063-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Hali Ambazo Kutayammamu Kunaruhusiwa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

063-Hali Ambazo Kutayammamu Kunaruhusiwa

 

 

Kutayamamu kunaruhusika katika hali mbili:

 

1- Maji yanapokosekana, ni sawa safarini au mjini.

 

2- Inapokuwa vigumu kuyatumia. Na hili lina picha mbalimbali zitakazoelezewa baadaye InshaAllaah.

 

Allaah Mtukufu Anasema:

((وإن كنتم جنبا فالطهروا وإن كنتم مرضى أو على سفر أو جاء أحد منكم من الغائط أو لامستم النساء فلم تجدوا ماء فتيمموا))

((Na mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni, na mkiwa wagonjwa au mkiwa safarini, au ametoka mmoja wenu chooni, au mmewagusa wanawake na hamkuyapata maji, basi tayamamuni)). [Al-Maaidah (5:6)].

 

Si Lazima Safari Iwe Ndefu Ili Msafiri Apate Ruksa Ya Kutayammamu

 

Endapo maji yatakosekana, itampasa msafiri atayamamu sawasawa ikiwa safari ni ndefu au fupi katika kauli mbili Swahiyh zaidi za Maulamaa, kwa vile safari katika Aayah Tukufu haikuainishwa kama ni fupi au ndefu. [Al-Muhalla (2/116) na Al-Mughniy (1/148)].

Ushahidi wa hilo ni:

 

1- Hadiyth ya ‘Aaishah (Allaah Amridhie), amesema:

“Tulitoka na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam) katika baadhi ya safari zake. Tulipokuwa Baydaa au Bidhaat Al-Jaysh, kidani changu kilikatika. Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam) alipiga kambi ili kukitafuta, na watu nao wakapiga kambi pamoja naye, hawako sehemu yenye maji na maji hawana. Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam) akalala mpaka akapambaukiwa bila kuwepo maji. Na hapo Allaah Mtukufu Akateremsha Aayah ya kutayamamu:

((فتيمموا صعيدا))

((Basi ukusudieni mchanga)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (334) na Muslim (764)].

 

2- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba yeye alitokea Al-Juruf na alipofika Al-Mirbad alitayamamu. Alipangusa uso wake na mikono yake miwili na akasali alasiri. Kisha aliingia Madiynah nailhali jua limepanda. Hakurejesha Swalaah. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik (Twahara uk.73) na Al-Bayhaqiy (1/224)].

 

Ash-Shaafi’iy amesema: Al-Juruf ni sehemu karibu na Madiynah.

 

Si Lazima Safari Iwe Halali

 

Ni sahihi kuwa msafiri hutayamamu katika safari yake (maji yanapokosekana) sawasawa ikiwa alisafiri safari ya halali au safari ya haramu. Kwa kuwa kutayamamu ni faradhi, haijuzu kuacha kinyume na ruksa nyinginezo. Na kwa vile kutayamamu ni hukmu isiyohusiana na safari tu, imeruhusiwa katika safari za haramu kama kupukusa juu ya khufu siku na usiku wake. [Al-Muhalla (2/137), Al-Mughniy (1/150) na Al-Awsatw (2/32)].

 

Ninasema:

 

“Na kwa vile faradhi haipomoki kwa msafiri, imekuwa ni lazima kwake afanikishe sharti ya kusihi kutayamamu, lakini madhambi atayapata kutokana na safari yake ya haramu. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

 

Share