041-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Mahala Pa Kusimama Imamu Na Maamuma

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

041-Mahala Pa Kusimama Imamu Na Maamuma

 

Alhidaaya.com

 

 

[1] Swalaah ya imamu na maamuma mmoja tu

 

Akiswali mtu mmoja tu na imamu, basi atasimama sambamba upande wake wa kulia –bila kurudi kidogo nyuma kama anavyosema Ash-Shaafi’iy- kutokana na yaliyomo ndani ya kisa cha Ibn ‘Abbaas aliposwali na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Kisha akasimama kuswali (yaani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)), nami nikasimama na kufanya kama alivyofanya. Kisha nikaenda na kusimama pembeni yake, naye akaweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa changu, akalikamata sikio langu la kulia na kulisokota. Kisha akaswali…”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (183) na Muslim (763)].

 

Na katika riwaya nyingine: [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (1/330) kwa Sanad Swahiyh lakini riwaya hii kidhahiri ni “Shaadhah”].

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoelekea kwenye Swalaah yake, nilirejea nyuma, Rasuli akaswali, na alipomaliza aliniambia: ((Vipi wewe? Nakuweka pembeni yangu nawe warudi nyuma!)). Hadiyth

 

Na Jaabir anasema katika kisa chake cha kuswali na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Akaja, akatawadha, kisha akasimama akaswalia nguo moja aliozifunga ncha zake kinyume. Nami nikasimama nyuma yake, akalikamata sikio langu na kuniweka kuliani kwake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (766) na Ahmad (3/351)].

 

Na katika kisa cha Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) -katika maradhi yake ya kifo- pembeni mwa Abu Bakr, ‘Aaishah amesema: “ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakaa sambamba pembeni mwa Abu Bakr. Abu Bakr akawa anaswali kwa Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na watu wanaswali kwa Swalaah ya Abu Bakr”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (683) na Muslim (418)].

 

[2] Swalaah ya imamu na watu wawili au zaidi

 

- Wakiswali watu wawili na imamu, watasimama nyuma yake safu moja kwa makubaliano ya Maswahaba Maulamaa na waliofuatia baada yao kinyume na Ibn Mas-’oud na Maswahibu zake wawili. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Jaabir aliyesema: “Kisha nikaja mpaka nikasimama kushotoni mwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akaukamata mkono wangu akanizungusha na kunisimamisha kuliani kwake. Kisha akaja Jabbar bin Swakhr, akatawadha, halafu akaja na kusimama kushotoni mwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaikamata mikono yetu sote, akatusukuma na kutusimamisha nyuma yake”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (3006) katika Hadiyth ndefu, Ibn Maajah (973) na Ahmad (3/421)].

 

Naye Anas anasema: “Tuliswali mimi na yatima katika nyumba yetu nyuma ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na mama yangu –Ummu Sulaym- yuko nyuma yetu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (727) na Muslim (658)].

 

Ama Ibn Mas-’oud, yeye alikuwa anaona kwamba mmoja asimame kuliani mwa imamu na mwingine kushotoni. Al-Aswad na ‘Alqa’mah waliswali pamoja na ‘Abdullah bin Mas-’oud nyumbani kwake. Wanahadithia hilo wakisema: “..Tukaenda ili tusimame nyuma yake, akatukamata mikono yetu, akamweka mmoja wetu kuliani kwake na mwingine kushotoni kwake. Aliporukuu, tuliweka mikono yetu juu ya magoti yetu. Anasema: Akaipiga mikono yetu, akapandanisha kati ya viganja vyake viwili, kisha akaviingiza baina ya mapaja yake mawili, halafu akasema: Hivi ndivyo alivyofanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (534), Abu Daawuud (613) na An-Nasaaiy (2/49)].

 

Lakini kundi la Maulamaa akiwemo Ash-Shaafi’iy linasema kwamba Hadiyth hii ya Ibn Mas-’oud ni Mansuwkh, kwa kuwa  alijifundisha Swalaah hii toka kwa Rasuli akiwa Makkah ambako utendaji na hukmu ulikuwa ni tofauti, nazo kwa sasa zimeachwa, na hukmu hii ilikuwa ni miongoni mwazo. Na Rasuli alipofika Madiynah aliiacha. Na ikiwa tutajaalia kwamba historia ya tukio haijulikani, basi Hadiyth hii haina ubavu wa kuzipinga Hadiyth zilizotangulia. [Naylul Aw-Twaar na Al-Muhalla].

 

- Wakiswali watu zaidi ya watatu na imamu, basi wote watasimama nyuma yake kwa Ijma’a ya Maulamaa. Hadiyth zenye kubainisha hili ni nyingi mno hazihesabiki.

