040-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Uimamu Na Hukmu Zake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

040-Uimamu Na Hukmu Zake 

 

 

· Fadhla Ya Uimamu

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir akisema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((Halitaacha kundi katika Umma wangu kuwa linaipigania haki na likiwashinda maadui mpaka kukurubia Siku ya Qiyaamah. Anasema: Atateremka ‘Iysaa bin Maryam (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam), na Amiri wao atasema: Njoo utuswalishe, naye atasema: Hapana, hakika nyinyi kwa nyinyi ni Maamiri. Ni Takrima ya Allaah kwa Umma huu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (156) na Ahmad (3/384)].

 

· Nani Anastahiki Zaidi Uimamu? Je, Ni Mweledi Zaidi Wa Kusoma Au Mtaalamu Aliyebobea Taaluma Ya Dini?

 

Maulamaa wana mielekeo miwili kuhusiana na suala hili: [Al-Mabsuutw (1/41), Al-Mudawwanah (1/83), Al-Majmuu (4/180) na Al-Mughniy (2/134)].

 

Wa kwanza:

 

Msomaji mweledi zaidi anastahiki.

 

Ni kauli ya Abu Haniyfah na Maswahibu zake, Ath-Thawriy na Ahmad. Dalili yao ni:

 

1- Hadiyth ya Abu Saiyd Al-Khudriyy aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Watu wakiwa watatu, basi awaswalishe mmoja wao, na mwenye haki zaidi ya kuswalisha ni yule aliyewazidi wenzake kwa kisomo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (672), An-Nasaaiy (2/77) na Ahmad (3/24)].

 

2- Hadiyth ya Abu Mas-’oud Al-Answaariy aliyesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Awaswalishe watu mwenye kukisoma zaidi Kitabu cha Allaah. Kama kisomo chao kiko sawa, basi awaswalishe mjuzi zaidi wa Sunnah. Kama wako sawa katika Sunnah, basi aliyehajiri mwanzo. Na kama wako sawa katika Hijrah, basi aliyetangulia katika Uislamu. Na mtu asimwongoze mtu katika madaraka yake ila kwa idhni yake, na asikae nyumbani kwake juu ya kiti chake ila kwa idhni yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (673), Abu Daawuud (582), At-Tirmidhiy (235), An-Nasaaiy (2/76) na Ibn Maajah (980)].

 

3- Hadiyth ya ‘Amri bin Salamah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( Swalini Swalaah fulani katika wakati fulani, na swalini Swalaah fulani katika wakati fulani, na wakati wa Swalaah unapoingia, basi mmoja wenu aadhini, na awaswalisheni mweledi wenu zaidi wa Qur-aan))…..Wakaangalia, na hakukuwepo stadi zaidi wa kusoma kuliko mimi, kwa kuwa nilikuwa nikipata ‘ilmu toka kwa wasafiri. Wakanitanguliza mbele umri wangu ukiwa miaka sita au saba hivi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4302), Abu Daawuud (585), An-Nasaaiy (2/80) na Ahmad (3/475)]. Hadiyth

 

4- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Muhaajiryna wa awali walipofika Al-‘Uswbah (ni sehemu iliyoko Qubaa) kabla ya kuja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Saalim aliyekuwa mtumwa wa Abu Hudhayfah alikuwa akiwaswalisha, naye alikuwa mweledi zaidi wao wa kusoma”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (692) na Abu Daawuud (588)].

 

Saalim alikuwa wakati huo bado ni mtumwa hajaachwa huru, lakini aliwaswalishwa pamoja na kuwa wao ni waungwana.

 

Wa pili:

 

Mtaalamu aliyebobea taaluma ya dini anastahiki zaidi kuliko msomaji stadi.

 

Ni kauli ya Maalik na Ash-Shaafi’iy, na riwaya toka kwa Abu Haniyfah na Ahmad. Dalili yao ni:

 

1- Ni kuwa linaweza kumtokea jambo ndani ya Swalaah ambalo hawezi kujua afanye vipi isipokuwa kwa kuwa na ujuzi, hivyo mjuzi anakuwa ni bora zaidi. Ni kama imamu au Kadhi Mkuu.

