025-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Qiyaamul Layl

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

025-Qiyaamul Layl

 

 

Qiyaamul layl huitwa Tahajjud. Jamhuri ya Maulamaa wanaielezea kama ni Swalaah ya Sunnah inayoswaliwa usiku baada ya kulalakatika usiku wowote katika mwaka. [Mughnil Muhtaaj (1/228)]

 

· Fadhila Za Qiyaamul Layl Na Kuraghibishwa Kwake

 

Swalaah ya Sunnah usiku wa manane kwenye kiza totoro, ina fadhila kubwa sana na thawabu adhimu zisizohesabika ambazo hakuna mtu yeyote awezaye kuzielezea. Ni nembo ya watu wema na ni sifa muhimu mahsusi ya Muttaqiyn.

 

Kutokana na fadhila yake kubwa, Allaah Mtukufu Alimwagiza Rasuli Wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aikabili na avaane na sharafu hii adhimu na fadhila hii kubwa ili aweze kuipata “Al-Maqaamu Al-Mahmoud” Akamwambia:

((وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا ))

((Na katika usiku, amka uswali (tahajjud) kuisoma (Qur-aan); ni ziada ya Sunnah kwako Asaa Rabb wako Akakuinua cheo kinachosifika)). [Al-Israa (17:79)]

 

Kuna Aayah na Hadiyth nyingi sana zinazoelezea fadhila za Qiyaamul Layl na kuraghibishia. Tutazitaja baadhi yake ili mwenye utashi na maisha hayo ya baraka aingiwe na hamu ya kujisikia na kujiridhisha nafsi yake, na akajiwekea azma ya kulitenda hilo angalau kwa kiasi kidogo.

 

1- Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

((لَيْسُوا سَوَاءً ۗ مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ أُمَّةٌ قَائِمَةٌ يَتْلُونَ آيَاتِ اللَّـهِ آنَاءَ اللَّيْلِ وَهُمْ يَسْجُدُونَ ))

((Hawako sawa sawa; miongoni mwa Ahlil-Kitaabi wako watu wenye kusimama (kwa utiifu) wanasoma Aayaat za Allaah nyakati za usiku na wao wanasujudu (katika Swalaah)). [Aal-‘Imraan (3:113)]

 

2 -Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

((وَعِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلَامًا   وَالَّذِينَ يَبِيتُونَ لِرَبِّهِمْ سُجَّدًا وَقِيَامًا))

(( Na Waja wa Ar-Rahmaan ni wale wanaotembea katika ardhi kwa unyenyekevu na upole, na majahili wanapowasemesha, wao husema: Salaam! ● Na wale wanaokesha usiku kwa ajili ya Rabb wao wakisujudu na kusimama)). [Al-Furqaan (25 :63 na 64)]

 

3- Anasema Subhaanah:

((يَا أَيُّهَا الْمُزَّمِّلُ قُمِ اللَّيْلَ إِلَّا قَلِيلًا نِّصْفَهُ أَوِ انقُصْ مِنْهُ قَلِيلًا أَوْ زِدْ عَلَيْهِ وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا))

((Ee uliyejifunika ● Simama (kuswali) usiku kucha isipokuwa kidogo tu ● Nusu yake, au ipunguze kidogo ● Au izidishe, na soma Qur-aan kwa kisomo cha utaratibu upasao, kuitamka vizuri na kutaamali)). [Al-Muzzammil ( 73: 1-4)]

 

4- Anasema Subhaanah:

((وَاذْكُرِ اسْمَ رَبِّكَ بُكْرَةً وَأَصِيلًا وَمِنَ اللَّيْلِ فَاسْجُدْ لَهُ وَسَبِّحْهُ لَيْلًا طَوِيلًا))

((Na lidhukuru Jina la Rabb wako asubuhi na jioni ● Na katika usiku msujudie na uswali kwa ajili Yake usiku mrefu)). [Al-Insaan (76: 25 na 26)]

 

5- Anasema Subhaanah:

((أَمَّنْ هُوَ قَانِتٌ آنَاءَ اللَّيْلِ سَاجِدًا وَقَائِمًا يَحْذَرُ الْآخِرَةَ وَيَرْجُو رَحْمَةَ رَبِّهِ ۗ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗإِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ))

(( Je, yule aliye mtiifu nyakati za usiku akisujudu, au akisimama (kuswali), anatahadhari na aakhirah na anataraji rahmah ya Rabb wake (ni sawa na aliyekinyume chake?). Sema: “Je, wanalingana sawa wale wanaouja na wale wasiojua?” Hakika wanakumbuka wenye akili tu)). [Az-Zumar (28 :9)]

 

6-Anasema Subhaanah:

(( إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ   آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُحْسِنِين كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ))

((Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu ● Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani ● Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha ● Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah)). [Adh-dhaariyaat ( 51:15-18)]

 

7- Anasema Subhaanah:

((إِنَّمَا يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا الَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِهَا خَرُّوا سُجَّدًا وَسَبَّحُوا بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ))

(( Hakika wanaamini Aayaat Zetu wale wanapokumbushwa nazo huporomoka kusujudu, na wakasabbih kwa Himidi za Rabb wao, nao hawatakabari ● Mbavu zao zinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa ● Basi nafsi yoyote haijuiyaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda)). [As-Sajdah (32 :15-17)]

 

8- Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema: “Rasuli wa Allaah aliulizwa: “Ni Swalaah ipi bora zaidi baada ya Swalaah za faradhi?” Akasema: ((Ni Swalaah usiku wa manane)). Akaulizwa: “Ni swawm ipi bora zaidi baada ya Ramadhwaan?” Akasema: ((Ni Mwezi wa Allaah wa Muharram)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1163), At-Tirmidhiy (438), Abu Daawuud (2429), An-Nasaaiy (3/207) na Ibn Maajah (1742)].

 

9- Imepokelewa na ‘Abdullaah bin Salaamah (Radhwiya Allaahu Anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( أيها الناس، أفشوا السلام وأطعموا الطعام، وصلوا الأرحام، وصلوا بالليل والناس نيام، تدخلوا الجنة بسلام))

((Enyi watu! Enezeni amani, lisheni watu chakula, ungeni ukoo, swalini usiku watu wakiwa wamelala, mtaingia Peponi kwa amani)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (1855), Ibn Maajah (1334) na Ahmad (7591). Angalia Asw-Swahiyhah (569)].

 

10- Abuu Maalik Al Asha-’ariy amepokea toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( إن في الجنة غرفا يرى ظاهرها من باطنها، وباطنها من ظاهرها، أعدها الله لمن أطعم الطعام وأفشى السلام وصلى بالليل والناس نيام))

((Peponi kuna vyumba; nje yake huonekana toka ndani yake, na ndani yake huonekana toka nje yake. Allaah Amevitayarisha kwa ajili ya mwenye kulisha chakula, akaeneza amani, akaswali usiku na watu wamelala)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Hibaan (509) na wengineo. Angalia Swahiyhut Targhiyb (614) na Swahiyhul Jaami’i (2123)].

 

11- Imepokelewa toka kwa ‘Amri bin ‘Absah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( أقرب ما يكون الرب من العبد في جوف الليل الآخر، فإن استطعت أن تكون ممن يذكر الله في تلك الساعة فكن))

((Wakati ambao Mola Huwa karibu zaidi na Mja Wake, ni mwisho wa usiku wa manane. Ikiwa wewe utaweza kuwa ni katika wanaomdhukuru Allaah katika saa hizo, basi fanya)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (3579) na An-Nasaaiy (572). Angalia Swahiyhut Targhiyb (624) na Swahiyhul Jaami’i (1184)].

 

12- Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu Anhu) anasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( رحم الله رجلا قام من الليل فصلى، وأيقظ امرأته ] فصلت [ فإن أبت نضح في وجهها الماء، ورحم الله امرأة قامت من الليل فصلت، وأيقظت زوجها ] فصلى [ فإن أبى نضحت في وجهه الماء))

((Allaah Amrehemu mtu aliyesimama usiku akaswali, na akamwamsha mkewe [akaswali]. Na kama atakataa, atamnyunyizia usoni maji. Na Allaah Amrehemu mwanamke aliyesimama usiku akaswali, na akamwamsha mumewe [akaswali]. Na kama atakataa, atamnyunyizia usoni maji)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud ( 1308), An-Nasaaiy (3/205), Ibn Maajah (1336) na Ahmad (2/250). Iko katika Swahiyhul Jaami’i (3488).]

