046-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Yanayofanyika Baada Ya Kumalizika Swalaah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

046-Yanayofanyika Baada Ya Kumalizika Swalaah

 

 

· Imamu Awaelekee Watu Baada Ya Kutoa Tasliym Na Akae Kidogo Kabla Hajaondoka

 

Imepokelewa toka kwa Samurah bin Jun-dub akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapomaliza kuswali, hutuelekea kwa uso wake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (845) na Muslim (2275)].

 

Hikma ya kuwaelekea maamuma kama inavyosemwa ni kuwafundisha mambo wanayoyahitajia kama ilivyo kwenye Hadiyth ya Zayd bin Khaalid Al-Juhaniy isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituswalisha Swalaah ya Alfajiri huko Al-Hudaybiyah baada ya mvua kunyesha usiku. Alipomaliza kuswali, aliwaelekea watu na kuwaambia:  ((Je, mnajua nini Kasema Mola wenu?)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (846) na Muslim (71)].

 

Kuna mengine yaliyosemwa kuhusiana na hikma ya hilo. Vyovyote iwavyo, hiyo ni Sunnah inayostahiki kufuatwa. Imesuniwa katika kuwaelekea, kuwe karibu zaidi kwa upande wake wa kuume. Imepokelewa toka kwa Al-Barraa akisema: “Tulipokuwa tunaswali nyuma ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tulikuwa tunapenda tuwe kuliani mwake, akituelekea kwa uso wake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (709) na Abu Daawuud (615)].

 

· Faida

 

Imesuniwa kwa imamu kabla hajawaelekea watu, akae akiwa ameelekea Qiblah kiasi cha kusema: “Allaahumma Anta as Salaam waminka as Salaam, Tabaarakta yaa Dhal Jalaali wal Ikraam”. Hivi ndivyo alivyokuwa akifanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni kama ilivyo kwenye Swahiyh Muslim (592) toka kwa ‘Aaishah na toka kwa Al Barraa bin ‘Aazib akisema: “Nilipeleleza Swalaah nilizoswali pamoja na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nikagundua kwamba muda takriban uko sawa wa kisimamo chake, kurukuu kwake na kuitadili kwake baada ya kurukuu, kusujudu kwake, kikao chake baina ya sijdah mbili, kusujudu kwake na kikao chake baina ya tasliym na kuondoka”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (471), Abu Daawuud (854), An-Nasaaiy (3/66) na Ahmad (4/294)].

 

Imepokelewa na Ummu Salamah akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikaa mahala pake muda kidogo.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (849), Abu Daawuud (1040), An-Nasaaiy (3/67) na Ibn Maajah (932)].

 

· Wanawake Waondoke Haraka Mara Tu Baada Ya Swalaah Kumalizika

 

Imepokelewa toka kwa Ummu Salamah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikaa mahala pake muda kidogo. Ibn Shihaab amesema: “Tunaona – na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi – ili wamalizike wanawake wenye kuondoka”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (849), Abu Daawuud (1040), An-Nasaaiy (3/67) na Ibn Maajah (932)].

 

Na kasema tena Ummu Salamah: “Akina mama wakati wa enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), walikuwa wanapotoa tasliym katika Swalaah ya faradhi husimama. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na wanaume walioswali, alikuwa akibakia hapo hapo alipo muda autakao. Na Rasuli wa Allaah anaposimama, na wanaume nao husimama”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (866) na wengineo].

 

Mahala pa kufanyika hili ni pale wanawake wanaposwali nyuma ya wanaume moja kwa moja, na ukawa mlango wa kutokea wote ni mmoja. Ama ikiwa kuna mlango maalum wa wanawake na sehemu yao maalum ya kuswalia ambapo wanaume hawawezi kuwaona, basi ni haki yao kubakia hapo waliposwalia ili kuleta tasbiyh, tahmiyd, tahliyl na nyiradi nyinginezo zinazofanywa kila baada ya Swalaah, kwa kuwa Malaika huwaombea rahma madhali wako kwenye sehemu waliyoswalia, na madhali wudhuu haujawatenguka. [Mfano wa haya yako kwenye Jaami’u Ahkaam An Nisaa cha Sheikh wetu Allaah Amhifadhi (1/287). Angalia kitabu changu cha Fiqhu As-Sunnah Lin-Nisai ukurasa wa 156].

 

Ninasema: “Linalopendeza ni kuwepo mlango maalumu wa akina mama – na hususan katika wakati huu wa fitna- ambao wanaume hawaruhusiwi kabisa kuingilia. Na asili ya hili ni kauli ya ‘Umar bin Al-Khattwaab aliposema: “Bora tungeuacha mlango huu kwa wanawake”. Ibn ‘Umar hakuingilia tena mlango huo mpaka alipokufa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (463) toka kwa Naafi’i toka kwa ‘Umar. Nayo inachukulika kwamba ameichukua toka kwa Ibn ‘Umar. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi].

 

· Yanayosemwa Wakati Wa Kutoka Msikitini

 

Imepokelewa toka kwa Abu Humayd au Abu Asyad (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anapoingia mmoja wenu Msikitini, basi amtolee salaam Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha aseme: “Allaahumma Iftah liy abwaaba Rahmatika”. Na anapotoka aseme: “Allaahumma inniy as-aluka min Fadhwlika”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (713), Abu Daawuud (465) na An-Nasaaiy (3/53)].

 

 

Share