044-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Hukmu Za Aliyetanguliwa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

044-Hukmu Za Aliyetanguliwa

 

Alhidaaya.com

 

 

· Kuipata Jamaa

 

Kuipata Jamaa kuko kwa aina mbili:

 

1- Kuipata fadhla ya Jamaa:

 

Hii hupatikana kwa kushirikiana maamuma na imamu katika sehemu ya Swalaah yake hata kama itakuwa ni katika kikao cha mwisho kabla ya tasliym. Hii ni kauli ya Jamhuri: Hanafi, Hanbali,  Ash-Shaafi’iy na baadhi ya wafuasi wa Maalik. [Ibn ‘Aabidiyn (1/483), Ad-Dusuwqiy (1/320), Mughnil Muhtaaj (1/231) na Kash-Shaaful Qinaa (1/460)].

 

Hili ni sahihi kwa kuwa lau kama asingelipata fadhla ya Jamaa kwa hilo, basi angelizuiliwa kumfuata, kwa kuwa wakati huo inakuwa ni ziada bila faida. Hili linatiliwa nguvu na kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema: ((Mnapoisikia adhana, basi nendeni kwa miguu katika Swalaah. Kuweni watulivu na makini, na wala msifanye haraka. Mnachokipata kiswalini, na mnachokikosa kikamilisheni)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (636) na wengineo. Imeshatajwa nyuma].

 

Imepokelewa toka kwa mtu mmoja wa Madiynah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisikia mchakato wa viatu vyangu akiwa kwenye sijdah. Alipomaliza kuswali aliuliza: ((Ni nani huyu niliyesikia mchakato wa viatu vyake?)) Nikasema: Ni mimi ee Mjumbe wa Allaah. Akasema: ((Umefanya nini?)). Akasema: Nimekukuta umesujudu, nami nikasujudu. Akasema: ((Hivyo hivyo fanyeni, lakini msiihesabu. Mwenye kunikuta nimerukuu, au nimesimama, au nimesujudu, basi awe pamoja nami katika hali niliyopo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/284) kwa Sanad Swahiyh. Ina Hadiyth mwenza kwa At-Tirmidhiy (591) kwa Sanad Dhwa’iyf, na nyingine kwa Abu Daawuud].

 

Lakini thawabu zake zinakuwa chini ya thawabu za yule aliyeipata Swalaah tokea mwanzoni. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

2- Kuipata hukmu ya Jamaa na matokeo yake:

 

Muradi wa hukmu ya Jamaa ni kuthibiti hukmu husishwa kwa kuzingatiwa kuwa yeye ni mwenye kumfuata imamu kama kusujudu naye kama alisahau kitu, au kuswali kwake Ijumaa rakaa mbili na mfano wa hivyo.

 

Kauli dhahiri zaidi ya Maulamaa ni kwamba hukmu ya Jamaa haithibiti ila kwa kuipata rakaa kamili pamoja na imamu [ juu ya mvutano mashuhuri kuhusu ni kipi hasa hupatikania kwacho rakaa. Litafafanuliwa hili, si mbali sana] kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kuipata rakaa katika Swalaah, basi kaipata Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: Takhriyj yake ishaelezwa, nayo imepitishwa na Al-Bukhaariy na Muslim].

Hii ni kauli ya Maalik, na chaguo la Sheikh wa Uislamu. [Ad-Dusuwqiy (1/320) na Majmuu Al-Fataawaa (23/330, 331)].

 

· Kuipata Rakaa

 

Maulamaa wametofautiana kuhusiana na kiasi ambacho maamuma anakuwa ni mwenye kuhesabiwa kwamba ameipata rakaa pamoja na imamu wake katika kauli mbili mashuhuri:

 

Ya kwanza:

 

Rakaa hupatikana kwa kuiwahi rukuu pamoja na imamu

 

Hii ni kauli ya Jamhuri ya Maulamaa na wengineo. [Al-Mabsoutw (2/95), Fat-hul Qadiyr (1/483), Al-Mudawwanah, Al-Umm (1/135), Al-Majmu’u (4/111), Al-Mughniy (1/299), Al-Furuw’u (1/587), Twarhu At-Tathriyb (2/365), na Hukmu Man Adraka Ar Rukuw’u cha Asw-Swan-’aaniy].

