020-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Yaliyokatazwa Ndani Ya Swalaah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

020-Yaliyokatazwa Ndani Ya Swalaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Ni mambo ambayo Hadiyth zimeyakataza au kuyafanya makruhu ndani ya Swalaah. Lakini mambo haya hayabatilishi Swalaah, bali hupunguza thawabu za mwenye kuswali. Mambo hayo ni:

 

1- Kukamata kiuno

 

Hili halijuzu kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah aliposema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kukamata kiuno ndani ya Swalaah. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1220) na Muslim (545)].

 

Na imepokelewa toka kwa ‘Aaishah kwamba alikuwa akichukizwa na mwenye kuswali anayeweka mkono wake kwenye kiuno chake akisema: “Mayahudi hufanya hivyo”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3458)].

 

Aidha, imepokelewa toka kwa Ziyaad bin Swubayh akisema: “Niliswali pembezoni mwa Ibn ‘Umar nikaweka mikono yangu juu ya kiuno changu. Alipomaliza kuswali alisema: “ Huu ni msalaba katika Swalaah. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikataza”.  [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (903), An-Nasaaiy (2/127) na Ahmad (2/30) kwa Sanad ambayo haina tatizo].

 

As-Sandiy anasema: “ Umbo la msalaba katika Swalaah ni kuweka mikono yake kwenye nyonga zake na wakati anaposimama huviweka kando viunga bega vyake.

 

2- Kunyanyua macho mbinguni

 

Hili halijuzu kutokana na kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

(( لينتهن أقوام عن رفع أبصارهم عند الدعاء في الصلاة إلى السماء أو لتخطفن أبصارهم))

(( Hakika watakoma watu kunyanyua macho yao mbinguni wakati wanapoomba du’aa katika Swalaah au macho yao yatanyakuliwa)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (429) na An-Nasaaiy (3/39)]..

 

3- Kuangalia kishughulishacho

 

Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah asemaye kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali na guo lenye mistari stari akasema: ((Mistari stari ya hili imenishughulisha. Lichukueni kwa Abu Jahm, mniletee guo zito)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (752) na Muslim (556)].

 

4- Kugeuka bila haja

 

Tumeshaeleza nyuma kwamba inajuzu kugeuka ndani ya Swalaah kwa haja. Lakini kama hakuna haja ya kufanya hivyo, basi haijuzu. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Nilimuuliza Rasuli wa Allaah kuhusiana na kugeuka ndani ya Swalaah akasema:

(( هو اختلاس يختلسه الشيطان من صلاة العبد))

((Huo ni mnyakuo anaounyakua shaytwaan katika Swalaah ya mja)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (752) na Muslim (556)].

 

5- Kushikamanisha vidole vya mikono

 

Ni karaha mtu kuingiza vidole vya mkono mmoja kwenye vidole vya mkono mwingine kwa Hadiyth ya Abuu Hurayrah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إذا توضأ أحدكم في بيته ثم أتى المسجد كان في صلاة حتى يرجع، فلا يقل هكذا، وشبك بين أصابعه))

((Anapotawadha mmoja wenu nyumbani kwake kisha akaenda Msikitini, anazingatiwa yuko ndani ya Swalaah mpaka arejee. Basi  asifanye hivi. Akavishikamanisha vidole vyake)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (1/206). Ipo katika Swahiyhul Jaami’i (445) na kuna Hadiyth nyingine kama hii katika Musnadi ya Ahmad (3/42) toka kwa Abuu Sa’iyd].

 

Imepokelewa toka kwa Ismaa’iyl bin Umaymah akisema: “ Nilimuuliza Naafi’i kuhusu mtu anayeswali huku ameshikamanisha vidole akasema: Ibn ‘Umar amesema: Hiyo ni Swalaah ya walioghadhibikiwa”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (2/261), na Al-Albaaniy katika Al-Irwaa (2/103) kasema ni Hadiyth Swahiyh].

 

6- Kuminya vidole vitoe sauti

 

Kufanya hivi hata kama ni kudogo ni karaha, kwa kuwa humpumbaza mtu mbali na Swalaah, na kama kutakuwa ni kwingi, basi ni haramu, kwa kuwa itakuwa ni kuichezea Swalaah.

