002-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Baadhi Ya Dalili Za Makundi Mawili

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

002-Baadhi Ya Dalili Za Makundi Mawili

 

 

[1]  WENYE KUSEMA SI KAFIRI

 

Wanasema kwamba hukmu ya Uislamu imeshathibiti kwake baada ya kuingia, nasi hatuwezi kumtoa kwenye Uislamu ila kwa uthibitisho. Kisha wakatoa dalili zifuatazo kuthibitisha kwamba mtu huyo hatoki kwenye Uislamu:

 

(a) 

Dalili zinazoonyesha kwamba Allaah Mtukufu Anayasamehe madhambi yote isipokuwa shirki tu. Ni kama:

1- Neno Lake Ta’alaa:

(( إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا))

((Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu)). [An Nisaa: (4:48)].

 

Wanasema kwamba kwa mujibu wa Aayah hii, mwenye kuacha Swalaah si kafiri, kwa kuwa anaingia ndani ya wigo wa Utashi wa Allaah (wa kusamehewa).

 

Wenye kusema ni kafiri wamejibu:

 

“Aayah hii haikanushi ukafiri wa mwenye kuacha Swalaah, kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Hakika baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imeelezewa nyuma kidogo].

 

Hivyo basi, mwenye kuacha Swalaah anaingia kwenye ujumuishi wa Aayah wenye kuashiria kwamba hilo (la kuacha Swalaah) ni katika mambo ambayo Allaah Hayasamehi, kwa kuwa mtu huyo ni mushrik kwa mujibu wa Hadiyth hii. Na lau tutachukulia kwamba mtu huyu ni kafiri na si mushrik na kwamba Aayah inaeleza kuwa kuna msamaha kwa makosa yaliyo chini ya shirki, basi hakuna ndani ya Aayah hii linaloonyesha kwamba Allaah Hasamehi ukafiri ambao hautokani na shirki, bali makusudio hapa ni kuwa Allaah Anasamehe yaliyo chini ya shirki. Ama yasiyo shirki katika mambo ya kikafiri (kama kumkadhibisha Allaah na Rasuli Wake au kuwatusi), hakuna katika Aayah linalogusia kwamba yanasamehewa, bali hilo linapingana na Qur-aan na Hadiyth zilizo wazi. Hivyo basi, kwa makadirio yote mawili, hakuna mashiko ya kuitumia Aayah katika kutolea hoja.” [Kitabu cha Dhwawaabit At-Takfiyr In-da Ahlis Sunnati wal Jama’a cha Al-Qarniy (uk. 158) kwa mabadilisho madogo]

 

(b)

Dalili zinazoonyesha kwamba mwenye kusema (Laa ilaah illa Allaah) ataingia peponi bila sharti la kuwepo Swalaah. Kati ya hizo ni:

 

2- Hadiyth ya Mu’aadh bin Jabal kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Hakuna mja yeyote anayeshuhudia kwamba hapana mola isipokuwa Allaah, na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah isipokuwa Allaah Humharamishia moto)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (128) na Muslim (32) na tamko ni lake. Kwa Al-Bukhaariy kuna: “..akisadikisha toka moyoni mwake”].

 

3- Hadiyth ya ‘Ubaadah bin Swaamit kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Mwenye kushuhudia ya kwamba hapana mola isipokuwa Allaah Mmoja Asiye na mshirika, na kwamba Muhammad ni Mja Wake na Rasuli Wake, na kwamba ‘Iysaa ni Mja wa Allaah na Rasuli Wake, na kwamba Neno Lake Alilitia kwa Maryam na roho itokayo Kwake, na kwamba Pepo ni kweli na Moto ni kweli, Allaah Atamwingiza Peponi kwa amali yoyote atakayokuwa nayo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3435) na Muslim (28)].

 

4- Hadiyth ya Mu’aadh bin Jabal kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Mtu ambaye maneno yake ya mwisho yatakuwa: Laa ilaaha illa Allaah, ataingia Peponi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3116)].

 

5- Hadiyth ya ‘Utbaan bin Maalik kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Hakika Allaah Amemharamishia Moto mwenye kusema: “Laa ilaaha illa Allaah” akitaka kwa hilo Uso wa Allaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (425) na Muslim (33)].

 

Wanasema kwamba katika Hadiyth hizi hakuna sharti ya kuwepo Swalaah ili aokoke na Moto na aingie Peponi.

