006-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Masuala Yanayohusiana Na Nyakati Za Swalaah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

006-Masuala Yanayohusiana Na Nyakati Za Swalaah 

 

Alhidaaya.com

 

 

[1] Wakati Ni Faradhi Muhimu Sana Kati Ya Faradhi Za Swalaah

 

- Kuiswali Swalaah katika wakati wake ni faradhi. Wakati ni faradhi muhimu zaidi kati ya faradhi za Swalaah. Allaah Ta’alaa Anasema:

((فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ ۚ فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا ))

((Mtakapomaliza Swalaah, mdhukuruni Allaah msimamapo, na mkaapo na mnapolala ubavuni mwenu Mtakapopata utulivu, simamisheni Swalaah (kama desturi), hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu)).

[An-Nisaa (4:103)]

 

Na kwa ajili hii, haijuzu kuichelewesha Swalaah mpaka wakati wake ukapita hata kama mtu ana janaba, au hadathi, au najsi nguoni, au hata kama hana cha kujisitiria uchi, au kwa dharura nyingineyo. Mtu (kulingana na rai sahihi) ataswali wakati huo kwa mujibu wa hali ilivyo. [Ibn Taymiyah kalikhitari hili katika Al-Fataawaa (22/30) na akalinasibisha kwa Jamhuri ya Maulamaa. Angalia Al-Furu’u (1/293), Al-Ummu (1/79) na Al-Majmu’u (1/182)]

 

- Allaah Ta’alaa Amewasifu wenye kuzihifadhi nyakati za Swalaah Akisema:

((الَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَاتِهِمْ دَائِمُون))

((Ambao wenye kudumisha Swalaah zao)). [Al-Ma’aarij (70:23)]

 

((وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَاتِهِمْ يُحَافِظُون))

(( Na ambao kwenye Swalaah zao ni wenye kuhifadhi)). [Al-Ma’aarij (70:23)]

 

Ibn Mas-’oud kasema: “Hilo ni katika nyakati zake”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Al-Mundhir katika Al-Awsatw (2/386) na At-Twabaraaniy kama ilivyo katika Al-Majma’a (7/129)].

 

Allaah Ta’alaa Amekufanya kuiswali Swalaah katika wakati wake ni katika amali bora zaidi na zinazopendeza zaidi Kwake. Imepokelewa na Ibn Mas-’oud (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Nilimuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Ni amali ipi inayopendeza zaidi kwa Allaah? (Katika riwaya nyingine: Iliyo bora zaidi) Akasema: ((Ni Swalaah katika wakati wake)). Nikauliza: Kisha ipi? Akasema: ((Kuwatendea wema wazazi wawili)). Nikauliza: Kisha ipi? Akasema: ((Ni Jihaad katika Njia ya Allaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (527) na Muslim (85)].

 

- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametahadharisha kuwatii viongozi katika suala la kuichelewesha Swalaah (ukapita wakati wake wa khiyari). Imepokelewa na Abu Dharri akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia: ((Utafanya nini ikiwa viongozi wako wanaichelewesha Swalaah na wakati wake?)) Nikamwambia: Unaniamuru nini? Akasema: ((Iswali Swalaah katika wakati wake, na kama utaipata pamoja nao basi swali nao, nayo kwako itakuwa Sunnah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (648) na At-Tirmidhiy (176). Angalia Taadhiymu Qadri As-Swalaat (1007) nilichokifanyia uhakiki].

 

- Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu Anhu amebainisha kwamba kuichelewesha Swalaah ukapita wakati wake wa khiyari (bila ya udhuru) kunakwenda kinyume na Hidaayah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kunaipoteza Swalaah. Imepokelewa toka kwa Az-Zuhriy akisema: “Niliingia kwa Anas bin Maalik huko Damascus nikamkuta analia. Nikamuuliza: “Nini kinachokuliza?” Akasema: “Sikijui kitu katika nilivyovipata (katika enzi ya Rasuli) isipokuwa Swalaah hii, na Swalaah hii hakika imepotezwa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (530)].