 

Na katika tamshi jingine:

(( إذا قاما وصليا ركعتين كتبا من الذاكرين الله كثيرا والذاكرات))

((Wakisimama wakaswali rakaa mbili, wataandikwa ni katika wanaume wenye kumdhukuru Allaah kwa wingi na wanawake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1309), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (1310) na Ibn Maajah (1335). Iko katika Swahiyhul Jaami’i (330)].

 

13- Imepokelewa toka kwa Abu Dharri toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( ثلاثة يحبهم الله...- فذكر منهم -.. ورجل سافر مع القوم فارتحلوا حتى إذا كان من آخر الليل وقع عليهم الكرى فنزلوا، فضربوا برؤوسهم، ثم قام فتطهر، وصلى رغبة لله عز وجل، ورغبة لله عز وجل، ورغبة فيما عنده))

((Watu watatu Allaah Anawapenda – kati ya aliowataja -..ni mtu aliyesafiri na watu, wakaenda mpaka ilipofika mwisho wa usiku, wakapatwa na usingizi wakapumzika na wakalala. Kisha mtu huyo akasimama, akatawadha, kisha akaswali kwa ajili ya raghba kwa Allaah ‘Azza wa Jalla, na kwa ajili ya hamu ya kuyapata yaliyoko Kwake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (5/176), At-Twayalsiy (468), At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr (2/1637) na Al-Bayhaqiy (9/160)].

 

14- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( عليكم بقيام الليل، فإنه دأب الصالحين قبلكم، وقربة إلى الله، ومنهاة عن الإثم، وتكفير للسيئات))

((Jilazimisheni kusimama usiku, kwani huo ndio mwenendo wa watu wema kabla yenu, ni kujikurubisha kwa Allaah, ni katazo la madhambi na kifutio cha mabaya)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Angalia Al-Irwaa (452) na Swahiyhul Jaami’i (3958)].

 

15- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba aliona njozi akamhadithia Hafswah, naye Hafswah akamhadithia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Rasuli akasema:

(( نعم الرجل عبد الله، لو كان يصلي من الليل))

((Mbora wa watu ni ‘Abdullaah, laiti angelikuwa anaswali usiku)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1122) na Muslim (2479)].

 

Na katika tamko jingine:

(( إن عبد الله رجل صالح، لو كان يكثر الصلاة من الليل))

((Hakika ‘Abdullaah ni mtu mwema, laiti angelikuwa anakithirisha kuswali usiku)).

Saalim anasema: “ ‘Abdullaah tokea baada ya hapo, alikuwa halali usiku isipokuwa kidogo”.

Al-Qurtubiy amesema: “Hakuwa akiswali usiku, na kutokana na hilo, ‘Abdullaah alipata zindusho kwamba kusimama usiku ni katika amali za kujikinga nazo na moto na kuukurubia. Na kwa ajili hiyo, hakuacha tena kuswali usiku baada ya hapo”.

 

16- Imepokelewa toka kwa Ummu Salamah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamka usiku mmoja (kwa mshtuko) akasema:

((سبحان الله، ماذا أنزل الليلة من الفتن، ماذا أنزل من الخزائن، من يوقظ صواحب الحجرات، يا رب كاسية في الدنيا عارية يوم القيامة))

((Subhaanal Laah! Ni wingi ulioje wa fitna zilizoteremshwa usiku huu! Ni wingi ulioje wa hazina za rahmah zilizofunguliwa! Nani atawaamsha walioko vyumbani? Ee (mwenye kusikia)! Huenda anayevaa duniani, asivae kitu Siku ya Qiyaamah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1126) na At-Tirmidhiy (2196)].

 

Hadiyth hii inatupa funzo kwamba mtu anatakiwa amwamshe mkewe usiku kwa ajili ya ‘ibaadah na hususan wakati wa kuteremka tukio fulani. Yamesemwa haya katika Al-Fat-h.

 

Ninasema: “Hii ni sehemu tu ya Aayah na Hadiyth kochokocho zinazogusia kuhusu fadhila za kusimama usiku na kuraghibisha hilo. Nyinginezo zitakuja Insha Allaah katika sehemu iliyobakia ya mlango wa “Qiyaamul Layl”, nazo huenda zikapata moyo mkweli ukanufaika, nami nikapata –Bi Idhnil Laahi – thawabu za kuongozea kwenye kheri”.  [Kati ya mambo muhimu yanayomsaidia mtu kusimama usiku, ni kusoma wasifu wa watu wema kuhusiana na suala hili. Kati ya yaliyo kusanya zaidi na yenye utamu zaidi katika niliyoyasoma kuhusiana na hili, ni yale yaliyoko katika kitabu cha “Ruhbaanul Layl” cha Sheikh Al-Habiyb Al-Hammaam mwandishi asiyeweka kalamu chini. Basi jitahidi ukipate]

 

· Wakati Wa Qiyaamul Layl

 

Swalaah ya usiku inajuzu kuiswali mwanzoni mwa usiku, katikati yake na mwishoni mwake. Yote hayo aliyafanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Hatukutaka kumwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku akiswali ila tulimwona, na hatukutaka kumwona amelala ila tulimwona”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1090), An-Nasaaiy (1627) na tamko ni lake, na At-Tirmidhiy (769)].

 

Al-Haafidh amesema katika Al-Fat-h (3/23): “Kwa maana kwamba kuswali kwake na kulala kwake kulikuwa kukitofautiana usiku, na hakuwa akipanga wakati maalumu, bali ilikuwa kwa mujibu wa itakavyowepesika kwake”.

 

· Wakati Wake Ulio Bora Zaidi

 

Imesuniwa kuswali Qiyaamul Layl katika theluthi ya mwisho ya usiku kwa ajili ya kuvipata Vipawa Adhimu vya Allaah katika masaa hayo ambapo hawaamki kwa ajili ya kumwabudu Allaah ila watu kidogo mno. Watu hawa ndio wanaopata kujibiwa du’aa zao, wanaokubaliwa toba zao, wanaopata maghfirah na kusitiriwa na kasoro zao.

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( ينزل الله إلى السماء الدنيا كل ليلة حين يبقى ثلث الليل فيقول: أنا الملك، من الذي يدعوني فأستجيب له، من الذي يسألني فأعطيه، من الذي يستغفرني فأغفر له)) وفي لفظ لمسلم (758) (( حتى ينفجر الفجر))

((Allaah Huteremka katika mbingu ya dunia kila usiku wakati inapobakia theluthi ya usiku Akasema: Mimi Ndiye Mfalme. Nani aniombaye Nikamjibu? Nani anitakaye haja Nikampa? Nani aniombaye maghfirah Nikamghufiria?)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1145) na Muslim (758) na tamko ni lake].

 

Na katika tamko la Muslim: ((Mpaka Alfajiri ipambazuke)).

 

Imepokelewa na ‘Amri bin ‘Absah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( أقرب ما يكون الرب من العبد في جوف الليل الآخر، فإن استطعت أن تكون ممن يذكر الله في تلك الساعة فكن))

((Wakati ambao Mola Huwa karibu zaidi na Mja Wake, ni mwisho wa usiku wa manane. Ikiwa wewe utaweza kuwa ni katika wanaomdhukuru Allaah katika saa hizo, basi fanya)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa hivi karibuni].

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin ‘Amri kwamba Rasuli wa Allaah amesema:

(( إن أحب الصيام إلى الله صيام داود، وأحب الصلاة إلى الله عز وجل صلاة داود، كان ينام نصف الليل، ويقوم ثلثه، وينام سدسه، وكان يصوم يوما ويفطر يوما ))

((Hakika Swiyaam inayopendeza zaidi kwa Allaah ni Swiyaam ya Daawuud, na Swalaah inayopendeza zaidi kwa Allaah ‘Azza wa Jalla ni Swalaah ya Daawuud. Alikuwa akilala nusu ya usiku, akisimama katika theluthi yake na akilala katika sudusi yake. Na alikuwa akifunga siku moja na kula siku moja)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1131) na Muslim (1159)].

 

 Na hivi ndivyo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akifanya. ‘Aaishah akiielezea Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: “Alikuwa akilala mwanzo wake, anasimama mwishoni mwake akaswali, kisha hurejea kwenye tandiko lake. Na mwadhini anapoadhini hutoka haraka. Na kama ana kitu hivi huoga, na kama hana, hutawadha akatoka”. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa hivi karibuni].