 

Wenye kusema ni kafiri wamejibu:

 

“Hadiyth hizi na zinginezo mfano wake zina vigawanyo viwili: Ima ni jumuishi zenye kuainishwa na Hadiyth zenye kuthibitisha ukafiri wa asiyeswali, au zisizo ainishi zenye kuainishwa na Hadiyth zinazoonyesha kwamba haiwezekani kwa mwenye kusema maneno hayo asiswali kama inavyobainika katika neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((..akitaka kwa hilo Uso wa Allaah)) au ((akisadikisha toka moyoni mwake)) na mfano wa hivyo. Hadiyth kama hizi zina ainisha kuwa kutamka shahada kwa niya safi na moyo kusadikisha kikweli, humzuia mtu asiache Swalaah, kwa kuwa utakasifu wake wa niya na ukweli wa moyo wake, vitamfanya aswali tu.  [Kitabu cha “Hukmu Taarikis Swalaat” cha Al’Allaamah bin ‘Uthaymiyn Rahimahul Laahu]

 

(c) 

Allaah Mtukufu Atamtoa motoni mtu ambaye hakufanya kheri yoyote katu.

 

[Kitabu cha “Hukmu Taarikis Swalaat” cha Al’Allaamah Al-Albaaniy Rahimahul Laahu (uk. 36)]

 

6- Katika Hadiyth ya Abu Sa’iyd kuhusiana na uombezi, baada ya kuelezea uombezi wa Waumini kwa nduguzo ili watolewe Motoni, Hadiyth inaendelea ikisema: ((…Watasema: Ee Mola wetu! Hakika tumewatoa wale Uliotuamuru, na katika waliobakia hakuna hata mmoja mwenye kheri!! Kisha Allaah Atasema: Malaika wamefanya uombezi, Manabii wamefanya uombezi, na Waumini wamefanya uombezi, na Amebakia Mrehemevu zaidi kuliko wote wenye huruma. Atakamata kamato la Moto lenye watu ambao hawakumfanyia Allaah jema lolote katu, wameungua mpaka wamekuwa makaa, kisha watapelekwa kwenye maji yaitwayo (Uzima) wamiminiwe. Wataota kama inavyoota punje katika taka za maji..)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6560) na Muslim (183)].

 

Wenye kusema ni kafiri wamejibu:

 

“Swalaah haiingii katika ujumuishi wa neno lake Rasuli Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam: “Hawakufanya kheri yoyote katu”. Vipi iwezekane asiyeswali aingie katika kundi la hawa huku akiwa ameangamia pamoja na wenye kuangamia!!:

((يَوْمَ يُكْشَفُ عَن سَاقٍ وَيُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ   خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ۖ وَقَدْ كَانُوا يُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ وَهُمْ سَالِمُونَ))

((Siku utakapofunuliwa Muundi na wataitwa kusujudu lakini hawatoweza ● Macho yao yatainama chini, udhalilifu utawafunika. Na hali walikuwa wakiitwa wasujudu (kuswali duniani) walipokuwa wazima wa afya)). [Al Qalam (68: 42 na 43)]

 

Kisha Hadiyth Swahiyh zinatutaarifu kwamba kila atakayetolewa motoni katika wale wenye Iymaan ya Tawhiyd, atajulikana kutokana na athari ya sijdah. Katika Hadiyth Marfu’u ya Abu Hurayrah, Rasuli anasema: ((Mpaka Allaah Atakapomaliza kuhukmu baina ya Waja Wake, na Akataka kumtoa kwa Rahma Zake yule Atakayemtaka katika wale waliokuwa wakishuhudia kwamba hapana mola isipokuwa Allaah, Atawaamuru Malaika wawatoe, nao watawatambua kwa alama zao za sijdah. Allaah Ameuharamishia Moto kuila athari ya sijdah ya mwanadamu. Malaika watawatoa wakiwa wamevimba, na hapo hapo watamiminiwa maji yajulikanayo kama “Maji ya uzima”. Atabakia mtu mwenye kuuelekea Moto kwa uso wake, kisha uso wake utageuzwa kuepushwa na Moto)). Anasema Abu Hurayrah: “Na huyo ndiye mtu wa mwisho kuingia Peponi”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6573-7337) na Muslim (182)].

