007-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Kulipa Swalaah Zilizopita

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

007-Kulipa Swalaah Zilizopita 

 

 

Swalaah iliyopita, ni Swalaah ambayo wakati wake maalum umetoka. Tumefanya uhakiki na kubaini kwamba Swalaah hazilipwi isipokuwa zile ambazo wakati wake ulitoka kwa udhuru kinyume na Jamhuri ya Maulamaa wanaosema kwamba ‘ibaadah zenye mpaka maalumu wa wakati, hupita kwa kupita wakati wake uliowekwa bila kuifanya, na ‘ibaadah hizo humganda mtu mpaka zitakapolipwa bila kutofautisha kati ya mwenye udhuru na asiye na udhuru.

 

·       

Je, Ni Lazima Kuilipa Haraka Swalaah Iliyopita?

 

Mtu ambaye Swalaah imempita bila ya udhuru wa kisharia, ni lazima ailipe haraka kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na aliyelala na mwenye kusahau: ((Aiswali anapoikumbuka, hakuna kafara yake isipokuwa hilo)). Hili ni agizo, nalo ni la wajibu wa hapo kwa papo. Makusudio ya hapo kwa papo ni uharaka wa kawaida usio wa kuvuta sana. Hii ni kauli ya wafuasi wa Maalik na Hanbali. [Ash-Sharhu As-Swaghiyr (1/3665) na Kash-Shaaful Qina’a (1/260)]

 

Wafuasi wa Hanafi na Shaafi’i wanaona kwamba ni vizuri kufanya haraka, na inajuzu pia kuchelewesha kidogo katika kulipa. [Haashiyatu Ibn ‘Aabidiyn (2/74) na Al-Majmu’u (3/69)]

Wanatoa dalili ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba wake walipoamka usingizini baada ya jua kuchomoza, hawakuswali ila baada ya kuhamia mahala pengine!

 

Wanajibiwa: “Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilitolea sababu hilo kwa kusema: ((Kila mtu akamate kichwa cha mnyama wake, kwani hapa ni mashukio ambayo shaytwaan alitujia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (680) na An Nasaaiy (1/80) toka kwa Abu Hurayrah].

 

Kizuizi cha kuswali ni kuwa mahala hapo shaytwaan alikuwepo, kwa hivyo basi, Hadiyth haionyeshi kutoa ruhusa ya kuvuta vuta wakati katika kulipa. Na juu ya msingi wa hili, ikiwa mtu ataamka baada ya jua kuchomoza, haitojuzu kwake arudi tena kulala mpaka aswali kwanza, kwani huo ndio wakati wake. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

·       

Mpangilio Wa Kuzilipa Swalaah Zilizopita

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah kwamba ‘Umar bin Al-Khattwaab alikuja siku ya Khandaq baada ya kuchwa jua. Akaanza kuwashutumu makafiri wa Kikureshi na kusema: “Ewe Rasuli wa Allaah! Sikukurubia kuswali Alasiri mpaka jua likawa limekurubia kuzama”. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Wal-Lahi sikuiswali)). Akatawadha, nasi tukatawadha, akaswali Alasiri baada ya kuchwa jua, kisha akaswali Magharibi”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (598) na Muslim (209)].

 

Imepokelewa na Abu Sa’iyd akisema: “Tulizuilika tusiweze kuswali Siku ya Khandaq mpaka ilipoingia sehemu ya usiku baada ya Magharibi, Allaah Alitutosha. Na hiyo ni Kauli Yake Ta’alaa:

((وَرَدَّ اللَّـهُ الَّذِينَ كَفَرُوا بِغَيْظِهِمْ لَمْ يَنَالُوا خَيْرًا ۚ وَكَفَى اللَّـهُ الْمُؤْمِنِينَ الْقِتَالَ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ قَوِيًّا عَزِيزًا ))

 Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwita Bilaal, akaqimu Adhuhuri akaiswali, tena aliiswali kwa utuvu na umakini kama anavyokuwa akiiswali katika wakati wake. Kisha akamwamuru aqimu Alasiri akaiswali, tena aliiswali kwa utuvu na umakini kama anavyokuwa akiiswali katika wakati wake. Kisha akamwamuru aqimu Magharibi akaiswali hivyo hivyo. Na hili lilikuwa kabla Allaah Ta’alaa Hajateremsha hukmu ya Swalaah ya vita: فإن خفتم فرجالا أو ركبانا “. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1/297), Ahmad (3/25), Ibn Khuzaymah (996) na Abu Ya’alaa (1296)].

