Mawlid: Hoja Za Wanaosherehekea Mawlid Na Majibu Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

Zifuatazo ni hoja za watetezi wa mawlid na majibu yake.

 

1-Hoja ya kwanza ya watetezi wa mawlid: 

Aayah katika Surat Yuunus:

((قُلْ بِفَضْلِ اللّهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَلِكَ فَلْيَفْرَحُواْ هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ))

((Sema: Kwa fadhila ya Allaah na Rahmah yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya)) [Yuunus:58] 

 

Jibu la hoja ya kwanza la watetezi wa mawlid:

Baadhi ya watetezi wa mawlid wanatoa hoja ya Aayah hii kuwa kauli ya  Allaah  سبحانه وتعالى wafurahi, basi ni kufurahia mazazi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم. Lakini tukitazama tafsiri ya Aayah hiyo kwa wafasiri wote wakubwa kama Ibnu Jariyr, Ibnu Kathiyr, Qurtubiy, Al-Baghaawiy, Ibnul-Arabiy na wengineo, hatukuti maana hiyo kabisa. Maana iliyotajwa na wafasiri ni wafurahi kwa yale yaliyowajia kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى  ya Uongofu na Dini ya haki. Na pia imefasiriwa kuwa, wafurahi kwa Qur-aan na Uislam, na imethibitisha haya  Aayah ya kabla yake inayosema:

((يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاء لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ))

((Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu , na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uongofu, na Rahmah kwa Waumini)) [Yuunus:57]

Nayo ni Qur-aan. Na kama pia Aayah ya 170 ya Suratul 'Imraan isemayo, ((Na ni wenye kufurahia fadhila Zake)). Vilevile imefasiriwa kuwa fadhila Zake ni Uislaam, na Rahma Zake ni Qur-aan.

Amesema Ibnu Kathiyr katika tafsiyr yake kuhusu: ((uongofu na Rahma kwa Waumini)), ni kupata uongofu na Rahma kwa waumini waliosadiki na kukinaika. Kama zinavyoonyesha kauli Zake Allaah سبحانه وتعالى nyingine:

((وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِلْمُؤْمِنِينَ وَلا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَاراً))  

((Na Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na Rahmah kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara)) [Al-Israa:82]

Na kauli Yake Allaah  :سبحانه وتعالى

((قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدىً وَشِفَاء))

((Sema: Hii Qur-aan ni uongofu na shifaa kwa wenye kuamini)) [Fuswilat:44]

 

Ama kuhusu Rahma kwa watu;  haiwi kwa mazazi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   bali ni kwa kupewa kwake Utume na kutumwa kufikisha ujumbe kwa watu. Na dalili ni kutoka katika Qur-aan na Sunnah.

Dalili kutoka katika Qur-aan ni kwamba yeye ni Rahma kwa viumbe wote kutokana na kutumwa kwake na wala haikutaja kuzaliwa kwake. Anasema Allaah  سبحانه وتعالى

((وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ))

((Nasi Hatukukutuma ila uwe ni Rahmah kwa walimwengu wote)) [Al-Anibyaa:107]

 

Na katika Sunnah ni Hadiyth:

عن أبي هريرة رضي الله عنه   قال: قيل : يا رسول الله ! ادع على المشركين . قال صلى الله عليه وسلم  (( إني لم أبعث لعانا  وإنما بعثت رحمة)) مسلم  

Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه ambaye amesema: Aliambiwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    "Waombee (walaaniwe) Washirikina". Akasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ((Mimi sikupewa utume (sikutumwa kuja kuwa) ni mlaaniji (mwenye kuwaombea laana watu) bali nimepewa utume kuwa ni Rahma)) [Muslim]

 

2-Hoja ya pili ya watetezi wa mawlid: 

Aayah katika Suratul-Ahzaab kwamba mawlid yanahusiana na kumswalia:

 ((إِنَّ اللَّهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيماً))