 

Wanasema: “Hadiyth inaonyesha wazi kabisa kwamba wale ambao Allaah Mtukufu Atawatoa Motoni kwa Rahma Zake, Malaika watawatambua kwa athari zao za sijdah, na hao bila shaka ni wenye kuswali. Ama neno la Waumini (katika Hadiyth ya Abu Sa’iyd): “Na katika waliobakia, hakuna hata mmoja mwenye kheri!!”, hii ni kwa mazingatio ya kuwa wanalijua hilo kwa dalili kwamba Allaah Amewaambia (kama ilivyo katika Hadiyth ya Abu Sa’iyd): “Basi watoeni wale mnaowajua kati yao”. Na kama si hivyo, basi ndani ya Moto wapo wenye kuswali katika umma huu na umma zilizotangulia  ambao hakuna awajuao isipokuwa Allaah, na hao Atawatoa kwa Rahma Yake. Ama wasioswali, hao hawatoki humo”. [Ni sehemu ya utangulizi wa Sheikh Muhammad ‘Abdul Maqsoud (Allaah Ampe afya njema) aliouandika kwenye Tasnifu ya Mamdouh (uk. 38 na zinazofuatia) kwa mabadilisho madogo]

 

(d) Hadiyth zinazofahamika kwamba kutoswali hakumtoi mtu katika Uislamu. Kati yake ni:

 

7- Hadiyth ya ‘Ubaadah bin Swaamit aliyesema: “Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( Allaah Amezifaradhisha Swalaah tano kwa Waja Wake. Atakayekutana Naye na Swalaah hizo akiwa hajapoteza chochote, atakutana Naye nailhali Yeye Anayo ahadi kwake ya kumwingiza kwayo Peponi. Na atakayekutana Naye na Swalaah hizo akiwa amepunguza chochote kwa kuzembea haki zake, atakutana Naye Akiwa Hana ahadi kwake. Akitaka Atamwadhibu, na Akitaka Atamsamehe)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Angalia Kitabu cha “Ta’adhiymu Qadris Swalaat” (1029) nilichokifanyia uhakiki. Nimezihakiki kwa kina Sanad Zake, nikapata yakini kwamba ni Dhwa’iyf. Al-Albaaniy (Rahimahul Laahu) anasema ni Swahiyh]

 

Wanasema: “Hadiyth hii inaonyesha kwamba mwenye kuacha baadhi ya Swalaah si kafiri kwa kuwa anaingia ndani ya wigo wa Mapendeleo ya Allaah”.

 

Wenye kusema ni kafiri wamejibu:

 

“Haijuzu kuichukulia Hadiyth hii kwa kuacha baadhi ya Swalaah, kwani Hadiyth imethibitisha mtu kuziswali Swalaah tano pamoja na kuzembea baadhi ya mawajibiko yake pale anaposema Rasuli: ((Na atakayekutana Naye na Swalaah hizo akiwa amepunguza chochote kwa kuzembea haki zake…)).

 

8- Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((La kwanza watakalohisabiwa watu katika amali zao ni Swalaah. Mola wetu Atawaambia Malaika (Naye Anajua zaidi): Mwangalieni Mja Wangu kama ameitimiza au kaipunguza. Ikiwa imetimia ataandikiwa imetimia, na kama imepungua chochote Atasema: Angalieni kama Mja Wangu ana Sunnah zozote. Kama anazo Atasema: Mkamilishieni Mja Wangu faradhi zake kwa Sunnah zake, kisha zitachukuliwa amali zake zikiwa hivyo)).  [Hadiyth Dhwa’iyf Marfu’u: Ina Sanad nilizozihakiki kwa kina katika Kitabu cha “Ta’adhiymu Qadris Swalaat (182) nilichokifanyia uhakiki. Tamiym Ad-Daariy anasema ni Swahiyh Mawquwf]

 

Wanasema: “Upungufu katika faradhi utakamilishwa na Sunnah, na upungufu huu unakusanya upungufu katika Swalaah yenyewe ya faradhi na unakusanya upungufu katika idadi ya faradhi”.

 

Wenye kusema ni kafiri wamejibu:

 

“Hadiyth haifai kuwa Marfu’u. Ina Sanad Dhwa’iyf na zilizo dhahiri zaidi: ((Ikiwa imefaa, basi amefaulu na kufuzu. Na ikiwa imeharibika, basi amepita utupu na amekula hasara)). Neno lake: ((Imefaa)), lina maana Swalaah iliyokamilika nguzo zake sawasawa, na hivyo haiswihi kulichukulia neno lake: ((..na kama imepungua chochote)) juu ya kuacha nguzo na masharti. Hivyo ni lazima kuuchukulia upungufu kama ni kuacha yaliyo chini ya hayo.” Kwa hoja hii, Hadiyth haifai kutolewa ushahidi.