 

Imepokelewa toka kwa Ummu Salamah Hadiyth kama hii.

 

Na katika Hadiyth ya Humayd bin ‘Abdul Rahmaan kuhusiana na Swahaba Mmoja wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesuhubiana naye katika safari anatuambia: “Kisha akasimama akaswali mpaka nikasema: Hakika ameswali kiasi cha alivyolala, kisha akalala mpaka nikasema: Hakika amelala kiasi cha alivyoswali. Halafu akaamka, akafanya kama alivyofanya mwanzoni, na akasoma mfano wa alivyosoma. Halafu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akafanya mara tatu kabla ya Alfajiri”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1626). Ina Hadiyth mwenza iliyopokelewa toka kwa Ummu Salamah].

 

Imepokelewa toka kwa Masrouq kwamba alimuuliza ‘Aaishah: “Ni wakati gani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali?” Akasema: “Alikuwa anapomsikia jogoo, hunyanyuka akaswali”.

 

Ni kawaida ya jogoo kuwika usiku wa manane au katika theluthi ya usiku.

 

· Adabu Za Qiyaamul Layl

 

Mtu ambaye Allaah Amekikunjua kifua chake na akataka kuswali Qiyaamul Layl, basi imesuniwa azichunge adabu zifuatazo:

 

1- Ajiandae kwa kufanya mambo yatakayomsaidia kuamka. Kati ya mambo hayo ni:

 

(a) Kulala mchana qayluulah kama itakuwa wepesi kwake.

(b) Kutokukesha katika yasiyokuwa na maslaha ya kisharia. Tumeshazungumzia kuhusu ukaraha wa kupiga gumzo baada ya ‘Ishaa isipokuwa katika maslaha ya kisharia.

(c) “Ni bora kwa aliyezidiwa na uvivu na kupondokea ureda na kujisikia, asikisheheneshi sana kitanda, kwani hilo huleta usingizi mwingi, mghafiliko na kuachana na majukumu ya mambo ya kheri”. [Faydhul-Qadiyr (5/180)]

 

Ninasema: “Tandiko la Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lilikuwa kavu. Imepokelewa toka kwa ‘Umar akisema: “Niliingia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nikamkuta  amelala juu ya mkeka nami nikakaa. Akaiteremsha izari yake, nayo ni moja tu, hana nyingine. Nikatahamaki kuona alama za mkeka kwenye ubavu wake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2468) na Muslim (1479) na tamko ni lake].

 

Na ‘Aaishah anasema: “Mto wake aliokuwa akilalia usiku, ulikuwa ni wa ngozi uliojazwa ufumwele”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (4146) na At-Tirmidhiy. Iko katika Swahiyhul Jaami’i (4714)].

 

2- Wakati anapolala, anuwie kwamba ataamka

 

Imepokelewa toka kwa Abu Ad-Dardaai kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( من أتى إلى فراشه وهو ينوي أن يقوم فيصلي من الليل، فغلبته عينه حتى يصبح كتب له ما نوى، وكان نومه صدقة عليه من ربه))

((Mwenye kwenda kulala nailhali ananuwia kwamba aamke usiku kisha usingizi ukamzidia mpaka akapambaukiwa, basi ataandikiwa alilolinuwia, na usingizi wake unakuwa ni swadaqah kwake toka kwa Mola wake)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1784), Ibn Maajah (1344) na Al-Bayhaqiy (3/15)].

 

3- Alale na wudhuu wake

 

Tumeeleza katika mlango wa wudhuu kwamba huu ulikuwa ni mwenendo wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

4- Alale kwa ubavu wake wa kuume

 

Imepokelewa toka kwa Hafswah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapolala, huweka mkono wake wa kulia juu ya shavu lake la kulia”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Angalia katika Swahiyhul Jaami’i (4523)].

 

Kulala kwa ubavu wa kulia ndiyo fitwrah kama itakavyokuja katika Hadiyth ya Al-Barraa bin ‘Aazib.

 

· Faida

 

Kuna siri nyeti kuhusiana na kulala Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ubavu wake wa kulia. Siri yenyewe ni kuwa damu nzito imening’inia upande wa kushoto. Na mtu anapolalia ubavu wake wa kushoto usingizi huwa mzito, kwa vile anakuwa yuko katika hali ya ushwari na utulivu, na hapo usingizi humzidia. Ama akilalia ubavu wake wa kulia, hapo hawi katika hali ya ushwari na utulivu, na usingizi haumchukui mzima mzima kwa vile moyo hauwi mtuvu na haupondokei kwenye utulivu. Na kwa ajili hiyo, madaktari wanawashauri watu kulalia ubavu wa kushoto ili kupata mapumziko kamili na usingizi mzuri. Lakini Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapendelea kulalia ubavu wa kulia ili mtu asilale usingizi mzito akashindwa kuamka kuswali Qiyaamul Layl. Kulalia ubavu wa kulia kuna manufaa zaidi kwa moyo, na kwa ubavu wa kushoto kuna manufaa zaidi kwa mwili. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”. [Zaadul Ma’ad cha Ibn Al-Qayyim (1/321/322)]

 

5- Akichelea kutoweza kuamka, basi aswali Witr kabla ya kulala

 

Ikiwa ataamka, ataswali kiasi atakacho lakini bila ya kuikariri Witr. Haya yashaelezwa katika mlango wa Witr.

 

6- Amdhukuru Allaah wakati anapolala

 

Kuna adhkaar nyingi zilizopokelewa kwa njia Swahiyh kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kati ya adhkaar hizo ni:

 

(a) Hadiyth ya ‘Aaishah asemaye: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapokwenda kulala kila usiku, huvikusanya viganja vyake, kisha huvipulizia akivisomea: (Qul Huwa Allaahu Ahad),  (Qul A’uwdhu bi Rabbil Falaq) na (Qul A’uwdhu bi Rabbi An Naas), halafu hujipangusa kwavyo mwili pale vinapoweza kufika katika viungo vyake. Huanza kupangusa kichwa chake na uso wake, kisha sehemu ya mbele ya mwili wake. Hufanya hivi mara tatu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5018) na Muslim (2192)].

 

(b) Imepokelewa na Abu Hurayrah kwamba shaytwaan alimwambia wakati alipotaka kumpeleka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Niache nikufundishe maneno ambayo Allaah Atakufaa nayo: Ukienda kulala, basi soma Aayatul Kursiy (Allaahu Laailaaha illaa Huwa Al-Hayyu Al-Qayyuwm….)mpaka mwisho, utaendelea kupata mlinzi toka kwa Allaah, na shaytwaan hatokukurubia mpaka upambazukiwe”. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Amekwambia kweli lakini ni mwongo mno, na huyo ni shaytwaan)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy ikiwa Mu’allaq (3275) na An-Nasaaiy katika “Mlango wa Amali za Mchana na Usiku” (959)].

 

(c) Imepokelewa toka kwa Abu Mas-’oud Al-Answaariy toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((Mwenye kuzisoma Aayah mbili za mwisho za Suwrat Al-Baqarah zitamtosheleza)).

 [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4008) na Muslim (808)].

 

Kwa maana kwamba zitamlinda na shari na adha. Imesemwa pia  kwa maana ya kuwa zitamtosheleza na kusimama usiku kuswali.

 

(d) Imepokelewa toka kwa Nawfal Al-Ashja’iy akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia: ((Soma: (Qul yaa ayyuhal kaafiruwn)) halafu lala ukiifanya Suwrah ya mwisho kuisoma, kwani ni utakaso na shirk)). [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (5055), At-Tirmidhiy (3401) na Ahmad (5/456). Angalia Swahiyh At-Targhiyb (604) na Swahiyhul Jaami’i  (1161)].

 

(e) Imepokelewa toka kwa Hudhayfah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotaka kulala husema: ((Bismika Al-Laahumma amuwtu wa ahyaa)), na anapoamka usingizini husema: ((Alhamdu lil Laahi Al Ladhiy Ahyaanaa ba’ada maa Amaatanaa wa ilahyi an nushuwr)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6312), Abu Daawuud (5049) na At-Tirmidhiy (3413)].