 

2- Wamezijibu Hadiyth zilizotangulia kwa kusema kuwa stadi zaidi wa kusoma katika Maswahaba ndiye mtaalamu zaidi wa taaluma ya dini, kwa kuwa walikuwa hawasomi Aayah kumi mpaka wafahamu maana zake na yaliyomo ndani yake kati ya elimu na amali. Nao wamejibiwa kuwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “ Kama kisomo chao kiko sawa, basi awaswalishe mjuzi zaidi wa Sunnah” linatoa dalili kwamba msomaji stadi ndiye wa kutangulizwa bila mpinzani.

 

3- Ni Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumtanguliza Abu Bakr awaswalishe watu wakati ugonjwa ulipomzidia, na Abu Bakr hakuwa stadi wao zaidi. Wamejibiwa kwamba kutangulizwa Abu Bakr kulikuwa ni ishara ya kuteuliwa kuwa Khaliyfah, na Khaliyfah ana haki zaidi na uimamu hata kama mwingine ni stadi zaidi wa usomaji kuliko yeye.

 

· Lenye Nguvu:

 

Mweledi zaidi wa kusoma ndiye anayestahiki zaidi kuwa imamu lakini kwa sharti kwamba awe anajua yote yanayopasa kuyajua kuhusu Swalaah. Na kama hayajui hayo, basi asiwe imamu kwa itifaki ya Maulamaa. [Fat-hul Baariy (2/171). Chapa ya Al-Maarifah].

 

Kisha swali linabaki: Nini makusudio ya msomaji mweledi zaidi?

Jamhuri wanasema kwamba ni yule anayesoma vizuri zaidi. Baadhi ya Mahanbali wanasema ni yule aliyehifadhi zaidi.

 

Ninasema: “Naam, ni yule  aliyehifadhi zaidi kutokana na Hadiyth zilizotangulia zinavyohabarisha, lakini kwa sharti kwamba kisomo chake kiwe sahihi na madhubuti, na kila herufi itoke kwenye ala yake (makhraji yake).

 

· Angalizo:

 

Haitakikani Kumfanya Imamu Asiyestahiki Uimamu Kwa Kuwa Tu Anaghani Mno Anaposoma

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abbaas Al-Ghaffaariy akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiyaeleza mambo sita anayoyakhofia juu ya Umma wake: Watoto wadogo kuendesha dola, kukithiri polisi na vyombo vya usalama, watawala kula hongo, kukata ukoo, kuua bila kujali, na mashabiki wenye kuifanya Qur-aan zumari. Wanamtanguliza mtu ambaye si mjuzi wao wala mbora wao awaghanie nyimbo))”. [Hasan kwa Sanad tofauti: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr (18/37), Ahmad (3/494) na Al-Bukhaariy katika At-Taariykh (7/80). Ina Hadiyth wenza zenye kuitilia nguvu].

 

Makusudio ya ughaniji unaolaumiwa hapa, ni ule wa chumvi ya kulazimisha unaopetuka qaaidah za lugha na tajwiydi, wa madoido ziada, wa kurembesha, na wa mahadhi yanayochukiwa na Maulamaa.

 

· Mtu Asiingie Kuswalisha Wakati Imamu Mteule Yupo Ila Kwa Ruksa Yake

 

Ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) – katika Hadiyth ya Ibn Mas-’oud iliyotangulia punde - ((Na mtu asimwongoze mtu katika madaraka yake ila kwa idhni yake)). [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma kidogo]

 

Imamu wa Msikiti kapewa mamlaka yake na wahusika, na kwa hivyo haijuzu mtu mwingine aswalishe ila kwa idhni yake, na kama si hivyo basi itakuwa ni fujo na migogoro. Wahusika inawabidi wamteue imamu anayefaa na anayestahiki kazi hiyo, na kama si hivyo, basi watapewa uimamu wahafidhi mamluki wasioswalisha itakikanavyo na wasiojua hukumu zake!!

 

· Ustahikivu Wa Uimamu Kiufupi

 

Ikiwa Msikiti una imamu mteule wa kudumu, basi huyo ndiye wa kuswalisha, na kama hayuko, basi atatangulizwa msomaji stadi na mjuzi zaidi wa Fiqhi ya Swalaah. Kama watu watalingana, basi atangulizwe mjuzi na mwelewa zaidi wao wa Sunnah. Wakilingana, basi aliyewatangulia wote kwa Hijrah, na kama watalingana, basi mkubwa wao zaidi kiumri. [Hijrah ni kuhama toka nchi ya Makafiri kwenda nchi ya Kiislamu. Hijrah hii inaendelea mpaka Siku ya Qiyaamah, haina ukomo].