((Hakika Allaah Anamteremshia Nabiy Rahma (na baraka). Na Malaika Wake pia (wanamuombea du’aa). Enyi mlioamini muombeeni Rahmah na msalimieni maamkizi ya amani.)) [Al-Ahzaab:56]

 

Jibu la hoja ya pili la watetezi wa mawlid:

Imaam Al-Bukhaariy anatuelezea tafsiri ya Aayah hiyo ni kuwa Maswahaba رضي الله عنهم walimuuliza Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuwa wamefahamu namna ya kumtakia amani juu yake, lakini hawafahamu jinsi ya kuswalia. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akawaambia waseme, 'Allahumma Swalli 'alaa Muhammad wa 'ala aali Muhammad...' hadi mwisho kama ilivyo kwenye tashahhud ya Swalaah.

Na maana au tafsiri ya Aayah hiyo imeelezwa na wafasiri wa Qur-aan ambao wamenukuu Hadiyth yenye kufafanua hivyo.   

Pia kumswali Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  si kwa mara moja kwa mwaka bali inatupasa tumsawalie kwa wingi kila mara kama ilivyothibiti fadhila zake katika Hadiyth ifuatayo:

عنْ عبد اللَّه بن عمرو بن العاص ، رضي اللَّه عنْهُمَا أنَّهُ سمِع رسُول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقُولُ : ((من صلَّى عليَّ صلاَةً ، صلَّى اللَّه علَيّهِ بِهَا عشْراً))   رواهُ مسلم

 Imetoka kwa 'Abdullah ibn 'Amru ibn Al-'Aasw  رضي اللَّه عنْهُمَا kwamba kamsikia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم anasema, ((Atakayeniswalia (kuniombea Rahma na amani) mara moja, Allaah Atamteremshia Rahma mara kumi)) [Muslim]

 

Pia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametufundishia nyakati kadhaa za kumswalia kama vile siku ya Ijumaa, baada ya adhaan, anapotajwa n.k wala hakuna dalili kwamba tumswalie siku ya kuzaliwa kwake

 

 3-Hoja ya tatu ya watetezi wa mawlid:

Kufurahikia kuzaliwa kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   ni jambo lililoamrishwa katika Qur-aan wakitaja Aayah mbili zifuatazo zinazohusiana na Nabii Yahya  عليه السلام   na Nabii 'Iysa  :عليه السلام

 ((وَسَلَامٌ عَلَيْهِ يَوْمَ وُلِدَ وَيَوْمَ يَمُوتُ وَيَوْمَ يُبْعَثُ حَيًّا))

((Na amani iwe juu yake siku ya kuzaliwa, na siku ya kufa, na siku ya kufufuliwa)) [Maryam: 15] Akimaanishwa Yahya عليه السلام  

 

((وَالسَّلَامُ عَلَيَّ يَوْمَ وُلِدتُّ وَيَوْمَ أَمُوتُ وَيَوْمَ أُبْعَثُ حَيًّا))

((Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa kuwa hai)) [Maryam: 33] Akimaanishwa 'Iysa عليه السلام  

 

Jibu la hoja ya tatu la watetezi wa mawlid:

Aayah inasema ((amani...)). Je, ina maana kwamba, neno 'amani' ni sawa na kufurahikia? Vile vile Aayah hizo hazikutaja kuhusu mazazi  pekee bali zimetaja; kuzaliwa, kufa na kufufuliwa. Sasa vipi ichukuliwe kuzaliwa pekee bila ya kufariki au kufufliwa? Wanavyuoni wamekubaliana kwamba tarehe hiyo ya 12 Rabiy'ul Awwal inayodaiwa kuwa kazaliwa, ndio tarehe ya kufariki kwake. Lakini hakuna uhakika wa tarehe ya kuzaliwa kwake kwa sababu watu walikuwa wakihesabu tukio kutokana na matukio fulani, na kuzaliwa kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   kulijulikana kuwa kazaliwa ‘aamul-fiyl (mwaka wa tukio la tembo) haikutajwa tarehe yake.      