 

(f) Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إذا قام أحدكم عن فراشه ثم رجع إليه فلينفضه بصنفة إزاره ثلاث مرات، فإنه لا يدري ما خلفه عليه بعده، وإذا اضطجع فليقل: "باسمك ربي وضعت جنبي، وبك أرفعه، فإن أمسكت نفسي فارحمها، وإن أرسلتها فاحفظها بما تحفظ به عبادك الصالحين))

((Anaponyanyuka mmoja wenu toka kitandani mwake, kisha akarejea tena, basi akikung’ute kwa ncha ya nguo yake mara tatu, kwani hajui alivyoviacha humo. Na anapolala aseme: “Kwa Jina Lako ee Mola wangu! Nimeuweka ubavu wangu, na kwa Msaada Wako naunyanyua, ikiwa Utaikamata nafsi yangu basi Irehemu, na ikiwa Utaiachia basi Ihifadhi kwa yale Unayowahifadhia Waja Wako wema”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6320) na Muslim (2714)].

 

(g) Imepokelewa toka kwa ‘Aliy bin Abiy Twaalib kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia yeye pamoja na Faatwimah wakati walipomuulizia kuhusu mtumishi:

(( ألا أدلكما على ما هو خير لكما من خادم: إذا آويتما إلى فراشكما فسبحا ثلاثا وثلاثين، واحمدا ثلاثا وثلاثين، وكبرا ثلاثا وثلاثين، فإنه خير لكما من خادم ))

((Je, niwaambieni lililo bora zaidi kwenu kuliko mtumishi? Mkienda kulala, basi semeni “Subhaana Allaah” mara 33, “Al Hamdu lil Laah” mara 33, na “Allaahu Akbar” mara 33. Hivyo ni bora zaidi kwenu kuliko mtumishi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3705) na Muslim (2727)].

 

(h) Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba alimwamuru mtu mmoja aliyelalia kitanda chake aseme: ((Ee Mola wangu! Wewe Umeiumba nafsi yangu na Wewe Ndiye Unayeilinda, mauti yake na uhai wake ni Kwako. Ukiipa uhai basi Ihifadhi, na Ukiifisha basi Ighufirie. Ee Mola wangu! Mimi nakuomba afya kamili)).

Ibn ‘Umar akasema: “Nimeyasikia haya toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2712), An Nasaaiy katika “Al-Yawm wa Al-Laylah” (796) na Ahmad (2/79)].

 

Imesuniwa amalizie adhkaar zilizotangulia ambazo zitakuwa nyepesi kwake kwa yaliyomo ndani ya Hadiyth hii ifuatayo:

 

(i) Imepokelewa toka kwa Al-Barraa bin ‘Aazib akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إذا أتيت مضجعك، فتوضأ وضوءك للصلاة ثم اضطجع على شقك الأيمن، وقل: اللهم أسلمت وجهي إليك، وفوضت أمري إليك، وألجأت ظهري إليك، رغبة ورهبة إليك، لا ملجأ ولا منجا منك إلا إليك، آمنت بكتابك الذي أنزلت، وبنبيك الذي أرسلت، فإن مت مت على الفطرة، فاجعلهن آخر ما تقول))

((Ukienda kulala, basi tawadha wudhuu wa Swalaah, kisha lalia ubavu wako wa kulia halafu sema: Ee Mola wangu! Nimeusalimisha uso wangu Kwako, nimetegemeza jambo langu Kwako, nimeuelekeza mgongo wangu Kwako. Nina raghba na hofu kuelekea Kwako, na hakuna makimbilio wala maokozi kutokana na Wewe ila Kwako. Nimekiamini Kitabu Chako Ulichokiteremsha, na Nabiy Wako Uliyemtuma. Ikiwa utakufa, basi utakufa katika fitwrah, basi yafanye kuwa ndiyo maneno yako ya mwisho)).

Nikasema kujikumbusha: “Na kwa Rasuli Wako Uliyemtuma”, akaniambia: ((Hapana, na kwa Nabiy Wako Uliyemtuma)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (247) na Muslim (2710)].

 

7- Apanguse uso kuondosha usingizi kama ataamka, amdhukuru Allaah na atawadhe

 

(a) Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( يعقد الشيطان على قافية رأس أحدكم إذا هو نام ثلاث عقد، يضرب على كل عقدة مكانها: عليك ليل طويل فارقد، فإن استيقظ وذكر الله تعالى انحلت عقدة، فإن توضأ انحلت عقدة، فإن صلى انحلت عقده كلها فأصبح نشيطا طيب النفس، وإلا أصبح خبيث النفس كسلان))

((Anapolala mmoja wenu, shaytwaan hufunga kisogoni mwake vifundo vitatu. Hukikita kila kifundo mahala pake (akimwambia): Umebakiwa na usiku mrefu, basi lala. Anapoamka akamtaja Allaah, kifundo kimoja hufunguka. Anapotawadha hufunguka kingine, na anaposwali cha tatu hufunguka. Hapo huwa mchangamfu na mwenye nafsi nzuri, na kama si hivyo, huwa na nafsi mbaya na mvivu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1142) na Muslim (776)].

 

(b) Imepokelewa toka kwa ‘Ubaadah bin Swaamit toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( من تعار من الليل فقال: لا إله إلا الله وحده لا شريك له، له الملك وله الحمد، وهو على كل شيء قدير، الحمد لله، وسبحان الله، ولا إله إلا الله، والله أكبر، ولا حول ولا قوة إلا بالله، ثم قال: اللهم اغفرلي، أو دعا، استجيب له، فإن توضأ وصلى قبلت صلاته))

((Mwenye kuamka usiku akasema: Laa ilaaha illa Allaahu wahdahuu laa shariyka lahu, lahul Mulku walahul Hamdu, wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr. Al-Hamdu lil Laah, wa Subhaana Allaah, wa laa ilaaha illa Allaahu, wa Allaahu Akbar, wa laa hawla walaa quwwata illaa bil Laah. Kisha akasema: Allaahumma Ighfir liy, au akaomba, du’aa yake hujibiwa. Na kama atatawadha akaswali, Swalaah yake hukubaliwa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1154), At-Tirmidhiy (3414), Abu Daawuud (5060) na Ahmad (5/313)].

 

(c) Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Nililala kwa khalati yangu Maymuunah mke wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mimi nililalia mto kwa upana, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mkewe wakalalia kwa urefu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akalala, na ilipoingia katikati ya usiku – au kabla yake kwa kidogo au baada yake kwa kidogo – aliamka, akakaa akiupangusa uso wake kwa mkono wake kutoa usingizi. Kisha akazisoma Aayah kumi za mwisho za Suwrat Aal-‘Imraan. Halafu akaenda kwenye kiriba cha ngozi, akatawadhia maji yake wudhuu kamili uliotimia, kisha akasimama kuswali…..” [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (183) na Muslim (763)]

 

Aayah zinazokusudiwa hapa ni:

((إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ....))

..mpaka mwisho wa Suwrat Aal-‘Imraan.

 

8- Apige mswaki

 

Imepokelewa toka kwa Hudhayfah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapoamka usiku (katika riwaya nyingine: kwa ajili ya tahajjud), alikuwa akisafisha kinywa chake kwa mswaki”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (246) na Muslim (255)].

 

Na imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Alikuwa akiswali usiku rakaa mbili mbili, kisha huondoka akaenda kupiga mswaki”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (228) na Ahmad (1784), nayo iko katika Swahiyhul Jaami’i (4837)].

 

Yaani hupiga mswaki kila baada ya rakaa mbili.

 

Mswaki unaweza kupigwa baada ya kuamka au baada ya kutawadha, na kila moja lina sababu yake.

 

9- Afungue Swalaah yake kwa kuswali rakaa mbili fupi

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaposimama usiku kuswali, hufungua Swalaah yake kwa rakaa mbili khafifu”. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (767) na Ahmad (22890)].

 

Imepokelewa na Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Anaposwali mmoja wenu usiku, basi afungue Swalaah yake kwa rakaa mbili khafifu)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (768), Abu Daawuud (1323) na At-Tirmidhiy katika Ash-Shamaail (265)].

 

Sababu ya rakaa mbili hizi ni kuuchangamsha mwili kwa ajili ya rakaa zinazofuatia. Hivi ndivyo bora zaidi, na kama hawezi, basi hapana ubaya kufungua kwa rakaa mbili ndefu, kwani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kufanya hivyo wakati fulani kama inavyothibitisha Hadiyth ya Hudhayfah asemaye: “Niliswali na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku mmoja, akafungua kwa Al-Baqarah nikadhani atarukuu katika Aayah 100 za mwanzo, naye akapitiliza. Nikadhani ataimaliza Suwrah yote katika rakaa moja, naye akapitiliza. Nikadhani atarukuu kabla hajaimaliza, kisha akaianza An-Nisaa akaisoma, kisha akaingia Aal-‘Imraan, akaisoma, naye akaisoma kwa utuvu na kwa kituo”. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (772), An Nasaaiy (1664) na Abu Daawuud (874)].

