028-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaat Al-Istikhaarah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

028-Swalaat Al-Istikhaarah

 

 

Mwenye kutaka kufanya jambo la halali, kisha akawa na shakashaka kama litakuwa na kheri ndani yake au litakuwa sawa, basi imesuniwa kwake  aswali rakaa mbili zisizo za faradhi - rakaa zozote mbili hata kama ni katika Sunnah za rawaatib – kisha aombe baada ya kuziswali kwa du’aa iliyokuja katika Hadiyth ifuatayo:

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatufundisha istikhaarah katika mambo yote. Aidha, anatufundisha Suwrah ya Qur-aan anasema:

((Akiazimia mmoja wenu kufanya jambo, basi aswali rakaa mbili zisizo za faradhi, kisha aseme: Allaahumma inniy astakhiyruka bi’ilmika, wa astaqdiruka biqudratika, wa as-aluka min fadwlikal Adhwiym, fainnaka Taqdiru walaa aqdiru, wa Ta’alamu walaa a’alamu, wa Anta ‘Allaamul Ghuyuub. Allaahumma in Kunta Ta’alamu anna haadhaal amra (atalitaja) khayrun liy fiy diyniy wa ma’aashiy wa ‘aaqibati amriy (au atasema: ‘aajilihi wa aajilihi) Faqdirhu liy wa Yassirhu liy, thumma Baariyki liy fiyhi. Wain Kunta Ta’alamu anna haadhal amra sharrun liy fiy diyniy wa ma’aashiy wa ‘aaqibati amriy (au atasema: ‘aajilihi wa aajilihi) Faswrifhu ‘anniy Waswrifniy ‘anhu, Waqdir liy al khayra haythu kaana, thumma Irdhwiniy bihi”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (719)].

 

Zifuatazo ni tanbihi ambazo inabidi zizingatiwe:

 

1-Istikhaarah hufanywa wakati mtu anapoazimia kufanya jambo la halali, na haifanywi katika mambo ya halali ila kwa ajili ya kuchagua la kheri zaidi kati yake. Pia haifanywi katika mambo ya wajibu au ya haramu.

 

2- “Baada ya kuiswali, inatakikana mtu alifanye lile ambalo anakuta kifua chake kimefunguka kwalo, asiutegemee ukunjufu aliokuwa ameulemea kabla ya kuswali, bali aliache chaguo lake moja kwa moja. Na kama si hivyo, basi atakuwa hamfanyii istikhaarah Allaah bali hawaa ya nafsi yake, na anaweza asiwe mkweli katika kuiomba kwake kheri na kujivua na ujuzi na uwezo na kuuthibitisha kwa Allaah Mtukufu. Akiwa mkweli katika hilo, atajivua uwezo, nguvu na chaguo lake mwenyewe.” [Yamenukuliwa haya kutoka Naylul Awtwaar (3/90) toka kwa An Nawawiy]

 

3- Si lazima aliyefanya istikhaarah aone njozi usingizini kama wanavyoitakidi watu wengi, bali inakuwa ni kwa lile ambalo kifua chake mtu kitalikunjukia, au jambo hilo litarahisishwa kwake kwa mujibu wa Alivyolikadiria Allaah.

 

4- Chaguo la Allaah linaweza kuja kinyume na mtu anavyotaka au kwa lile ambalo analiona kama ni shari. Hapa ni lazima asalimishe jambo lake kwa Allaah.

 

(( كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ))

((Mmeandikiwa shariy’ah kupigana vita nako kunachukiza mno kwenu. Na asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni khayr kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui)). [Al-Baqarah (2:216)]

 

5- Istikhaarah ni du’aa, hakuna ubaya kuikariri.

 

· Tanbihi

 

Kuna Hadiyth isemayo:

(( إذا هممت بأمر فاستخر ربك فيه سبع مرات))

((Ukiazimia jambo, basi mfanyie istikhaarah Mola wako mara saba)). Hadiyth hii ni batili na haifai.

 

 

Share