 

9-Hadiyth Marfu’u ya ‘Aaishah isemayo: ((Madaftari mbele ya Allaah ni matatu: Daftari ambalo Allaah Hajali kwalo chochote, daftari ambalo Allaah Hatoacha kitu humo, na daftari ambalo Allaah Hatosamehe kitu. Ama daftari ambalo Allaah Hatosamehe kitu ni shirki. Ama daftari ambalo Allaah Hajali kitu ni kujidhulumu mja mwenyewe kwa yaliyo baina yake na Mola wake kwa kuacha siku moja ya funga, au Swalaah aliyoiacha, kwani Allaah Ta’alaa Huyasamehe na kuyaachilia kama Atataka)). [Hadiyth Dhwa’iyf Marfu’u: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (6/240). Angalia Kitabu cha “Dhaiyful Jaami’i (3022). Iko Hadiyth nyingine kama hii ambayo Swalaah haikutajwa, Al-Albaaniy kasema ni Hasan]

 

Wenye kusema ni kafiri wamejib

 

“Kwa kuongezwa neno: ((kwa kuacha siku moja ya funga, au Swalaah aliyoiacha)), Hadiyth inakuwa ni Dhwa’iyf!!

 

10- Hadiyth ya Nasr bin ‘Aasim Al Laythiy aliyoipokea toka kwa mtu miongoni mwao kwamba mtu huyo alimjia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasilimu lakini kwa sharti kwamba aruhusiwe kuswali Swalaah mbili tu, na Rasuli akamkubalia. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (5/363)].

 

Wamesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimkubalia mtu huyo kusilimu huku akijua kwamba hatoswali isipokuwa Swalaah mbili tu kati ya tano!!”

 

Wenye kusema ni kafiri wamejibu:

 

“Hadiyth haielezi kwamba Swalaah wakati huo zilikuwa ni tano!!”

 

Inavyoonekana ni kuwa hili lilikuwa wakati Swalaah za faradhi zilikuwa ni mbili tu kabla ya kuwa ni tano. Au inaweza kuwa ni katika mlango wa kumkubalia mtu kusilimu pamoja na kuvunja mwiko. Na hili ni mahsusi kwa Rasuli peke yake, mwingine haruhusiwi kulifanya baada yake.

 

(d)

 Wamechukulia kuwa ni ukafiri mdogo uliotajwa kwenye Hadiyth zenye kueleza kwa bayana ukafiri wa asiyeswali

 

11- Wamesema: “Katika Hadiyth nyingi, tumeuchukulia ukafiri uliotajwa kuwa si ukafiri unaomtoa mtu katika Uislamu kama Hadiyth zisemazo:

((KumtukanaMuislamu ni ufasiki na kumuua ni ukafiri)).

((Mambo mawili waliyonayo watu ni ukafiri kwao: Kutusi nasaba za watu, na kumlilia maiti kwa mayowe))pamoja na Hadiyth zote zenye kusema: ((Si katika sisi mwenye kufanya kadha…)).

Na hapa ni hivyo hivyo”.

 

Wenye kusema ni kafiri wamejibu:

 

“Haya hayaswihi kwa mambo haya yafuatayo: [Kitabu cha “Hukmu Taarikis Swalaat” cha Ibn ‘Uthaymiyn (uk. 14- pamoja na Tasnifu ya Sheikh Mamdouh) kwa mabadilisho madogo]

 

Kwanza: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameifanya Swalaah kuwa ni mpaka unaotenganisha kati ya ukafiri na Iymaan, na kati ya Waumini na makafiri. Mpaka hukipambanua kilichomo ndani yake na hukitenga na kingine. Na hapa, viwili vilivyomo ndani ya mpaka havifanani na wala haviingiliani.

 

Pili: Swalaah ni nguzo kati ya nguzo za Kiislamu, na kumwelezea asiyeswali kama ni kafiri kunahukumia kumtoa nje ya Uislamu. Sababu ni kuwa yeye amevunja nguzo kinyume na kumwita kafiri mtu aliyefanya kitendo kati ya vitendo vya kikafiri.

 

Tatu: Kuna Hadiyth nyinginezo zinazotutaarifu kwamba asiyeswali ni kafiri ukafiri unaomtoa nje ya Uislamu. Hivyo ni lazima kuuchukulia ukafiri huo kama ulivyo ili uendane sambamba na Hadiyth.

 

Nne: Ukafiri uliotajwa katika Hadiyth walizozitolea hoja hapa umekuja ukiwa bila ya alif na laam “Nakirah”, au kwa tamko la kitenzi. Na hii inaonyesha kuwa ni sehemu ya ukafiri, au ni ukafiri katika kitendo hiki. Ukafiri huu haumtoi mtu katika Uislamu. Ama kuhusu kuacha Swalaah, Rasuli ameutaja ukafiri kwa alif na laam kuonyesha kwamba anakusudia ukafiri wa kweli”.