 

4-Hoja ya nne ya wa watetezi wa mawlid:

Kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akifunga siku ya Jumatatu ambayo ilikuwa siku ya kuzaliwa kwake kama ilivyotajwa katika Hadiyth ifuatayo, na hivyo basi aliiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake:

عن أبي قتادة رضي الله عنه : أن النبي صلى الله عليه وسلم سئل عن صوم يوم الاثنين فقال: ((ذلك يوم ولدت فيه وأنزل علي فيه))  رواه الإمام مسلم

Imetoka kwa Abu Qataadah  رضي الله عنه kwamba aliulizwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kuhusu kufunga Jumatatu akasema: ((Hiyo ni siku niliyozaliwa na siku ulioteremshwa kwangu [Utume])) [Imaam Muslim]

 

Jibu la hoja ya nne la watetezi wa mawlid:

Kuiadhimisha siku kuzaliwa kwake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  ilikuwa kwa niyyah ya kumshukuru Allaah ndipo akawa anafanya ibada hiyo ya kufunga na wala hakusherehekea hata siku moja mawlid.  

Pia Mtume  صلى الله عليه وآله وسلم hakufunga siku maalum katika mwezi huu wa Rabiy'ul Awwal. Hakufunga tarehe 12 wala siku yoyote ile isipokuwa siku za Sunnah zinazojulikana Jumatatu na Alkhamiys pamoja na masiku meupe ambayo alifunga kila mwezi.     

 

5-Hoja ya tano ya watetezi wa mawlid:

Kwamba Maswahaba walimpokea Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    alipoingia Madiynah kwa qaswiydah na wengine walikuwa wakimsomea mashairi na qaswiydah za kumsifu na yeye alikuwa akikubali kusomewa hayo mashairi.

Jibu la hoja ya tano la watetezi wa mawlid:

Wanavyoni wametaja kwamba hakuna dalili ya kusomewa qaswiydah ya kupokelewa alipoingia Madiynah ambayo inataja: “Twala'al-badru 'alaynaa, min thaniyaatil wadaa'”.  Historia za kuaminika hazikutaja kuwa Mtume alipita njia hiyo ya Thaniyaat al wadaa' wakati wa kuelekea Madiynah.

Pia haikuthibitika kwamba Maswahaba walikuwa wakimsomea mashairi na qaswyidah siku ya kuzaliwa kwake, bali ilikuwa zaidi kunapotokea ushindi wa vita dhidi ya maadui.

 

6-Hoja ya sita ya watetezi wa mawlid:

Kwamba kusherehekea Mawlid ni kumpenda, kumuadhimisha, kumtukuza na ni kumbukumbu ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kwa walimwengu na kwamba inatupasa tufanye hivyo ili vizazi vyetu pia vipate kumtambua Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

Jibu la hoja ya sita la watetezi wa mawlid:

Kumkumbuka na kumuadhimisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    kunatupasa kila siku katika maisha yetu kwa kumpenda na kufuata Sunnah zake, wala si kwa mara moja tu kwa mwaka.

Pia kumbukumbu ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kwa walimwengu na vizazi vyetu zimeshabainishiwa na Allaah سبحانه وتعالى katika Qur-aan na Sunnah nazo kwa kila siku; Anasema Allaah سبحانه وتعالى  

 ((وَرَفَعْنَا لَكَ ذِكْرَكَ))

 ((Na Tukakutukuza utajo wako)) [Ash-Sharh:4]

 

Na kutukuzwa huko ni katika Swalah zetu tunapomswalia katika tashahhud, katika kutimiza Hajj na Swawm,  katika adhaan na iqaamah za Swalah, kwenye khutba, kumswalia anapotajwa jina lake, katika du’aa, tunaposoma au kusikia Hadiyth zake, katika kufuata Sunnah zake, katika vikao vya darsa na kadhalika, kwa hiyo ni kumbukumbu ya kila siku, kila wakati katika maisha yetu na sio siku moja tu kwa mwaka. 

