019-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Mambo Yaliyoruhusiwa Ndani Ya Swalaah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

019-Mambo Yaliyoruhusiwa Ndani Ya Swalaah

 

 

Vitendo Vilivyoruhusiwa

 

1- Kumbeba mtoto

 

Imepokelewa na Abuu Qataadah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali huku amembeba Umaamah binti Zaynab binti wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Anaposujudu, humweka chini, anaponyanyuka humbeba”.[Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (516), Muslim (543) na wengineo].

 

2- Kutembea hatua chache kwa dharura

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali nyumbani na mlango kaufunga kwa ndani. Nilipokuja niligonga, naye akatembea akaja kuufungua, kisha akarejea na kuendelea na Swalaah yake, na mlango ulikuwa mwelekeo wa Qiblah”.  [Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (598), Abuu Daawuud (910) na An-Nasaaiy (3/11). Al-Albaaniy kaipa daraja ya Hasan].

 

3- Kutaharaki kwa ajili ya kumwokoa mtoto au kumzuia mtu asiporomoke shimoni au asipatwe na adha

 

Imepokelewa toka kwa Al-Azraq bin Qays akisema: “Tulikuwa Al-Ahwaaz tukipigana na Makhawaarij. Nilipokuwa ukingoni mwa mto, mara nikamwona mtu anaswali [Ni Abuu Barzah Al-Aslamiy] akiwa ameshikilia ugwe mkononi. Mnyama wake akaanza kufanya matata naye akaanza kumfuata. Na mimi nimepigana pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) vita kati ya sita, au saba, au nane na nikashuhudia namna alivyokuwa akifanya wepesi. “ [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1211)].

 

Al-Haafidh katika Al-Fat-h (3/82) anasema: “Konteksi ya kisa hiki inaonyesha kwamba Abuu Barzah hakuikata Swalaah yake, nayo inatiliwa nguvu na riwaya ya ‘Amri bin Marzouk isemayo: “Akamkamata kisha akarejea kinyume nyume. Ikiwa aliikata Swalaah yake, asingelijali kurudi kukipa mgongo Qiblah. Na katika kurejea kwake kinyume nyume kunaonyesha kwamba kwenda katika makusudio yake hakukuwa kwa hatua nyingi”.

 

·       

Faida

 

Inaingia katika hili kwamba inajuzu kwako ikiwa unaswali na simu ikalia kwa mfano, uifungue ili mpigaji ajue kwamba uko kwenye Swalaah.

 

4- Kumzuia mtu asipite mbele yake katika Swalaah yake

 

Tumeielezea Hadiyth ya Abuu Sa’iyd kuhusiana na amri ya kupambana na anayepita mbele ya mwenye kuswali.

 

5- Kuua nyoka, nge au chochote chenye madhara

 

Imepokelewa na Abuu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru kuwaua nge na nyoka wakati wa Swalaah. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (921), An-Nasaaiy (1202), At-Tirmidhiy (390) na Ibn Maajah (1245) na tamshi ni lake, nayo ni Hadiyth Swahiyh].

 

6- Kumbonyeza aliyelala kwa haja

 

‘Aaishah anasema: “Nilikuwa nikiinyoosha miguu yangu katika Qiblah cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati anaswali. Anaposujudu hunibonyeza (nikaikunja), na anaposimama nainyoosha”.

 

7- Kuvua viatu na mfano wake kwa haja

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy akisema: “Wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anaswali na Maswahaba zake, alivivua viatu vyake akaviweka kushotoni mwake. Maswahaba walipoona hivyo, nao pia walivivua viatu vyao.” [“Takhriyj” yake ishaelezewa].

 

8- Kutema mate nguoni au kwenye leso

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema:

(( إن أحدكم إذا قام يصلي فإن الله تبارك وتعالى قبل وجهه، فلا يبصقن قبل وجهه ولا عن يمينه، وليبصق عن يساره تحت رجله اليسرى فإن عجلت به بادرة فليقل بثوبه هكذا))

((Hakika mmoja wenu anaposimama kuswali, basi Allaah (Tabaaraka wa Ta’alaa Huukabili) uso wake. Basi atahadhari asije kutema mate mbele yake au kuliani kwake, bali ateme kushotoni mwake chini ya mguu wake wa kushoto. Na ikiwa mate yatamzidi nguvu, basi afanye hivi kwa nguo yake)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (3008) na Abuu Daawuud (477)]. Kisha akaikunjia kunjia nguo yake.

