. Ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema kuwa pindi tunapotaka msaada Kwake basi tuutafute msaada huo kwa Subira na Swalaah na hapo Yeye Atakuwa pamoja nasi kama Anavyosema:

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٣﴾

Enyi walioamini! Tafuteni msaada kwa subira na Swalaah; hakika Allaah Yu pamoja na wanaosubiri. [Al-Baqarah: 153]

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45]

 

 

Swalaah pia Inafuta madhambi na kutukinga na machafu; Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ

na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari.  [Al-'Ankabuwt: 45]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ ۚ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ﴿١١٤﴾

Na simamisha Swalaah katika ncha mbili za mchana na sehemu ya kwanza ya usiku; hakika mema yanaondosha maovu. Hivyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.  [Huwd: 114]

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amelinganisha Swalaah na mto ambao mtu akioga ndani yake mara tano kwa siku, basi hakika mtu huyo hatokuwa mchafu. Kwa hivyo kuswali kwetu, daima kunafuta madhambi madogo yaliyotendeka baina ya kila Swalaah.

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((أَرَأَيْتُمْ لَوْ أَنَّ نَهْرًا بِبَابِ أَحَدِكُمْ يَغْتَسِلُ مِنْهُ كُلَّ يَوْمٍ خَمْسَ مَرَّاتٍ هَلْ يَبْقَى مِنْ دَرَنِهِ شَيْءٌ؟)) قَالُوا: لَا يَبْقَى مِنْ دَرَنِهِ شَيْءٌ. قَالَ: ((فَذَلِكَ مَثَلُ الصَّلَوَاتِ الْخَمْسِ يَمْحُو اللَّهُ بِهِنَّ الْخَطَايَا))     رواه البخاري ومسلم

 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mnaonaje ingelikuwa kuna mto mbele ya nyumba ya mmoja wenu kisha akawa anaoga humo kila siku mara tano, je atabakiwa na uchafu?)) Wakasema: “Habakiwi na uchafu”. Akasema: ((Hivyo ni mfano wa Swalaah ambazo Allaah hufuta madhambi kwayo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ametufaradhishia Swalaah ili daraja zetu zipande, thawabu zetu zizidishwe, na madhambi yetu yafutike, na kwa ajili yake Atuingize Jannah na Atuokoe na Moto.

 

 

Walakini, Swalaah ni kama upanga wenye makali pande zote mbili. Tukiihifadhi, itatupa Nuru kwenye nyoyo zetu, makaburi yetu, na Siku ya Qiyaamah. Itatushuhudia wakati ambao tunahitaji shahidi ili tuokoke na adhabu ya Moto.

Faida hizo zinapatikana kutoka katika Hadiyth zifuatazo:

 

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو بن العاص عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنَّهُ ذَكَرَ الصَّلاةَ يَوْمًا فَقَالَ:  ((مَنْ حَافَظَ عَلَيْهَا كَانَتْ لَهُ نُورًا وَبُرْهَانًا وَنَجَاةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ، وَمَنْ لَمْ يُحَافِظْ عَلَيْهَا، لَمْ يَكُنْ لَهُ نُورٌ وَلا بُرْهَانٌ وَلا نَجَاةٌ وَكَانَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مَعَ قَارُونَ وَفِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَأُبَيِّ بْنِ خَلَفٍ)) أخرجه الإمام أحمد في مسنده

 

Kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Amru ibn Al-'Aaasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba siku moja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitaja kuhusu Swalaah akasema: ((Atakayeihifadhi atakuwa na nuru na uongofu, na kufuzu siku ya Qiyaamah, na asiyeihifadhi hatokuwa na nuru wala uongofu wala kufuzu, na siku ya Qiyaamah atakuwa pamoja na Qaaruwn, Fir'awn, Haaman na Ubayy bin Khalaf)) [Musnad Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh]

 

Pia:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ َقَالَ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ ((إِنَّ أَوَّلَ مَا يُحَاسَبُ بِهِ الْعَبْدُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مِنْ عَمَلِهِ صَلاتُهُ فَإِنْ صَلُحَتْ فَقَدْ أَفْلَحَ وَأَنْجَحَ وَإِنْ فَسَدَتْ فَقَدْ خَابَ وَخَسِرَ فَإِنْ انْتَقَصَ مِنْ فَرِيضَتِهِ شَيْءٌ قَالَ الرَّبُّ عَزَّ وَجَلَّ انْظُرُوا هَلْ لِعَبْدِي مِنْ تَطَوُّعٍ فَيُكَمَّلَ بِهَا مَا انْتَقَصَ مِنْ الْفَرِيضَةِ ثُمَّ يَكُونُ سَائِرُ عَمَلِهِ عَلَى ذَلِكَ)) الترمذي و أبوا داود والنسائي وابن ماجه وأحمد

 

Imepokelewa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah  wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kitu cha kwanza kinachohesabiwa katika ‘amali za mja wa Allaah Siku ya Qiyaamah ni Swalaah zake. Zikiwa zimetimia, hapo tena atakuwa kaneemeka na kafuzu, na zikiwa zina kasoro atakuwa kaanguka na kala khasara. Ikiwa pana upungufu katika Swalaah zake za fardhi Allaah ‘Azza wa Jalla Atasema: “Tazama ikiwa mja wangu ana Swalaah zozote za Sunnah ambazo zinaweza kufidia zile zilizopungua, hapo tena ‘amali yake iliyobaki itaangaliwa hivyo hivyo)). [At-Tirmidhiy, Abu Daawuwd, An-Nasaaiy, Ibn Maajah na Ahmad]

 

Hivyo basi tukiipuuza Swalaah, itatoa ushahidi dhidi yetu, wakati ambao tunahitajia shahidi zaidi. Lazima tujihadhari tusiwe miongoni mwa watu waliopoteza Swalaah kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akawaahidi adhabu ya Moto. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا ﴿٥٩﴾

Wakafuata baada yao waovu, walipoteza Swalaah na wakafuata matamanio; basi watakutana na adhabu motoni. [Maryam: 59]

 

 

Na tuzingatie maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth:

 

عن جَابِر بن عبد الله عن النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهم عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قال: ((إِنَّ بَيْنَ الرَّجُلِ وَبَيْنَ الشِّرْكِ وَالْكُفْرِ تَرْكَ الصَّلَاةِ))   رواه مسلم  

Kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Baina ya mtu na shirki, na kufru, ni kuacha Swalaah)) [Muslim]

 

 

  

Cheo cha Swalaah katika Dini ni kama mfano wa mlingoti wa nyumba, ukiwepo, nyumba itakuwa madhubuti na vifaa vyake vyote vitalingana mahali pake. Lakini isipokuweko, basi jengo lote litabomoka na kuwa halina maana.

 

Na hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hatuamrishi kuswali tu, bali Anatuamrisha tuimarishe Swalaah, jambo ambalo ‘Ulamaa wa Tafsiyr wamekubaliana kuwa kuimarisha Swalaah, ina uzito zaidi kuliko kuswali tu bila ya kuimarisha ipasavyo. Na kuimarisha Swalaah ina maanisha ni kutimiza shuruti zote za twahara, kuelekea Qiiblah, usafi wa mahali pa kuswali na vasi la kuswalia na  mengineyo.  

 

 

‘Ulamaa hawakuacha kuandika kuhusu Umuhimu wa Swalaah, hivyo vitabu vingi vimeandikwa juu yake.  

 

Ili kupata faida ziada  kuhusu Swalaah bonyeza kiungo kifuatacho:

 

Swalaah - Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

Wa biLaahit-tawfiyq

 

 

 

Share