031-Hiswnul-Muslim: Ipasavyo Kufanya Na Kusema Mwenye Kuota Ndoto Njema Au Mbaya

Hiswnul-Muslim

031-Ipasavyo Kufanya Na Kusema Mwenye Kuota Ndoto Njema Au Mbaya

www.alhidaaya.com

 

Bonyeza Hapa Usikilize

 

 

[114]

 

Anayeota ndoto mbaya anatakiwa afanye yafuatayo:  

 

1- Apulize kushotoni kwake mara tatu.

 

2-Aombe kinga kwa Allaah kutokana na shaytwaan kwa shari aliyoiota (aseme:

 

أَعـوذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْـطانِ الرَّجيـم

A’uwdhu biLLaahi minash-shaytwaanir-rajiym – mara tatu)

 

 

3-Asimuhadithie mtu yeyote[1]  

 

 

4-Agueuke upande mwengine (alioota ndoto mbaya)[2]    

 

 

[115]

 

5-Ainuke kuswali akitaka[3]   

 

 

 

[1]Hadiyth ya Abu Qataadah bin Rib-’iyy;  imesemekana jina lake pia ni: Al-Haarith na pia imesemekana ni: ‘Amruw (رضي الله عنه), Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) amesema:  ((Ndoto nzuri inatoka kwa Allaah, na ndoto mbaya ni kutoka kwa shaytwaan. Atakapoota mmoja wenu kinachomchukiza, basi atakapozindukana, apulize kushotoni mwake mara tatu na aombe kinga kwa Allaah kutokana na shari yake, basi hakitamdhuru [kitu])). Na riwaayah nyingine: ((Atakayeota mmoja wenu atakachokipenda, asimhadithie yeyote isipokuwa yule anayempenda. Na atakapoota anachokichukia asimhadithie mtu, na apulize kushotoni mwake mara tatu na aombe kinga kwa Allaah kutokana na shaytwaanir-rajiym kwa shari aliyoiota, basi haitamdhuru [kitu])) Kauli hizo ni kutoka Hadiyth katika Muslim (4/1772) [2261], Al-Bukhaariy [7044].   

[2]Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنهما), Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) amesema: ((Atakayeoota mmoja wenu ndoto anayoichukia, ateme mate kushotoni mwake mara tatu, na aombe kinga kwa Allaah kutokana na shaytwaan mara tatu, na ageuke [kulala] upande mwengine)) - Muslim (4/1773) [2262].   

[3]Hadiyth ya Abu Hurayrah (رضي الله عنه), Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) amesema: ((Wakati [wa Qiyaamah] utakapokaribia, ndoto ya Muumini haitaongopa. Na ndoto ya kweli kabisa ni ya yule ambaye ni mkweli kabisa katika kauli zake. Na ndoto ya Muumini ni sehemu moja ya sehemu arubaini na tano ya Unabii. Na ndoto ni [aina] tatu: Ndoto nzuri ambayo ni bishara kutoka kwa Allaah. Ndoto inayohuzunisha ambayo ni kutoka kwa shaytwaan. Ndoto kutokana na [jambo] analoliwaza mtu akilini mwake. Basi anapoota mmoja wenu asichokipenda, asimame na aswali wala asihadithie watu))

- Muslim (4/1773) [2263]

 

 

Share