 

Haya ndiyo yanayofahamika kutokana na maneno ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyomwambia Maalik bin Al Huwayrath pamoja na watu aliokuwa nao wakati walipotaka kurejea kwa watu wao:

((Swalini kama mlivyoniona nikiswali. Na Swalaah inapowadia, basi mmoja wenu aadhini, na mkubwa wenu zaidi kiumri awaswalishe)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (631) na Muslim (674)].

 

· Si Sharti Imamu Awe Yule Aliyewapiku Wote

 

Bali unajuzu uimamu wa kila ambaye uimamu wake unaswihi kumswalisha imamu anayestahiki zaidi uimamu kuliko yeye. Ni kama Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposwali nyuma ya Abu Bakr wakati wa maradhi yake aliyofia. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (684)].

 

Aidha, Rasuli aliswali rakaa ya pili ya Swalaah ya Alfajiri nyuma ya ‘Abdul Rahmaan bin ‘Awf.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim toka Hadiyth ya Al-Mughiyrah].

 

· Watu Ambao Uimamu Wao Unaswihi

 

1- Kipofu

 

Imepokelewa toka kwa Muhammad bin Ar-Rubay’i ya kwamba ‘Utbaan bin Maalik alikuwa akiwaswalisha watu wake naye ni kipofu, na kwamba alisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Hakika inakuwa ni giza na mafuriko na mimi ni mtu kipofu, basi swali ee Rasuli wa Allaah nyumbani kwangu katika sehemu ambayo nitaifanya kuwa ndio kijimsikiti changu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwendea kisha akamuuliza: ((Ni wapi unataka niswali?)). Akamwonyesha sehemu ya nyumba, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaswali hapo. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (667) na Muslim (33)].

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa Ibn Maktoum uongozi wa kuswalisha watu Madiynah. [Swahiyh Lighayrih: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Hibaan (2134) na Abu Ya’alaa (4456). Ina Hadiyth mwenza ya Ibn ‘Abbaas].

 

· Faida

 

Kwa mujibu wa kauli yenye nguvu, inajuzu kwa mwenye ulemavu wowote kumswalisha mzima asiye na ulemavu, kwa kuwa hakuna tofauti kati yake na kipofu. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi. [Angalia As-Saylu Al-Jarraar (1/253)].

 

2- Mtumwa na aliyewahi kuwa mtumwa

 

Imepokelewa na Ibn ‘Umar akisema: “Muhaajiriyn wa awali walipofika Al-‘Uswbah (ni sehemu iliyoko Qubaa) kabla ya kuja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Saalim aliyekuwa mtumwa wa Abu Hudhayfah alikuwa akiwaswalisha, naye alikuwa mweledi zaidi wao wa kusoma”. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa nyuma kidogo].

 

Maswahaba wakubwa wa Kikureshi, wote kwa pamoja, waliafiki kumtanguliza Saalim, na wakati huo alikuwa ni mtumwa, hajaachwa huru bado. Kutangulizwa huku kunatoa dalili ya kujuzu mtumwa kuwa imamu.

 

Imepokelewa toka kwa Naafi’i bin ‘Abdul Haarith ya kwamba ‘Umar alimwambia: “Ni nani unayemtumia kuwaongoza watu wa Bondeni?” Akasema: “Ni Ibn Abzaa”. Akauliza: “Ni nani Ibn Abzaa?” Akasema: “Alikuwa ni katika watumwa wetu”. Akauliza: “Umewawekea mtumwa wa zamani kuwaongoza?” Akajibu: “Ni msomaji mzuri wa Kitabu cha Allaah ‘Azza wa Jalla na mjuzi wa taaluma ya mirathi”. ‘Umar akasema: “Ama mimi, hakika nimemsikia Nabiy wenu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hakika Allaah Huwanyanyua kwa Kitabu hiki watu, na Huwashusha wengine kwacho)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (817), Ibn Maajah (218) na Ahmad (1/35)].

 

Kwa haya, Jamhuri wanaona kwamba uimamu wa mtumwa unaswihi kinyume na Maalik.

 

2- Mtoto mtambuzi

 

Tumeshaeleza nyuma kwamba ‘Amri bin Salamah aliwaswalisha watu wake akiwa mtoto wa miaka sita au saba wakati Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowaamuru awaswalishe mwingi wao kwa kisomo.