 

Ninasema: “Ni stahikivu mno kwa mtu mwenye kujithamini, awe anachunga nyakati za Swalaah kwa kuziswali mwanzo wa nyakati zake (isipokuwa Swalaah ya “Ishaa kama hakuna uzito) kwa kutekeleza Kauli Yake Ta’alaa:

(( وَلِكُلٍّ وِجْهَةٌ هُوَ مُوَلِّيهَا ۖ فَاسْتَبِقُوا الْخَيْرَاتِ ۚ أَيْنَ مَا تَكُونُوا يَأْتِ بِكُمُ اللَّـهُ جَمِيعًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ))

(( Na kila mmoja ana upande wa kuuelekea. Basi shindaneni kwenye mambo ya khayr. Popote mtakapokuwa Allaah Atakuleteni nyote pamoja (Qiyaamah). Hakika Allaah juu ya kila kitu ni Muweza)). [Al-Baqarah (2:148)]

 

((أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ))

(( Hao wanakimbilia katika mambo ya kheri; na wao ndio wenye kuyatanguliza)). [Al-Muuminuwn (23:61)]

  

Na kwa ajili pia ya kuifuata Sunnah ya Rasuli wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wallaahu Al-Musta’anu”.

 

[2] Ni Kwa Nguzo Gani Mtu Huipata Swalaah Katika Wakati Wake?

 

Maulamaa wana kauli mbili kuhusiana na suala hili:

 

Ya kwanza:

 

Huipata kwa takbiyr ya kuhirimia. Hii ni rai yenye nguvu ya Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Al-Majmu’u (3/49), Al-Awsatw (2/348), na Al-Ikliyl (1/304)]

Hoja yao ni:

 

1- Kuipata sehemu ya Swalaah (nayo ni takbiyr ya kuhirimia) ni kama kuipata yote kwa kuwa Swalaah haigawanyiki. [Al-Mubdi’i (1/353). Lakini kwa mujibu wa Abu Haniyfah, Swalaah yake inabatilika kama jua litachomoza hata kama imebakia rakaa moja katika Swalaah ya Alfajiri!! Na hii ni kinyume na dalili]

 

2- Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuipata sijdah katika Alasiri kabla jua halijazama, au Alfajiri kabla jua halijachomoza, basi ameipata Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (609) na Ahmad (6/78)].

 

Wamesema: “Sijdah ni sehemu ya Swalaah, nayo ni sawa kabisa na takbiyr ya kuhirimia”.

 

Ya pili:

 

Huipata kwa kuipata rakaa kamili iliyo ndani ya wakati. Ni rai ya Maalik na riwaya toka kwa Ahmad. Sheikh wa Uislamu ameikhitari, nayo ndiyo yenye nguvu zaidi kutokana na haya yafuatayo: [Mawaahibul Jaliyl (1/408), Ad-Dusuwqiy (1/182) na Al-Inswaaf (1/439)]

 

1- Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuipata rakaa katika Swalaah, basi ameipata Swalaah nzima)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (580) na Muslim (607)]

Na neno: “Mwenye kuipata” ni sentensi sharti, na maana yake ni kuwa mwenye kupata chini ya rakaa basi hakuipata, kwani kuipata kunafungamana na rakaa kamili, na kutofungamanisha na rakaa kamili, ni sawa na kutengua yaliyosemwa na Rasuli. Na kufungamanisha na takbiyr ni sawa na kufuata lile ambalo Rasuli amelitengua.

 

2- Ama Hadiyth isemayo: ((Mwenye kuipata sijdah..)), makusudio yake ni rakaa kamili. Ni katika mlango wa kuita sehemu ya kitu kwa kukikusudia chenyewe kizima. Ndio maana wakati mwingine anasema: ((Mwenye kuipata rakaa)), na wakati mwingine ((Mwenye kuipata sijdah..)), na haya yote yanaonyesha kwamba makusudio ni mamoja, nayo ni rakaa kamili. Ibn ‘Umar amesema: “Nilihifadhi toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sijdah mbili kabla ya Adhuhuri na sijdah mbili baada yake”, yaani rakaa mbili. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

·       

Mwenye Kupata Sehemu Ya Wakati Kisha Akapata Udhuru

 

Udhuru ukitokea ghafla baada ya wakati kuingia kama wendawazimu, kupotewa fahamu, hedhi, nifasi na kadhalika, basi hapa kutakuwa na hali mbili:

 

1- Wakati wa Swalaah uwe umepita kwa kitambo cha kuweza kuswali chini ya rakaa moja kamili ya faradhi. Hapa haitomlazimu kuilipa baada ya kuondoka udhuru.[Al-Majmu’u (3/71)]

 

2- Wakati wa Swalaah uwe umepita kwa kitambo cha kuweza kuswali rakaa kamili. Kuna kauli mbili kuhusiana na ulazima wa kuilipa zilizoelezewa katika mlango wa hedhi. [Angalia yaliyotangulia. (1/209)]