 

- Haijuzu maamuma kumtangulia imamu, kwa kuwa haiswihi kumfuata imamu isipokuwa kama yuko mbele ya maamuma. Jamhuri wanasema kwamba mwenye kumtangulia imamu Swalaah yake ni batili. Lakini Maalik, Is-Haaq, Abu Thawr na Daawuud wanaona kwamba inajuzu kama nafasi itakuwa finyu, na wengine wanasema kwa hali yoyote yajuzu. [Ibn ‘Aabidiyn (1/551), Ad-Dusouqiy (1/331), Mughnil Muhtaaj (1/490), Kash-Shaaful Al-Qinaa’a (1/485), na Al-Inswaaf (2/280)].

 

[3] Swalaah pembeni ya imamu kwa aliyekosa nafasi Msikitini

 

Anayeingia Msikitini, akakuta Msikiti umejaa na safu zimekamilika, anaruhusiwa kuzipenya safu kwenda kwa imamu kusimama pembeni yake. Hili alilifanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika maradhi yake wakati Abu Bakr alipokuwa anaswalisha watu. “Abu Bakri alipomwona, alirejea nyuma, naye akamwashiria aendelee kama alivyo. Rasuli akakaa sambamba pembeni ya Abu Bakri”. [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma kidogo].

 

Na pia kisa cha kwenda Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Bani ‘Amri bin ‘Awf ili kuwasuluhisha, na akamkuta Abu Bakri anawaswalisha watu. Kisa kinasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaja na watu wako kwenye Swalaah. Akajipenyeza mpaka akasimama kwenye safu……”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (684) na Muslim (421)].

 

Na katika tamshi la Muslim: “Akazipenya safu mpaka akasimama mbele ya safu ya mbele”.

 

[4] Swalaah ya mwanamke na imamu

 

Mwanamke akiswali na imamu, basi atasimama nyuma ya safu za wanaume hata kama hakuna wanawake wenzake. Atasimama peke yake kwenye safu ya mwisho. Na kama ataswali yeye peke yake na imamu, basi atasimama nyuma yake, na si kuliani kwake.

 

Ummu Salamah anasema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotoa tasliym, wanawake husimama anapomaliza tasliym yake, naye hukaa kidogo mahala pake kabla hajasimama. Tunaona –na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi- kwamba hilo ni ili wanawake waondoke kabla mwanamume yeyote hajawakuta”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (870), Abu Daawuud (1040), An-Nasaaiy (2/66) na Ibn Maajah (932)].

 

Na Anas amesema: “Niliswali mimi na yatima nyuma ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na mama yangu Ummu Sulaym yuko nyuma yetu”. [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma kidogo].

 

Naye Ibn Mas-’oud amesema: “Wanaume na wanawake wa Bani Israa’iyl walikuwa wakiswali pamoja. Mwanamke mwenye mpenzi wake, alikuwa akivaa visigino virefu ili apate kimo zaidi mbele ya mpenzi wake, na hapo wakateremshiwa hedhi”. Ibn Mas-’oud alikuwa akisema: “Wawekeni nyuma pale Alipowarudisha Allaah”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (5115) na At-Twabaraaniy (9384)].

 

Na kama wataswali imamu, mwanamume mmoja na mwanamke mmoja, basi mwanamume atasimama sambamba kuliani mwa imamu, na mwanamke atasimama peke yake nyuma yao. Imepokelewa toka kwa Anas kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimswalisha yeye pamoja na mwanamke. Rasuli akamweka yeye kuliani kwake, na mwanamke nyuma yao kidogo. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (269) na Ibn Abu Shaybah (2/88)].

 

· Faida

 

Ikiwa mwanamke atavunja miiko kwa kuswali mbele ya safu za wanaume, basi Swalaah yake itajuzu kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri. Lakini Hanafi wanasema kuwa Swalaah ya wanaume ndiyo itakuwa batili, na si ya mwanamke!!.

 

Ninasema:

“La sahihi ni kuwa Swalaah yake mwanamke ndiyo inayobatilika kutokana na Hadiyth isemayo: ((Mwenye kuswali peke yake nyuma ya safu, hana Swalaah)), na kwa kusimama Ummu Salamah peke yake nyuma ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Anas na yatima. Na hili linatujulisha kwamba Swalaah yake hubatilika akiswali mbele ya wanaume au akiwa nao pamoja. Lakini hili ni kama hakuna dharura ya kufanya hivyo”.

