Imaam Ibn Baaz: Atakayefufua Tendo Jema (Sunnatun-Hasanah)

 

 

Usahihi Wa Hadiyth

 

Atakayefufua Tendo Jema (Sunnatun-Hasanah) 

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI: 

 

Kuhusu kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

مَنْ سَنَّ فِي الْإِسْلَامِ سُنَّةً حَسَنَةً فَعُمِلَ بِهَا بَعْدَهُ كُتِبَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِ مَنْ عَمِلَ بِهَا...

Atakayefufua tendo jema katika Uislaam na watu wakalitenda baada yake, basi ataandikiwa ujira sawa na yule atakayelitenda.

 

Mpaka Siku Ya Qiyaamah. Je hii  ni Hadiyth?  Na kama ni Hadiyth, je, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliacha jambo (la Sunnah) kwetu ambalo hakulifanya yeye ili lije kutendwa baada yake katika Uislaam? Tunaomba utufahamishe kwa kutufafanulia wazi jambo hili.

 

 

 

JIBU:

 

 

Hadiyth hii ni Swahiyh nayo inatuonyesha hukumu ya kuruhusu kuhuisha Sunnah, kuifundisha na kutahadharisha bid'ah na maovu. Kwa sababu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 مَنْ سَنَّ فِي الْإِسْلَامِ سُنَّةً حَسَنَةً فَعُمِلَ بِهَا بَعْدَهُ كُتِبَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِ مَنْ عَمِلَ بِهَا ، وَلَا يَنْقُصُ مِنْ أُجُورِهِمْ شَيْءٌ . وَمَنْ سَنَّ فِي الْإِسْلَامِ سُنَّةً سَيِّئَةً فَعُمِلَ بِهَا بَعْدَهُ كُتِبَ عَلَيْهِ مِثْلُ وِزْرِ مَنْ عَمِلَ بِهَا ، وَلَا يَنْقُصُ مِنْ أَوْزَارِهِمْ شَيْءٌ   أخرجه مسلم في صحيحه

“Atakayefufua tendo jema katika Uislaam na watu wakalitenda baada yake, basi ataandikiwa ujira sawa na yule atakayelitenda, na hakipungui chochote katika ujira wao. Na atakayebuni kitendo kibaya katika Uislamu na watu wakakifanya baada yake, basi ataandikiwa dhambi sawa na yule atakayekifanya, na wala hakipungui chochote katika madhambi yao.” [Muslim]  

 

Mfano pia ni Hadiyth

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ أَنَّ النبي صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : ((مَنْ دَعَا إِلَى هُدًى كَانَ لَهُ مِنْ الْأَجْرِ مِثْلُ أُجُورِ مَنْ تَبِعَهُ لَا يَنْقُصُ ذَلِكَ مِنْ أُجُورِهِمْ شَيْئًا، وَمَنْ دَعَا إِلَى ضَلَالَةٍ كَانَ عَلَيْهِ مِنْ الْإِثْمِ مِثْلُ آثَامِ مَنْ تَبِعَهُ لَا يَنْقُصُ ذَلِكَ مِنْ آثَامِهِمْ شَيْئًا))   رواه مسلم  

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema ((Atakayelingania kwenye uongofu atapata thawabu (ujira) wa yule atakayemfuata bila ya kupungukiwa chochote katika thawabu zao. Na atakayeelekeza katika upotofu atapata dhambi mfano wa dhambi za yule atakayefuata bila ya kupungukiwa chochote katika dhambi zao)) [Muslim]

 

Na pia Hadiyth ya Abuu Masw-uwd Al-Answaariy:

 

“Atakayeongoza katika khayr, basi atapata mfano wa ujira wa mtendaji.” [Muslim katika Swahiyh yake]

 

 

Maana ya Atakayefufua tendo jema katika Uislaam” ni kuihuisha, kuidhihirisha na kuifichua Sunnah ambayo imefichika kwa watu (au imeghafiliwa na watu). Muislaam anapoidhihirisha kwa watu, hupata thawabu kama za atakayetenda kitendo hicho. Lakini haimaanishi kuzusha jambo kwa maana, kanzisha kitendo kipya. Kwa sababu Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kakataza kuzusha jambo akasema:

 

كل بدعة ضلالة   أخرجه مسلم في صحيحه 

“Kila bid'ah ni upotofu [Muslim katika Swahiyh yake]

 

Na maneno yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yanasadikisha yenyewe kwa yenyewe wala hayapingani na kwa Ijmaa’ ya ‘Ulamaa (wote wanakubaliana).

 

Kwa hiyo, ilivyokusudiwa katika Hadiyth ni kuihuisha Sunnah na kuidhihirisha kwa watu. Mfano, mtu mwenye elimu kutokea katika nchi ambayo hakuna mafunzo ya Qur-aan au hakuna mafunzo ya Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kisha yeye akayarudisha mafunzo hayo kwa kuwawekea walimu wafundishe mafunzo ya Qur-aan na Sunnah.  

