045-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Jamaa Zaidi Ya Moja Ndani Ya Msikiti Mmoja

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

045-Jamaa Zaidi Ya Moja Ndani Ya Msikiti Mmoja 

 

 

[Ibn ‘Aabidiyn (1/331), Al-Badaai-’i (1/153), Ad-Dusuuqiy (1/332), Al-Mughniy (2/180), Kash-Shaaful Qinaa (1/457), Al-Majmu’u (4/221), Al-Ummu (1/180) na Al-Awsatw (4/215)].

 

Msikiti haukosi kuwa na moja kati ya hali mbili:

 

[1] Msikiti ulioko kwenye soko, au barabarani au kwenye mapitio ya watu ambapo huingia humo kundi baada ya kundi. Msikiti huu inajuzu kukariri Jamaa bila ya ukaraha kwa makubaliano ya Maulamaa.

 

[2] Msikiti wenye menejimenti kamili na imamu mteule

Msikiti huu ndio mahala pa makhitalifiano kati ya Maulamaa. [Waliojuzisha kukariri Jamaa bila ya ukaraha ni ‘Atwaa, Al-Hasan, An-Nakh-’iy, Qataadah, Ahmad na Is-Haaq. Lakini Jamhuri wamelifanya makruhu zimazima ingawa wamevutana kati yao katika kuainisha ukaraha huo].

 

Kulihakiki hili kiuwazi ni kusema kuwa kukariri Jamaa kwenye Msikiti kama huu kuna hali mbili:

 

Hali ya kwanza:

 

Liwe jambo la kutokezea tu. Kiasili ni kwamba watu wote huswali pamoja na imamu mteule isipokuwa kwa yule aliyechelewa kwa udhuru. Wakati mwingine huingia watu wawili au watatu wakamkuta imamu ashatoa tasliym, na hawa wataruhusika kuswali Jamaa nyingine bila ya ukaraha. Asili ya hili ni Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriy ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona mtu akiswali peke yake akasema: ((Je, hakuna mtu wa kumtolea swadaqah huyu akaswali pamoja naye?)). [Hadiyth Swahiyh kwa Sanad zake. Abu Daawuud (574), At-Tirmidhiy (220), Ahmad (3/5, 45) na wengineo].

 

Anas bin Maalik alilifanya hilo. Imepokelewa toka kwa Abu ‘Uthmaan akisema: “Alitujia Anas Ibn Maalik katika Msikiti wa Banu Tha-’alabah akauliza: Je, mshaswali? (Ilikuwa Swalaah ya Alfajiri) Tukasema: Ndio. Akamwambia mtu mmoja: Adhini. Akaadhini na kuqimu, kisha akaswali katika Jamaa”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/321), ‘Abdul Razzaaq (3417) na Ibn Al-Mundhir (4/215)].

 

Imepokelewa toka kwa Salamah bin Kuhayl ya kwamba Ibn Mas-’oud aliingia Msikitini akakuta watu washaswali. Akaswali Jamaa na ‘Al-Qamah, Al-Aswad na Masruwq. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (2/323) na Ibn Al-Mundhir. Ina Hadiyth mwenza kwa ‘Abdul Razzaaq (2884)].

 

Hakuna Swahaba yeyote aliyejulikana kwamba amewapinga, na Swalaah ya Jamaa kama tulivyoeleza nyuma, inaizidi kwa daraja Swalaah ya mtu peke yake.

 

Hali ya pili:

 

Liwe jambo lililozoeleka, la kila siku, lililokubaliwa. Ni kama kukubaliana kila kundi (wenye mapote tofauti au mfano wake) liswali upande fulani wa Msikiti, au katika wakati maalumu tofauti na kundi jingine. Hili bila shaka lina ukaraha kwa kuwa halikuweko wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala kizazi cha mwanzo, linasambaratisha umoja kati ya Waislamu, na linawavuta watu kuwa wavivu na magoigoi wa kuhudhuria na kuiwahi Jamaa ya kwanza kwa kisingizio cha kusubiri Jamaa ya pili.

 

Hili ndilo angalizo na tamshi la Maalik na Ash-Shaafi’iy wakati walipochukizwa na kukariri Jamaa ndani ya Msikiti mmoja. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

·Aliyeswali Peke Yake Kisha Akaja Msikitini Kwenye Jamaa, Basi Aswali Jamaa Na Watu

 

Hili ni jambo linalopendeza kwa ajili ya kupata fadhla ya Jamaa. Katika milango ya nyuma, tulielezea neno la Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa watu wawili ambao hawakuswali aliowaona nyuma ya safu. (walikuwa washaswali nyumbani walikofikia). Aliwaambia: ((Msifanye. Mkiswali nyumbani mlikofikia, kisha mkaja kwenye Msikiti wenye Jamaa, basi swalini pamoja nao, kwani kwenu hiyo ni Sunnah)). [Hadiyth Swahiyh: Imeelezewa mara nyingi].

 

Imepokelewa toka kwa Abu Dharri kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniuliza: ((Utafanya nini ukiwa unatawaliwa na viongozi wanaochelewesha Swalaah na wakati wake, au wanaiua Swalaah na wakati wake?)) Nikasema: “Unaniamuru nini?” Akasema: ((Swali Swalaah katika wakati wake, na kama utaipata pamoja nao, basi swali, kwani hiyo ni Sunnah kwako)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (648). Imeshaelezewa nyuma].

 

Maulamaa wote wamekubaliana juu ya kupendeza kuiswali Swalaah mara nyingine kwa Jamaa. Wamelielezea hilo kwa uchambuzi kwenye vitabu tanzu. Kati ya hayo, wameitoa kando Swalaah ya Magharibi –Hanafi, Maalik na Hanbali-  [Ibn ‘Aabidiyn (1/479), Al-Badaai-’i (1/287), Ad Dusuuqiy (1/320), Al-Mawaahib (2/84), Al-Mughniy (2/111), na Kash-Shaaful Qina’a (1/212)] wakisema kwamba hairejeshwi kwa kuwa ni Witri ya mchana, na pia Witri. Haya yashaelezewa kirefu nyuma.

 

· Ikiwa Ameswali Faradhi Kwa Jamaa, Je Ataswali Tena Kama Ataikuta Jamaa?

 

[Vitabu rejea vilivyotangulia pamoja na Al-Muhadh-dhab (1/102) na Asnaa Al-Matwaalib (1/212)].  

 

Inavyoelekea ni kuwa hilo limesuniwa pia. Ash-Shaafi’iy na Hanbali wamelisema hili, kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwaambia watu wale wawili: ((Mkiswali)), kunathibitisha kuswali mtu peke yake au kwa Jamaa, na kwa ujumuishi wa neno lake: ((kwani kwenu hiyo ni Sunnah)). Maalik amelikataa hilo la kuswali tena isipokuwa kama litafanyika kwenye Msikiti Mtakatifu wa Makkah, Msikiti wa Nabiy na Baytul Maqdis (Al-Masjid Al-Aqswaa) kutokana na ubora wa Misikiti hiyo. Kauli ya kuswali mara nyingine ndiyo yenye nguvu zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

 

Share