 

Kauli kama hii kaisema Ibn ‘Umar, Ibn Mas-’oud, Zayd bin Thaabit na Maswahaba wengineo. Hoja ya kauli hii ni:

 

1- Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuipata rakaa ya Swalaah, basi ameipata Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (850) na Muslim (607)]. Wamelichukulia tamshi la “rakaa” kwamba linakusudiwa rukuu.

 

2- Uchukulifu huu wameutilia nguvu kwa riwaya ya Ibn Khuzaymah kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah kwa tamshi la: ((Mwenye kuipata rakaa ya Swalaah [kabla imamu hajanyoosha mgongo wake] basi ameipata)). [Munkari kwa tamko hili: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Khuzaymah (1595), Al-Bayhaqiy (2/89), Ad Daaraqutwniy (1/346) na Al-‘Uqayliy kwenye Adh-Dhwu’afaa (4/398). Ziada imefanywa katika maneno ya Az-Zuhriy, na Al-Bukhaariy kaifanyia “ikhraaj” katika Juz’u Al-Qira-ati ukurasa wa 47 kwa njia hiyo hiyo bila ziada].

Wamesema kwamba hili linaonyesha kuwa makusudio ya rakaa ni rukuu!!

 

3- Hadiyth Marfu’u iliyohadithiwa toka kwa Abu Hurayrah: ((Mkifika kwenye Swalaah nasi tumesujudu, basi sujuduni lakini msiihesabie kitu, na mwenye kuipata rakaa basi ameipata Swalaah)).  [Hadiyth Munkari: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (893), Ad-daaraqutwniy (1/347), Al-Haakim (1/216) na Al-Bayhaqiy (2/89). Katika Sanad yake yuko Yahya bin Abu Sulaymaan. Al-Bukhaariy kasema: “Ni Hadiyth Munkari”. Abu Haatim kasema: “Ni Hadiyth Mudhwtwarib, haina nguvu”. Lakini Al-Albaaniy ameiimarisha katika Al-Irwaa (2/261) na Asw-Swahiyhah (1188) kwa vigezo visivyo imara].

 

4- Hadiyth ya Abu Bakrah ya kwamba alimwahi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye rukuu, naye akarukuu kabla hajafika kwenye safu. Akalieleza hilo kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Rasuli akamwambia: ((Allaah Akuzidishie pupa lakini usifanye tena)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (783) na wengineo].

 

Wamesema: Ni wazi kuwa rakaa ilihesabiwa, na kwa hivyo hakuamuriwa kuirejesha, na haiwezekani kwamba aliisoma Al-Faatihahh ndani yake. Ama neno lake: ((Lakini usifanye tena)), hilo ni katazo la kuingia kwenye Swalaah kabla ya kuifikia safu.

 

5- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Ukija na imamu yuko kwenye rukuu, nawe ukaweka mikono yako juu ya magoti yako kabla hajanyanyua kichwa chake, basi umeipata”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/243) na Al-Bayhaqiy (2/90)].

 

6- Imepokelewa toka kwa Zayd bin Wahab akisema: “Nilitoka pamoja na ‘Abdullah bin Mas-’oud toka nyumbani kwake kwenda Msikitini. Tulipofika katikati ya Msikiti, imamu alirukuu, na ‘Abdullah akapiga takbiyr kisha akarukuu nami nikarukuu pamoja naye. Kisha tukajivuta mbele tukiwa kwenye rukuu mpaka tukaifikilia safu, na watu wakanyanyua vichwa vyao. Imamu alipomaliza Swalaah, nilisimama – nikidhani kwamba sikuipata rakaa - na ‘Abdullah akanikamata mkono, akanikalisha na kuniambia: Hakika umeipata”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/255), Atw-Twahaawiy (1/397) na Al-Bayhaqiy (2/90)].

