029-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaat At-Tasbiyh

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

029-Swalaat At-Tasbiyh

 

 

Swalaah ya Tasbiyh ni aina ya Swalaah za Sunnah ambayo huswaliwa kwa picha maalumu itakayokuja kufafanuliwa. Imeitwa “Swalaah ya Tasbiyh”  kwa vile ina tasbiyh nyingi ndani yake zinazofikia sabini na tano katika kila rakaa moja.

 

· Hukmu Yake

 

Maulamaa wametofautiana kuhusu hukumu yake kutokana na kukhitilafiana kwao juu ya uthibiti wa Hadiyth iliyoizungumzia Swalaah hii. Hadiyth hii ni ya Ibn Abbaas anayesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia ‘Abbaas bin ‘Abdil Muttalib:

((Ee ‘Abbaas! Ee ami yangu kipenzi! Je, nikupe? Je, nikutunuku? Je, nikukurubishie? Je, nikufanyie? Mambo kumi ukiyafanya, Allaah Atakughufiria madhambi yako; ya mwanzo yake na ya mwisho yake, ya zamani yake na ya sasa yake, ya kukosea yake na ya kukusudia yake, madogo yake na makubwa yake, na ya siri yake na ya wazi yake. Mambo kumi ni wewe uswali rakaa nne, utasoma katika kila rakaa Al-Faatihah pamoja na sura yoyote. Ukimaliza kusoma katika rakaa ya kwanza, utasema ukiwa bado umesimama: “Subhaana Allaah wal Hamduli Laahi wa laailaaha illa Allaahu Allaahu Akbar” mara kumi na tano. Kisha utarukuu na utasema hivyo hivyo mara kumi ukiwa umerukuu. Kisha utanyanyua kichwa chako toka kwenye rukuu na utayasema hayo hayo mara kumi. Halafu utakwenda kusujudu na utayasema hayo hayo mara kumi ukiwa ndani ya sijdah. Kisha nyanyua kichwa chako toka kwenye sijdah, na utayasema mara kumi, kisha sujudu tena na useme mara kumi, halafu nyanyua kichwa chako uyaseme mara kumi. Na hizo ni mara sabini na tano katika kila rakaa. Utafanya hivi katika rakaa nne. Ukiweza kuiswali kila siku mara moja, basi swali. Kama huwezi, basi mara moja kila ijumaa, na kama hukuweza, basi kila mwezi mara moja. Kama hukuweza, basi mara moja kila mwaka, na kama hukuweza, basi mara moja katika umri wako)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Kuna mvutano katika kuifanya kuwa Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1297), Ibn Maajah (1387), Al-Haakim (1/318-319), Al-Bayhaqiy (3/51), At-Twabaraaniy (11/161), Abu Na’iym katika Al-Hilyah (1/2-25-26) na wengineo kupitia njia mbalimbali toka kwa Ibn ‘Abbaas, na njia zote ni Dhwa’iyf. Ina Hadiyth wenza lakini zote hazifai kuitilia nguvu. Na kwa ajili hiyo, Al-Haafidh amesema katika At-Talkhiys (2/7): “Kiukweli ni kuwa Sanad zake zote ni Dhwa’iyf ingawa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas inakurubia sharti ya kuwa ni Hasan isipokuwa ni “Shaadh” kutokana na upekee wake usio wa kawaida, kutokuwa na muundo wa kukinaisha akili na kutofautiana kabisa na miundo ya Swalaah nyinginezo”. Ninasema: “Maulamaa wengi wamesema kuwa Hadiyth hii ni Dhwa’iyf kama Al Imaam Ahmad (ambaye inasemekana alijirudi na kusema si Dhwa’iyf), At-Tirmidhiy na Ibn Al-‘Arabiy. Ibn Al-Jawziy ameiweka kwenye kitabu chake cha Al-Mawdhuwaat, na Maulamaa waliobobea hifdh ya Hadiyth wamemjibu kwa hilo. Sheikh wa Uislamu amesema ni Dhwa’iyf, na Ibn Khuzaymah na Adh-Dhahabiy hawako huku wala kule]

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na hukmu yake katika kauli tatu:

 

Ya kwanza:

 

Ni Sunnah. Limesemwa hili na baadhi ya Maulamaa akiwemo Ibn Mubaarak na baadhi ya Mashaafi’i. [Al-Majmu’u (3/647) na Nihaayatul Muhtaaj (2/119)]

Hawa wamesema kwamba Hadiyth hiyo ni Swahiyh na wao wanaikubali.

