Historia Ya Keki Na Mishumaa Katika Kuadhimisha Siku Ya Kuzaliwa (Birthday)

 

Historia Ya Keki Na Mishumaa Katika Kuadhimisha Siku Ya Kuzaliwa (Birthday)

 

Imetarjamiwa Na: Ummu Ummu Ayman

 

Alhidaaya.com

 

 

Historia ya keki ya sherehe ya kuzaliwa (Birthday)

 

Kuna wanosema kuwa Wagiriki walikuwa na desturi ya kupeleka keki katika mahekalu yao ya Mungu (wa kike) wa mwezi, Artemis. Walichukua keki zenye umbo la duara kuashiria mwezi mpevu. 

 

Maoni mengine ni kuwa desturi ya keki ya birthday ilianza huko Ujerumani. Mkate ulitengenezwa katika umbo la nguo alizokuwa akizongewa mtoto Yesu. Geburtstagorten ni aina nyengine ya keki ya Kijerumani ambayo ilikuwa ikitumika katika birthday.

 

Mamia ya miaka iliyopita ilikuwa ni kawaida kuongezea vitu vidogo vidogo vya kupendezesha/kushangazia katika keki za birthday. Wakati wageni wanapopata kipande cha keki, vitu tofauti vinatumika kuagulia maisha ya baadae. Mapeni yanaashiria utajiri mkubwa, na kofia ya kidole inayovaliwa wakati wa kushonea  inamaanisha kutooa au kutoolewa kamwe.

 

Historia Ya Mishumaa Katika Birthday:

 

Alama nyingine ya sherehe za siku ya kuzaliwa ni mishumaa. Wagiriki waliokuwa wakipeleka keki zao kwa Artemis waliweka mishumaa juu ya keki kwa sababu iliifanya keki ionekane ina’gara kama mwezi mpevu.

 

Wajerumani ambao walifahamika kuwa ni watengenezaji wazuri sana wa mishumaa, walianza kutengeneza mishumaa midogo kwa ajili ya keki zao. Baadhi ya familia za Kijerumani zilitumia mshumaa mmoja mkubwa kuashiria mwangaza wa maisha. Mshumaa huo uliwekwa alama za mistari na nambari (mara nyingi nambari 12) ambazo zitaunguzwa kila mwaka.

 

Watu wengine wanaamini kuwa mishumaa inawekwa juu ya keki kwa sababu za kidini.

 

Wengine wanaamini kuwa moshi unaotoka katika mishumaa hiyo inapeleka maombi yao mbinguni.

 

Siku hizi watu wengi wanafanya maombi yao kimya kimya wakati wanapozima mishumaa yao. Wanaamini kuwa kuzima mishumaa yote kwa mpulizo mmoja kunaleta bahati njema.

 

Vipi Sherehe Za Siku Ya Kuzaliwa Zilianza:

 

Utamaduni wa sherehe ya kuzaliwa ulianza bara la Ulaya miaka mingi iliyopita. Ilikuwa ikiogopewa kwamba mashetani walivutiwa zaidi kwa watu katika siku zao za kuzaliwa. Ili kuwalinda na madhara, ndugu na marafiki huja kwa mtu mwenye birthday yake wakiwa na mawazo na maombi mazuri. Kupeana zawadi kunaleta furaha/uchangamfu zaidi na kuwafukuza mashetani hao. Hivi ndivyo sherehe za siku ya kuzaliwa zilivyoanza

 

Mwanzoni ilikuwa ni wafalme tu ndio walioonekana ni umuhimu kwao kuwa na sherehe za siku ya kuzaliwa (inawezekana hivi ndivyo desturi ya mataji yanayovaliwa katika birthday ilivyoanza?). Kadri muda ulivyopita, watoto nao walishirikishwa katika sherehe hizi. Sherehe za mwanzo za birthday za watoto zilikuwa zikifanyika Ujerumani na ziliitwa Kinderefeste.