 

Shu’ubah mwachwa huru wa Ibn ‘Abbaas amesema: “Niliswali pembezoni mwa Ibn ‘Abbaas nikavivunja vidole vyangu. Nilipomaliza Swalaah aliniambia: “Mwanaharamu we! Unavunja vidole vyako nawe uko ndani ya Swalaah?!” [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Shaybah (2/334), na katika Al-Irwaa (2/99) imepewa daraja ya Hasan]

 

7- Kujizungushia nguo na kuiacha mikono ndani ukarukuu na kusujudu ikiwa ndani

 

Ni kwa Hadiyth ya Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kufanya “As-Sadl” ndani ya Swalaah.  [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (629) na At-Tirmidhiy (376) kwa Sanad Swahiyh].

 

“As-Sadl” ni kujizungushia nguo na kuiingiza mikono ndani, na wakati wa kurukuu na kusujudu inabakia humo humo.

 

8- Kwenda miayo

 

Haijuzu kuivuta sana, bali ni wajibu kuizuia kwa kuweka mkono kwenye kinywa kwa Hadiyth ya Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( التثاؤب ]في الصلاة[ من الشيطان فإذا تثاءب أحدكم فليكظم ما استطاع))

((Kwenda miayo [ndani ya Swalaah] kunatokana na shaytwaan. Anapokwenda mmoja wenu miayo, basi ajizuie awezavyo)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3289), Muslim (2994) na At-Tirmidhiy  (368), na ziada ni yake].

 

Hakuna uhalali wa kusema “A’uwdhu bil Laahi” kwa kuwa hakuna dalili inayothibitisha hilo. Ni ada iliyoenea kwa watu wengi bila kuwa na dalili yoyote.

 

9- Kutema mate upande wa Qiblah au upande wa kulia

 

Ni kwa Hadiyth ya Jaabir aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إن أحدكم إذا قام يصلي فإن الله تبارك وتعالى قبل وجهه، فلا يبصقن قبل وجهه ولا عن يمينه، وليبصق عن يساره تحت رجله اليسرى فإن عجلت به بادرة فليقل بثوبه هكذا))

((Hakika mmoja wenu anaposimama kuswali, basi Allaah Tabaaraka wa Ta’alaa Huukabili uso wake. Basi atahadhari asije kutema mate mbele yake au kuliani kwake, bali ateme kushotoni mwake chini ya mguu wake wa kushoto. Na ikiwa mate yatamzidi nguvu, basi afanye hivi kwa nguo yake)). Kisha akaikunjilia nguo yake sehemu juu ya sehemu. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (3008). Ishatajwa nyuma].

 

10- Kufumba macho

 

Ikiwa mtu atafanya hivyo kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah, basi ni haramu, kwani kunaingia katika mlango wa bid-’a, na kama si kwa lengo hilo, basi ni makruhu kwa kuwa anakwenda kinyume na Sunnah.

 

Ibn Al-Qayyim anasema: [Zaadul Ma’ad (1/294)]

 

“Haikuwa ni katika maongozi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufumba macho ndani ya Swalaah. Linaloonyesha kwamba hakuwa akifumba ni kunyoosha kwake mkono ndani ya Swalaah ya Kupatwa Jua ili akikamate kishada alipoiona Pepo. Pia kuuona Moto, mwanamke aliyeingia humo kwa kumtesa paka, pamoja na mdokozi aliyekuwa akiwaibia mahujaji kwa kutumia bakora yake. Aidha, kusukumana na mnyama aliyetaka kupita mbele yake wakati anaswali…[ametaja Hadiyth nyingi, kisha akasema:] Hadiyth hizi na nyinginezo, zote kwa pamoja zinatupa faida kwamba Rasuli hakuwa akifumba macho yake ndani ya Swalaah”.

 

11- Kunyoosha viungo

 

Ni karaha kujinyoosha isipokuwa kama ni kidogo kwa haja. Hii ni kwa vile kitendo hicho hakiendani na khushuu katika Swalaah. Ibn Abuu Shaybah (1/349) amepokea toka kwa Sa’iyd bin Jubayr akisema: “Kujinyoosha hupunguza (thawabu za) Swalaah”.

 

12- Kushikamanisha viganja katika rukuu

 

Hii ni kwa kuweka tumbo la kiganja kwenye tumbo la kiganja kingine, kisha kuviweka viganja viwili kati ya magoti mawili na mapaja mawili. Hili mwanzoni lilikuwa likiruhusiwa, kisha likakatazwa.