 

10- Aifungue Swalaah yake ya usiku kwa moja ya du’aa zifuatazo baada ya takbiyr:

 

(a) Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaposimama usiku kuswali tahajjud husema:

(( اللهم لك الحمد أنت قيم السموات والأرض ومن فيهن، ولك الحمد أنت نور السموات والأرض ومن فيهن، ولك الحمد أنت ملك السموات والأرض ومن فيهن، ولك الحمد، أنت الحق ووعدك الحق، ولقاؤك حق، وقولك حق، والجنة حق، والنار حق، والنبيون حق، ومحمد حق، والساعة حق، اللهم لك أسلمت، وبك آمنت، وعليك توكلت، وإليك أنبت، وبك خاصمت، وإليك حاكمت، فاغفر لي ما قدمت وما أخرت، وما أسررت وما أعلنت، ] وما أنت أعلم به مني [ أنت المقدم، وأنت المؤخر، لا إله إلا أنت، ولا إله غيرك، ولا حول ولا قوة إلا بالله))

Allaahumma lakal hamdu Anta Qayyimus Samaawaati wal Ardhi waman fiyhinna, wa lakal hamdu Anta Nuurus Samaawaati wal Ardhi waman fiyhinna, wa lakal hamdu Anta Malikus Samaawaati wal Ardhi waman fiyhinna, wa lakal hamdu, Anta Al-Haqqu wa wa’adukal haqqu, wa liqaauka haqqun, wa qawluka haqqun, wal Jannatu haqqun, wan Naaru haqqun, wan Nabiyyuwna haqqun, wa Muhammadun haqqun, was Sa’atu haqqun. Allaahumma laka aslamtu, wa bika aamantu, wa ‘alayka tawakkaltu, wa ilayka anabtu, wa bika khaaswamtu, wa ilayka haakamtu, Faghfirliy maa qaddamtu wamaa akh-khartu, wa maa asrartu wa maa a’alantu, [wamaa Anta A’alamu bihii minniy] Anta Al-Muqaddimu, wa Anta Al-Muakh-khiru, laa ilaaha illaa Anta, walaa ilaaha ghayruka, walaa hawla walaa quwwata illaa bil Laahi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1069) na Muslim (769)].

 

(b) Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiifungua Swalaah yake anaposwali usiku kwa kusema:

(( اللهم رب جبريل وميكائيل وإسرافيل فاطر السموات والأرض، عالم الغيب والشهادة، أنت تحكم بين عبادك فيما كانوا فيه يختلفون، اهدني لما اختلف فيه من الحق بإذنك، إنك تهدي من تشاء إلى صراط مستقيم ))

Allaahumma Rabba Jibryla wa Miykaaiyla wa Israafiyla Faatwiras Samaawaati wal Ardhi, ‘Aalimal ghaybi wash shahaadati, Anta Tahkumu bayna ‘ibaadika fiymaa kaanuw fiyhi yakhtalifuwna, Ihidiniy limakhtulifa fiyhi minal haqqi bi idhnika. Innaka Tahdiy ilaa swiraatwin mustaqiymin)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (770)].

 

(c) Imepokelewa na Hudhayfah kwamba yeye alimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali usiku na alikuwa anasema:

(( الله أكبر (ثلاثا) ذو الملكوت والجبروت والكبرياء والعظمة))

(( Allaahu Akbar (mara tatu), Dhul Malakuwti wal Jabaruwti wal Kibriyaai wal ‘Adhwamati)). [Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud ( 873) na An-Nasaaiy (1069). Angalia Al-Mishkaat (1200)].

 

Ninasema: “Ana khiyari ya kuomba du’aa yoyote aitakayo kati ya du’aa nyingine za kufungulia Swalaah tulizozitaja katika mlango wa “Mawajibiko ya Swalaah”.

 

11- Arefushe kisimamo awezavyo bila ya kujitia uzito

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( أفضل الصلاة طول القنوت))

((Swalaah bora zaidi ni yenye kisimamo kirefu zaidi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (756) na wengineo].

 

An Nawawiy kasema: “Makusudio ya “qunuwt” hapa ni kisimamo kwa makubaliano ya Maulamaa kwa mujibu wa ninavyojua. Ash-Shaafi’iy ana dalili pamoja na yule anayesema kama yeye. Anasema: “Kurefusha kisimamo ni bora zaidi kuliko kukithirisha rukuu na sijdah”.

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akirefusha kisimamo. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisimama usiku mpaka miguu yake ikavimba…”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3748) na Muslim (2820)].

 

Tushaeleza nyuma katika Hadiyth ya Hudhayfah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma Al-Baqarah, An-Nisaai na Aal-‘Imraan katika  rakaa moja.

Aidha, imepokelewa na Ibn Mas-’oud akisema: “Niliswali pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akarefusha mpaka nikadhamiria kufanya jambo baya”. Akaulizwa: “Ulidhamiria nini?” Akajibu: “Niliazimia kukaa nimwache”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1135) na Muslim (773)].

 

Al-Haafidh katika Al Fat-h (3/19) anasema: “Katika Hadiyth, kuna dalili kwamba kurefusha Swalaah za usiku, ni chaguo lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na Ibn Mas-’oud alikuwa imara mwenye kuhifadhi kumfuata Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Naye hakuazimia kukaa ila baada ya kisimamo kupindukia zaidi ya alivyozoea”.

 

· Faida

 

Kurefusha hakuhusiani na kisomo tu, bali kumesuniwa vile vile katika rukuu, sijdah, kikao, dhikr, du’aa na katika vipengele vyote vya Swalaah. Katika Hadiyth ya Hudhayfah inayoelezea kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma Al-Baqarah, An-Nisaai na Aal-‘Imraan katika rakaa moja, Hadiyth inaendelea ikisema: “Kisha alirukuu akawa anasema: “Subhaana Rabbiya Al-‘Adhiymi”, na rukuu yake ilikuwa takriban sawa na kisimamo chake, kisha akasema: “Sami’a Allaahu liman Hamidah”, kisha akasimama sana takriban sawa na alivyorukuu, kisha akasujudu akasema: “Subhaana Rabbiyal A’alaa”, na sijdah yake ilikuwa kiasi cha kisimamo chake”. [“Takhriyj” yake ishaelezwa].

 

Na katika Hadiyth ya ‘Aaishah: “Anabakia katika sijdah yake kiasi cha mtu kusoma Aayah hamsini kabla hajanyanyua kichwa chake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1336), Ibn Maajah (1358) na Ahmad (6/83)].

 

Ninasema: “Kurefusha huku kisomo na nguzo nyinginezo, si sharti katika Swalaah ya usiku, bali kufanya hivyo ni bora na ukamilifu zaidi kwa mwenye kuweza. Katika baadhi ya nyakati, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika kila rakaa kiasi cha Aayah 50 au zaidi.. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (994)]na alikuwa akisema:

(( من صلى ليلة بمائة آية لم يكتب من الغافلين ))

((Mwenye kuswali usiku kwa Aayah mia moja, hatoandikwa kati ya watu wenye kughafilika)). [Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh. Angalia Asw-Swahiyhay (643) na Swahiyhut Targhiyb (636)].

 

12- Anaweza kuswali kwa kusimama au kukaa. Zimekuja kwa njia sahihi aina tatu za namna alivyokuwa akiswali Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku:

 

Ya kwanza: Alikuwa akiswali kwa kusimama kama ilivyobainika katika Hadiyth zilizotangulia.

 

Ya pili: Alikuwa akiswali kwa kukaa, na anarukuu kwa kukaa. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakufa mpaka zikawa Swalaah zake nyingi ni kwa kukaa”. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraj” na Muslim (735) na An-Nasaaiy (1656)].

 

Na katika riwaya nyingine, ni kuwa alifanya hivi aliponenepa na kupata mwili.

 

Pia ‘Aaishah amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali usiku mrefu kwa kusimama, na usiku mrefu kwa kukaa. Anaposwali kwa kusimama, hurukuu akiwa amesimama, na anaposwali kwa kukaa, hurukuu akiwa amekaa”. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraj” na Muslim (730), Abu Daawuud (955) na An-Nasaaiy (3/219)].