 

Wagiriki waliamini kuwa kila mtu ana nguvu za kiroho zinazomlinda na pia mashetani wanaohudhuria wakati wa kuzaliwa kwake na kumuangalia muda wote wa maisha yake. Nguvu hizi za kiroho zina uhusiano wa kiroho na mungu wa siku ambayo mtu huyo amezaliwa.

 

Warumi pia wanakubaliana na mawazo hayo. Mawazo hayo yaliletwa na imani za wakristo kuwa zinaendana na fikira za watawa wao na watukufu mbalimbali.

 

Desturi ya kuwasha mishumaa juu ya keki imeanza kwa wagiriki. Keki za asali za duara kuashiria mwezi na viwashio pamoja na mishumaa viliwekwa katika sehemu maalum ya mahekalu ya (Artemis). Mishumaa ya birthday, imani za kijadi, zina hadhi maalumu isiyo ya kawaida ya kukubaliwa kwa maombi. Kuwasha mishumaa na moto wa muhanga umekuwa na athari maalum za kiroho tokea pale mtu alipoiweka mara ya kwanza kwa ajili ya mungu wake. Kwa hivyo mishumaa ya birthday ni heshima na ina faida kubwa katika kumpatia bahati njema mtoto mwenye kuzaliwa siku hiyo.

 

Sherehe hizi za birthday pia zinahusiana na kuwaiga mayahudi na wakiristo jinsi wanavyofanya sherehe zao hizo. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, kwa kutuonya juu ya kutoiga desturi na tamaduni zao:

 

Imetoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) - Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Mtafuata nyendo  za wale waliokuja  kabla yenu  hatua kwa hatua mpaka itafika hadi wakiingia katika shimo la kenge, na nyinyi mtaingia pia.” Wakasema (Swahaba): “Ee Rasuli wa Allaah, je, unamaanisha) Mayahudi na Manaswara?  Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Hivyo nani basi mwengine?” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Vile vile katika Hadiyth Swahiyh iliyotoka kwa ‘Abdullaah bin 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

 

"Yeyote atakayeigiza (atakayejifananisha na) watu basi naye ni kama wao"  [Ibn Hibbaan]

 

Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika kusherehesha (yaani kuifasiri) Aayah hii,  

وَالَّذِينَ لَا يَشْهَدُونَ الزُّورَ

Na wale ambao hawashuhudii uongo, [Al-Furqaan: 72]

 

“Ama kwa upande wa sikukuu za Washirikina, wamechanganya shaka zao, matamanio yao na uongo wao, hakuna lolote kwao lenye faida yoyote ya kidini, na kadri wanavyotaka kupata wanayoyataka kwa haraka ndivyo wanavyoishia na machungu. Kwa hiyo wao ni waongo, na washuhudieni ina maana washughulikieni.

 

Aayah hii jinsi ilivyo inawasifu na kuwapongeza,

 

 Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uongo [Al-Furqaan: 72 ] 

 

ambayo inamaanisha kuwataka watu kujiepusha na kushiriki katika sikukuu zao na aina yengine ya uongo. Tunafahamu kuwa ni vibaya kuhudhuria sherehe zao kwa sababu sherehe hizo zimeitwa az-zuwr (yaani uongo)

 

Aayah hii inaonyesha kuwa ni haraam kufanya hivi kwa sababu nyingi, kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Taa’alaa) Ameziita (sherehe hizo) az-zuwr. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amewakemea wale wenye kusema uongo hata kama hakuna yeyote atakayedhurika na uongo huo, kama katika Aayah inayokataza dhwihaar (namna ya talaka ambayo mume humwambia mkewe “wewe nakuona kama mgongo wa mama yangu”. Na kwa hakika wanatamka maneno mabaya na uongo (zuwran)” [al Mujaadilah 58:2]. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema (tafsiiyr ya Aayah:

 وَإِنَّهُمْ لَيَقُولُونَ مُنكَرًا مِّنَ الْقَوْلِ وَزُورًا

Na hakika wao bila shaka wanasema yasiyokubalika na kauli ya kuchukiza na uongo. [Al-Mujaadalah :2]

 

Kwa hiyo yule anaefanya az-zuwr  ameshutumiwa katika namna hii.”
 