 

7-Hoja ya saba ya watetezi wa mawlid:

Kwamba kuna bid'atun-hasanah (bid'ah nzuri).

Jibu la hoja ya saba la watetezi wa mawlid:

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  alipotaja kuhusu bid'ah amesema:

((....وإِيَّاكُمْ ومُحْدثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٍ ضلالَةٌ ))  رواه أبو داود ، والترمذِي وقال حديث حسن صحيح

((…na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu)) [Abu Daawuud, At-Trimidhiy kasema Hadiyth hasan sahiyh]

 

Imetajwa:  'Kullu bid'atin dhwalaalah' (KILA bid'ah ni upotofu). Na ikiwa kauli hii wanaipinga kuwa si KILA bid'ah, basi wanasemaje kuhusu kauli za Allaah  سبحانه وتعالى Anaposema:

 ((كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ الْمَوْتِ))

((Kila nafsi itaonja mauti)) [Al-'Imraan: 185]

 

 ((وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَآئِرَهُ فِي عُنُقِهِ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا ))

((Na kila mtu Tumemfungia amali yake shingoni mwake. Na Siku ya Qiyaamah Tutamtolea kitabu atakachokikuta kiwazi kimekunjuliwa)) [Al-Israa:13]

 

Na,

 

((كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ))

 ((Kila nafsi imo rahanini kwa mabaya iliyoyachuma))  [Al-Mudathhir:38]

 

 Na

((وَكُلُّ شَيْءٍ فَعَلُوهُ فِي الزُّبُرِ)) ((وَكُلُّ صَغِيرٍ وَكَبِيرٍ مُسْتَطَرٌ))

((Na kila jambo walilolifanya limo vitabuni)) ((Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa))  [Al-Qamar:52-53]

Je, tutakanusha kwamba sio kila nafsi itaonja mauti? Au si kila mtu amefungiwa amali zake shingoni? Au si kila nafsi iko rahanini? Au si kila jambo tunalolifanya dogo na kubwa liko vitabuni? Bila shaka kauli ya Allaah سبحانه وتعالى Inathibitisha kuwa kila binaadamu atakufa na kila mmoja ana hesabu yake atakayoikuta siku ya Qiyaamah. Kwa hiyo kauli ya 'kullu bid'atin dhwalaalah' (kila bid'ah ni upotofu) pia ina maana hiyo hiyo bila yakuwekwa “isipokuwa” (mawlid ni bid’ah hasanah).  

 

8-Hoja ya nane ya watetezi wa mawlid:  

Kwamba kuna baadhi ya mambo yamefanyika baada ya kufa kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  na mengineyo yanaendelea kutendeka kwa hiyo ni bid'ah. Miongoni mwao ni; kukusanywa Qur-aan na kuwekwa katika Mswahafu na Abu Bakar  رضي الله عنه, kisha baadaye kuwekwa harakaat (vokali) katika Mswahafu. Pia 'Umar ibnul Khatwaab  رضي الله عنه kuihamishwa Maqaam Ibrahiym kuwa mbali kidogo na Al-Ka’bah.  Pia kuongezwa adhaan ya pili na ya tatu siku ya Ijumaa na 'Uthmaan bin 'Affaan رضي الله عنه . Pia Maswahaba hawakutumia kipaza sauti katika adhaan, au hawakufanya twawaaf juu katika ghorofa za Masjid Al-Haram, au hawakupanda magari bali walipanda ngamia, au hapakuweko na zana za utamaduni za kujifunza Dini kama radio, televisheni, mitandao, CD's na kadhalika. Kwa hiyo kutumia vitu hivyo pia ni bid'ah. 