 

Sheikh wa Uislamu anaona kwamba haimlazimu kulipa, kwa kuwa udhuru umemtokea katika wakati ambapo anaruhusiwa kuichelewesha Swalaah naye si mwenye kukiuka mipaka, na kwa kuwa pia haikuripotiwa na yeyote kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru mwanamke yeyote kuilipa Swalaah baada ya kupata hedhi katika wakati wake, na hili linatokea sana. Hii ndiyo hoja yenye nguvu ingawa kuilipa ni akiba zaidi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

[3] Nyudhuru Za Kuichelewesha Swalaah Na Wakati Wake

 

1,2-  Ni kulala na kusahau:

 

Mtu aliyelala au aliyesahau mpaka wakati wa Swalaah ukapita, basi huyo anasameheka. Atalazimika kuiswali Swalaah hiyo iliyompita anapoamka au anapokumbuka kutokana na Hadiyth ya Anas bin Maalik kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuisahau Swalaah, basi aiswali anapokumbuka, hakuna kifutio chake isipokuwa hilo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (597) na Muslim (314-316)].

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa safarini pamoja na Maswahaba wake walilala na hakikuwaamsha isipokuwa joto la jua baada ya kuchomoza. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: ((Hakuna taksiri katika kulala, bali taksiri ni kwa yule ambaye hakuiswali Swalaah mpaka ukaingia wakati wa Swalaah nyingine. Mwenye kufanya hilo, basi aiswali anapozindukana, na inapokuja kesho aiswali katika wakati wake)). [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa nyuma kidogo].

 

Kuiswali Swalaah wakati mtu anapoamka au anapoikumbuka, kiuhakika si kama anailipa bali anaiswali kawaida kwa kuwa huo ndio wakati alionao na hakuna wakati mwingine zaidi. [Angalia: As-Saylul Jarraar (1/188)]

 

·       

Tanbihi:

 

Kauli za Maulamaa zimegongana kuhusiana na maana ya neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((na inapokuja kesho aiswali katika wakati wake)) katika Hadiyth ya Abu Qataadah iliyotangulia. Lililo sahihi zaidi ambalo wahakiki wamelikubali ni yale aliyoyaeleza An Nawawiy akisema kwamba maana yake ni kuwa Swalaah ikimpita mtu akailipa, basi wakati wake haubadiliki; utageuka kuwa mustakbali lakini unabakia kama ulivyo. Na inapokuja kesho yake, ataiswali Swalaah ya kesho katika wakati wake uliozoeleka, na hii haimaanishi kwamba anailipa Swalaah iliyompita mara mbili, yaani mara moja hapo hapo na mara nyingine kesho yake. [Sharhu Muslim cha An Nawawiy (2/988)]

 

3- Kulazimishwa:

 

Mwenye kulazimishwa asiswali kabisa, au hata kuswali kwa kuashiria, au akalazimishwa kutenda yaliyo kinyume na Swalaah, basi huyo anasameheka. [Al-Majmu’u (3/67), Haashiyat  Ad-Dusuwqiy (1/200) na Al-Ashbaahu wa An-Nadhwaair (208)]

 (Atazilipa udhuru unapoondoka). Na ikiwa ataweza kuashiria kwa kichwa, basi itampasa aswali kwa wakati na hatokuja kulipa kwa mujibu wa kauli sahihi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

4- Kukusanya Swalaah mbili kwa anayeruhusiwa kukusanya:

 

Mwenye kukusanya Swalaah mbili kwa jam’u ya kuchelewesha, anakuwa anaiswali Swalaah ya kwanza katika wakati wa Swalaah ya pili. Naye kiuhalisia haambiwi kwamba ameichelewesha wakati wake ukapita, isipokuwa kidhahiri inaonekana hivyo. Katika hali hii ya kukusanya, wakati wa Swalaah zote mbili unakuwa ni mmoja. Vipengele vya hukmu za kukusanya kati ya Swalaah mbili vitakuja kuelezewa mbeleni InshaAllaah.