 

7- Imepokelewa toka kwa Abu Umaamah bin Sahl akisema: “Nilimwona Zayd bin Thaabit ameingia Msikitini na watu wako kwenye rukuu. Akatembea hata asiweze kuifikia safu akiwa amerukuu. Akapiga takbiyr na kurukuu, kisha  akajisogeza akiwa kwenye rukuu mpaka akafika kwenye safu”.

 

Na katika tamko jingine toka kwa Khaarijah bin Zayd: “ Kisha rakaa hiyo huhesabiwa, sawasawa akiifikia safu au hakuifikia”. [Hadiyth Swahiyh: Riwaya ya kwanza imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twahaawiy (1/398), na ya pili imefanyiwa na Al-Bayhaqiy (2/91) na wengineo. Angalia Al-Irwaa (2/264)].

 

Ya pili:

 

Haihesabiwi rakaa ambayo aliyetanguliwa hakusoma Al-Faatihahh nyuma ya imamu.

 

Ni kauli ya Al-Bukhaariy na Ibn Hazm pamoja na Taqiyyu Ad Diyn As Subkiy ambaye ni katika wafuasi wa Ash-Shaafi’iy. Ash-Shawkaaniy, Al-‘Allaamah Al-Mu’allamiy Al-Yamaaniy na wengineo wameitilia nguvu kauli hii. [Al-Qiraa-at Khalfal Imaam (164), Al-Muhalla (3/243), Naylul Awtwaar (2/  ) na Wahal Yudriku Al Maamuum Ar rak-’at cha Al-Mu’allamiy (uk 43)].

 

Hoja zao ni:

 

1- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mnapoisikia adhana, basi nendeni kwenye Swalaah, na ni juu yenu kuwa watulivu na wastahivu, na wala msifanye haraka. Mlichokipata kiswalini, na kilichokupiteni basi kikamilisheni)). [Hadiyth Swahiyh: Imeshaelezwa nyuma].

 

Wamesema: Mwenye kuipata rukuu, basi ashapitwa na kisimamo na kisomo cha Al-Faatihahh, na vyote viwili ni faradhi ambayo Swalaah haitimii ila kwavyo. Na kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inaamuru kuyalipa yaliyopita na kuyakamilisha. Hivyo haijuzu kukihusisha kitu katika hayo bila kuwepo kauli nyingine, na hakuna njia ya kupatikana kwake.

 

2- Ama Hadiyth isemayo: ((Mwenye kuipata rakaa katika Swalaah, basi ameipata Swalaah)), hii ni haki na hoja inayowarudi wenyewe. Kwa kuwa pamoja na hivyo, hakupomoki kukilipa ambacho mtu hakukipata katika Swalaah bila khilafu yoyote. Na katika Hadiyth hakuna kwamba mwenye kuipata rukuu anakuwa amekipata kisimamo.

 

Ninasema: “Wamelichukulia neno “rakaa” kwa maana ya rakaa kamili, na huu ndio uhalisia wa tamko.”

 

3- Ama nyongeza: “kabla imamu hajanyoosha mgongo wake”, hii haiswihi. Na ukomo wa jambo ni kuwa mmoja wa wasimulizi ilimpitikia dhana kwamba maana ya Hadiyth ni: “Mwenye kuipata rukuu pamoja na imamu, basi kaipata rakaa”, na hapo akaongeza ziada hii kwa ajili ya kubainisha zaidi kwa mujibu wa dhana yake. Baadhi yao wamejuzisha ya kuwa ziada hii ni ya Az Zuhriy ambayo imewakanganya baadhi ya wenye ufahamu mdogo.

 

4- Vile vile Hadiyth: ((Mkifika kwenye Swalaah nasi tumesujudu…)), Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, haifai kwa hoja.