Jibu la hoja ya nane la watetezi wa mawlid:

Kufuata waliyoyatenda Makhalifa hao watukufu, basi ni jambo aloamrisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ambaye amesema:

 ((... أُوصِيكُمْ بِتَقْوى اللَّه، وَالسَّمْعِ وَالطَّاعَةِ وإِنْ تَأَمَّر عَلَيْكُمْ عَبْدٌ حبشيٌ، وَأَنَّهُ مَنْ يَعِشْ مِنْكُمْ فَسَيرى اخْتِلافاً كثِيرا . فَعَلَيْكُمْ بسُنَّتي وَسُنَّةِ الْخُلُفَاءِ الرَّاشِدِينَ الْمَهْدِيِّينَ ، عضُّوا عَلَيْهَا بالنَّواجِذِ، وإِيَّاكُمْ ومُحْدثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٍ ضلالَةٌ)  رواه أبو داود ، والترمذِي وقال حديث حسن صحيح

((Nakuusieni kumcha Allaah, usikivu na twaa hata ikiwa kiongozi wenu (Au atakayekuamrisheni) ni Mtumwa wa Kihabashi. Mtakaoishi miongoni mwenu mtaona ikhtilafu nyingi. Kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waliongoka baada yangu. Ziumeni kwa magego (zikamateni kwa nguvu wala msiziache). Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu) [Abu Daawuud, At-Trimidhiy kasema Hadiyth hasan sahiyh] 

Na kukusanywa Qur-aan katika Mswahafu ilikuwa kwa sababu hapo awali Qur-aan ilihifadhiwa katika vifua vya Maswahaba. Ikatokea haja ya kuikusanya Qur-aan katika Mswahafu kwa vile Maswahaba wengi waliohifadhi Qur-aan waliuliwa katika vita vya Yamaamah, Maswahaba wakaingiwa na hofu kwamba Qur-aan itakujwa kupotea na haitawafikia vizazi vya mbele. Ndipo ilipokusanywa baada ya ushauri mzito baina ya Makhalifa na Maswahaba. Kisha baada ya hapo ikaja kuwekewa harakaat kwa sababu kulihofiwa kwamba Qur-aan itakuja kusomwa kimakosa kwa vile lugha ya Kiarabu ilianza kupotea ufasaha wake, na si wepesi kuisoma lugha ya kiarabu bila ya harakaat kwa wasio na ujuzi wa hali ya juu wa lugha ya Kiarabu.  Likawa ni jambo lisilokuwa na budi kutendwa kwa sababu Qur-aan ni Mwongozo kwa walimwengu.

Kuhusu kufanya twawaaf ghorofani pia ni jambo lisilokuwa na budi ili ‘ibaadah hiyo ya muhimu kabisa itimizwe. Haiingii akilini kwamba watu wote waweze kufanya twawaaf ardhini kwa sababu ya msongamano wa Waislamu hapo.

Ama kuhusu vipaza sauti, njia za usafirishaji, vifaa vya utamaduni vya kujifunzia na kadhalika, vyote hivyo ni nyenzo tu za kuwepesisha kutekeleza ibada zetu. Kuchanganya nyenzo na ibada ni jambo lilisilokuwa la mantiki. Na Allaah  سبحانه وتعالى Mjuzi wa ghaibu, Amejua kuwa hali za Waislamu zitafikia kuhitajika hayo. Mfano kuhusu usafiri wa watu baina ya nchi kufika Makkah kutimiza Hajj, iwezekanaje usafiri kwa ngamia?  

Kwa hiyo panapotokea jambo linalohitajika kuwepesisha ibada zetu, Wanavyuoni hufutu jambo ambalo halina budi kutendwa kwa ajili ya manufaa ya Ummah. Na Allaah Anajua zaidi.

 اللَّهُمَّ  اَرِنا الْحَقَّ حَقاً وَارْزُقْنا اتِباعَه وَارِنا الباطِلَ باطلاً وَارْزُقْنا اجْتِنابه

Allaahumma Arinal-Haqqa Haqqaw-War-Zuqnat-tibaa'ah, Wa Arinal-Baatwila Baatwilaw-War-Zuqnaj-tinaabah.

Ee Allaah, Tuonyeshe haki kuwa ni haki Na Uturuzuku kuifuata. Na Tuonyeshe batili kuwa ni batili na Uturuzuku kuiepuka.

 

 

Share