 

5- Kizaazaa cha vita:

 

Ikiwa hofu imetanda kiasi cha mtu kutoweza kuswali kwa njia yoyote ile hata kwa moyo wake, basi habebeshwi kosa endapo kama wakati wa Swalaah utamtoka  (kwa mujibu wa moja ya kauli mbili za Maulamaa). Kwa kuwa ikiwa ataswali wakati huo, hatoweza kukijua anachokisoma au anachokifanya na hususan wakati vita vinapoumana. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliichelewesha Swalaah ya Alasiri katika vita vya Khandaq mpaka jua likazama. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (598) na Muslim (631). Angalia Ash-Sharhul Mumti’i (2/23) na Naylul Awtwaar (2/36)].

 

Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Vita vilipamba moto Alfajiri ya kukombolewa Tustar. Hawakuswali isipokuwa baada ya jua kuchomoza”. [Ibn Hazm ameiweka katika Al Muhallaa (2/244) na kaitilia nguvu kwa riwaya ya Mak-huol toka kwa Anas. Amesema: “Mak-houl hakumwahi Anas”. Ninasema: “Abu Haatim Ar Raaziy kama ilivyo katika Al-Maraasiyl (1/121) na At-Tirmidhiy kama ilivyo kwenye At-Tahdhiyb (1/290), amethibitisha kwa mwanawe kwamba Mak-houl ameisikia toka kwa Anas. Na kama katika Isnadi hakuna isipokuwa huyu, basi ni Swahiyh. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”]

 

[4] Anayepata Sifa Ya Kuwajibikiwa Na Swalaah Kabla Ya Wakati Wake Haujatoka

 

Mtoto anapobaleghe, au akili ikamrejea mwendawazimu, au fahamu zikamrejea aliyepotewa nazo, au mwenye hedhi au nifasi akatwaharika kabla ya kutoka wakati wa Swalaah kwa kiasi ya rakaa moja au zaidi, basi itawalazimu kuiswali. Lakini je, itawalazimu kuziswali Swalaah za kabla ya Swalaah hiyo zinazojumuishwa kwake? Swali hili litakuwa wazi kwa mfano ufuatao: Ikiwa mwanamke mwenye hedhi atatwaharika kabla ya kuchwa jua, au kabla ya kuchomoza Alfajiri, basi Maulamaa wana kauli tatu kuhusiana na hali hii:

 

Ya kwanza: Akitwaharika kabla ya kuchwa jua, ni lazima aswali Adhuhuri na Alasiri, na kama akitwaharika kabla ya Alfajiri, ni lazima aswali Magharibi na ‘Ishaa. Haya yamehadithiwa toka kwa ‘Abdul Rahman bin ‘Awf, Ibn ‘Abbaas na Abu Hurayrah. Ni rai yenye nguvu ya Twaawus, An-Nakh’iy, Mujaahid, Rabiy’ah, Maalik, Al-Layth, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Abu Ath-Thawr na Is-Haaq. Hawa wote ni Jamhuri ya Maulamaa. [Ikhtilaaful ‘Ulamaa (uk. 380), Al-Awsatw (2/243), Masaail Ahmad cha Ibn Haaniy (1/131) na Bidaayatul  Mujtahid (1/133)]

 

Na hoja yao ni:

 

1- Yaliyosimuliwa toka kwa ‘Abdul Rahmaan bin ‘Awf akisema: “Mwenye hedhi akitwaharika  kabla jua halijazama, ataswali Adhuhuri na Alasiri, na akitwaharika kabla ya kuchomoza Alfajiri, ataswali Magharibi na ‘Ishaa”. [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah, (2/336), na kutoka kwake Ibn Al-Mundhir (2/243) na ‘Abdul Razzaaq (1285)]

 

2- Yaliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “ Akitwaharika kabla ya Magharibi, ataswali Adhuhuri na Alasiri, na akitwaharika kabla ya Alfajiri, ataswali Magharibi na ‘Ishaa. [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-daaramiy (889), Ibn Abu Shaybah (2/337) na Ibn Al-Mundhir (2/244)]

Imenukuliwa mfano wake toka kwa Abu Hurayrah.