 

9- Kuiweka sawa nguo au kujikuna

 

Imepokelewa na Jariyj Adh-Dhwaby akisema: “Aliyyi alikuwa anaposimama kuswali, huweka mkono wake wa kulia juu ya kifundo cha mkono wake wa kushoto. Huendelea kufanya hivyo mpaka anaporukuu isipokuwa kama ataiweka sawa nguo yake au kujikuna”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abuu Shaybah (1/391) na Al-Bukhaariy (2/58) akiielezea kwa tamko la mkato].

 

Ibn ‘Abbaas anasema: “Mtu anaweza kukitumia kiungo chake chochote cha mwili atakavyo katika Swalaah yake”.[Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2/58) akiielezea kwa tamko la mkato].

 

10-  Kusema “Subhaanal Laah” kwa wanaume na kupiga kikofi kwa mwanamke ikiwa patatokea jambo

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( من نابه شيء في صلاته فليسبح، فإنه إذا سبح التفت إليه، وإنما التصفيح للنساء))

((Anayetokewa na jambo katika Swalaah yake, basi aseme “Subhaanal Laah”, kwani anaposema hivyo hutanabaikiwa, lakini wanawake hupiga kikofi)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1201) na Muslim (421) na tamko ni lake. Maneno التصفيح  na التصفيق yana maana moja, nayo ni kupiga tumbo la kiganja kwa tumbo la kiganja kingine].

 

·       

Faida

 

“Nimejua kwamba mwanamke kisharia hasemi Subhaanal Laahi anapotokewa na jambo katika Swalaah, lakini ikiwa jambo lililomtokea ni la dharura, inajuzu aseme Subhaanal Laah kama hakuna wanaume. Imepokelewa na Asmaa binti Abiy Bakr akisema: “ Nilimwendea ‘Aaishah wakati jua lilipokuwa limepatwa, nikawakuta watu wamesimama wakiswali, naye pia amesimama anaswali. Nikauliza: “Watu wana nini?” Akaashiria kwa mkono wake mbinguni akisema: Subhaanal Laah”. Imepasishwa na Maimamu wawili.

 

11- Kugeuka kulia au kushoto kwa ajili ya haja

 

Imepokelewa na Jaabir akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitujulisha kuwa hajisikii vizuri, tukaswali nyuma yake akiwa yeye amekaa huku Abuu Bakri akitusikilizisha takbiyr yake. Akatugeukia akatuona tumesimama. Akatuashiria tukae, nasi tukakaa, tukaswali pamoja naye huku tumekaa”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (413), An-Nasaaiy (3/9) na Abuu Daawuud (588)].

 

Na katika Hadiyth ya Sahl bin Sa’ad: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja watu wakiwa katika Swalaah, akapenya mpaka akasimama katika safu, watu wakapiga vikofi. Abuu Bakri alikuwa hageuki katika Swalaah, na watu walipozidi kupiga vikofi, aligeuka akamwona Rasuli wa Allaah..”[Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (684), Muslim (421) na wengineo].

 

12- Kuashiria kwa kichwa au mkono kwa ajili ya haja

 

Jaabir anasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinituma huku yeye akielekea kwenda kwa Bani Al-Mustwalaq. Nikamjia na yeye anaswali juu ya ngamia wake. Nikamsemesha na yeye akaashiria kwa mkono wake hivi. Kisha nikamsemesha akaashiria kwa mkono wake hivi huku mimi namsikia akisoma na kuashiria kwa kichwa chake. Alipomaliza aliniuliza: “Umefanya nini kwa jambo nililokutuma? Sikuweza kukujibu kwa kuwa nilikuwa ninaswali”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (540) na Abuu Daawuud (926)].

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimjibu kwa ishara kijakazi ambaye Ummu Salamah alikuwa amemtuma kwake ili amuulize kuhusu rakaa mbili alizoziona akiziswali. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4370) na Muslim (834)].

 

13- Kujibu salamu kwa ishara kwa aliyekusalimia

 

Mtu akikusalimia ukiwa unaswali, inajulikana kuwa haijuzu kumjibu kwa maneno, lakini inajuzu kumjibu kwa ishara ya mkono. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka kuelekea Qubaa ili akaswali huko. Ma-Answaar wakamjia, wakamsalimia na yeye yuko ndani ya Swalaah. Nikamwambia Bilaal: Ulimwonaje Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwajibu wakati walipokuwa wakimsalimia? Akasema: Hivi; akakunjua kiganja chake [Akaelekeza tumbo lake chini na mgongo wake juu]. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (915) kwa Sanad Swahiyh].