 

Mfano mwingine, ni mtu kukuta katika nchi watu wanayoa ndevu zao au wanazikata, kisha yeye akaamrisha wazifuge na wasinyoe. Hivyo basi atakuwa ameihuisha Sunnah hii tukufu katika nchi hiyo ambayo watu walikuwa hawaijui au imeachwa mpaka ikasahulika. Atapata thawabu sawa na thawabu za watakaojaaliwa kupata Hidaaya ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) naye akawa ni sababu. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

قصوا الشوارب وأعفوا اللحى وخالفوا المشركين متفق على

“Kateni masharubu na acheni ndevu, muwe tofauti na washirikina.’ [Hadiyth hii imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Ibn 'Umar Radhwiya Allaahu 'anhumaa]  

 

Juu ya hivyo, pindi watu wakiona kwamba mwalimu mwenyewe kafuga ndevu, kisha wakamfuata, mwalimu huyo huwa pia amehuisha Sunnah hiyo kwao. Na kufuga ndevu ni Sunnah ya kuwajibika wala haifai kuiacha kwa sababu ya maamrisho yaliyomo katika Hadiyth iliyotajwa hapo juu.  Basi yeye kufuga ndevu ikawa ni kigezo kwa watu atapata thawabu sawa na thawabu za atakeyemuiga kufuga ndevu. 

 

 

Mfano mwengine ni kukuta katika nchi fulani watu hawaswali Swalaah ya Ijumaa kwa sababu ya kutokujua kwao (umuhimu wake), kisha yeye akawafundisha na kuwaswalisha, basi atapata thawabu na thawabu zao pia. Au pia kukuta watu katika nchi nyingine ambao hawatambui Swalaah ya Witr, akawafundisha kisha nao wakamfuata. Na mifano kadhaa kama hiyo kuhusu ‘ibaadah au amali njema zinazojulikana na kukubalika katika Shariy’ah (hukumu) ya Kiislaam, akazidhihirisha baada ya kuwa hazikutambulika kwao au zimesahaulika au hazifuatwi na watu.

 

 

Hivyo, atakayezifufua Sunnah hizo, akazidhihirisha na kuzieneza ndiye yule aliyekusudiwa katika Hadiyth kuwa 'kafanya kitendo kizuri (Sunnatun-hasanah) katika Uislaam kwa maana; ameidhihirisha kwa watu, basi huyo mtu ndiye  atakayekuwa miongoni mwa wale walokusudiwa katika kauli: Atakayefufua tendo jema katika Uislaam..

 

Lakini haimaanishi kwamba aanzishe (azushe) jambo katika Dini lisiloamrishwa na Allaah.  Kwani uzushi ni upotofu kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh:

 

  وأياكم ومحدثات الأمور فإن كل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة

“Tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila uzushi ni bid'ah na kila bid'ah ni upotofu.”

 

Vile vile Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

“Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu basi kitarudishwa.” [Al Bukhaariy]

 

Na katika kauli nyingine,

 

 من أحدث في أمرنا هذا ما ليس منه فهو رد متفق عليه.

“Atakayezusha katika mambo yasiyokuwa yetu basi (kitendo hicho) kitarudishwa. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema katika khutbah za Ijumaa:

 

((أما بعد فإن خير الحديث كتاب الله وخير الهدى هدى محمد صلى الله عليـه وسلم وشر الأمور محدثاتها وكل بدعة ضلالة)) خرجه مسلم في صحيحه

“Amma ba'ad. Hakika lililokuwa bora kabisa la kuhadithia ni Kitabu cha Allaah, na mwongozo ulio bora ni mwongozo wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na jambo ovu kabisa ni uzushi wake na kila uzushi ni upotofu.” [Muslim katika Swahiyh yake]

 

Kwa hiyo ibaada yoyote isiyotokana na Allaah, haifai (kuifundisha) kuilingania, na atakayeifundisha hapati thawabu bali atakuwa anaeneza bid'ah kwa watu na huyo atakayeileta (kwa kuitangaza na kuieneza kwa watu) atakuwa ni katika yule anayeongoza katika upotofu na Allaah (Subhaana wa Ta'aalaa) Amemlaumu na kumhoji huyo mtu mwenye kutenda hivyo kwa kauli Yake: 

 

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ ۚ

Je, wanao washirika waliowaamuru Dini yale ambayo Allaah Hakuyatolea kwayo idhini? …)) [Ash Shuwraa: 21]  

 

[Al-Mawqi' Ar-Rasmiy li-Samaahat Ash-Shaykh Al-Imaam Ibn Baaz]

 

 

 

 

 

 

Share