 

(e) 

-12 Wameubebesha ukafiri wa asiyeswali uliotajwa kwenye Hadiyth kwa yule aliyeacha Swalaah kwa kupinga na kukataa

 

Wenye kusema ni kafiri wamejibu:

 

“Ubebeshaji huu una mawili ya kutahadhariwa: La kwanza ni kutengua wasifu alioutoa Rasuli na kuuwekea hukmu. Wasifu huu ni ukafiri na sio kupinga au kukataa. La pili ni kuuchukulia wasifu ambao Rasuli hakuufanya ni kiini au kitovu cha hukmu. Kwani kupinga na kukataa ulazima wa Swalaah tano, kunawajibisha ukafiri kwa yule ambaye haijashindikana kwake kulijua hilo sawasawa akiswali au asiswali. Hivyo basi, inabainika kwamba kuzibebesha Hadiyth kuwa zinamkufurisha mwenye kuacha Swalaah kwa kupinga ulazima wake tu, si sahihi. [Tasnifu ya Ibn ‘Uthaymiyn (uk. 12)]

 

(g)- 13 Wamesema: “Sisi hatujawahi kusikia katika enzi yoyote kwamba asiyeswali hakuoshwa, au kuswaliwa, au kuzikwa kwenye makaburi ya Waislamu, au kunyimwa mirathi, au kuachanishwa mke na mume kwa sababu ya kuacha Swalaah. Na kama angelikuwa ni kafiri, basi angefanyiwa hukmu hizi. [Al-Mughniy (2/446). Ametilia nguvu kutokufurishwa asiyeswali].

 

[1] WENYE KUSEMA NI KAFIRI

 

Hawa wametoa hoja kwa dalili zifuatazo:

 

(a) 

Hadiyth bayana zenye kumkufurisha asiyeswali. Kati ya Hadiyth hizo ni:

 

1- Hadiyth ya Jaabir kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Hakika kati ya mtu na kati ya shirki na ukafiri, ni kuacha Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imeshaelezwa nyuma]

 

2- Hadiyth ya Buraydah bin Al-Haswiyb aliyesema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((Ahadi iliyopo kati yetu na wao ni Swalaah, mwenye kuiacha basi amekufuru)). [Hadiyth Swahiyh: Imeshaelezwa nyuma].

 

Wenye kusema si kafiri wamejibu:

 

“Tumeshasema kuwa anayekusudiwa ni yule aliyeupinga na kuukataa ufaradhi wa Swalaah, au ukafiri unaokusudiwa hapa ni ule usiomtoa mtu katika Uislamu.”

 

3- Yaliyopokelewa Marfu’u toka kwa Anas:

((Mwenye kuacha Swalaah kwa kukusudia, basi amekufuru waziwazi)). [Hadiyth Dhwa’iy: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twabaraaniy katika Kitabu cha “Al-Awsatw”. Angalia Kitabu cha “Dhwa’iyful Jaami’i” (5530).

 

Wenye kusema si kafiri wamejibu:

 

“Hadiyth ni Dhwa’iyf, haifai kwa dalili. Na kama ni Swahiyh, tungeijibu kama tulivyoijibu Hadiyth iliyotangulia”.

 

4- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amesema:

((Vishikio vya Uislamu na amri za dini ni tatu, na juu yake ndiyo misingi ya Uislamu. Mwenye kuacha moja kati ya hayo, basi huyo ni kafiri ambaye damu yake ni halali: Kushuhudia kwamba hapana mungu isipokuwa Allaah, Swalaah za faradhi, na kufunga Ramadhwaan)). [Hadiyth Dhwa’iy: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Ya’alaa. Angalia Kitabu cha “Adh-Dhwa’iyfah” (94)]

 

Wenye kusema si kafiri wamejibu:

 

“Hadiyth ni Dhwa’iyf Marfu’u, haifai kutolewa dalili. Na kama itakuwa Swahiyh, ukafiri utakaochukuliwa ni ule usiomtoa mtu kwenye Uislamu. Ama neno lake “Damu yake ni halali”, kuuawa kwake kutachukuliwa kwamba ni adhabu ya kisharia “hadd” na si kwamba ni kafiri”.

 

(b)

Aayah na Hadiyth zinazofahamisha kwamba asiyeswali ni kafiri. Kati ya hizo ni:

 

5- Neno Lake Ta’alaa:

((فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ ۗ وَنُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ))

((Wakitubu, na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa Zakaat; basi ni ndugu zenu katika Dini. Na Tunafasili waziwazi Aayaat kwa watu wanaojua)). [At Tawbah (09: (11)]

 

Wamesema: “Ili upatikane udugu kati yetu na washirikina, ni lazima watubie shirki yao, wasimamishe Swalaah na watoe Zakaat. Na kama litakosekana mojawapo ya haya, basi udugu utakuwa haupo. Na udugu hauondoki kwa ufasiki au ukafiri mdogo usiomtoa mtu katika Uislamu, bali kwa kutoka nje ya Uislamu”.