 

Ya pili:

 

Haina ubaya (inajuzu). Hili wamelisema baadhi ya Mahanbali. [Al-Mughniy (2/132)]

Wamesema: “Ikiwa hakuna Hadiyth iliyothibiti kuhusiana na Swalaah hii, basi Swalaah hii ni katika amali bora, na Hadiyth Dhwa’iyf inatosha kuipitisha!!

 

Na kwa ajili hiyo, Ibn Qudaamah amesema katika Al-Mughniy (2/132): “Ikiwa mtu ataiswali basi hakuna ubaya, kwani Sunnah na ‘ibaadah za fadhila si lazima zithibitishwe na Hadiyth Swahiyh!!

 

Ya tatu:

 

Swalaah hii haipo. Ni kauli ya Al-Imaam Ahmad. Amesema: “Linanishangaza jambo”. Akaulizwa: “Kwa nini?” Akasema: “Hakuna chochote Swahiyh kilichoizungumzia”, akaikung’uta mikono kuonyesha anakataa. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (2/132)]

 

An Nawawiy amesema: “Jambo la kusema kwamba Swalaah hii ni Sunnah ni lazima liangaliwe, kwa kuwa Hadiyth yake ni Dhwa’iyf, nayo imebadili mfumo wa Swalaah ujulikanao. Inatakikana lisifanywe jambo bila Hadiyth, na Hadiyth ya Swalaah hii si thabiti.  [Al-Majmu’u (3/548)]

 

Ninasema: “Kauli hii ya mwisho ndiyo yenye uzito zaidi kwa kuwa Hadiyth haijathibiti mbali na utaratibu wa Swalaah hiyo kukhalifiana na Swalaah nyinginezo. Lakini ikiwa mtu ana sifa za kufanya ijtihadi, na akakuta kwamba Hadiyth ni Swahiyh kwa mujibu wa ijtihaad yake, basi imesuniwa kwake kuiswali. Ama kauli ya pili yenye kujuzisha pamoja na udhwa’iyf wa Hadiyth, nayo pia ni kauli dhwa’iyf kutokana na mambo mawili:

 

1- La sawa ni kuwa Hadiyth Dhwa’iyf haifanyiwi kazi kabisa, si katika amali bora wala katika amali nyinginezo zozote. Huu ndio msimamo wa Maulamaa wahakiki wakiongozwa na Al-Bukhaariy, Muslim, Yahya bin Ma’iyn, Ibn Hazm na wengineo.  [Angalia Tamaam Al-Minnah (uk. 34) na utangulizi wa Swahiyhut Targhyb (1/16-36)]

 

2- Wanaosema kwamba Hadiyth Dhwa’iyf inaweza kutumiwa katika amali bora wameweka masharti kadhaa. Kati ya masharti hayo ni kuwa amali hiyo iwepo kisharia. Na Swalaah hii kwa muundo huu, haipo kisharia isipokuwa kwa Hadiyth hii, nasi hatuwezi kuiswali kama ni amali bora inayotambulika kisharia.

 

· Tanbihi

 

Kwa wanaosema kwamba Swalaah hii inajuzu, tunawaambia kwamba kuipangia Swalaah hii tarehe 27 ya Mwezi wa Ramadhwaan na watu kukusanyika Msikitini ili kuiswali, ni bid-’a isiyo na asili yoyote. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

 

Share