 

Ash-Shaafi’iy pekee ndiye anayekubali hili kinyume na Jamhuri wanaokataa, lakini Hadiyth inawarudi wenyewe. Na mwenye kusema kwamba hao walilifanya hilo kwa ijtihada yao wenyewe na Rasuli hakuliona, basi hakutenda haki, kwa kuwa haiwezekani likapitishwa jambo lisilojuzu wakati Wahyi bado unashuka. Ni kama Abu Sa’iyd na Jaabir walivyotoa dalili ya kujuzu kumwagia maji ya uzazi nje ya utupu wa mwanamke kwa kuwa wao walilifanya katika enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na kama hilo lingekuwa limekatazwa, basi Qur-aan ingelikataza. [Fat-hul Baariy (8/23) chapa ya Al-Maarifah].

 

3- Fasiki

 

Katika kauli mbili sahihi zaidi za Maulamaa, fasiki anafaa kuwa imamu. Hii ni kauli ya Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy na riwaya toka kwa Ahmad. [Al-Mabsuutw (1/40), Al-Majmu’u (4/123) na Al-Inswaaf (2/252)].

 

Yanayoarifu hilo ni:

 

(a) Ujumuishi wa Hadiyth zilizotangulia katika kumtanguliza msomaji zaidi wa Kitabu cha Allaah.

 

(b) Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Wanawaswalisheni, na kama watafanya sawa, basi thawabu mtapata nyinyi, na kama wakikosea, basi thawabu mtapata nyinyi, na wao watabeba makosa yao)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (294) na Ahmad (2/355)].

 

(C) Hadiyth ya ‘Ubaydullah bin ‘Uday bin Al-Khayyar ya kwamba aliingia kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allahu Anhu) akiwa amezingirwa akamwambia: “Wewe ni imamu mkuu, na yamekufika haya tunayoyaona. Anatuswalisha imamu wa fitna, nasi twahofia kuwa tunafanya makosa”. Akamwambia: Swalaah ndiyo amali bora kabisa wanayoifanya watu. Na kama watu watafanya amali bora, basi fanya nao, lakini wakifanya ubaya, basi uepuke ubaya wao.“ [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (695) na ‘Abdul Razzaaq (1991)].

 

(d) Maswahaba akiwemo Ibn ‘Umar, waliswali nyuma ya Al-Hajjaaj bin Yuusuf, naye ni fasiki mbaya kabisa. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1660) na An-Nasaaiy (5/254)].

 

Lakini pamoja na kujuzu, ni karaha kuswali nyuma yake kutokana na Hadiyth ya Thawbaan aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Kwa hakika ninauogopea Umma wangu viongozi wa dini wapotoshi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (2229), Abu Daawuud (4252) na Ahmad (6/278)].

 

Ikiwezekana kumfuata asiye fasiki, basi inatakikana kumwacha fasiki, na kama haiwezekani kwa kuwa Jamaa yaweza kutatizika, basi itajuzu kumfuata kama ilivyotangulia. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

· Faida

 

Haijuzu kuswalishwa na kafiri kwa kuwa Swalaah yake haiswihi kwake mwenyewe. Allaah Anasema:

((وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ))

(( Kwa yakini umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka zitaporomoka ‘amali zako na bila shaka utakuwa miongoni mwa waliokhasirika”)). [Az-Zumar (:65)]

 

Na Anasema tena:

((وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا))

(( Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya ‘amali yoyote ile, Tutayafanya   chembechembe za vumbi zinazoelea hewanizinazotawanyika )). [Al-Furqaan (25:23)]

 

5- Asiyejulikana itikadi yake wala hali yake

 

Maimamu wote wanne na wengineo wamekubaliana kwamba Swalaah inaswihi nyuma ya imamu asiyejulikana kuwa anafanya mambo ya bid-’a au ufasiki, na kwamba si sharti ya kufuata kwamba maamuma ajue itikadi ya imamu wake wala kumjaribu kwa kumuuliza itikadi yake, bali ataswali nyuma ya asiyejulikana hali yake. [Majmu’u Al-Fataawaa cha Sheikh wa Uislamu (23/351)].

 

Hii ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Wanawaswalisheni, wakifanya sawa basi thawabu ni zenu, na wakikosea basi thawabu ni zenu na makosa ni juu yao)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa nyuma kidogo].