 

Wenye kusema si kafiri wamejibu:

 

“Kwamba dalili walizozitoa katika kuthibitisha kwamba asiyeswali si kafiri zinatangulizwa juu ya Aayah. Aayah inabebeshwa juu ya ukamilifu wa udugu na si juu ya asili ya udugu. Kama tulivyomtoa mzuiaji wa Zakaat toka kwenye ukafiri kwa Hadiyth: ((Kisha ataiona njia yake; ima kuelekea Peponi au kuelekea Motoni)). [Hadiyth Swahiyh: Itakuja kamili mwanzoni mwa mlango wa Zakaat]. Na hii ni baada ya kutaja adhabu ya asiyetoa Zakaat.

 

6- Kauli Yake Ta’alaa:

((فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ وَلَا يُظْلَمُونَ شَيْئًا))

((Wakafuata baada yao waovu, walipoteza Swalaah na wakafuata matamanio; basi watakutana na adhabu motoni ● Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda mema; basi hao wataingia Jannah na wala hawatadhulumiwa chochote)). [ Maryam 19 (59 na 60) ]

Wamesema: “Neno Lake: ((Ila aliyetubia na akaamini)) ni dalili kwamba wakati wao walipoipoteza Swalaah na kufuata matamanio, hawakuwa ni Waumini”.

 

Wenye kusema si kafiri wamejibu:

 

“Makusudio ya Neno Lake Ta’alaa ((na akaamini)), ni ima alidumu katika iymaan yake, au aliingia katika iymaan kamili kwa kujikita katika Swalaah”.

 

7- Neno Lake Ta’alaa kuwazungumzia watu wa motoni:

((مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَر قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ وَلَمْ نَكُ نُطْعِمُ الْمِسْكِينَ وَكُنَّا نَخُوضُ مَعَ الْخَائِضِين وَكُنَّا نُكَذِّبُ بِيَوْمِ الدِّينِ حَتَّىٰ أَتَانَا الْيَقِينُ ))

(((Watawauliza): “Nini kilichokuingizeni motoni?”● Watasema: “Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali ● “Na wala hatukuwa tunalisha masikini ●“Na tulikuwa tunatumbukia kwenye upuuzi pamoja na wanaotumbukia upuuzini ● “Na tulikuwa tunaikadhibisha Siku ya malipo ● “Mpaka ikatufikia yakini (mauti))). [ Al Muddath-thir 74 (42-47) ]

 

Wamesema: “Ima kiwe kila kitendo katika vitendo hivi ndicho kilichowaingiza motoni na kuwafanya kuwa katika wahalifu, na ashirio liko wazi, au viwe ni vitendo vyote kiujumla, na hili bila shaka ni kwa ajili ya kuushadidia ukafiri wao na adhabu yao. Na kama si hivyo, basi kila kitendo kati ya hivyo kinahitajia adhabu, kwa kuwa haijuzu kujumuishwa kwenye adhabu kisicho na athari kwenye kile chenye adhabu yake peke”.

 

Wenye kusema si kafiri wamejibu:

 

“Aayah imeeleza kwamba wao wameingia Motoni na haikutaja muda wa kukaa wao humo au kama watakaa milele, hivyo basi haiwi ni hoja. Lakini hoja inabakia katika kumfanya asiyeswali kuwa katika wahalifu, na wahalifu katika Kitabu cha Allaah ni makafiri. Nasi tunauchukulia uhalifu huu kuwa ni ule usiomtoa mtu katika Uislamu!! Kinachotatiza uchukuliaji huu ni kwamba Allaah Ta’alaa Amewafanya Waumini kuwa mkabala na wahalifu:

((أَفَنَجْعَلُ الْمُسْلِمِينَ كَالْمُجْرِمِينَ))

(( Je, Tuwafanye Waislamu (watiifu) sawa kama wahalifu?)) [Al Qalam (68:35) ]

  

Hivyo maana haifai kuwa: ((Je, Tuwafanye Waislamu kama Waislamu?)), na hili liko wazi.

 

8- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Mwenye kuswali Swalaah yetu, akaelekea Qibla chetu na akala kichinjwa chetu, basi huyo ni Muislamu. Ni haki yake haki zetu, na ni juu yake yaliyo juu yetu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (391), At-Tirmidhiy (2608), na An-Nasaaiy (3966) kwa mfano wake].