 

14- Kunyanyua kichwa katika sujudi ili kujua mambo yakoje ikiwa imamu atarefusha sijda

 

Ukiwa ndani ya sijdah katika Swalaah ya jamaa, imamu akarefusha sijdah, au ukawa hujaisikia takbiyr, au mfano wa hilo, inajuzu unyanyue kichwa ili kupeleleza jambo. Imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin Shaddaad toka kwa baba yake akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitutokea katika moja ya Swalaah mbili za ‘Ishaa akiwa amembeba ima Al-Hasan au Al-Husayn. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatangulia akamweka, kisha akapiga takbiyr ya Swalaah. Na katikati ya Swalaah alisujudu na sijdah ikawa ndefu. Nikanyanyua kichwa, mara nikamwona mtoto yuko juu ya mgongo wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye yuko ndani ya sijdah, nami nikarudi tena kwenye sijdah yangu. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomaliza Swalaah yake watu walisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Umesujudu sijdah ndefu ndani ya Swalaah yako mpaka tukadhani kwamba kuna jambo limetokea, au pengine unateremshiwa wahyi”. Akasema: ((Hayo yote hayajatokea, lakini mwanangu alinipanda mgongoni, nikachukia kumharakisha mpaka ashuke)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (2/230 kwa Sanad Hasan].

 

15- Kuangalia kwenye Msahafu na kusoma kutoka humo katika Swalaah ya Sunnah kwa haja

 

Hakuna ubaya kusoma kutoka kwenye Msahafu katika Swalaah ya usiku kwa mfano ikiwa mtu anataka kurefusha kisomo na yeye hakuhifadhi Qur-aan. Imepokelewa toka kwa Al-Qaasim akisema kwamba ‘Aaishah alikuwa akisoma kwenye Msahafu katika Swalaah zake mwezi wa Ramadhwaan. [Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdur Raaziq (2/240) na Ibn Abuu Daawuud katika Al-Maswaahif (192)].

 

Al-Qaasim amesema: “Mtumwa alikuwa akimswalisha ‘Aaishah kwa kusoma toka kwenye Msahafu”.  [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy ikiwa Mu’allaq katika Kitabu cha Adhana mlango wa “Mtumwa kuwa imamu”. Ibn Abuu Shaybah amesema ni Mawsuul (2/338) na Ibn Abuu Daawuud katika Al-Maswaahif ukurasa wa 192]

 

Haijuzu kufanya hivi katika Swalaah ya faradhi, au katika Swalaah ya Sunnah kama haihitajiki.

 

(A)           

Maneno Yenye Kuruhusiwa Na Mfano Wake

 

1- Kumtatua imamu

 

Ikiwa imamu atatazikiwa katika kisomo, inajuzu kwa aliye nyuma yake kumtatua, kwa kuwa ikiwa hatamtatua, matokeo yake yatakuwa ni kubadili Maneno ya Allaah. Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin ‘Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Swalaah fulani, akasoma, akatatizikiwa. Alipomaliza alimuuliza Ubayya: “Je, umeswali nasi?” Akajibu: “Ndio”. Akamuuliza: “Basi kipi kimekuzuia?” [Imefanyiwa “ikhraaj”na Abuu Daawuud (894) na Ibn Hibaan (1/316-Ihsaan) kwa Sanad Swahiyh].

 

·       

Faida

 

1- Inatakikana imamu asitatuliwe kwanza madhali atakuwa akikariri kariri Aayah ili kujikumbusha. Kumsubiria itakuwa ni bora zaidi.

 

2- Imamu hatatuliwi kama atanyamaza bila kubabaika katika kisomo chake isipokuwa tu kama mnyamao wake utakuwa mrefu. Kunyamaa kwa imamu kunawezekana kuwa anayataamuli anayoyasoma.

 

3- Imamu akikosea kosa lisilo haribu maana katika kisomo chake, basi hatatuliwi.

 

Imepokelewa toka kwa Ubayya bin Ka’ab kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( Mimi nimesomeshwa Qur-aan…kwa visomo (lugha) saba, hakuna humo isipokuwa yaliyo wazi yenye kutosheleza. Ukisema: Ghafuuran Rahiyman, au ukasema: ‘Aliyman Hakiyman, basi Allaah ni hivyo madhali hukubadili aayah ya adhabu kwa rehma, au aayah ya rehma kwa adhabu)).  [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (20646) kwa Sanad Swahiyh].