 

3- Adhuhuri na Alasiri, au Magharibi na ‘Ishaa, hukusanywa katika hali ya dharura katika wakati wa moja ya Swalaah mbili. Ikiwa atatwaharika mwishoni mwa mchana, basi wakati wa Adhuhuri unakuwa bado uko na hivyo ataiswali kabla ya Alasiri. Na kama akitwaharika mwishoni mwa usiku, basi wakati wa Magharibi unakuwa bado uko katika hali ya dharura na hivyo ataiswali kabla ya ‘Ishaa. [Majmu’u Al-Fataawaa. Angalia pia Sharhul ‘Umdah cha Ibn Taymiyah (Mjalada wa Pili)]

 

Ya pili: Akitwaharika katika wakati wa Alasiri, ni lazima aswali Alasiri lakini si lazima aswali Adhuhuri. Hii ni rai yenye nguvu ya Al-Hasan, Qataadah, Ath-Thawriy na Abu Haniyfah. [Ikhtilaaf Al-Ulamaa (uk. 380), Al-Awsatw (2/245) na Al-Aswl (1/330)]

 

Hoja yao ni:

 

1- Kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kuipata rakaa ya Swalaah, basi ameipata Swalaah nzima)). Wanasema: “Alif na Laam” katika “As-Swalaah الصلاة “ ni ya “Al-‘Ahdi”, kwa maana kuwa ameipata Swalaah ambayo ameipata rakaa ndani ya wakati wake. Ama Swalaah ya kabla yake, yeye anakuwa hakupata chochote katika wakati wake, na wakati huo unakuwa umeshapita, naye hakuwa mwenye sifa ya ulazima. Sasa vipi itakuwa lazima kwake?! [Ash-Sharhul Mumti’i (2/130)]

 

2- Hatukhitalifiani kuwa mwenye kuacha Swalaah mbili mpaka jua likakurubia kuzama kwa rakaa moja, kisha akaingia kuswali kwa kuzikusanya, akaswali rakaa moja kabla jua halijazama na rakaa saba baada ya kuzama, kwamba huyo anakuwa amemwasi Allaah na anashutumiwa. Ikiwa amekusudia katika hali ya kutokuwa na udhuru, basi haijuzu kufanywa hukmu ya wakati ambao pameruhusiwa kukusanya kati ya Swalaah mbili kuwa hukmu ya wakati ambao pamekatazwa kukusanya kati ya Swalaah hizo. [Al-Awsatw cha Ibn Al-Mundhir (2/245)]

 

3- Tunakubaliana kwamba lau kama ameipata rakaa moja katika Swalaah ya Adhuhuri, kisha kikatokea kizuizi cha kisharia, ni kuwa atalazimika kulipa Adhuhuri tu pamoja na kwamba wakati wa Adhuhuri ni wakati wa Adhuhuri na Alasiri katika hali ya udhuru na kukusanya. Hivyo, tofauti iko wapi katika masuala mawili? Ikiwa watasema: “Tofauti yetu ni kwa mujibu wa athari toka kwa Maswahaba”, basi wataambiwa kwamba ikiwa athari zao ni Swahiyh, basi zitachukuliwa juu ya uakiba na uhadhari basi kwa ajili ya kuchelea uwezekano wa kuwa kizuizi kimeondoka kabla ya kumalizika wakati wa Swalaah ya kwanza, na hususan hedhi, kwani mwenye hedhi anaweza asitambue kutwaharika kwake ila baada ya kupita muda. [Ash-Sharhul Mumti’i cha Ibn ‘Uthaymiyn (2/130) kwa mabadilisho madogo]

 

Ya tatu: Mwanamke akitwaharika kabla ya jua kuchwa kwa kitambo cha kuweza kuswali Swalaah mbili, basi ataswali Adhuhuri na Alasiri. Na kama wakati hautoshi isipokuwa kwa Swalaah moja tu, atalazimika kuswali Alasiri peke yake. Na hii ni kauli ya Maalik na Al-Awzaa’iy. [Al-Awsatw (2/246) na Bidaayatul Mujtahid (1/133)]

 

Lenye Nguvu

 

Ninaloliona mimi ni kuwa kauli ya pili ndio yenye nguvu zaidi. Ama ya kwanza ni ya hadhari na akiba, na ya tatu ni makimbilio ya mwisho kama wakati ni mfinyu. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

[5] Ikiwa Mtu Hakuswali Mpaka Wakati Wa Swalaah Ukatoka Bila Ya Udhuru

 

Mafuqahaa wana kauli mbili kuhusiana na hukmu ya kuilipa Swalaah hii:

 

Ya kwanza: Ni lazima ailipe. Ni kauli ya Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Maimamu wanne na wengineo mpaka An-Nawawiy amethubutu kudai kuwa ni Ijma’a ya Maulamaa wote. [Al-‘Inaayah (1/485-pamoja na Fat-hul Qadiyr), Ad-Dusuwqiy (1/264), Al-Majmu’u (3/71), Al-Insaaf (1/342) na Al-Mumti’i (2/133)] Dalili yao ni haya yafuatayo:

 

1- Hadiyth zinazogusia wajibu wa kulipa Swalaah kwa mwenye kusahau. Wanasema kwamba kutokana na yanayofahamika kwenye Hadiyth hizo, wajibu wa kulipa kwa mwenye kufanya kusudi unakuwa na uzito zaidi.