 

[5] Swalaah ya mwanamke na wanawake wenzake

 

Mwanamke akiswalisha jamaa ya wanawake wenzake, basi atasimama katikati yao, hatokuwa mbele ya safu yao ya kwanza. Hili ni sitara zaidi kwake. Imepokelewa toka kwa Rabtwah Al-Hanafiyyah akisema kwamba ‘Aaishah aliwaswalisha na akasimama katikati yao katika Swalaah ya faradhi. [Hadiyth Swahiyh kwa Hadiyth wenza zenye kuitilia nguvu: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (3/141), Ad-Daara Qutwniy (1/404) na Al-Bayhaqiy (3/131)].

 

Imepokelewa toka kwa Hujayrah toka kwa Ummu Salamah kwamba aliwaswalisha na akawa katikati yao.  [Hadiyth Swahiyh kwa Hadiyth wenza zenye kuitilia nguvu: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (3/140), Ad-Daara Qutwniy (1/405) na Al-Bayhaqiy (3/131)].

 

Na ikiwa mwanamke atawaswalisha wenzake na akasimama mbele yao, basi kwa mujibu wa mwono wenye nguvu zaidi, Swalaah yake itakuwa ni sahihi yenye kutosheleza kwa kuwa hakuna dalili ya kuibatwilisha. Lakini hilo litakuwa ni kinyume cha ubora.  Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

[6] Wanaposimama watoto wa kiume katika Swalaah

 

Imesimuliwa kwamba: “Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwaweka wanaume mbele ya watoto, na watoto nyuma yao, na akina mama nyuma ya watoto.” Lakini ni Dhwa’’iyf, haifai. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (677) na Ahmad (5/341) toka kwa Abu Maalik Al Ash-ariy].

 

Imamu Al-Albaaniy amesema: “Ama kuwaweka watoto nyuma yao, sikupata katika hili isipokuwa Hadiyth hii, na hoja haisimami kwayo. Basi mimi sioni ubaya watoto kusimama pamoja na watu wazima ikiwa safu itakuwa na nafasi. Na Swalaah ya yatima pamoja na Anas nyuma ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni hoja juu ya hilo”. [Tamaam Al-Minnah ukurasa wa 282].

 

Ninasema: “Hadiyth ya Anas kuhusu kuswali yeye pamoja na yatima nyuma ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tushaielezea. Na lau kama watoto wangelikuwa wanazuiwa kusimama safu moja na wanaume, basi Anas angelisimama kuliani mwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na yatima angesimama nyuma yao, na Ummu Sulaym naye nyuma yao wote. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.”

 

· Swalaah Ya Imamu Na Maamuma Katika Sehemu Ya Mnyanyuko

 

1- Imamu kuwa juu na maamuma chini

 

Ni karaha kwa imamu kuwa juu na maamuma kuwa chini. Hii ni kauli ya Jamhuri, ni sawasawa kuwa juu kwake ni kwa haja au bila haja. Imepokelewa toka kwa Hammaam: “Kwamba Hudhayfah aliwaswalisha watu huko Al-Madaain akiwa sehemu ya juu. Abu Mas-’oud (Muanswaar) akaikamata kanzu yake akamvuta. Alipomaliza Swalaah alimwambia: “Je, hujui kwamba wao walikuwa wakikatazwa hilo?” Akasema: “Naam. Nilikumbuka uliponivuta”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (597), Ibn Khuzaymah (1523), Al-Haakim (1/210) na Al-Bayhaqiy (3/108). Hakuna kinachoogopewa humo isipokuwa “an-‘anah” ya Al-A’amash].

 

Ash-Shaafi’iy kasema: “Ninapendelea kwa imamu anayewafundisha maamuma wake Swalaah, aswalishe juu ya kitu kilichonyanyuka ili wamwone na kufuatilisha vitendo vyake”. Na hili ni kwa riwaya toka kwa Ahmad kwa Hadiyth ya Sahl bin Sa’ad wakati alipoulizwa kuhusu mimbari akasema: “Kisha nikamwona Rasuli wa Allaah akiswali juu yake (yaani vigogo vya mimbari). Akapiga takbiyr akiwa juu yake, kisha akarukuu akiwa juu yake, halafu akateremka kinyumenyume na kusujudu juu ya mimbari asili, kisha akarudi. Alipomaliza aliwaelekea watu na kuwaambia: “Enyi watu! Mimi nimefanya hivi ili munifuate na mjifunze ninavyoswali”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (917) na Muslim (544)].

 

Ninasema: “Ikiwa kuna faida ya imamu kusimama sehemu iliyonyanyuka kama kuwafundisha watu na mfano wake, basi hakuna ubaya kutokana na Hadiyth hii. Pia kama hilo litalazimu kama kujaa sehemu ya juu ya Msikiti aliko imamu na watu wengine wakaswalia chini”.