 

2- Kuirudia rudia Aayah moja katika Swalaah ya Sunnah

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Dharri kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliisoma Aayah hii akairudia rudia mpaka asubuhi:

 

((إِن تُعَذِّبْهُمْ فَإِنَّهُمْ عِبَادُكَ ۖ وَإِن تَغْفِرْ لَهُمْ فَإِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ))

((“Ukiwaadhibu, basi bila shaka hao ni waja Wako; na Ukiwaghufuria basi hakika Wewe Ndiye Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.”)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1010), Ahmad (20831) na Al-Haakim. Katika Sanad yake kuna ulaini].

 

Na Masrowq anasema: “Tamiym Ad-Daariyy aliirudia rudia Aayah hii:

 

((أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ))

((Je, wanadhania wale waliochuma maovu kwamba Tutawafanya sawa na wale walioamini na wakatenda mema, sawasawa uhai wao na kufa kwao? Uovu ulioje wanayouhukumu))

[Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abuu Shaybah katika Al-Muswannaf (2/477)].

 

Imepokelewa toka kwa Sa’iyd bin ‘Ubayd akisema: “Nilimwona Sa’iyd bin Jubayr akiwaswalisha watu mwezi wa Ramadhwaan huku akiikariri Aayah hii:

((أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ كَانُوا مِن قَبْلِهِمْ ۚ كَانُوا هُمْ أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَآثَارًا فِي الْأَرْضِ فَأَخَذَهُمُ اللَّـهُ بِذُنُوبِهِمْ وَمَا كَانَ لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مِن وَاقٍ))

Pamoja na:

((يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ • الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ))

Akiikariri mara mbili au tatu. [Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq katika Al-Muswannaf (2/492)].

 

Ninasema: “Hili halikunukuliwa kwa upande wa Swalaah ya faradhi, hivyo kuliacha ni bora zaidi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

3- Kulia na kutoa mlio wa hisia ya uchungu, huzuni na kadhalika

 

Kulia katika Swalaah ikiwa ni kwa kumkhofu Allaah, kukumbuka Pepo au Moto na mfano wake, kunakuwa ni jambo zuri analolipwa mtu thawabu. Jambo hili halibatwilishi Swalaah kama wanavyodhani baadhi ya watu. Aidha, ikiwa kulia ni kwa ajili ya maumivu, au msiba nawe ukashindwa kujizuia, basi hakuna ubaya.

 

Zifuatazo ni baadhi ya dalili zinazothibitisha hili:

 

1- Allaah Mtukufu Amewasifu wenye kulia Aliposema:

 

((أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ مِن ذُرِّيَّةِ آدَمَ وَمِمَّنْ حَمَلْنَا مَعَ نُوحٍ وَمِن ذُرِّيَّةِ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْرَائِيلَ وَمِمَّنْ هَدَيْنَا وَاجْتَبَيْنَا ۚ إِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُ الرَّحْمَـٰنِ خَرُّوا سُجَّدًا وَبُكِيًّا))

(( Hao ndio ambao Allaah Amewaneemesha miongoni mwa Manabii katika kizazi cha Aadam, na miongoni mwa Tuliowabeba pamoja na Nuwh (katika jahazi), na katika kizazi cha Ibraahiym na Israaiyl na miongoni mwa Tuliowaongoa na Tukawateua. Wanaposomewa Aayaat za Ar-Rahmaan huporomoka kifudifudi wakisujudu na kulia)).

 

Na Neno Lake Ta’alaa:

(( وَيَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ يَبْكُونَ وَيَزِيدُهُمْ خُشُوعًا ))

(( Na wanaporomoka kifudifudi huku wanalia na inawazidishia unyenyekevu )).

 

Aayah hizi mbili zinamjumuisha aliye ndani ya Swalaah na aliye nje ya Swalaah.

 

2- Imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin Ash-Shukhayr akisema: ”Nilimjia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa anaswali, na kifuani mwake kuna mvumo kama mvumo wa maji yachemkayo chomboni”.[Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1214), Abuu Daawuud (1/328) na Ahmad (4/25), na Sanad yake ni Swahiyh].