 

Imepokelewa toka kwa Musw-‘ab bin  Sa’ad akisema: “Niliswali pembezoni mwa baba yangu, kisha nikaweka mikono yangu kati ya magoti yangu. Baba yangu akanambia: “Kamata magoti yako kwa viganja vyako”, nami nikafanya vile vile kama mwanzo. Akanipiga mikono yangu miwili na kuniambia: Sisi tumekatazwa hivi, na tumeamuriwa tuyakamate magoti kwa viganja”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (790) na Muslim (535), na tamko ni lake].

 

13- Kusoma Qur-aan wakati wa kurukuu na kusujudu

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( ألا وإني نهيت أن أقرأ القرآن راكعا أو ساجدا))

((Tambueni kwamba mimi nimekatazwa kusoma Qur-aan nikiwa nimerukuu au nimesujudu)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (479) na ishaelezwa nyuma].

 

14- Kutandaza mikono miwili wakati wa kusujudu

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

(( اعتدلوا في السجود، ولا يبسط أحدكم ذراعيه انبساط الكلب))

((Lingamaneni katika sijdah, na mmoja wenu asitandaze mikono yake kama anavyoitandaza mbwa)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (823), Muslim (493) na wengineo].

Haifai kutandaza mikono miwili juu ya ardhi, bali vifundo viwili hunyanyuliwa kama tulivyoeleza nyuma.

 

15- Kuikusanya na kuifumbata nguo wakati wa kusujudu au kunyanyua mikono ya nguo

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “ Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuriwa asujudu juu ya viungo saba, na amekatazwa asibane au kuikusanya nguo au nywele”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (809) na Muslim (490), na tamko ni lake].

 

16- “Al-Iq’aa”, nako ni kuambatisha matako chini, kuinyanyua miundi miwili na kuiweka mikono chini.

 

Mkao huu haufai katika Swalaah kwa Hadiyth ya ‘Aaishah kuhusiana na sifa ya Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambapo anasema: “Alikuwa akikataza mkao wa shaytwaan”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (498)].

 

Mkao huu ndio huo tulioutaja wa “al-iqaa”.

 

Na katika Hadiyth ya Abuu Hurayrah anasema: “..na ametukataza tusidokoe mdokoo wa jogoo, na kukaa kikao cha mbwa”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/265) kwa Sanad Dhwa’iyf].

 

·       

Faida

 

“Al-Iq’aa” kwa maana hii haijuzu kwa dalili zilizotangulia. Lakini ninatanabahisha hapa kwamba neno hili lina maana nyingine ambayo ni kusimamisha miguu miwili, na kuweka matako mawili juu ya visigino wakati wa kikao kati ya sijdah mbili. Kikao hiki kinaruhusika kisharia.

 

17- Kuweka mkono chini wakati wa kikao ila kwa udhuru

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu anapokaa katika Swalaah kutegemea mkono wake wa kushoto”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1/260), Ahmad (2/116), Al-Haakim (1/230) na Al-Bayhaqiy (2/136)].

 

Na katika riwaya nyingine Ibn ‘Umar amesema: “Usikae hivi, kwani wanaoadhibiwa ndivyo wanavyokaa”.

 

18- Mgonjwa kusujudu juu ya kitu kilichonyanyuka

 

Ikiwa mgonjwa ataweza kusujudu chini, basi itakuwa ni wajibu kwake, lakini kama hawezi, ataashiria kwa kichwa. Si lazima aweke mto au mfano wake ili asujudie juu yake.

 

Hii ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimzuru mgonjwa katika mmoja wa Maswahaba wake, nami nilikuwa naye. Akaingia kwa mgonjwa akamkuta anaswali juu ya ujiti, na mgonjwa akaweka kipaji chake juu ya ujiti. Rasuli akamwashiria, kisha akaondosha ujiti. Mgonjwa akachukua mto na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

((Achana nao, kama utaweza kusujudu juu ya ardhi (ni bora), na kama huwezi, basi ashiria. Inama zaidi kwenye sijdah yako kuliko unavyoinama katika rukuu)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr (12/270). Ina Hadiyth mwenza ya Jaabir kwa Al-Bazzaar (1/275) katika kitabu cha Kashful Astaar, na Al-Bayhaqiy (2/306). Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh katika Asw-Swahiyha (323)]