 

9- Hadiyth ya Mihjan bin Al-Adra’i Al-Aslami ya kwamba alikuwa katika kikao na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam, halafu adhana ikaadhiniwa, Rasuli akanyanyuka kisha akarejea huku Mihjan akiwa amekaa vile vile. Rasuli akamuuliza: ((Kitu gani kinakuzuilia usiswali? Kwani wewe siMuislamu?)) Akajibu: “Hapana, lakini niliswali kwa watu wangu”. Rasuli Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam akamwambia: ((Ukija, swali pamoja na watu hata kama ulikwishaswali)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (857), Ahmad (15800), na Al-Bayhaqiy (2/300). Ndani yake kuna Busra bin Mihjan ambaye hajulikani kwa kauli yenye nguvu].

 

10- Hadiyth ya Mu’aadh Marfu’u: ((Mwenye kuacha Swalaah ya faradhi kwa kusudi, basi Dhima ya Allaah iko mbali naye)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Angalia Kitabu cha “Ta’adhiymu Qadris Swalaat” (921) nlichokifanyia uhakiki, chapa ya Al-‘Ilm]

 

Wamesema: “Lau kama angelikuwa anabakia kwenye Uislamu, basi angelikuwa na dhima ya Uislamu”.

 

Wenye kusema si kafiri wamezijibu Hadiyth hizi na zingine zenye maana hizi wakisema:

 

“Baada ya kuthibiti yanayofahamisha kwamba hatoki kwenye Uislamu, zitakuwa zinabebeshwa maana ya ukamilifu wa Uislamu na sio asili yake, kwa kukusanya kati ya dalili”.

 

(c) 

Hadiyth zinazotutaarifu kwamba damu ya asiyeswali ni halali. Kati ya hizo ni:

 

11- Hadiyth ya Abu Sa’iyd kuhusiana na kisa cha mtu aliyemwambia Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mche Allaah”. Kisa kinasema: “Khalid bin Al-Waliyd akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Je, niikate shingo yake?” Rasuli akasema: ((Hapana, pengine anaswali)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4351) na Muslim (1064)].

 

Wamesema: “Rasuli ameifanya Swalaah kuwa ni kizuizi cha kuuawa mtu huyo wakati Maswahaba walipoazimia kumuua walipoona uwezekano wa kuwa kwake ni kafiri”.

 

Wenye kusema si kafiri wamejibu:

 

“Inawezekana kuhalalika kumuua asiyeswali kuwa ni adhabu tu ya kisharia “hadd” na si kwa ajili ya ukafiri!!”

 

Wamejibiwa: “Wanaouliwa kwa adhabu ya kisharia “hadd” kwa Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni: ((Mzinifu aliyeoa, nafsi kwa nafsi, na mwenye kuiacha dini yake, mwenye kufarikiana na jamaa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6878) na Muslim (1676)].

 

Mwenye kuacha Swalaah si mzinifu, wala muuaji, bali anabakia kuwa ni mwenye kuiacha dini yake. Na kwa hili, si kila aliyesema kwamba asiyeswali hakufuru kasema kwamba anauliwa kama itakavyokuja kubainishwa.

 

(d)

Hadiyth zinazotutaarifu kwamba ni marufuku kuwapiga pande viongozi na kuwasusia isipokuwa kama hawakusimamisha Swalaah. Kati yake ni:

 

12- Hadiyth ya Ummu Salamah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtaletewa viongozi, kisha mtajua (mabaya yao) na mtakemea. Mwenye kuchukia basi ameokoka, na mwenye kukemea basi amesalimika, lakini mwenye kuridhia na kuwafuata (kaangamia) )). Wakasema: "Je, tuwapige vita?" Akasema: ((Hapana, madhali wanaswali)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1854), At-Tirmidhiy (2266) na Abu Daawuud (4760)].

 

Imethibiti kwamba haijuzu kuwapiga vita viongozi ila tu kama watakufuru ukafiri dhahiri shahiri kama katika Hadiyth ya 'Ubaadah inayoelezea kumpa kwao Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bay-'i. Hadiyth inasema: (( Na wala tusizozanie madaraka na watu wake, isipokuwa mkiona ukafiri dhahiri kwao wenye dalili toka kwa Allaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (7055) na Muslim (1709)].

 

Hivyo basi, imejulikana kwamba kuacha Swalaah ni ukafiri mkubwa wa dhahiri shahiri.

 

(e) 

Ukafiri wa asiyeswali ni kauli ya Jamhuri ya Maswahaba bali watu wengi wameelezea Ijma’a yao juu ya kauli hiyo

 

13- ‘Abdullaah bin Shuqayq amesema: "Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa hawaoni kitu chochote kuacha kwake katika amali ni ukafiri isipokuwa Swalaah". [Isnadi yake ni Swahiyh. Imeshaelezewa nyuma].

