064-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Mwenye Maji Kidogo Ambayo Hayatoshi Ila Kwa Baadhi Ya Viungo Vyake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

064-Mwenye Maji Kidogo Ambayo Hayatoshi Ila Kwa Baadhi Ya Viungo Vyake

 

 

Katika suala hili, Maulamaa wamehitilafiana katika mielekeo miwili:

 

Wa kwanza:

 

Ataosha viungo awezavyo kuviosha na vilivyobaki atatayamamu. Haya ni madhehebu ya Ahmad, Ibn Hazm na moja kati ya kauli mbili za Ash-Shaafi’iy. [Al-Muhalla (2/137), Al-Mughniy (1/150) na Al-Awsatw (2/32)].

 

Hoja yao ni Neno Lake Allaah Mtukufu:

((فاتقوا الله ماستطعتم))

((Mwogopeni Allaah kiasi muwezavyo)). [At-Taghaabun ( 64:16)].

 

Na kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam):

      ((إذا أمرتكم بأمر فائتوا منه ماستطعتم))

((Nikiwaamuruni jambo, basi lifanyeni kiasi muwezavyo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (7288) na Muslim (3199)].

 

Ibn Hazm amesema:

 

“Na huyu anaweza kuviosha baadhi ya viungo vyake vya wudhuu au kuoga sehemu ya kiwiliwili chake, lakini hawezi sehemu zilizosalia, hapo ikafaradhishwa kwake aoshe kwanza viungo anavyoweza kuviosha katika wudhuu au josho hadi kiungo atakachokifikia, na maji yanapoisha, itamlazimu kutayamamu kwa viungo vilivyosalia kwa kulazimika. Na hilo ni lazima, kwani hana maji mengine ya kujitwaharishia. Basi ni wajibu kwake kufidia kwa mchanga kama Alivyoamuru Allaah Mtukufu”.

 

Wa pili:

 

Atatayamamu tu moja kwa moja. Mwelekeo huu ni madhehebu ya Abuu Haniyfah, Maalik na moja ya kauli mbili za Ash Shaafi’iy. Pia mjumuiko wa Masalaf wamesema hili hili. [Al-Majmu’u (2/312) na Majmu’u Al-Fataawaa (21/453)].

 

Wamesema:

“Haikusanywi pamoja twahara ya maji na twahara ya tayamumi; ni ima hii au ile”.

Ibn Al-Mundhir ametoa dalili kuunga mkono mwelekeo huu akisema: [Al-Awsatw ya Ibn Al-Mundhir (2/34)].

 

“Allaah Mtukufu Anasema:

((وإن كنتم جنبا فاطهروا))

((Mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni))

 

Amewajibisha kwa mwenye janaba kuoga kwa maji, na kama hakuyapata, basi atayamamu. Na Amewajibisha kwa mwenye kumfanyia mkewe dhwihaar, amwache huru mtumwa, na kama hakumpata, basi afunge miezi miwili. Na alipokuwa mwenye kumiliki sehemu ya mtumwa lakini kiilivyo ni kama hammiliki na Allaah Akamfaradhishia kufunga, basi mwenye  maji ya kuoshea baadhi ya viungo vyake tu, amekuwa ni kama asiyenayo Akamfaradhishia kutayamamu. Na jibu kuhusu mwenye kufanya tamattui na ana fedha pungufu za kununulia mnyama wa kuchinja, au aliyevunja kiapo chake na uwezo wake uko chini ya kuwalisha masikini kumi, basi hukmu yao ni kama ya hao tuliowataja.

 

Ama kufaradhiwa faradhi mbili kwa hao tuliowataja, hilo halijuzu.”

 

Ninasema:

 

“Na huenda lililo dhahiri zaidi ni kuwa atatayamamu tu moja kwa moja  ili kutokusanya kati ya asili na badali. Pia ni kwa vile, lau kama hana maji ya kutosha kwa viungo vyake vyote vya wudhuu au vya josho na akatumia badali (kutayamamu), basi anakuwa amefanya lile aliloliweza katika Amri ya Allaah na Rasuli Wake pia. Na linalonidhihirikia mimi ni kuwa huyu ambaye anatayamamu baada ya kuosha baadhi ya viungo vyake, bila shaka anakuwa ameipata twahara kwa kutayamamu tu, na wala si kwa kuosha na kutayamamu kwa pamoja, kwani kuosha baadhi ya viungo vyake kunakuwa hakuna maana yoyote baada ya kuwa na uhakika kwamba maji aliyonayo hayamtoshi. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

Mwenye Maji Akihofia Kukabiliwa Na Kiu Yeye Mwenyewe, Au Mwenzake, Au Mnyama Wake Kama Atayatumia

 

Ibn Al-Mundhir amesema: [Al-Awsatw (2/28)]

 

“Maulamaa tunaowajua vyema, wote wamekubaliana kuwa msafiri akijihofia nafsi yake kiu naye ana kiasi kidogo tu cha maji ya kujitwaharishia, basi atayabakisha maji yake kwa ajili ya kunywa, na atatayamamu”.

 

Na Ibn Qudaamah amesema: [Al-Mughniy (1/165). Tazama Al-Majmu’u (2/281)]

 

“Mwenye kuhofia wanyama wake, huhofia kupotea mali yake. Mfano wake ni kama mtu kuyapata maji, na kati yake na maji hayo kukawa na mwizi anayeweza kupora chochote katika mali yake, au mnyama mkali anayeweza kumdhuru mnyama wake. Na kama akimkuta mwenye kiu anayemhofia kufa, itamlazimu amnyweshe na yeye atatayamamu”.

 

 

Share