 

5- Ama Hadiyth ya Abiy Bakrah, wao hapo hawana hoja kabisa, kwa kuwa hakuna linalobainisha kwamba alitosheka na rakaa hiyo, na kwamba hakuilipa.

 

6- Ama athar kutoka kwa Maswahaba, hizo zinapingwa na kauli ya Abu Hurayrah isemayo: “Kwamba haihesabiwi rakaa mpaka asome Ummul Qur-aan”. Na kauli ya baadhi yao, si hoja kwa mwingine.

 

· Kauli Yenye Nguvu Zaidi

 

Baada ya kuzipitia dalili za makundi mawili, ninaloliona mimi ni kuwa hoja za Jamhuri, hoja kama hizi haziwezi kuturidhisha kuwa zina nguvu ya kutengua nguzo za kisimamo na kusoma Al-Faatihahh, kwa kuwa asili ni kubakia Hadiyth juu ya ujumuishi wake, na kuibeba dhima ya Swalaah kikamilifu. Na’am, hatupingi kuwa kauli ya kwamba mtu huipata rakaa ina nguvu kutokana na kuungwa mkono na kundi la Maswahaba Wasomi, na pia hatumlaumu yeyote mwenye kuona hivyo.

 

Ama mimi, bado ningali natafakuri. Lakini, naona kuwa mwenye kuingia akamkuta imamu amerukuu, basi atangoja mpaka aitadili, kisha atajiunga naye lakini hatohesabu chochote kwa ajili ya kuondokana na mvutano na kuwa salama na dini yake. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

Faida Zinazohusiana Na Mas-ala Yaliyopita (Kwa Mujibu Wa Kauli Ya Jamhuri).

 

[1] Je, anaweza mtu kurukuu kabla ya kuifikia safu ili aipate rukuu?

 

Tumeshaeleza nyuma kwamba Abu Bakrah aliporukuuu kabla ya kuifikia safu, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: ((Allaah Akuzidishie pupa lakini usifanye tena)). [Hadiyth Swahiyh: Imeshaelezwa nyuma kidogo].

 

Akamkataza asije kurukuu tena kabla ya kufika kwenye safu.

 

Ama Hadiyth ya ‘Abdullah bin Az Zubayr ya kwamba alisema juu ya mimbari: “ Akiingia mmoja wenu Msikitini na watu wamerukuu, basi arukuu wakati anapoingia, kisha ajisogeze akiwa kwenye rukuu mpaka aingie kwenye safu, kwani hilo ni Sunnah”, [Wapokezi wake wanaaminika: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (1/214), Ibn Khuzaymah (1571) na Al-Bayhaqiy (3/106) kupitia kwa Ibn Jariyj toka kwa ‘Atwaa. Na Ibn Jariyj huyu ni mdanganyifu, na kaitaja kuwa ni fulani toka kwa fulani (‘an-’anah) tukijua kwamba baadhi yao wanaichukulia riwaya yake toka kwa ‘Atwaa kama ni Mawswuul] tunakuta kwamba kuna maneno kidogo yaliyosemwa kuhusiana na Isnadi yake, na pia kuna mvutano kuhusiana na Umarfu’u wa neno lake “hilo ni Sunnah”. Isitoshe, vyovyote iwavyo, kauli hiyo haina uimara wowote wa kuikinza Hadiyth Swahiyh ya Abu Bakrah. Tunakubali kwamba hili limethibiti kwa kitendo cha Ibn Mas-’oud na wengineo, lakini pia katazo limethibiti toka kwa Maswahaba wengineo kama Abu Hurayrah na Ubayya bin Ka’ab.

 

Lililo bora ni mtu asirukuu kabla ya kuifikia safu kutokana na usahihi wa katazo la kufanya hivyo na udhaifu wa rai kinzani. Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ashasema: ((Mlichokipata kiswalini, na kilichokupiteni basi kikamilisheni)). [Hadiyth Swahiyh: Imeshaelezwa nyuma kidogo].