 

2- Maamuma kuwa juu na imamu kuwa chini

 

Hakuna dalili ya kuzuia maamuma kuswali juu na imamu chini na hususan ikiwa itabidi kama kujaa sehemu ya chini ya Msikiti na wengine wakaswalia juu. Lakini kuswalia huko ni lazima kuwe kwa namna ambayo maamuma anaweza kumsikia imamu, kumfuata na kwenda naye sambamba akiwa nyuma yake. Hatakiwi kuwa mbele yake ila kwa udhuru. Hili linatiliwa nguvu na kitendo cha Abu Hurayrah. Alikuwa juu ya jengo lililo juu ya Msikiti, na alikuwa akimfuata imamu. [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abi Shaybah (2/223), ‘Abdul Razzaaq (4888) na Al-Bayhaqiy (3/111)].

 

Na imepokelewa toka kwa Sa’iyd bin Sulaym akisema: “Nilimwona Saalim bin ‘Abdallah akiswali Swalaah ya Magharibi juu ya paa la Msikiti akiwa na mtu mwingine, yaani akimfuata imamu”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Shaybah (2/233)].

 

· Kumfuata Imamu Nyuma Ya Kizuizi

 

Ikiwa maamuma ataswali nje ya Msikiti na imamu yuko ndani, au akaswali ndani ya Msikiti lakini kipo kizuizi kati yao, basi itajuzu ikiwa safu zitaungana. Maimamu wote wamekubaliana juu ya hili. [Majmu’u Al-Fataawaa (23/407)].

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alikuwa anaswali usiku katika chumba chake na ukuta wa chumba ukiwa mfupi. Watu walikuwa wakikiona kiwiliwili chake na kumfuata katika Swalaah yake”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (729) na Muslim (782)].

 

Chumba hicho ni mkeka uliokuwa ukimwekea kizuizi usiku Msikitini kama ilivyo kwenye baadhi ya riwaya za Hadiyth.

 

Imepokelewa toka kwa Jublah bin Abi Sulaymaan akisema: “Nilimwona Anas bin Maalik akiswali kwenye nyumba ya Abu ‘Abdullah iliyo juu ya Msikiti na yenye mlango wa kuingilia Msikitini. Alikuwa akiswali Ijumaa hapo na akimfuata imamu”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Shaybah (2/223) ‘Abdul Razzaaq (5455) na Al-Bayhaqiy (3/111)].

 

Ikiwa watapanga safu na kukawa kati yao na safu nyingine barabara ambayo watu wanapita, au mto wa kupita meli, basi hili lina kauli mbili ambazo ni riwaya toka kwa Ahmad. Kauli ya kwanza inasema kuwa hilo halifai kama asemavyo Abu Haniyfah, na ya pili inasema kwamba inajuzu kama wasemavyo Maalik na Ash-Shaafi’iy. [Majmu’u Al-Fataawaa (23/407) na Al-Mughniy]..

 

Kauli hii ndiyo yenye nguvu zaidi kwa kuwa hakuna Hadiyth au Ijma’a yoyote yenye kuzuia hilo. Al-Hasan kasema: “Hakuna ubaya ukiswali na kati yako na imamu kuna mto”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy ikiwa Mu’allaq (2/250-Fat-h), ‘Abdul Razzaaq kaifanya Mawsuul (5453) na Ibn Abu Shaybah (2/149)].

 

Lakini inatakikana maamuma aweze kujua vitendo vya imamu kama kusikia takbiyr ya imamu au kuiona safu ya mbele. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowaona Maswahaba zake wanajiweka weka nyuma aliwaambia:

((Njooni mbele mnifuate, na wa nyuma wenu wawafuate wa mbele wenu. Hawataacha watu kuwa wanajiweka weka nyuma mpaka Allaah Awaweke nyuma)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (438), Abu Daawuud (480) An-Nasaaiy (2/83) na Ibn Maajah (978)].

 

Na kwa ajili hiyo, Ibn Mujlaz anasema: “Atamfuata imamu hata kama kutakuweko barabara au ukuta kati yao ikiwa atasikia takbiyr ya imamu”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Al-Bukhaariy kasema ni Mu’allaq (2/250-Fat-h), na Ibn Abu Shaybah kasema ni Mawswuwl (2/223) kwa Sanad Swahiyh].

 

Ninasema: “Haifichikani kwamba sababu ya utengano huu ni dharura kama kujaa Msikiti na viwanja vilivyoungana. Na kama si hivyo, basi asili ni kuungana safu na kukurubiana. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.”

 

· Angalizo:

 

Swalaah ya kumfuata imamu kwa njia ya idhaa (redio) haifai.

 

 

Share