003-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Hukmu Za Kidunia Kwa Asiyeswali

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

003-Hukmu Za Kidunia Kwa Asiyeswali

 

 

Tuliyoyaeleza ni hukmu za aakhirah kwa asiyeswali. Ama kwa hapa duniani, hukmu zake ni hizi zifuatazo:

 

[1] Kwa wenye kusema ni fasiki na si kafiri

 

Kwa mujibu wa hawa, asiyeswali ni fasiki muasi, naye ni sawa na Waislamu wengine wafanyaji maasi; ni haki yake haki zao, na ni juu yake yaliyo juu yao. Lakini wamekhitalifiana kwa kauli mbili kuhusu nini kiongozi amfanye:

 

(a) 

Atauawa kama adhabu ya kisharia “haddi”.

Maalik na Ash-Shaafi’iy wanasema kwamba atatakwa aswali endapo kama wakati utakuwa mfinyu, na ataonywa kwamba atauawa kama ataichelewesha Swalaah wakati wake ukapita. Na kama ataichelewesha mpaka wakati wake ukatoka, italazimu auawe, na hauawi mpaka atubishwe wakati huo huo. Na kama atashikilia msimamo wake, basi atauawa kama ni adhabu ya kisharia. Wengine wamesema kwamba atapewa muda wa siku tatu.

 

Baadhi ya Mahanbali wanaosema si kafiri, wanaona kwamba ataitwa aambiwe: “Swali, na kama huswali tutakuua”. Akiswali ataachiliwa, na kama akikataa ni lazima auawe. Na hauawi ila baada ya kuhabisiwa siku tatu ambapo kila wakati wa Swalaah ataitwa ili aswali. Akiswali ataachwa, na kama hakuswali atauawa kama adhabu ya kisharia. Halafu wamekhitalifiana namna ya kumuua. Jamhuri yao wamesema kwamba atapigwa upanga wa shingo.

Na wote hawa wamekubaliana kwamba baada ya kuuawa ataoshwa, ataswaliwa, atazikwa katika makaburi ya Waislamu na atarithiwa.

 

(b) 

Hatouawa bali atafanyiwa izara na atawekwa kifungoni mpaka afe au atubie

Ni rai yenye nguvu ya Az-Zuhriy, Ibn Al-Musayyib, ‘Umar bin ‘Abdul Aziyz, Abu Haniyfah, Daawuud Adh-Dhwaahiriy, Al-Muzniy na Ibn Hazm. Hawa wametoa dalili ya Hadiyth isemayo:

((Si halali damu ya Muislamu anayeshuhudia kwamba hapana mungu isipokuwa Allaah na kwamba mimi ni Rasuli wa Allaah isipokuwa kwa moja ya matatu….)) Hadiyth hii tushaieleza nyuma na Hadiyth zenye maana hii kama ((Nimeamriwa niwapige vita watu mpaka waseme “Laailaaha illa Allaah”, wakisema hilo watazihifadhi damu zao na mali zao kutokana nami ila kwa haki zake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (25) na Muslim (22)].

 

[2] Kwa wenye kusema ni kafiri

 

Atafanyiwa hukmu zote za kafiri murtadi. Kati ya hizo ni: [Tasnifu ya Ibn ‘Uthaymiyn (uk. 20-24) pamoja na Tasnifu ya Sheikh Mamdouh]

 

1- Uwalii (usimamizi) wake utapomoka, hawezi tena kuwa walii kwa jambo lililoshurutishwa awe walii kama kumwozesha binti yake au kuwasimamia watoto wake wadogo na mfano wa hivyo.

 

2- Harithi wala harithiwi kwa kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Muislamu hamrithi kafiri, wala kafiri hamrithi Muislamu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4283) na Muslim (1614)].

 

3- Ni marufuku kuingia Makkah.

 

4- Alichochinja hakifai kuliwa kinyume naMuislamu na Ahlul Kitaab.

 

5- Akifa haswaliwi wala haombewi du’aa baada ya kufa.

 

6- Haruhusiwi kuoa mwanamke wa Kiislamu kwa kuwa yeye ni kafiri kama ilivyo marufuku kwa mwanamume wa Kiislamu kumwoa mwanamke wa kikafiri. Na kwa mujibu wa maimamu wanne, ndoa huvunjika endapo kama mume au mke ataritadi.

 

Kiongozi atamtaka asiyeswali aswali, na kama hatoswali atauawa. Kama atatubia na kuswali basi ataachiwa. Na kama hatofanya hivyo, basi atamuua kwa hukmu ya kuritadi. Na hili si kwa mtu yeyote, bali ni kwa kiongozi tu. Hili ni muhimu watu walijue!!

 

 

Share