Na katika Hadiyth: Anas ibn Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema:

Watu wa Jaahiliyah walikuwa wana siku mbili katika kila mwaka wakicheza (wakisherehekea), alipofika Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah akasema: “Mlikuwa mna siku mbili mkicheza (mkisherehekea) na sasa Allaah Amekubadilishieni kwa zilizo bora zaidi kuliko hizo; Siku ya Fitwr (‘Iydul Fitwr) na siku ya Al-Adhwhaa (‘Iydul Adhw-haa))   [Abu Dawuud, An-Nasaaiy na imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy].

 

Hii inaonyesha wazi kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila shaka ameukataza umma wake kusherehekea sikukuu za makafiri, na amejitahidi kuondosha uwezekano wa njia zote. Ukweli kuwa dini ya Ahlul-Kitaab imekubaliwa haimaanishi kuwa sikukuu zao pia zimekubalika au ziendelezwe na ummah huu, kama ambayo kufuru zao nyengine na madhambi yao hayakukubaliwa. Kwa hakika, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda kwa undani kuuamrisha ummah wake kujitofautisha nao katika mambo mengi ambayo ni mubaah (yaani yaliyokubalika) na namna nyingi za ‘ibaadah ili kuepusha (njia) zitazowapeleka wao kufanana nao katika mambo mengine pia. Suala hili la kujitofautisha liwe ni kikwazo katika masuala yote, kwa sababu kwa kadri mnavyotofautiana zaidi na watu wa motoni, na uwezekano wa kufanya matendo wanayoyafanya unakuwa ni mdogo zaidi.

 

Kwanza: Hadiyth

 

"Kila ummah una sikukuu zao, na hii ni sikukuu yetu"

 

Inamaanisha khususan kuwa, kila watu wana sikukuu zao, kama Alivyosema Allaah (tafsiyr ya Aayah)

لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا

..Kwa kila (ummah) katika nyinyi Tumeujaalia shariy’ah na manhaj. [Al-Maaidah: 48]

 

Hii inamaanisha kuwa kila taifa lina dasturi zake.  Ama laam katika li-kulli (Kwa kila...) inamaanisha khususan. Kwa hiyo iwapo Mayahudi wana sikukuu zao na Wakristo wana sikukuu zao, hizi ni kwa wao tu, na sisi hatupaswi kushiriki chochote katika sikukuu hizo, kama ambavyo hatushirikiani katika qibla (upande wa kuelekea katika sala) au katika sheria zao.

وَلِكُلٍّ وِجْهَةٌ هُوَ مُوَلِّيهَا ۖ

Na kila mmoja ana upande wa kuuelekea.   [Al-Baqarah: 148]

 

Pili: sharti moja lililowekwa na ‘Umar ibn al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na wakakubaliana nalo Maswahaba na mafuqahai (wanavyuoni) wote baada yao: kuwa Ahlul-kitaab wote waliokubali kuishi chini ya dola ya Kiislam (ahl al-dhimmah) wasisherehekee sikukuu zao wazi wazi katika miji ya Kiislam (ardhi zilizo chini ya sheria ya kiislam). Iwapo waislam wamekubali kuwazuia kusherehekea wazi wazi, vipi iwe sahihi kwa waislam wenyewe kusherehekea sikukuu zao hizo? Iwapo muislam atasheherekea sikukuu hizo, haiwi kufanya hivyo ni vibaya zaidi hata kuliko kwa makafiri wenyewe kusherehekea wazi wazi?

   

 

Share