 

Na Anas bin Maalik anasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((Mwenye kuswali Swalaah yetu, akaelekea Qiblah chetu na akala kichinjwa chetu, basi huyo ni Muislamu mwenye Dhima ya Allaah na Dhima ya Rasuli Wake. Basi msimfanyie Allaah udanganyifu katika Dhima Yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1/391), Abu Daawuud (2641), At-Tirmidhiy (2608) na An-Nasaaiy (2/105)].

 

Ibn Hazm kasema: [Al-Muhallaa (4/51)].

 “Akiswali nyuma ya mtu anayedhani kuwa ni Muislamu, kisha akajua kwamba ni kafiri au anacheza tu, au hajabaleghe, basi Swalaah yake ni kamili, kwa kuwa Allaah Hakumkalifisha kuyajua yaliyomo ndani ya nyoyo za watu, bali tumekalifishwa yale tuyaonayo kidhahiri. Hivyo, tunaloamrishwa Swalaah inapoqimiwa ni kuswalishwa na mtu tunayemwona kidhahiri, na mwenye kufanya hivyo, basi anakuwa ameswali kama ilivyoamrishwa..”.

 

Lakini Jamhuri wamesema: “Ni lazima aswali tena akija kujua kwamba imamu wake ni kafiri”.

 

4- Mwanamke kuswalisha Jamaa ya wanawake

 

Katika mlango wa hukmu ya Jamaa ya wanawake, tulieleza kwamba ‘Aaishah na Ummu Salamah waliwaswalisha wanawake wenzao.

 

Ama mwanamume na kijana kuswalishwa na mwanamke, hilo haliswihi kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri ya Masalaf na Makhalaf kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

((Hawatofaulu watu waliomtawalisha mwanamke juu yao)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4425), At-Tirmidhiy (2262) na An-Nasaaiy (8/227)].

 

Na pia ni kuwa haikuthibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba alijuzisha mwanamke kumswalisha mwanamume au wanaume mbali na kuwa hakuna tukio lolote kuhusu jambo hili lililotokea enzi ya Rasuli wala enzi ya Maswahaba wala enzi ya Taabi’iyna.

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliziweka safu zao nyuma ya safu za wanaume kuchelea fitna. Hivyo, mwanamume kumfuata mwanamke ni kinyume na haya yaliyotajwa. Na huwezi kusema kwamba asili ni kufaa hilo!! Kwa kuwa sisi tunasema: “ Yamekuja yenye kuarifu kwamba wanawake hawafai kuongoza jambo lolote, na hili ni katika jumla ya mambo, bali ndilo la juu na tukufu zaidi”. [As-Saylu Al-Jarraar (1/250)].

 

· Mwenye Kuwaswalisha Watu Na Wao Wanamchukia

 

Imepokelewa na Abu Umaamah akisema: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Watu watatu Swalaah zao hazivuki masikio yao (hazikubaliwi kabisa): Mtumwa aliyetoroka mpaka arejee, mwanamke aliyelala nailhali mumewe ameghadhibika naye, na imamu anayeongoza watu na wao wanamchukia)). [Hasan kwa Sanad tofauti: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (360). Ina Hadiyth mwenza kwa Abu Daawuud (593) na Ibn Maajah (970)].

 

Makamio haya ni mahususi kwa mtu ambaye watu wanamchukia kwa sababu ya dini yake, kwenda kwake kinyume na Sunnah au mengineyo mengi ambayo yamekuwa ni mtihani katika zama zetu hizi toka kwa maimamu ambao hima yao kubwa ni kujikita Misikitini ili kupata mishahara. Wengi wao hawaijui dini, na wamekuwa chanzo cha matatizo yote na kwa watu wao. Tunajilinda kwa Allaah na yenye kuchusha.

 

Ama imamu mwenye kusimamisha Sunnah, basi madhambi watayapata wanaomchukia. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa Usamah madaraka awaongoze watu, lakini watu hao waliupinga na kuukosoa uongozi wake. Rasuli akasema:

((Kama mnaukosoa na kuupinga uongozi wake, basi mshaukosoa na kuupinga uongozi wa baba yake kabla yake.  Basi naapa kwa Allaah! Hakika yeye alikuwa anastahiki uongozi, na hakika yeye ni katika watu wanaopendeka zaidi kwangu, na hakika huyu bila shaka, ni katika watu wanaopendeka zaidi kwangu baada yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4250) na Muslim (2426)].

 

 

Share