 

Katika Hadiyth hizi mbili, tunaona kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizilipa Swalaah zilizompita kimpangilio. Na hapa ndipo Jamhuri ya Maulamaaikasema kwamba ni lazima kuzipangilia Swalaah zilizompita mtu ingawa wamekhitalifiana kati yao kuhusiana na chambuzi zake. [Al-Badaai-’i (1/131), Sharhu As-Swaghiyr (1/367), Al-Mughniy (1/607) na Naylul Awtwaar (2/36)]

 

Wametolea dalili kwa kitendo cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwamba wakati wa Swalaah ya kulipwa ni mfinyu zaidi kuliko wakati wa Swalaah iliyopo, na kwa hivyo ni wajibu kuitanguliza ile iliyofinyika.

 

Ash-Shaafi’iy anasema: [Rawdhwat At-Twaalibiyna (1/269)]

 “ Ni Sunnah kufanya hivyo na si lazima, kwa kuwa kitendo alichokifanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) peke yake bila na wengine, hakionyeshi kwamba ni lazima”.

 

·       

Vinavyoondosha Mpangilio

 

1- Ufinyu wa wakati wa Swalaah iliyopo

[Al-Binaayah (2/628), Al-Mughniy (1/610), Al-Inswaaf (1/444), Al-Kharshiy (1/301) na Al-Awsatw (2/415)]

 

Ufinyu hupomosha mpangilio, kwa kuwa ufaradhi wa wakati uliopo ni muhimu zaidi kuliko ufaradhi wa kupangilia. Mtu ataswali Swalaah iliyopo kisha atailipa iliyompita. Na hii ni kauli ya Abu Haniyfah na riwaya toka kwa Ahmad pamoja na Ibn Al-Musayyib, Al-Hasan, Al-Awzaaiy, Ath-Thawriy na Is-Haaq. Ama Ash-Shaafi’iy, yeye anasema kuwa hakuna kabisa wajibu wa kupangilia kama ilivyotangulia.

 

Ama wafuasi wa Maalik (na riwaya toka kwa Ahmad, ‘Atwaa na Al-Layth), hawa wanasema kwamba mtu atafanya mpangilio hata kama wakati wa Swalaah iliyopo utatoka!!

 

Ninasema: “Kauli ya kwanza ina mwelekeo zaidi na hasa hasa pakizingatiwa kuwa suala la wajibu wa kupangilia lina mvutano.”

 

2- Kupitwa na Jamaa

 

Mtu ambaye kwa mfano amepitwa na Adhuhuri, halafu akachelea kwamba kama atailipa ataikosa jamaa ya Alasiri, basi hapo mpangilio utaondoka na ataswali Alasiri kwa jamaa, halafu atailipa Adhuhuri baada yake. Hii ni riwaya toka kwa Ahmad na ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. [Al-Inswaaf (1/444-445)]

 

Aidha, anaweza kujiunga nao katika Jamaa ya Alasiri kwa niya ya Adhuhuri – kwa mujibu wa fatwa inayojuzisha kutofautiana niya ya maamuma na ya imamu, na hili litakuja kuelezewa – kisha aswali Alasiri.  La kwanza linaweza kuwa na nguvu zaidi, na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

3- Kupitwa na Swalaah ambayo hawezi kuilipa peke yake kama Swalaah ya Ijumaa.

 

Kama atakumbuka kwamba ana Swalaah iliyompita baada ya kuqimiwa Swalaah ya Ijumaa, basi atatanguliza kwanza Ijumaa kwa kuwa hatoweza kuilipa na wakati wake humalizika kwa kumalizika Swalaah. Hii ni riwaya toka kwa Ahmad. [As-Saabiq (1/444) na Al-Mumti’i (2/141)]

 

4- Kusahau.

 

Kama ataswali Swalaah zilizompita bila mpangilio kwa kusahau, basi hapana kitu kutokana na ujumuishi wa Kauli Yake Ta’alaa:

 

((لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ ۗ رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلْنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا بِهِ ۖ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۚ أَنتَ مَوْلَانَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ )) 

(( Allaah Hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake. Itapata (thawabu) iliyoyachuma, na ni dhidi yake (kwa maovu) iliyojichumia. “Rabb wetu Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Rabb wetu, Usitubebeshe mzigo kama Ulivyoubebesha juu ya wale waliokuwa kabla yetu. Rabb wetu, Usitutwike tusiyoyaweza, na Tusamehe, na Tughufurie na Turehemu, Wewe ni Mola Mlinzi wetu, basi Tunusuru dhidi ya watu makafiri)). [Al-Baqarah (2:286)]

 

Katika Hadiyth, Allaah Ta’alaa Alisema: “Naam”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (125)]

 

Na katika riwaya nyingine: “Nishafanya”. Na pia kutokana na Hadiyth isemayo:

((Hakika Allaah Ameusamehe umati wangu walilolikosea, walilolisahau na walilolazimishwa)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (2045) na wengineo. Angalia Al-Irwaa (82)].

