31-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kulisindikiza Jeneza

Kulisindikiza Jeneza:
 
 
Hii ni moja katika haki miongoni mwa haki za Waislamu kwa nduguye kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), “Haki ya Muislamu kwa nduguye Muislamu ni tano: Kujibu salamu, kumtembelea mgonjwa, kulisindikiza jeneza, kuitikia mwito na kumuombea mwenye kupiga chafya.” (Bukhari na Muslim)
Mambo yafuatayo huchungwa katika kubeba Jeneza:
·         Jeneza kubebwa mabegani, sio vizuri kubebwa kwa gari ila itakapokuwa ni dharura.
·         Lifuatwe kuanzia nyumbani, kuswaliwa hadi anapomalizwa kuzikwa.
·         Kumpeleka kwa mwendo wa haraka lakini sio kulikimbiza jeneza.
·         Inajuzu kuwa mbele ya jeneza au nyuma yake, kuliani mwake au kushotoni mwake, ila aliyepanda gari au mnyama anatakiwa akae nyuma ya jeneza.
·         Haifai kufuata kwa maombolezo na makelele, au kwa kubeba vijinga vya moto au kufuatwa na wanawake au kwa sauti hata ikiwa ni kwa kufanya dhikri. Mfano wa hayo; kilichoenea miongoni mwa watu wanapobeba jeneza husema, ‘wahidu’ yaani semeni, ‘Laa ilaha illa llah’ hii ni miongoni mwa bid’a na ni makosa katika kusindikiza jeneza kufanya hivyo. Na katika jumla ya makosa mengine hali kadhalika ni kuwa kwa wale wanaobeba jeneza kwa gari huweka kaseti na radio yenye kusoma Qur’an au kutoa khutuba, hili nalo halifai na ni kinyume na Sunna katika kulifuata jeneza ni vizuri watu wakawa na subira, kuwa na mazingatio katika tukio hili zima kwani aliyebebwa leo ni ndugu yao na kesho atabebwa yeye.
Share