15-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Amani Kwa Makkah Na Kuepushwa Na Masanamu

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

15- Amani Kwa Makkah Na Kuepushwa Na Masanamu

 

 

"رَبِّ اجْعَلْ هَـٰذَا الْبَلَدَ آمِنًا وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ"

 

 

“Ee Rabb wangu! Ujaalie mji huu (Makkah) uwe wa amani,  na Uniepushe na wanangu kuabudu masanamu.  [Ibraahiym: (35)]

 

 

Ni katika du’aa za baba yetu Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam). Inabeba ndani yake maana na makusudio makubwa.

 

Amemwomba Allaah Aujaalie mji wa Makkah uwe mji wa amani, na Allaah Akamtakabalia du’aa yake kisharia na kiqadar, hata ikawa ni marufuku mtu kubeba silaha ndani ya mji huu.  Na hata yule anayekusudia ubaya kwa mji huu, Allaah Humvunjilia mbali na Humwonjesha adhabu kali kama Alivyowafanya watu wa tembo na wengineo.

 

"وَمَن يُرِدْ فِيهِ بِإِلْحَادٍ بِظُلْمٍ نُّذِقْهُ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ"

 

“Na yeyote anayekusudia humo kufanya upotofu kwa dhulma Tutamuonjesha adhabu iumizayo”.  [Al-Hajj: (25)]

 

Mbali na kuuombea mji huu amani, Nabiy huyu kutokana na huruma na ukarimu wake uliopitiliza, aliwaombea watu na wakazi wake kwa Allaah Awaruzuku mazao na matunda kwa wingi ambayo ni moja kati ya neema kubwa.

 

"وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ اجْعَلْ هَـٰذَا بَلَدًا آمِنًا وَارْزُقْ أَهْلَهُ مِنَ الثَّمَرَاتِ مَنْ آمَنَ مِنْهُم بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ قَالَ وَمَن كَفَرَ فَأُمَتِّعُهُ قَلِيلًا ثُمَّ أَضْطَرُّهُ إِلَىٰ عَذَابِ النَّارِ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ"

 

“Na pindi aliposema Ibraahiym: Rabb wangu! Ufanye mji huu (Makkah) kuwa wa amani, na Waruzuku watu wake matunda, atakayemwamini Allaah miongoni mwao na Siku ya Mwisho.  (Allaah) Akasema:  Na atakayekufuru basi Nitamstarehesha kidogo kisha Nitamsukumiza katika adhabu ya moto. Na ubaya ulioje mahali pa kuishia!”.  [Al-Baqarah: (126)]

 

Na baada ya kuuombea mji huu amani ambayo ni moja kati ya neema kubwa, alijiombea mwenyewe pamoja na wanawe Allaah Awaepushe na ibada ya masanamu.  Akamwomba Amkite juu ya tawhiyd safi takasifu kutokana na uchafu wote wa shirki, na kila lile ambalo linaweza kuichafua tawhiyd yake na  ya kizazi chake.  Huu ndio Uislamu wa kweli. Muislamu asijiangalie yeye tu, bali na wanawe pia, mkewe na nduguze Waislamu. 

 

"وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا

 

Na wale wanaosema: Rabb wetu! Tutunukie katika wake zetu na dhuria wetu viburudisho vya macho yetu, na Tujaalie kuwa waongozi kwa wenye taqwa. [Al-Furqaan: (74)].

 

Ibn Kathiyr (Rahimahul Laah amesema:  “Kila mwenye kuomba anatakiwa ajiombee mwenyewe, wazazi wake wawili na watoto wake”.

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

1-  Kwamba kila Muislamu anatakiwa akithirishe sana du’aa hii ili kupata kinga kutokana na dhambi kubwa na ya hatari zaidi ambayo ni shirki.  Shirki ni dhulma kubwa zaidi kuliko zote, na ni dhambi isiyosamehewa mtu akifa nayo bila kutubia.

 

2-  Mwombaji anatakiwa ayatupe malalamiko yake kwa Allaah kwa yale anayoyaogopa na kuyahofia.  Huu ndio mwenendo wa Manabii katika maombi yao.  Katika mwendelezo wa du’aa, Nabi Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) anasema:

 

"رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ ۖ فَمَن تَبِعَنِي فَإِنَّهُ مِنِّي ۖ وَمَنْ عَصَانِي فَإِنَّكَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ"

 

Rabb wangu! Hakika hao (masanamu) wamepoteza watu wengi.   Basi atakayenifuata, huyo yuko nami, na atakayeniasi, basi hakika Wewe Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu”.  [Ibraahiym: (36)]

 

Naye Nabiy Ya’aquwb (‘Alayhis Salaam) baada ya kupata mtihani wa kupotelewa na mwanawe Yuwsuf (‘Alayhis Salaam) alimlalamikia Rabbi wake akisema:

 

"قَالَ إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ"

 

“Akasema: Hakika mimi nashitakia dhiki ya majonzi yangu na huzuni zangu kwa Allaah.  Na najua kutoka kwa Allaah yale msiyoyajua”.  [Yuwsuf: (86)]

 

Naye Ayyuwb baada ya kuugua muda mrefu, aliomba huku akisema:

 

"وَأَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ "

 

“Na Ayyuwb, alipomwita Rabb wake:  Hakika mimi imenigusa dhara, Nawe Ndiye Mbora zaidi wa Kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu”. [Al-Anbiyaa: (83)]

 

3-  Ni lazima Muislamu aziepuke sababu na hali zote zinazowapoteza watu kuacha dini yao. 

 

"رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ

 

“Rabb wangu!  Hakika hao (masanamu) wamepoteza watu wengi”.

 

 

4-  Inatakikana kwa kila mmoja wetu ajiombee mwenyewe salama na watoto wake kutokana na madhambi makubwa vyovyote yeye afikiavyo kwa utiifu kwa Allaah na kufanya ‘ibaadah.

 

 

5-  Umuhimu wa kulipa hima suala la tawhiyd na aqiydah, na katika ujumla wake kuomba du’aa Kwake Allaah tu.

 

 

 

Share