 

Hili ndilo lililopo katika madhehebu ya Hanafi na Hanbali kinyume na Maalik na riwaya toka kwa Ahmad. [Al-Binaayah (2/629), Al-Mughniy (1/609), Al-Kharshiy (1/301)]

 

5- Kutokujua

 

Asiyejua wajibu wa kupangilia akaswali bila mpangilio, basi hakuna kitu juu yake, kwa kuwa kutokujua ni ndugu ya kusahau katika Kitabu cha Allaah na Sunnah ya Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hii ni riwaya toka kwa Ahmad na chaguo la Sheikh wa Uislamu, na Mahanafi pia. [Al-Inswaaf (1/445) na Al-Binaayah (2/629)]

 

·       

Kuilipa Swalaah Iliyopita Kwa Umbo Lake Lilivyo

 

Wafuasi wa Hanafi na Maalik (na kauli toka kwa Ash-Shaafi’iy), Abu Thawr na Ibn Al-Mundhirwanaona kwamba umbo la Swalaah yenye kulipwa linafungamanishwa na wakati wake ule ule wa asili ili ulipaji huo uendane na utendaji wake. [Majma’a Al-Anhur (1/164), Ash-Sharhu As-Swaghiyr (1/365), Rawdhwat At-Twaalibiyna (1/269) na Ikhtilaaf Al-‘Ulamaa (uk wa 60)]

 

Aliyesahau Swalaah ya ‘Ishaa (ambayo husomwa kwa sauti) kisha akaikumbuka mchana, basi ataisoma kwa sauti kama ilivyo, na hivyo hivyo kwa Swalaah zinazosomwa kimya kimya. Wanatolea dalili kwa Hadiyth ya Abu Sa’iyd iliyotangulia kuhusiana na kisa cha Khandaq anaposema: “Akaqimu Adhuhuri akaiswali, tena aliiswali kwa utuvu na umakini kama alivyokuwa akiiswali katika wakati wake”. Hadiyth. Na hii ilikuwa ni baada ya Magharibi.

Ama Mahanbali na Mashaafi’i, wanaona kwamba umbo hufungamanishwa na wakati ule wa kuilipa!!

 

Na ikiwa mtu alisahau kuswali akiwa mjini kwake kisha akakumbuka akiwa safarini, basi ataiswali kamili kama ilivyo bila kuipunguza juu ya rai ya kundi la kwanza. Ash-Shaafi’iy na Ahmad wamekubaliana nao juu ya hililakini wamekataa kinyume cha hivyo wakisema: “Akiisahau Swalaah ya safari kisha akaikumbuka mjini kwake baada ya kurudi, basi ataiswali kamili. [Al-Ummu (1/161), Al-Majmu’u (4/249), Al-Mughniy (1/570) na Ikhtilaaful ‘Ulamaa (uk. 60)]

 

·       

Kuzilipa Sunnah Za Rawaatib

 

Inaruhusiwa kuzilipa Sunnah za rawaatib kama zimempita mtu kwa mujibu wa kauli sahihi ya Maulamaa. Limesimuliwa hili toka kwa Ibn ‘Umar, na ni kauli yenye nguvu ya Al-Awzaa’iy, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-Haaq, Muhammad bin Al-Hasan, Al-Mazniy na wengineo. [Rawdhwat At-Twaalibiyna (1/337), Al-Inswaaf (2/178). Angalia kauli nyinginezo kwenye Kitabu cha Naylul Awtwaar]

 

Hili litakuja kuelezewa kichambuzi katika mlango wa “Swalaah za Sunnah” Insha-Allaah.

 

·       

Adhana Na Iqaamah, Na Kuswali Kwa Jamaa Katika Swalaah Ya Kulipa

 

Aliyepitwa na Swalaah na akataka kuilipa, anaruhusiwa kuadhini na kuqimu. Pia waliopitwa na jamaa, wanaruhusiwa kuilipa kwa Jamaa. Na hii ni kutokana na Hadiyth ya Abu Qataadah kuhusiana na kisa cha kulala Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba wake wakapitwa na Swalaah ya Alfajiri mpaka jua likachomoza. Katika Hadiyth hiyo, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Bilaal: ((Simama uwaadhinie watu Swalaah)). Jua lilipochomoza na pakapambauka sawasawa, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaswalisha. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (595), Abu Daawuud (439) na An-Nasaaiy (2/105)]

 

Na katika tamshi la Hadiyth ya Ibn Mas-’oud: “Akamwamuru Bilaal akaadhini, kisha akaqimu na Rasuli akatuswalisha”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (1/450) na Ibn Hibaan (1580)].

 

Na hii ndiyo kauli yenye nguvu ya Jamhuri ya Maulamaa.

 

 

Share