 

[2] Je, ni sharti atulizane kwenye rukuu ili aipate rakaa? [Al-Mubdi’u (2/48), Al-Inswaaf (2/224) na Al-Majmuw’u (4/113)].

 

Baadhi ya Mafuqahaa wamesema kwamba ni lazima maamuma atulizane kwenye rukuu kabla imamu hajanyanyuka kupita mpaka wa rukuu yenye kutosheleza na akusanyike pamoja naye kwenye utulizano. Lakini wengi wamesema kwamba ataipata rakaa kwa kurukuu ikiwa yeye ametulizana, na wengine wameliachilia, hawakuweka sharti ya kutulizana.

 

[3] Akifanya shaka ya kuipata rukuu pamoja na imamu [Al-Inswaaf (2/224) na Al-Majmu’u (4/114)]

 

La sahihi ni kwamba haipati kwa kuwa kiasili haipo, na kwa kuwa hukmu ya kuhesabiwa rakaa, ni kwa kuipata rukuu kwa wenye kusema hivyo. Hivyo haipatikani ila kwa yakini.

Na imesemwa: Anakuwa ni mwenye kuipata, kwa kuwa asili ni kubakia rukuu ya imamu na kutoitadili mpaka ithibitike kuwa ameitadili kihakika.

 

[4] Je, inamtosheleza takbiyrah moja tu wakati wa kuiwahi rukuu? [Al-Inswaaf (2/224), Al-Majmu’u (4/112) na Qawaaid Ibn Rajab (Al-Qaaidah 18)]

 

Akimwahi imamu katika rukuu, basi takbiyrah moja tu itamtosheleza. Atapiga takbiyrah ya kuhirimia, nayo itamtosheleza na takbiyrah ya kurukuu. Na kama atapiga takbiyrah mbili; moja ya kuhirimia na nyingine ya kurukuu, basi itakuwa ni bora zaidi.

 

·Faida:

 

Ni lazima aipige takbiyrah ya kuhirimia akiwa amesimama. Na kama ataitamka takbiyrah yote au sehemu yake baada ya kuinama, basi haitofaa kwa kuwa atakuwa ameileta mahala pasipo pake, na kusimama pia ni nguzo ya Swalaah.

 

[5] Je, imamu atasubiri kama atahisi mtu anaingia ili aipate rukuu au Jamaa?

 

Inafaa kisharia kwa imamu kuirefusha zaidi rakaa ya kwanza kuliko ya pili ili watu waweze kuipata rakaa ya kwanza kama alivyokuwa akifanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Imepokelewa toka kwa Abu Qataadah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika rakaa mbili za mwanzo Ummul Kitaab na Suwrah mbili, na katika rakaa mbili za mwisho Faatihahtul Kitaab. Baadhi ya nyakati alikuwa akisoma kwa sauti tumsikie, na alikuwa akirefusha zaidi rakaa ya kwanza kuliko rakaa ya pili. Hivi hivi katika Alasiri, na hivi hivi Alfajiri [Tukapata uhakika kwamba anataka watu waipate rakaa ya kwanza].[ Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (776), Muslim (451) na Abu Daawuud (798) na nyongeza ni yake mwenyewe].

 

Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd akisema: “ Swalaah ilikuwa inaqimiwa, kisha mtu akaenda Al-Baqiy na kufanya shughuli zake, halafu akatawadha, kisha akaja na kumkuta Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bado yuko katika rakaa ya kwanza kutokana na kuirefusha”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (454), An-Nasaaiy (2/164) na Ibn Maajah (825)].

 

Na hapa ndipo walipoichukulia dalili baadhi ya wenye kusema kwamba rakaa inapatikana kwa kuiwahi rukuu. Dalili ni kuwa imamu akihisi kwamba kuna mtu anaingia naye yuko kwenye rukuu, basi amngoje ili aipate rakaa kama hilo halitowataabisha maamuma. Kalisema hili Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Is-Haaq. [Al-Mughniy (1/236) na Naylul Awtwaar (3/166)].

 

 

Share