05-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kutekeleza haki za watu

 
Kutekeleza haki za watu:
 
Hapana shaka kuwa katika mambo ambayo yatamfaa mja baada ya kifo chake ni kuhakikisha kuwa katika mwisho wa uhai wake amesharejesha haki za watu, na aombe kwa wale ambao wana haki zao kwake wachukue haki zao hizo, au aliovunja heshima/ hadhi warejeshe heshima hizo kabla hajafariki au mfano wa mambo kama hayo au vinginevyo apate msamaha kutoka kwa watu hao.
 
Akishindwa kufanya hivyo kwa sababu nyingi mfano kwa udhaifu aliokuwa nao, au kwa maradhi yake au vile vile kutokuwepo wenye haki hizo, au kutokuwepo kwa haki hizo kwake yeye, ikiwa hali ndivyo hivyo ilivyo basi wakiwepo jamaa zake wenye kutaka kumnufaisha basi na watoe haki hizo na kuwapa wenyewe kabla ya kifo chake na ikishindikana lifanyike baada ya kifo chake.
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Mwenye haki ya nduguye kwake kamvunjia heshima na hadhi yake au ana deni la mtu basi na arejeshe haki hizo kabla ya kufika siku ambayo haitakubaliwa dinari au dirhamu yake, akiwa ana amali njema alizofanya basi zitachukuliwa amali hizo na kupewa huyo sahibu yake, ikiwa hana amali njema alizofanya basi atapewa maovu ya sahibu yake.”
Share