 

Ya tatu: Alikuwa akisoma huku amekaa, na inapobakia kidogo katika kisomo chake, husimama akarukuu akiwa amesimama. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali kwa kukaa, na husoma huku amekaa. Na inapobakia kiasi cha Aayah thelathini au arobaini, husimama akasoma huku amesimama, kisha hurukuu, halafu husujudu, kisha hufanya katika rakaa ya pili hivyo hivyo”. [Hadiyth Swahiyhy: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1118) na Muslim (731) na tamko ni lake].

 

13- Anapohisi uvivu, au kuchoka, au kulemewa na usingizi, basi alale na anapochangamka aswali.

 

Imepokelewa na Anas akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia Msikitini akakuta kamba imefungwa kati ya nguzo mbili akauliza: ((Nini hii?)) Wakajibu: “Ni ya Zaynab anaposwali. Anapohisi uvivu au kuchoka, huikamata”. Akasema: ((Ifungueni, aswali mmoja wenu anapokuwa mchangamfu, akihisi uvivu au kuchoka, basi alale)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1150) na Muslim (784)].

 

Imepokelewa na ‘Aaishah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إذا نعس أحدكم في الصلاة، فليرقد حتى يذهب عنه النوم، فإن أحدكم إذا صلى وهو ناعس، لعله يذهب يستغفر فيسب نفسه))

((Akisinzia mmoja wenu wakati anaswali, basi alale mpaka usingize umwishe, kwani anaposwali mmoja wenu huku anasinzia, anaweza akaona kwamba anastaghfir kumbe anajitusi mwenyewe)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (212) na Muslim (786)].

 

Pia Abu Hurayrah anasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إذا قام أحدكم من الليل، فاستعجم القرآن على لسانه، فلم يدر ما يقول: فليضطجع))

((Anaposwali mmoja wenu usiku, Qur-aan ikakanganyika ulimini mwake asiweze kukijua anachokisoma, basi alale)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhaaj” na Muslim (787), Abu Daawuud (1311) na Ibn Maajah (1372)].

 

14- Airattil Qur-aan na aipambe sauti yake

 

Allaah Anasema:

((أَوْ زِدْ عَلَيْهِ وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا))

((Au izidishe, na soma Qur-aan kwa kisomo cha utaratibu upasao, kuitamka vizuri na kutaamali)) [Al-Muzzammil (73:4)].

 

Imepokelewa toka kwa Hafswah akisema: “Rasuli wa Allaah alikuwa akisoma Suwrah akiirattil mpaka inakuwa ndefu kuliko iliyo ndefu yake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (733), Maalik (311) na An-Nasaaiy (1658)].

 

Naye Ya’alaa bin Mamlak alimuuliza Ummu Salamah namna kisomo cha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kinavyokuwa na anavyoswali. Ummu Salamah akakielezea kisomo chake akawa anakisifu kiuchambuzi herufi kwa herufi. [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh: Angalia Al-Mishkaat (1210) na Swifatus Swalaat (uk 124)].

 

Anakusudia uratili bora na kisomo murua.

 

Qataadah anasema: Nilimuuliza Anas: Ni vipi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasoma?” Akasema: “Kisomo chake kilikuwa ni kuvuta”. Kisha akasoma: Bismil Laahi Ar Rahmaan Ar Rahiym: Anavuta Bismil Laahi, anavuta Ar Rahmaan, na anavuta Ar Rahiym”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5046), An-Nasaaiy (1014) Abu Daawuud (1465) kwa muhtasari, Ibn Maajah (1353) na Ahmad (11835)].

 

Makusudio ni kuwa alikuwa akivuta herufi za “madda” na “al liyn” katika matamshi yake kwa kipimo kinachojulikana.

 

Ummu Salamah anasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikikata kisomo chake Aayah kwa Aayah: ((Al Hamdu lil Laahi Rabbil ‘Aalamiyna) kisha anasimama, (Ar Rahmaan Ar Rahiym) kisha anasimama”. [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh: Angalia Swahiyhul Jaami’i (4876)].

 

Imesuniwa aghani akisoma Qur-aan kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Si katika sisi asiyeghani akisoma Qur-aan)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (7527). Kana kwamba iliyo Swahiyh toka kwa Abu Hurayrah, ni Hadiyth inayofuatia. Lakini pamoja na hivyo, wameifanyia “ikhraaj” kwa tamko hili akina Abu Daawuud (1469), Ahmad (1396) na wengineo toka kwa Sa’iyd na wengineo kwa tamko lake]

 

Na pia kutoka kwa Abu Hurayrah amesema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( ما أذن الله لشيء ما أذن لنبي حسن الصوت يتغنى بالقرآن يجهر به))

((Allaah Hakusikiliza kitu kama Anavyomsikiliza Nabii mwenye sauti nzuri, anayeghani vizuri kwa kuisoma Qur-aan kwa sauti)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5023) na Muslim (792)].

 

Maana ya kughani ni kuirembesha sauti kwa kuinyanyua na kwa kiimbo kwa picha ya kuhuzunika, kwa namna itakayozilainisha nyoyo na kububujisha machozi lakini kwa sharti ya kutopetuka wigo uliowekwa na mabingwa wa taaluma ya visomo. Ama kuvuta sana kisomo na kuingiza madoido ya kuchupa hadi kuyatoa maneno nje ya mahala pake, hilo ni makruhu kwa mujibu wa Jamhuri ya Maulamaa. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

· Je, Kisomo Ni Kwa Sauti Au Kwa Sauti Ya Chini?

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma kwa sauti ya chini katika Swalaah za usiku baadhi ya nyakati, na wakati mwingine akisoma kwa kunyanyua sauti. Imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin Abiy Qays akisema: “Nilimuuliza ‘Aaishah: Je, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma kwa kunyanyua sauti katika Swalaah yake au akisoma kwa sauti ya chini? Akajibu: Alikuwa akisoma kwa kunyanyua sauti, na alikuwa akisoma kwa sauti ya chini. Nikasema: Allaahu Akbar, namshukuru Allaah Aliyefanya wasaa katika jambo hili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (307), An-Nasaaiy (1199), Abu Daawuud (1437) na Ahmad (6/73)].

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Kisomo cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kilikuwa kinaweza kusikika na aliyeko chumbani, naye akiwa nyumbani”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1327), At-Tirmidhiy katika Ash-Shamaail (275-muhtasar) na Ahmad (1/271)].

 

Yaani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya wastani kati ya kunyanyua na kuteremsha sauti.

 

Ninasema: “Hili ndilo linalopendeza. Imepokelewa toka kwa Abu Qataadah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka usiku na mara akamkuta Abu Bakri anaswali kwa sauti ya chini. Akapita kwa ‘Umar akamkuta anaswali kwa sauti ya juu. Na wawili hao walipokutana kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Rasuli alisema: ((Ee Abu Bakr! Nimekupitia nawe unaswali kwa sauti ya chini)). Akasema: “Nimemsikilizisha niliyemnong’oneza ee Mjumbe wa Allaah! Akamwambia ‘Umar: ((Nimekupitia nawe unaswali kwa sauti ya juu)). Akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Ninamzindusha aliyelala usingizi wa mang’amung’amu, na ninamfukuza shaytwaan”. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ee Abu Bakr! Nyanyua sauti yako kidogo)). Na akamwambia ‘Umar: ((Punguza kidogo sauti yako)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1329) na At-Tirmidhiy (447)].

 

Hivi ndivyo ulivyokuwa usikilizaji wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wa Qur-aan kwa sauti za Ma’ashaairah, na Abu Muusa wakati alipokuwa akisoma usiku akamwambia: ((Ee Abu Muusa! Laiti ungeniona nami nakusikiliza kisomo chako jana. Hakika umepewa sauti nzuri ajabu kama sauti ya ukoo wa Daawuud)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1322)].

 

An Nawawiy amesema: “Zimekuja Hadiyth kuhusiana na fadhila za kusoma kwa sauti, na athar kuhusiana na fadhila za kusoma kwa sauti ya chini. Maulamaa wamesema: Kuoanisha kati ya mawili haya ni kuwa kusoma kwa sauti ya chini kunakuwa mbali zaidi na riyaa, nako kunakuwa ni bora zaidi kwa anayechelea hilo. Na kama mtu hachelei hilo, basi kusoma kwa sauti ni bora lakini kwa sharti kwamba asisababishe kero kwa mwingine mwenye kuswali, au aliyelala au mwingineyo”.