 

Hili linajibiwa: “Mwenye kusema kuwa aliyefanya kusudi halipi, hakusema kuwa hali yake ni nafuu zaidi kuliko aliyesahau, bali kinachozuilia wajibu wa kulipa kwa mwenye kufanya kusudi ni kuwa dhambi hazimwondokei, hivyo kulipa hakuna faida. Hivyo basi, kusema kuwa ni wajibu kulipa bila kuwepo kinachothibitisha ni upuuzi kinyume na aliyesahau au aliyelala. Hawa Rasuli amewaamuru kulipa na akaeleza wazi kwamba kulipa ni kafara kwao, na hakuna jingine zaidi ya hilo. [Naylul Awtwaar (2/32)]

 

Kisha kipimo cha kitu hufanywa kwa kinachofanana nacho na si kwa kile kilicho kinyume nacho, na hili halina mjadala. Kinyume cha kusudi ni sahau, na kinyume cha maasia ni utiifu, basi vipi vitakuwa katika kipimo kimoja?!” [Al-Muhallaa (2/237). Kuna utafiti murua kabisa uliofanywa kwa ajili ya kuwajibu wenye kusema kuwa ni wajibu kulipa]

 

2- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na kulipa kwa mwenye kulala na mwenye kusahau: ((Hakuna kafara yake isipokuwa hilo)). Wanasema: “Hadiyth inaonyesha kwamba anayekusudiwa ni mwenye kufanya kusudi, kwa kuwa aliyelala na aliyesahau, hao hawana dhambi, hivyo makusudio ya mwenye kusahau ni mwenye kuacha”.

 

Hili linajibiwa: “Kwamba maneno haya yanamaanisha kuwa si lazima kulipa kwa aliyelala au aliyesahau kwa kutokuwepo dhambi walilolifanya kafara kuwa mwega wake wakati ambapo Hadiyth Swahiyh zinaeleza wazi kwamba hilo ni wajibu kwa wawili hao!! Isitoshe, kafara inaweza kuwa kwa kosa kama inavyokuwa kwa kusudi, na hili li wazi”.

 

3- Ulinganisho wa aliyefungua kwa makusudi katika mwezi wa Ramadhwaan kuwa ni lazima alipe sawa na yule aliyemwingilia mkewe mchana wa Ramadhwaan.

 

Hili linajibiwa: “Hadiyth inayothibitisha wajibu wa kulipa kwa mwenye kuingilia mchana wa Ramadhwaan ni dhwa’iyf. Al-Bukhaariy na Muslim wameifanyia Hadiyth hiyo “ikhraaj” bila ya nyongeza isemayo: “Na funga siku badala ya ile uliyojamii”, na nyongeza ni dhwa’iyf, haitegemewi”. [Angalia Majmu’u Al-Fataawaa (22/40), Nasbu Ar-Raayah (2/453) na At-Talkhiysw (2/219)]

 

4- Wanaweza kusaidiwa posho ya dalili ambayo wao hawakuitoa kwa Hadiyth isemayo: ((Basi deni la Allaah lina haki zaidi ya kulipwa)), tukisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameziita ‘Ibaadah (Hijjah na Swaum) ni deni. [Hadiyth Swahiyh: Itakuja katika mlango wake, Insha-Allaah]

 

Hili linajibiwa: “Kutokana na hili, ni lazima wajuzishe kuswali kabla ya kuingia wakati wa Swalaah!! Kwani deni linaweza kulipwa kabla muda wake haujafika. Ufafanuzi zaidi utakuja katika dalili la kundi jingine.

