062-Al-Jumu’ah: Utangulizi Wa Suwrah

 

062-Al-Jumu’ah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 11

 

Jina La Suwrah: Al-Jumu’ah

 

Suwrah imeitwa Al-Jumu’ah (Ijumaa), na yanayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، رضى الله عنه قَالَ كُنَّا جُلُوسًا عِنْدَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَأُنْزِلَتْ عَلَيْهِ سُورَةُ الْجُمُعَةِ

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Tulikuwa tumekaa pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akateremshiwa Suwrah Al-Jumu’ah. [Al-Bukhaariy]

 

Na pia Hadiyth iliyonukuliwa katika Fadhila. Na pia kutajwa katika Aayah namba (9).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Neema na Fadhila walioyojaaliwa Ummah (wa Kiislamu kutumiwa) Rasuli wao (صلى الله عليه وآله وسلم) na kubainisha fadhila ya siku ya Ijumaa. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kutaja vile ambavyo Allaah (سبحانه وتعالى) Ameuchagulia Ummah huu, na katika hivyo ni Swalaah ya Ijumaa, pamoja na kibainisha baadhi ya hukumu zake.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuthibitishwa kwamba kila kilichomo mbinguni na ardhini Kinamsabbih Allaah Mwenye Sifa Tukufu.

 

2-Imetajwa madhwhari ya Neema za Allaah kwa Ummah wa Kiislamu kwa Kuwatumia Rasuli ili awasomee Aayah Zake, awatakase na awaelimishe Qur-aan na Sunnah.

 

3-Mayahudi wamekemewa kwa kutokukifanyia kazi Kitabu chao (Tawraat), ambacho wameteremshiwa na Allaah (سبحانه وتعالى) kwa ajili ya kuwaongoza, na kubatilisha madai yao ya kwamba wao ni vipenzi vya Allaah.

 

4-Imetanabahishwa kwamba hakuna atakayeweza kuyakimbia mauti!

 

5-Suwrah imekhitimishwa kwa kuamrishwa Waumini kuhifadhi Swalaah ya Ijumaa, na kuikimbilia inaponadiwa, na amri ya kuacha yote yanayomshughulisha mtu wakati wa kuitekeleza. Kisha amri ya Kumdhukuru Allaah kwa wingi baada ya kumalizika Swalaah. Na tahadhari ya kuiacha, na kuwakemea watu walioiacha kwa kukimbilia biashara zao.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

Ni Sunnah Kuisoma Katika Rakaa Ya Kwanza Ya Swalaah Ya Ijumaa:

 

عَنِ ابْنِ أَبِي رَافِعٍ، قَالَ اسْتَخْلَفَ مَرْوَانُ أَبَا هُرَيْرَةَ عَلَى الْمَدِينَةِ وَخَرَجَ إِلَى مَكَّةَ فَصَلَّى لَنَا أَبُو هُرَيْرَةَ الْجُمُعَةَ فَقَرَأَ بَعْدَ سُورَةِ الْجُمُعَةِ فِي الرَّكْعَةِ الآخِرَةِ ‏ إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ - قَالَ - فَأَدْرَكْتُ أَبَا هُرَيْرَةَ حِينَ انْصَرَفَ فَقُلْتُ لَهُ إِنَّكَ قَرَأْتَ بِسُورَتَيْنِ كَانَ عَلِيُّ بْنُ أَبِي طَالِبٍ يَقْرَأُ بِهِمَا بِالْكُوفَةِ ‏.‏ فَقَالَ أَبُو هُرَيْرَةَ إِنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ بِهِمَا يَوْمَ الْجُمُعَةِ ‏.‏

 

Amesimulia Ibn Abiy Raafi’i (رضي الله عنه): Marwaam alimteua Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kama naibu wake katika mji wa Madiynah, na yeye mwenyewe akaondoka kuelekea Makkah. Basi Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) alituswalisha Swalaah ya Ijumaa akasoma baada ya Suwratul-Jumu’ah katika Rakaa ya pili:

 

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ

“Wanapokujia wanafiki.” [Al-Munaafiquwn (63:1)

 

Kisha nikamdiriki Abuu Hurayrah wakati alipoondoka nikamwambia: Umesoma Suwrah mbili ambazo ‘Aliy Bin Abiy Twaalib alikuwa akizisoma katika mji wa Kuwfah. Abu Hurayrah akasema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akizisoma siku ya Ijumaa (katika Swalaah). [Muslim]

 

 

 

 

Share