 

15- Atadaburi Aayaat, ajilinde, asabbih katika kisomo, na alie katika Swalaah

 

(a) Imekuja katika Hadiyth ya Hudhayfah aliposwali pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “..anasoma kwa utuvu na kwa kituo, akiipita Aayah yenye tasbiyh husabbih, akiipitia yenye maombi huomba, akiipita ya kujilinda, hujilinda….”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1010) na Ibn Maajah (1350). Angalia Swifatus Swalaahat uk. 121].

 

“Inatakikana kwa Waumini wote wawe hivyo, bali wawe zaidi kuliko yeye. Ikiwa Allaah Amemghufiria madhambi yake yaliyopita na yajayo, basi wao wamo hatarini”. [Faydhul Qadiyr cha Al-Minaawiy (5/160) chapa ya Al-Maktabat At-Tijaariyyah]

 

(b) Imepokelewa toka kwa Abu Dharri akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikesha akiikariri Aayah moja mpaka Alfajiri. Aayah yenyewe ni:

(( إِن تُعَذِّبْهُمْ فَإِنَّهُمْ عِبَادُكَ ۖ وَإِن تَغْفِرْ لَهُمْ فَإِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ))

 

 (c) Imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin Ash-Shukhayr akisema: ”Nilimjia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa anaswali, na kifuani mwake kuna mvumo kama mvumo wa maji yachemkayo chomboni [kwa sababu ya kulia]. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (904), An-Nasaaiy (1214) na Ahmad (15722)].

 

(d) Tulielezea nyuma kauli ya ‘Aaishah – wakati Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwamuru Abu Bakr awaswalishe watu – isemayo: “Abu Bakr ana moyo laini, na anaposimama mahala pako, watu hawamsikii….” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (664) na Muslim (418)].

 

Yaani kwa sababu ya kulia. Na katika riwaya nyingine: “Hakika Abu Bakri ana moyo laini, anaposoma hawezi kujizuia kulia..”.

 

(e) ‘Abdullaah bin Shaddaad amesema: “Niliusikia mkwamo wa kilio kwa ‘Umar nami niko swafu ya mwisho akisoma:

(( قَالَ إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ))

[Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy ikiwa Mu’allaq, na Sai’yd bin Mansour ameifanya Mawsuwl (1138), Ibn Abu Shaybah (5/405), ‘Abdur Raaziq (2/114) na Al-Bayhaqiy katika Ash-Sha’ab (2/364). Sheikh wa Uislamu (22/623) amesema: “Athar hii imehifadhiwa toka kwa ‘Umar”]

 

16- Akithirishe du’aa – saa za mwisho wa usiku – ndani ya Swalaah na nje ya Swalaah

 

Kutokana na kama tulivyoeleza kwamba katika nyakati hizi Mola (Tabaaraka wa Ta’alaa) Huteremka katika wingu wa dunia kwa ajili ya kumjibu mwombaji du’aa na kumpa mtaka haja, haja yake.

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إن في الليل لساعة، لا يوافقها رجل مسلم يسأل الله خيرا من أمر الدنيا والآخرة إلا أعطاه إياه وذلك كل ليلة ))

((Hakika katika usiku kuna saa, haisadifu saa hiyo Muislamu akimwomba Allaah kheri yoyote katika mambo ya dunia au aakhirah isipokuwa Humpa, na hiyo ni kila usiku)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (757)].

 

Tushazitaja nyuma du’aa za Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati anapoianza Swalaah yake ya usiku.

 

Imesuniwa akithirishe zaidi du’aa katika sijdah, kwani hapo ndipo penye uhakika zaidi wa kujibiwa. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( أقرب ما يكون العبد من ربه وهو ساجد، فأكثروا فيه من الدعاء ))

((Wakati ambao mja huwa karibu zaidi na Mola wake, ni pale anapokuwa amesujudu, basi kithirisheni hapo du’aa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (482), An-Nasaaiy (1137) na Abu Daawuud (875)].

 

Na anasema tena:

(( أما السجود، فأكثروا من الدعاء فيه، فقمن أن يستجاب لكم))

((Ama sijdah, basi kithirisheni kuomba du’aa hapo, kwani ni stahikivu kwenu kujibiwa humo du’aa )). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika mlango wa “Mawajibiko ya Swalaah”].

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: Nilimkosa Rasuli wa Allaah ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) usiku kitandani. Nikapapasa kumtafuta na mkono wangu ukagusa tumbo la nyayo zake mbili zikiwa zimesimamishwa na yeye yuko katika sijdah. Alikuwa akisema:

((اللهم أعوذ برضاك من سخطك، وبمعافاتك من عقوبتك، وأعوذ بك منك، لا أحصي ثناء عليك، أنت كما أثنيت على نفسك))

((Allaahumma a’uwdhu bika biridhwaaka min sakhatwika, wa bimu’aafaatika min ‘uquwbatika, wa a’uwdhu bika minka, laa uhswiy thanaan ‘alayka, Anta kamaa Athnayta ‘alaa nafsika)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (486) na wengineo].

 

17- Imesuniwa kumwamsha mke kuswali usiku

 

Hili limezungumziwa katika mlango wa “Fadhila za kuswali usiku”.

 

18- Alale baada ya kuswali na kabla ya Alfajiri

 

Ili iwe ni kama kitenganishi kati ya Swalaah ya Sunnah na Swalaah ya faradhi. Kulala huku huleta uchangamfu wa kuiswali Swalaah ya Alfajiri, kwa kuwa ikiwa mtu ataunganisha Swalaah ya usiku na Swalaah ya Alfajiri, hatokuwa na dhamana ya kupata uchangamfu na khushuu wakati wa kuswali kutokana na tabu na mchoko. Dalili za kupendezeshwa hili zimeelezwa katika mlango wa “Witr”.

 

19- Ni karaha kuacha kuswali usiku kwa mtu aliyezoea

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amri akisema: “ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia: ((Ee ‘Abdullaah! Usiwe kama fulani. Alikuwa akiswali usiku akaacha kuswali usiku)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1152) na Muslim (1159)].

 

· Qiyaamul Layl Wakati Wa Misukosuko

 

Majanga yanaposhitadi, mambo yakashindikana, hapo inakuwa hakuna tena njia isipokuwa kugonga mlango wa Mfalme Mwenye Kumiliki hatamu ya kila kitu, kusimama mbele yYake na kumwomba kwa unyenyekevu ndani ya giza totoro.

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aliyy (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Hakuna aliyekuwa amepanda farasi Siku ya Badr isipokuwa Al-Miqdaad. Ungeshangaa ungetuona, hakuna yeyote katika sisi isipokuwa alilala ila Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) chini ya mti akiswali na akilia mpaka pakapambauka”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (973). Angalia Swahiyhut Targhyb (546)].

 

Imepokelewa toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mwaka wa Vita vya Taabuk, alisimama usiku akaswali. Maswahaba wakakusanyika nyuma yake wakimchunga mpaka akamaliza kuswali na kujumuika nao”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (6771)].

 

· Idadi Ya Rakaa Za Qiyaamul Layl

 

1- Idadi inayopendeza

 

Imesuniwa idadi ya rakaa za Qiyaamul Layl isizidi rakaa 11 au 13. Idadi hii ndio aliyojichagulia mwenyewe Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

(a) Imepokelewa toka kwa Masrouq akisema: “Nilimuuliza ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) kuhusiana na Swalaah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku. Akasema: Ni saba, tisa na kumi na moja pasina rakaa mbili za Alfajiri”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1139)].

 

(b) Ibn Salamah bin ‘Abdur Rahmaan naye alimuuliza, ‘Aaishah akasema: “Hakuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akizidisha zaidi ya rakaa kumi na moja, si katika Ramadhwaan au katika miezi mingineyo. Huswali nne, usiulize vipi uzuri wake na vipi urefu wake, kisha huswali nne, usiulize vipi uzuri wake na vipi urefu wake, kisha huswali tatu”. [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa karibuni].

 

(c) Ibn ‘Abbaas amesema: “Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa ni rakaa 13, yaani usiku”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1138) na Muslim (764)].