 

Ya pili: Hapaswi kuilipa, bali hata Swalaah hiyo haiswihi. Yamesemwa haya na ‘Umar bin Al-Khattwaab na mwanawe ‘Abdullaah, Sa’ad bin Abu Waqqaas, Ibn Mas-’oud [Ibn Hazm amesema: “Hatumjui Swahaba aliyekhilafiana na hilo], Al-Qaasim bin Muhammad, Budayl Al-‘Uqayliy, Muhammad bin Siyriyn, Mutwarrif bin ‘Abdullah, ‘Umar bin ‘Abdul ‘Aziyz, kundi la Maulamaa wa Kishafii, Al-Jawzjaaniy, Abu Muhammad Al-Barbahaariy, Ibn Battwah, Daawuud Adh-Dhwaahiriy na Ibn Hazm. Ni chaguo la Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah, Al-‘Allaamah Al-Albaaniy na Ibn ‘Uthaymiyn. [Al- Muhallaa (2/235- na zinazofuatia), Majmu’u Al-Fataawaa (22/40) Fat-hul Baariy cha Ibn Rajab kama ilivyo katika Al-Inswaaf (1/443), Al-Mumti’i (2/133) na Naylul Awtwaar (2/31-32)]

 

Hii ndio kauli yenye nguvu zaidi. Na dalili ya hili ni:

 

1- Kauli Yake Ta’alaa:

 

((فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ ۚ فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا ))

(( Mtakapomaliza Swalaah, mdhukuruni Allaah msimamapo, na mkaapo na mnapolala ubavuni mwenu Mtakapopata utulivu, simamisheni Swalaah (kama desturi), hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu)). [An-Nisaa (4:103)].

 

Swalaah ni ‘ibaadah yenye pande mbili zenye mipaka. Ina mwanzo wake na mwisho wake. Hivyo basi, haijuzu kuiswali kabla ya wakati wake au baada ya wakati wake, hakuna kitenganishi kati ya pande hizi ila kwa Aayah au Hadiyth yenye amri mpya kama ilivyo kwa mwenye kulala na mwenye kusahau na wengineo wenye nyudhuru. Ni kama vile vile ilivyo katika Hijjah, na kufunga Ramadhwaan.

 

Aidha, inajulikana kwamba ikiwa mtu ataswali kabla ya wakati kwa kusudi, basi Swalaah yake ni batili kwa makubaliano ya Maulamaa wote, na hali inakuwa hivyo hivyo kama ataiswali baada ya wakati wake.

 

2- Kauli Yake Ta’alaa:

 ((فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّين  •الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ))

(( Basi Ole kwa wanaoswali ... • Ambao wanapuuza Swalaah zao)). [Al-Maa’uwn (107:4-5)]

 

3- Kauli Yake Ta’alaa:

 

((فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا))

(( Wakafuata baada yao waovu, walipoteza Swalaah na wakafuata matamanio; basi watakutana na adhabu motoni)). [ Maryam (19:59)]

 

Lau kama mwenye kuacha Swalaah kwa makusudi anaweza kuipata baada ya kutoka wakati wake, basi asingeliingia katika makamio wala asingelikutana na adhabu. Kama ambavyo hakuna makamio wala adhabu kwa yule mwenye kuichelewesha hadi mwisho wa wakati wake, akaiswali na kuipata.

 

4- Hadiyth isemayo: ((Mwenye kuisahau Swalaah, basi aiswali anapoikumbuka)), [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa nyuma kidogo], nayo ni dalili ya kwamba mwenye kufanya kusudi, basi hailipi Swalaah, kwani neno (Mwenye kusahau) ni sharti, na kukosekana sharti kunahitajia kukosekana chenye kushurutiwa. Hivyo basi, ambaye hakusahau, haswali.

 

5- Kulipa ni lazimisho la kisharia, na sharia haijuzu ila kutoka kwa Allaah kupitia ulimi wa Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na haipasi kulipa isipokuwa kwa amri mpya (kwa lililo sahihi katika usuul), na hakuna dalili kuhusiana na amri ya kulipa. Na lau kama kulipa kungelikuwa ni wajibu kwa mwenye kufanya kusudi ya kuacha Swalaah mpaka wakati wake ukatoka, Allaah Mtukufu Asingelighafilisha hilo wala Rasuli Wake, Wasingelisahau hilo wala Wasingelifanya kusudi ya kututaabisha kwa kuacha kulibainisha.

 

((وَمَا نَتَنَزَّلُ إِلَّا بِأَمْرِ رَبِّكَ ۖ لَهُ مَا بَيْنَ أَيْدِينَا وَمَا خَلْفَنَا وَمَا بَيْنَ ذَٰلِكَ ۚ وَمَا كَانَ رَبُّكَ نَسِيًّا))

(( Na (sisi Malaika) hatuteremki ila kwa amri ya Rabb wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Ni Yake Yeye yaliyoko mbele yetu, na yaliyoko nyuma yetu, na yaliyoko baina ya hayo. Na Rabb wako si Mwenye kusahau kamwe)). [Maryam (19:64)].