 

3- Imepokelewa toka kwa ‘Aliyyi akisema: “Hakuna aliyekuwa amepanda farasi Siku ya Badr isipokuwa Al-Miqdaad. Ungelituona, ungekuta sote tumelala isipokuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) chini ya mti akiswali na akilia mpaka pakapambauka”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (1026) na Ibn Khuzaymah (2/53), na Sanad yake ni Swahiyh].

 

4- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Rasuli wa Allaah alipozidiwa na maumivu, aliulizwa nani aswalishe. Akasema: ((Mwamuruni Abu Bakri awaswalishe watu)). ‘Aaishah akamwambia: “ Abu Bakri ana moyo laini, anaposoma hawezi kujizuia kulia. Akasema: ((Mwamuruni aswalishe)). Akamkariria tena na Rasuli akasema:(( Mwamuruni aswalishe, hakika nyinyi ni (kama) wanawake wa Yusuf)).  [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (682)].

 

5- ‘Abdullaah bin Shaddaad amesema: “Nilisikia mtetemo wa ‘Umar nami niko safu ya mwisho akisoma:

((  قَالَ إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ))

((Akasema: “Hakika mimi nashitakia dhiki ya majonzi yangu na huzuni zangu kwa Allaah. Na najua kutoka kwa Allaah yale msiyoyajua.”)) [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy katika mlango wa adhana. Angalia Fat-hul Baariy (2/206). Ibn Taymiyah katika Al-Fataawaa (22/623) ameeleza kwamba athar hii imehifadhiwa toka kwa ‘Umar].

 

·       

Faida

 

Sauti ya kuugulika kama “aah” au ya maumivu kama “ooh”, hazibatwilishi Swalaah, lakini ni karaha kuzifanya bila haja.

 

3- Kupuliza kwa haja fulani

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar akisema: “Jua lilipatwa wakati wa enzi ya Rasuli wa Allaah. Katika sijdah yake ya mwisho alipuliza: “Uf uf”, kisha akasema: ((Mola wangu! Je, Hukuniahidi kwamba Hutowaadhibu mimi nikiwa pamoja nao? Je, Hukuniahidi kwamba Hutowaadhibu nailhali wanaomba maghfirah?)) [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1194), An-Nasaaiy (3/137) na Ahmad (2/159), na wapokezi wake ni watu wa kuaminika. Al-Bukhaariy (2/62) ameileta kwa tamko la kutothibiti usahihi wake kutokana na hitilafu katika riwaya ya ‘Atwaa bin As-Saaib ambaye alikuwa amekoroga. Lakini Hammaad bin Salamah alikuwa ameisikia kutoka kwa ‘Atwaa kabla ya kukoroga katika kauli ya Ibn Ma’iyn na Abuu Daawuud]

 

Imepokelewa na Ayman bin Naayil akisema: “Nilimwambia Qudaamah bin ‘Abdullaah bin ‘Ammaar Al-Kullaabiy  ambaye alikuwa swahibu wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ninakerwa na manyoya ya njiwa kwenye Al-Masjidul Haraam tunaposujudu akasema: “Pulizeni”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (2/253), na Al-Haafidh katika Al-Fat-h kaipasisha kuwa Hadiyth Swahiyh (3/85)].

 

4- Kujikohoza kwa ajili ya haja

 

Hakuna ubaya kufanya katika Swalaah. Hii ni kwa vile Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuzungumza ndani ya Swalaah aliposema: ((Haifai ndani yake maneno ya watu)), na kujikohoza au kutoa mgumio wa ishara haviitwi kuwa ni maneno, kwani vyenyewe pamoja na matamshi mengine havileti maana ya kufahamika, na wala mtendaji wake haambiwi kazungumza, bali makusudio yake yanafahamika kutokana na dalili, hivyo ni kama ishara tu.  [Majmu’u Al-Fataawaa cha Ibn Taymiyah (22/617)]

 

5- Maneno machache kwa ajili ya maslaha ya Swalaah

 

Maneno kwa ajili ya maslaha ya Swalaah hayaibatilishi ikiwa yatasemwa na imamu au maamuma lakini yasiwe mengi bali ya ufahamisho tu.

