12-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Toshelezo La Allaah

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

12-Toshelezo La Allaah

 

 

"حَسْبِيَ اللَّهُ لا إِلَـهَ إِلاَّ هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَهُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ"

 

Amenitosheleza Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye.  Kwake nimetawakali. Naye Ni Rabb wa ‘Arsh Adhimu”.  [At-Tawbah: (129)]

 

Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifundishwa kuisema du’aa hii wakati makafiri wanapompinga na kukataa haki aliyowaletea, na pale walipokataa nasaha zake na mawaidha ya haki.   Du’aa hii ni ya kutaka Msaada wa Allaah dhidi ya wapingaji hao, na kutawakali kwa Allaah pamoja na matatizo yote yanayomsumbua mtu.

 

Du’aa hii ina maana:  “Rabbi wangu Ndiye Mwenye Kunitosha mimi na yote yenye kunipa ghamu, na hakuna mwingine wa kuabudiwa kwa haki ila Yeye tu, na Kwake tu nimetegemea, na Ni Yeye Pekee tu ninayemwamini katika kuniletea yenye kunifaa na kuniondoshea yenye kunidhuru”.

 

Na Yeye pia Ndiye Anayemiliki ‘Arshi ambayo ndiyo kiumbe kikubwa zaidi kuliko vyote, chenye kuzunguka kila kitu, na Yeye Yuko juu yake kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye Mwenyewe Allaah.

 

Du’aa hii iko katika muundo taarifu lakini ndani yake kuna ombi.  Kana kwamba mwombaji anasema:  Nitosheleze ee Rabbi wangu na kila kitu kinachonisumbua na kinachoniogopesha”.  Imekusanya dhana kamili njema, yakini kwa Allaah, kumpwekesha Allah, kumtegemea Yeye tu na kumsifu.  Yeye tu Ndiye Astahikiye kuogopwa, na Kwake tu mambo yote yanarejea.

 

Du’aa hii ina fadhila kubwa sana.  Imepokelewa toka kwa Abud Dardaai kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَنْ قالَ فِي كُلّ يَوْمٍ حِينَ يُصْبحُ، وَحِينَ يُمْسِي : حَسْبِيَ اللَّهُ لا إِلهَ إِلاَّ هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَهُوَ رَبُّ العَرْشِ العَظِيمِ، سَبْعَ مَرَّاتٍ كَفَاهُ اللَّهُ تَعالى ما أهمَّهُ مِنْ أمْرِ الدُّنْيا والآخِرَة"

 

“Mwenye kusema kila siku anapopambaukiwa na anapoingiliwa na jioni: Amenitosheleza Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Kwake nimetawakali. Naye Ni Rabb wa ‘Arsh Adhimu, mara saba, Allaah Ta’aalaa Atamtosheleza na kila linalomletea ghamu katika mambo ya dunia na aakhirah”. [Imesimuliwa na Ibn As-Sunniyy katika kitabu chake cha “Amalul Yaymi wa Al Laylati]

 

Tunajifunza kutokana na du’aa hii yafuatayo:

 

1-  Du’aa hii ina umuhimu mkubwa kutokana na fadhila zake zilizoelezewa kwenye Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Ni muhimu sana kuisoma asubuhi na jioni mara saba kila siku, itakuondoshea ghamu na hamu zote za dunia na aakhirah.

 

2-  Kutawakali ni sababu ya Allaah kumtosheleza Mja Wake. Ni kama Alivyosema:

 

"وَمَنْ يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَهُوَ حَسْبُهُ"

 

Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza.   [At-Twalaaq: (3)]

 

3-  Ubora wa neno la Tawhiyd. Kuna uokozi ndani yake duniani na aakhirah.

 

 

4-  Umuhimu wa kutawassali kwa Allaah kwa Tawhiyd Yake, kutawakkali Kwake, na Ubwana Wake kwa Kiumbe Chake kikubwa zaidi kuliko vyote (‘Arshi).

 

 

5-  Du’aa kama inavyokuwa kwa tamshi la ombi, pia inakuwa kwa tamshi taarifu.

 

 

 

 

Share