061-Asw-Swaff: Utangulizi Wa Suwrah

 

061-Asw-Swaff: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa wengi.

 

Idadi Za Aayah: 11

 

Jina La Suwrah: Asw-Swaff  

 

Suwrah imeitwa Asw-Swaff (Safu), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (4).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Mahimizo kwa Waumini juu ya kuinusuru Dini. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Mahimizo juu ya Jihaad katika Njia ya Allaah kwa mali na nafsi, na kumuitikia Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).  

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kubainishwa kwamba, kila kilichomo mbinguni na ardhini Kinamsabbih (Kumtakasa) Allaah (سبحانه وتعالى).

 

2-Waumini wametahadharishwa kutokuvunja ahadi kwa kusema maneno kisha wasitekeleze wayasemayo, na kwamba hivyo ni chukizo kubwa mbele ya Allaah.

 

3-Imetajwa aliyoyasema Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) kuwalaumu watu wake kwa maudhi waliyomfanyia, na watu wake kujiingiza katika upotofu.  

 

4-Imetajwa da’wah ya Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام) kwa wana wa Israaiyl, na kushuhudia yaliyotajwa katika Tawraat ya kuja kwa Rasuli aitwaye Ahmad ambaye ndiye Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). Lakini alipowajia kwa Ishara za wazi walikanusha Risala ya Allaah na kudai ni sihri ya wazi.

 

5-Imebainishwa kwamba, madhalimu wametaka kuikanusha Qur-aan aliyoteremshiwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), lakini Allaah Ameipa nguvu haki japokuwa makafiri wamechukia. 

 

6-Waumini wameongozwa kutenda yatakayowaepusha na adhabu za Allaah, na kutenda yaliyo bora kwao, ambayo yatawapatia makazi mazuri ya Jannah yenye kudumu milele, nayo ni kumwamini Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), na kufanya Jihaad katika Njia ya Allaah kwa mali na nafsi zao.

 

7-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwahimiza Waumini kuwaiga wafuasi wa Nabiy Iysaa (عليه السّلام).

 

 

 

 

 

 

 

Share