 

19- Kupangusa vijiwe sehemu ya kusujudia na kucheza cheza

 

Inafaa ikiwa ni kwa haja ya dharura sana lakini mara moja tu. Kuacha itakuwa ni bora zaidi ikiwa kuwepo kwa vijiwe hivyo hakumwathiri mtu kufanya khushuu. Ni kwa Hadiyth ya Mu’ayqiyb kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mtu mmoja aliyekuwa anauweka sawa mchanga pale anaposujudu:

((Ikiwa ni mwenye kufanya, basi ni mara moja tu)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1207) na Muslim (546)].

 

Na katika riwaya nyingine: ((Usipanguse ukiwa katika Swalaah, na kama itabidi ufanye, basi sawazisha vijiwe mara moja tu)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1/249). An-Nawawy amesem kwamba Isnadi yake iko juu ya sharti ya Al-Bukhaariy na Muslim].

 

·       

Faida

 

Ikiwa mchanga au vijiwe vitakamata kipaji kutokana na kusujudu juu ya ardhi, basi ni karaha kuviondosha kwa kuwa ni kitendo kinachomshughulisha mtu mbali na Swalaah yake, na hususan kama kitendo kitakariri.

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Sa’iyd akisema: “Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisujudu kwenye maji na udongo mpaka nikaona alama ya udongo katika kipaji chake”.  [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (669) na Muslim (1167)].

 

Ibn Mas-’oud anasema: “Manne si katika mambo ya staha. Akataja kati yake: Mtu kupangusa vumbi la usoni wakati yuko ndani ya Swalaah”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (2/285). Al-Albaaniy katika Al-Irwaa (1/97) kasema kuwa ni Hadiyth Swahiyh].

 

Lakini ikiwa vumbi hilo linamkera na kumsumbua mwenye kuswali, basi atalifuta na kuliondosha. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

20-Kutanguliza magoti mawili kabla ya mikono miwili chini wakati wa kwenda kusujudu

 

Imepokelewa na Abuu Hurayra akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إذا سجد أحدكم فلا يبرك كما يبرك البعير وليضع يديه قبل ركبتيه))

((Anaposujudu mmoja wenu, basi asitangulize magoti kama anavyofanya ngamia, bali aweke mikono yake kabla ya magoti yake)). [Takhriyj yake imeelezwa nyuma].

 

21- Kuashiria kwa mikono miwili pambizo mbili wakati wa kutoa tasliym

 

Desturi hii ambayo imekatazwa katika Swalaah, imeenea kwa watu wengi wa kawaida wake kwa waume.

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir bin Samrah akisema: “Tulikuwa tunaposwali pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tunasema: As-Salaam ‘alaykum wa rahmatul Laahi, As-Salaam ‘alaykum wa rahmatul Laahi; akaashiria pambizo mbili kwa mkono wake. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia:

(( علام تومئون  بأيديكم كأذناب خيل شمس؟ إنما يكفي أحدكم أن يضع يده على فخذه ثم يسلم على أخيه، من على يمينه وشماله))

((Mnaashiria kitu gani kwa mikono yenu kama mikia ya farasi waliotibuka? Hakika inamtosha mmoja wenu kuweka mkono wake juu ya paja lake, kisha atoe tasliym kwa nduguye aliyeko kuliani na aliyeko kushotoni)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (431), An-nasaaiy (1185) na Abuu Daawuud (998)].

 

22- Kumtangulia imamu

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( أما يخشى أحدكم إذا رفع رأسه قبل الإمام أن يجعل الله رأسه رأس الحمار، أو يجعل الله صورته صورة حمار))

((Je, haogopi mmoja wenu Allaah kukigeuza kichwa chake kichwa cha punda kama atakinyanyua kabla ya imamu, au Allaah kuifanya sura yake kuwa sura ya punda?)) [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (691), Muslim (427) na wengineo].

 

23- Baada ya kutengwa chakula au kubanwa na haja ndogo au kubwa

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Nimemsikia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( لا صلاة بحضرة الطعام ولا وهو يدافعه الأخبثان))

((Hapana Swalaah chakula kikiwa tayari, wala kwa aliyebanwa na haja ndogo au haja kubwa)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (560) na Abuu Daawuud (89)].

 

 

 
Share