 

(d) Imepokelewa toka kwa Zayd bin Khaalid Al-Juhaniy akisema: Hakika niliifuatilia kwa macho Swalaah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akaswali rakaa mbili khafifu, kisha akaswali rakaa mbili ndefu ndefu ndefu, halafu akaswali rakaa mbili si ndefu kama za kabla yake. Kisha akaswali rakaa mbili si ndefu kama za kabla yake, halafu akaswali rakaa mbili si ndefu kama za kabla yake, kisha akaswali rakaa mbili si ndefu kama za kabla yake, halafu akaswali Witr. Na hizo ni rakaa kumi na tatu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (765)].

 

Baadhi ya Maulamaa wanasema kwamba Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa ni rakaa kumi na moja. Ama rakaa mbili za mwisho, baadhi wamesema ni rakaa mbili za Alfajiri, na wengine wamesema ni rakaa mbili za Sunnah ya ‘Ishaa. Hili likipita katika baadhi ya riwaya, basi halipiti kwenye riwaya nyinginezo. Na wengine wamesema ni rakaa mbili ambazo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifungulia kwazo Swalaah yake. Huenda kauli hii ikawa na mwelekeo bora zaidi. [Ni kauli aliyoichagua Al-Haafidh katika Al Fat-h (3/21)]

 

2- Je, inajuzu kuongeza zaidi ya idadi hii?

 

Suala hili limezusha mvutano kati ya wanafunzi ambao bado hawajakomaa kielimu na ndugu zetu wenye pupa ya kuifuata Sunnah ya Rasuli. Wanasema kwamba haijuzu kuzidisha zaidi ya rakaa kumi na moja wakimfuata mmoja kati ya Maulamaa Wakubwa wa enzi yetu ya leo. Huenda ‘Aalim huyu kwa kufanya hivi, amepata thawabu moja.

 

Lakini Jamhuri ya Salaf na Khalaf wanasema kwamba inajuzu kuzidisha zaidi ya idadi hii wakisisitiza kwamba kufanya hivyo ni Sunnah. Na kwa ajili hiyo, Al-Qaadhwiy ‘Ayyaadh anasema: “Hakuna mvutano wa kusema kwamba kuna mpaka maalumu wa kutozidishwa au kutopunguzwa katika hilo, na kwamba Swalaah ya usiku ni katika ‘ibaadah ambazo kila rakaa zinavyoongezeka, na ndivyo thawabu nazo zinavyoongezeka. Lakini mabishano yapo katika kitendo chake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hilo alilojichagulia yeye mwenyewe. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

Ibn ‘Abdul Barri amesema katika At-Tamhiyd: “Hakuna kabisa mahitalifiano kati ya Waislamu kwamba Swalaah ya usiku haina mpaka maalumu, na kwamba Swalaah hiyo ni ya Sunnah, na ni kitendo cha kheri na amali njema. Mwenye kutaka atakalilisha na mwenye kutaka atakithirisha”.

 

Ninasema: “Yenye kuonyesha usahihi wa msimamo huu ni haya yafuatayo: [Sheikh wetu Mustwafa Al-‘Adawiy – Allaah Ainyanyue daraja yake – ana tasnifu murua inayozungumzia kuhusu “Idadi ya rakaa za Swalaah ya Usiku”. Katika tasnifu hii, amelimaliza na kulifungia kazi suala hili, nami nimefaidika sana nayo]

 

1- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Swalaah ya usiku ni rakaa mbili mbili, ukichelea Alfajiri, basi swali Witr rakaa moja)). [Hadiyth Swahiyh:”Takhriyj” yake ishaelezwa nyuma].

 

2- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Jisaidie mwenyewe kwa kukithirisha sijdah)). [Hadiyth Swahiyh:”Takhriyj” yake ishaelezwa nyuma].

 

3- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hakika wewe hutosujudu sijdah moja kwa ajili ya Allaah, isipokuwa Allaah Atakunyanyulia kwayo daraja moja na kukupomoshea kwayo kosa moja)). [Hadiyth Swahiyh:”Takhriyj” yake ishaelezwa nyuma].

 

4- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kujichagulia mwenyewe idadi hii, hakumaanishi kuwa idadi iwe ni hiyo hiyo tu kutokana na haya yafuatayo:

 

(a) Kitendo chake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakihusishi kauli yake kama inavyoelezwa katika taaluma ya Uswuul.

 

(b) Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakukataza kuzidisha zaidi ya rakaa kumi na moja, bali ametuainishia Swalaah ambayo Allaah Anaipenda zaidi, nayo ni Swalaah ya Daawuud Alayhis Salaam katika theluthi ya usiku.

 

Na kwa ajili hiyo, Sheikh wa Uislamu (22/272-273) amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuweka idadi maalum ya rakaa katika Qiyaam Ramadhwaan, na yeye hakuwa akizidisha zaidi ya rakaa kumi na tatu katika Ramadhwaan na katika miezi mingineyo yote, lakini alikuwa akirefusha sana rakaa. Na mwenye kudhani kwamba Qiyaam Ramadhwaan ina idadi maalumu iliyowekwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isiyozidishwa wala kupunguzwa, basi amekosea.

 

(c) Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumwamuru anayeswali usiku kuswali kwa idadi hii. Na lau kama tutajaalia kwamba aliamuru – na hili hakuna aliyelisema – basi haifai vile vile ahusishe ujumuishi wa dalili zilizotangulia kutokana na yaliyobainishwa katika taaluma ya Uswuul ya kuwa cha jumla hakiainishwi na moja ya vipengele vyake isipokuwa wakati wa kukinzana.

 

5- Mwenye kutaka kwenda sawia na Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi ni lazima aende nayo sambamba kihesabu, kisifa, kiidadi na kinamna. Na nyuma tumeelezea namna Rasuli alivyokuwa akirefusha Swalaah ya usiku akiswali idadi hii ya rakaa. Mtu akiziangalia Aayah zilizogusia nyuma kuhusu fadhila za Qiyaamul layl, atakuta kwamba mhimili wake ni muda wa kisimamo. Basi ikiwa mtu anayetaka kwenda sawia na Sunnah ya Rasuli hawezi urefushaji huo – na hususan ikiwa anawaswalisha watu - je tutamzuia kuongeza idadi ya rakaa ili iwe nafuu kwake na kwa wanaomfuata, na chachu kwake ya kuweza kusimama theluthi ya usiku?!! Na je aliyeswali rakaa kumi na moja kwa muda wa saa moja ni bora kuliko aliyeswali rakaa ishirini au zaidi au chini ya hapo kwa muda wa saa nne?!!

Naam, hakuna mabishano ya kwamba lau kama atakwenda sawia na Sunnah katika idadi na wakati basi hilo ni bora, na kama hawezi basi ataswali kwa mujibu wa itakavyokuwa wepesi kwake.

 

6- Imethibiti kwamba ‘Umar bin Al-Khattwaab aliwakusanya watu katika Qiyaam Ramadhwaan (Tarawehe). Watu hawa waliswalishwa na Ubayya bin Ka’ab na Tamiym Ad Daariy kwa rakaa ishirini na moja. Walikuwa wakisoma Suwrah ndefu na kuondoka wakati Alfajiri inapokurubia. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdur Razzaaq (7730) na Ibn Al-Ja’ad (2926), na kupitia kwake Al-Bayhaqiy (2/496). Wao wanasema ni rakaa ishirini]

 

Imethibiti vile vile kwamba aliwakusanya kuswali rakaa kumi na moja kama itakavyokuja kuelezwa katika mlango wa Tarawehe.

 

· Kulipa Qiyaamul Layl

 

Imesuniwa kuilipa Qiyaamul Layl mchana kabla ya Adhuhuri kwa aliyezoea ikiwa itampita kwa sababu ya usingizi au ugonjwa. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali mchana rakaa kumi na mbili ikiwa atapitwa na Swalaah ya usiku kwa sababu ya maumivu au jinginelo. [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa katika mlango wa “Kulipa Witr”].

 

Imepokelewa toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( من نام عن حزبه أو عن شيئ منه، فقرأه بين صلاة الفجر وصلاة الظهر، كتب له كأنما قرأه من الليل))

((Mwenye kulala asifanye uradi wake, au sehemu ya uradi huo, halafu akaja kuusoma kati ya Swalaah ya Alfajiri na Swalaah ya Adhuhuri, huandikiwa kama aliyeusoma usiku)). [Hadiyth Swahiyh: Imeelezwa katika mlango wa “Kulipa Witr”].

 

 

 

Share