12-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kutokutekeleza Usia wenye madhara

Kutokutekeleza Usia wenye madhara:
 
 
Mja atakapousia usia ambao ndani yake mna madhara kwa mfano; kuwazuilia watu wake haki na kuwapa wasiostahiki haki hiyo, au kuusia katika vitu ambavyo ni bid’a na kinyume na sheria wakati wa kupeleka jeneza na kuswalia, hali kadhalika wakati wa kuzika kwa mfano kuusia watu waomboleze kwa makelele na mfano wa hayo, basi ni juu ya kila aliyehudhuria katika usia huo amtanabahishe kwa hilo ili aweze kutubia na kulibadilisha atakapokufa kabla ya hilo kufanyika basi jamaa zake warejeshe haki hizo kwa wanaohusika na kutokutekelezwa kwa usia huu wenye dhulma na uovu ndani yake. Haki za Allah ni kubwa zaidi kuliko haki ya maiti wao juu yao, hakuna utiifu wa kumtii mja katika kumuasi Allah (Subhaanahu wa Ta'ala).
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Atakayezua jambo katika dini yetu hii ambalo halipo basi atarejeshwa nalo.” (Bukhari na Muslim)
 
Umran bin Hiswin (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema, ‘Mtu mmoja aliwaacha huru watumwa sita alipokuwa anataka kufa, wakaja warithi wake katika mabedui wakaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) na kumueleza jambo hilo, Mtume akawauliza “Kafanya hivyo!” akaendelea kusema, “lau tungelijua hilo tusingemswalia” akasema Umar, ‘Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akawafanyia kura baina yao kisha akawaacha huru wawili na wanne akawarejesha kwa watu wao.” (Ahmad na Muslim)  
 
Share