 

Linalothibitisha haya ni Hadiyth mashuhuri ya Dhul Yadayn kuhusiana na kisa cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwaswalisha watu Alasiri akisema: “Akatoa tasliym baada ya rakaa mbili. Akasimama Dhul Yadayn akauliza: Je, umepunguza Swalaah ee Rasuli wa Allaah au umesahau?” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Hakuna lolote katika hayo mawili)). Akasema: “Ilikuwa ni sehemu ya hayo ee Rasuli wa Allaah”. Rasuli wa Allaah akawaelekea watu akawauliza: “Je, Dhul Yadayn anasema kweli?” Wakajibu: “Ndio ee Rasuli wa Allaah”. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakamilisha rakaa mbili zilizobakia, kisha akasujudu sijdah mbili akiwa amekaa baada ya kutoa tasliym.  [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (714), Muslim (573) na wengineo].

 

Mwelekeo wa kutoa dalili hii ni kuwa imamu na maamuma wamezungumza kwa ajili ya maslaha ya Swalaah kabla hawajaimaliza. Hivyo imekuwa ni katika hukumu ya Swalaah.

 

6- Kusema “Al-Hamdu” kwa anayepiga chafya

 

Inajuzu kwa anayepiga chafya kwenye Swalaah amhimidi Allaah kwa yeye mwenyewe lakini aliye pembeni mwake hamjibishi kwa “Yarhamukal Laahu”. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Rifa’ah bin Maalik aliyesema: “Niliswali nyuma ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nikapiga chafya na kusema: “Alhamdu Lillaahi hamdan kathiyran twayyiban mubaarakan ‘alayhi kamaa Yuhibbu Rabbunaa wa Yardhwaa”. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomaliza Swalaah aliuliza: ((Nani aliyezungumza ndani ya Swalaah?)). Rifa’ah akajibu: “Ni mimi ee Rasuli wa Allaah”. Rasuli akasema: ((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake, hakika Malaika thelathini na ushee walishindana nani kati yao apande nalo)).[Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (404) na An-Nasaaiy (2/245). Al-Bukhaariy pia kaifanyia “ikhraaj” lakini hakumtaja Al-‘At Twaas].

 

Ash-Shawkaaniy anasema: “Inaonyesha tena ruhusa ya kumhimidi Allaah ndani ya Swalaah kwa aliyepiga chafya. Na hili linatiliwa nguvu na ujumuishi wa Hadiyth zinazogusia uhalali wake, kwani hazikupambanua kati ya Swalaah na kwingineko”.

 

Ninasema: “Linalotilia nguvu hili vile vile ni yale yaliyokuja katika Hadiyth ya Mu’aawiyah bin Al-Hakam aliyesema: “Nilipokuwa naswali pamoja na Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mtu mmoja alipiga chafya akasema: “Al-Hamdu lil Laah”, nami nikamwambia: “Yarhamukal Laahu”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (537) na Abuu Daawuud (930)].

 

Tunafahamu hapa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kumwambia aliyepiga chafya “Yarhamukal Laahu”, lakini hakumkataza mpigaji kusema “Al-Hamdu lil Laah”, hivyo basi, inaonyesha kujuzu kwake. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

7- Kumhimidi Allaah kwa jambo la furaha

 

Hadiyth ya Sahl bin Sa’ad kuhusiana na kisa cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenda kwa Bani ‘Amri bin ‘Awf  ili kusuluhisha kati yao inasema kwamba Abuu Bakri aliwaswalisha. Na Rasuli alipokuja wao wakiwa bado ndani ya Swalaah, Abu Bakri alitaka kurejea nyuma. Rasuli wa Allaah akamwashiria abaki kama alivyo. Abu Bakri akanyanyua mikono yake, na akamhimidi Allaah ‘Azza wa Jalla kutokana na amri hiyo ya Rasuli wa Allaah. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (684) na Muslim (431)].

 

8- Kumsemesha anayeswali na kumuuliza jambo

 

Tumeeleza nyuma kisa cha Jaabir wakati Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomtuma kwa Bani Al-Muswtwalaq kuwa alipokuja kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimkuta ndani ya Swalaah na akamsemesha. Rasuli hakumjibu bali alimwashiria kwa mkono wake.  [Muslim (540)].

 

Pia imeelezwa nyuma Hadiyth ya Asmaa aliyesema: “Nilimjia ‘Aaishah wakati jua lilipopatwa, kutahamaki nikawaona watu wamesimama wanaswali, naye pia kasimama anaswali. Nikamuuliza: “Watu wana nini?” Akaniashiria mbinguni kwa mkono wake”. [Al-Bukhaariy (1220) na Muslim (545)].

 

 

Share