 

6- Hadiyth: ((Anayepitwa na Swalaah ya Alasiri, ni kama aliyepokonywa ahli wake na mali yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa nyuma kidogo]

 

Ni sawa na kusema kuwa kilichopita haiwezekani kukirejesha tena. Na ikiwa kitapatikana au ikawezekana kukipata, basi kisingelipita kama ambavyo Swalaah yenye kusahauliwa, haipiti kamwe. Na lau ingeliwezekana kuilipa iliyoachwa makusudi, tungelisema kwamba imempita kwa uongo na kwa batili!!

 

7- Mwenye kuwajibisha kuilipa kwa aliyeiacha makusudi ataulizwa: “Swalaah hii unayomwamrisha aiswali, je ni ile ambayo Allaah Amemwamrisha, au ni Swalaah nyingine?” Akisema: “Ni hiyo hiyo”, tutamwambia: “Basi mwenye kufanya kusudi ya kuiacha si mwasi, kwa kuwa amefanya lile Alilomwamrisha Allaah Ta’alaa, na hakuna madhambi kwa mujibu wa kauli yako!! Na hakuna lawama kwa mwenye kufanya kusudi ya kuacha Swalaah mpaka wakati wake ukatoka!!” Na hili hakunaMuislamu anayelisema. Na kama atasema: “Siyo ile ambayo Allaah Ameiamuru”, basi tutamwambia: “Umesema kweli”. Na hili ni jibu tosha kwa kuwa wao wamekiri kwamba wamemwamuru kile ambacho Allaah Hakukiamuru. [Angalia Al-Muhallaa (2/235-na zinazofuatia) na Al-Ihkaam cha Ibn Hazm (1/301)]

 

Ninasema: “Kauli hii ndiyo yenye nguvu zaidi. Wenye kwenda kinyume nayo, hawana kifaacho kutegemewa kama dalili. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

·       

Mwenye Kuipoteza Swalaah Miaka Mingi Ya Umri Wake

 

Kwa kusema kwamba mwenye kuacha Swalaah kwa kusudi bila ya udhuru mpaka wakati wake ukatoka si wajibu kwake kuilipa wala hilo haliswihi, tunajengea juu ya kauli hiyo kwamba mwenye kuacha Swalaah kwa miaka mingi ya umri wake, kisha akatubia kwa Allaah na akalingamana sawa katika dini yake, basi huyo hatozilipa Swalaah zote zilizompita sawasawa tukimhukumia kwamba ni kafiri wakati alipokuwa haswali au la. Lakini hii ni kinyume na Jamhuri ya Maulamaa wanaosema kwamba ni lazima azilipe Swalaah zote zilizompita!! [Ibnu ‘Aabidiyn (2/62) Ad-Dusuwqiy (1/264) na Mughnil Muhtaaj (1/308)]

 

·       

Na Vipi Kuhusu Mwenye Kuiacha Kwa Makusudi?

 

Hukmu ya kutoilipa Swalaah kwa mwenye kuiacha mpaka muda wake ukatoka bila ya udhuru, haimaanishi kuwa anahafifishiwa mambo, bali mambo yalivyo ni kuwa hilo ni adhabu na ghadhabu kutokana na kitendo chake hicho. Dhambi halimwondokei hata kama ataiswali Swalaah hiyo mara elfu moja baada ya wakati wake isipokuwa kama atatubia kwa Allaah na kuomba maghfirah. Hili ndilo linalompasa; kuomba tawbah na maghfirah, kukithirisha kheri na kuswali Swalaah za Sunnah kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): (( Jambo la kwanza atakalofanyiwa hisabu mtu Siku ya Qiyaamah katika amali zake ni Swalaah. Kama ni sahihi, basi amefaulu na kufanikiwa, na kama ni mbovu, basi amepita utupu na amekula hasara. Na kama kimepungua chochote katika faradhi yake, Mola (Tabaaraka wa Ta’alaa) Atasema: Angalieni! Je, Mja Wangu anazo Swalaah za Sunnah zikamilishie kilichopungua katika faradhi zake? Kisha amali zake zilizobakia huchukuliwa juu ya hilo)). [Haya yashazungumziwa. Angalia Al-Muhallaa (2/235), Al-Fataawaa (22/40-41) na Tuhfat Al-Ahwadhy (2/463)]

 

 

Share