 

'Umar bin Al-Khattwaab amesema: "Naam, mwenye kuacha Swalaah hana fungu la Uislamu ". [Isnadi yake ni Swahiyh. Angalia Kitabu cha "Ta'adhiymu Qadris Swalaat" (923-931) nilichokifanyia uhakiki].

 

Ibn Mas-’oud amesema: "Asiyeswali hana dini". [Sanad yake ina ulaini. Angalia Kitabu cha "Ta'adhiymu Qadris Swalaat" (935-937) nilichokifanyia uhakiki].

 

Abud Dardaai amesema: "Hana Iymaan asiyeswali". [Sanad yake ni Hasan. Angalia Kitabu cha "Ta'adhiymu Qadris Swalaat" (945) nilichokifanyia uhakiki].

 

Wenye kusema si kafiri wamejibu:

 

"Kauli ya Jamhuri ya Maswahaba si hoja madhali Ijma’a yao haijafungika pamoja, na Ijma’a haidhaminiki. Kwa kuwa Ibn Hazm amenukuu kauli hii toka kwa 'Umar bin Al-Khattwaab, Mu'aadh, ‘Abdur Rahmaan bin 'Awf, Abu Hurayrah na wengineo na akasema baada ya hapo: "Sisi kutomjua Swahaba yeyote katika hawa aliyepingana na hili hakuonyeshi kwamba hakuna wengine waliopingana nalo!!"

 

Kundi lenye nguvu zaidi

 

“Baada ya kutaja sehemu ya dalili za pande zote mbili pamoja na malumbano yao, bila shaka mwenye kuyatizama hayo, ataona kwamba kwa mujibu wa dalili zilizotolewa na kila kundi katika suala hili, inakuwa si wepesi kukata ni nani aliye sawa na ni nani aliyekosa. Aidha, kutilia kwangu nguvu kundi fulani, hakuizidishii kauli yoyote nguvu, lakini lenye nguvu kwa mujibu wa mwono wangu kwa upande wa usuwl ni kusema: "Asiyeswali ni kafiri, na hasa hasa kama atatubishwa na kiongozi. Kwa kuwa mtu anayeikiri Swalaah moyoni mwake, na anaitakidi kwamba ni wajibu, hawezi kuendelea kushikilia msimamo wa kukataa kuswali mpaka auawe. Haiingii akilini aitwe mbele ya hadhira huku akiuona upanga unang'aa juu ya kichwa chake, akifungwa kamba na akitiwa kitambaa machoni, halafu aambiwe: Swali, la sivyo tutakuua, kisha aseme: Niueni! Mimi sitoswali kamwe, kisha mtu huyo awe baada ya yote hayo niMuislamu!!". [Angalia Kitabu cha "Majmu'u Al-Fataawaa (22/48, 49) na "As-Swalaat" cha Ibn Al-Qayyim (uk.41)]

 

·       

Tanbihi

 

Makusudio ya “Taariku Swalaah” anayehukumiwa kuwa ni kafiri, ni yule asiye swali kamwe na anaendelea kung'ang'ania msimamo wake wa kuacha Swalaah na kudai kwamba anaamini kwamba ni wajibu. Ama watu wengi ambao mara wanaswali mara wanaacha, hawa ni wale wasioihifadhi, na hawa wako ndani ya wigo wa makamio, lakini hawahukumiwi kama ni makafiri. [Angalia Kitabu cha "Majmu'u Al-Fataawaa (22/ 49)]

 

Kiini cha ukufurishaji katika kuacha Swalaah si tu kuacha, bali kiini chake ni kuiacha kabisa nzima nzima na kuigomea katu katu, au kuiacha kwa picha yake nzima kiasi cha kustahiki asiyeswali kuambiwa kwamba ameipoteza na kuipa mgongo. Kiini hiki ndicho kile kinachofahamika katika Neno Lake Ta’alaa:.

((فَلَا صَدَّقَ وَلَا صَلَّىٰ • وَلَـٰكِن كَذَّبَ وَتَوَلَّى))

((Kwani hakusadiki (Qur-aan na Rasuli) na wala hakuswali •Lakini alikadhibisha na akakengeuka)). [Al Qiyaamah (31 na 32) ] … Hivyo ukengeukaji umefanywa kuwa ndio kitovu cha ukafiri. Ni maarufu kwamba si kila anayeacha Swalaah au baadhi ya Swalaah anakuwa ni mwenye kuipa mgongo Swalaah moja kwa moja. Allaah Ndie Mjuzi Zaidi. [Kitabu cha "Dhwawaabitut Takfiyr” cha Al-Qarniy (uk. 159-161) kwa mabadilisho madogo].

 

 

Share